Majambazi yamteka mfanyabiashara Dar

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,006
Majambazi yamteka mfanyabiashara Dar
Mwandishi Wetu
Daily News; Sunday,August 31, 2008 @09:21

SAKATA linalowahusisha polisi mkoani Tanga wanaodaiwa kuwaachia watuhumiwa wa ujambazi, limechukua sura mpya baada ya wahalifu hao kumteka mfanyabiashara jijini Dar es Salaam na kumlazimisha awape Sh milioni 150 ili wasimuue.

Inadaiwa Juni mwaka huu, Herman Mchivi, aliuza gari lisilo lake kwa Thomas na raia mwingine wa kigeni ambaye hajafahamika, likasafirishwa hadi Kampala Uganda likakamatwa huko na kurudishwa Dar es Salaam.

Inadaiwa gari hilo aina ya Toyota Hilux 2.8 lenye rangi nyeusi lilikuwa likimilikiwa na mfanyabiashara huyo, Adam Mhagama, anayeishi Dar es Salaam.

Adam baadaye aliamua kuliuza gari lake hilo kwa mkazi mwingine wa Dar es salaam (jina tunalo) na Herman akatumwa alipeleke kwa aliyelinunua. Habari za kiuchunguzi zinaonyesha kwamba hakufanya hivyo na badala yake akaliuza kwa watu wawili wanaodaiwa kuwa ni raia wa kigeni.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari hizi, Mtanzania huyo na mmoja wa raia hao wa kigeni aliyetajwa kwa jina moja la Thomas, walikamatwa kwa nyakati tofauti na katika mazingira tofauti na baadaye gari husika kukamatwa Kampala.

Habari zaidi zinasema kwamba Herman alikamatwa Iringa na mwenzake alikamatwa hotelini Bagamoyo, baada ya polisi kumzidi nguvu katika chumba alichokuwa amefikia.

Herman alikamatwa akituhumiwa kuuza gari lisilo lake na kushirikiana na raia huyo wa kigeni anayetuhumiwa kununua gari la wizi na pia kupora kwa kutumia silaha mkoani Tanga.

HabariLeo Jumapili ina taarifa kuwa, mfanyabiashara huyo ambaye aliwaeleza wahalifu hao kuwa hana kiasi hicho cha fedha, haijafahamika kama yupo hai au wamemuua.

Wahalifu hao huenda walimteka Adam Jumapili iliyopita au Jumatatu asubuhi wiki hii.

Awali kulikuwa na taarifa zilizodai kuwa wahalifu hao waliachiwa katika mazingira ya kutatanisha katika kituo cha polisi Chumbageni, Tanga.

Inadaiwa kabla ya kutekwa, Adam alilazimika kuhama nyumbani kwake kwa kuhofia kuuawa kwa kuwa wahalifu hao walikwenda kuvunja na kumkosa na walitoa ujumbe kutishia maisha yake, ikiwa ni pamoja na azma ya kumuua.

Taarifa za kutekwa kwa Adam zilipatikana Jumatatu wiki hii na tangu wakati huo haikufahamika kuwa watekaji na yeye walikuwa wapi ingawa Jumatano wiki hii gazeti hili lilipata habari kuwa inaaminika Adam anashikiliwa mkoani Tanga.

Hadi Ijumaa asubuhi Adam alikuwa hai, alizungumza na mmiliki wa gari hilo (jina tanalo) anayeishi Dar es Salaam ambapo inasadikiwa alisema kuwa waliomteka wanataka awape fedha hizo wanazodai kuwa zipo kwenye akaunti yake ili wamuache hai.

Chanzo cha habari hizi kimeeleza kuwa Adam aliwaambia majambazi hao kuwa hana kiasi hicho cha fedha kwenye akaunti yake, na kwamba, fedha zilizopo ni robo tu ya kiasi wanachotaka.

Wahalifu hao wanadaiwa kuwa na silaha na vifaa vya kisasa vya kunasa mawasiliano ya simu vilivyowasaidia kuwatoroka polisi kwa nyakati tofauti Tanga, Pwani na Dar es Salaam.

Makao Makuu ya Polisi akiwamo Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba na Polisi Mkoa wa Tanga, wanazo taarifa kuhusu suala hilo.

Ijumaa alasiri gazeti hili lilimpigia simu Mkuu wa Polisi wa mkoa wa Tanga, Simon Sirro hakukuwa na majibu, jana mchana pia simu hiyo ilikuwa ikiita tu.

Taarifa tulizonazo ni kuwa hadi Ijumaa asubuhi Adam na watekaji hao walikuwa katika eneo lisilofahamika mkoani Tanga, kwa sasa haifahamiki wapo wapi.

Tunazo pia taarifa kuwa hadi Ijumaa asubuhi gari lililosababisha sakata hilo lilikuwa Tanga, wahalifu hao waliahidi kulirudisha kwa mmiliki Jumatano lakini hawakufanya hivyo.

Vyanzo vya habari hizi vimedai Herman ni fundi magari, ambaye alikuwa akifanya kazi katika gereji ya Adam jijini Dar es Salaam, alipewa gari alipeleke kwa mkazi wa Dar es Salaam aliyenunua gari kwa Adam.
 
Back
Top Bottom