Maisha bora kwa kila Mtanzania: Inakuwaje Rais Kikwete anakuwa mkali kwa TUCTA kuliko kwa Mafisadi?!

mfukunyunzi

Senior Member
Mar 4, 2011
142
26
YARABI toba! Eti bado yupo
anayeamini kabisa kwamba
maisha bora kwa kila Mtanzania
yatakuja kama mlivyoahidiwa
kabla ya kura zenu?
Nasema kama yupo poleni sana.
Wote si mmemsikia Mkuu wa
Kaya akisema hata baada ya
miaka minane hakuna mshahara
wa kilo tatu na ushei mliokuwa
mkiomba ili hicho ndiyo kiwe
kima cha chini?
Nawaambia hayo si maneno
yangu, kama miaka minane ijayo
bado hatutawe za kuwalipa
watendaji wetu bei hiyo, bado
mnaona ndoto za kuwa na
maisha bora kwa kila Mtanzania?
Wakati mwingine nasema siasa
kumbe ni si hasa! Hivi wakati ule
wakiomba kura zetu
walimaanisha nini walipotuambia
maisha bora kwa kila mmoja
wetu yanakuja?
Wakaongeza na kibwagizo
kingine kwamba eti Bongo yenye
neema ni kazi inayowezekana.
Mbona hivi vibwagizo haviendani
na kauli kwamba pamoja na
dhahabu, almasi, tembo, swala,
misitu, Mlima Kilimanjaro na
Zanzibar yetu bado hatuwezi
kamwe kuwalipa watu wetu kima
cha chini cha hizo laki tatu.
Nasema kwamba mimi simo
kabisaa.
Watu wanadai eti ni mara ya
kwanza walimuona JK akiwa
kwenye sura ya ukali. Kumbe
mlitakaje enyi wana? TUCTA si
walishaonyesha mapema
kwamba hawataki mzaha wakati
huu?
Katika historia ya taifa letu ni
mwaka upi wafanyakazi
walishawahi kuwatosa viongozi
wa serikali kwenye maadhimisho
ya sikukuu yao? Watafiti
wananiambia ni mwaka huu tu.
Nimesikia mwaka huu
kulikuwepo Mei Mosi mbili. Mei
Mosi original na Mei Mosi
academia. Moja wakafanyia
uwanja mkubwa na nyingine
wakakutana Mnazi Mmoja na
Lukuvi.
Maajabu hayakomi duniani.
Sikukuu ya kitaifa halafu mgeni
rasmi awe mkuu wa mkoa? Ina
maana sikukuu za kimkoa mgeni
rasmi atakuwa mkuu wa
kitongoji?
Nasema ngoja nifunge hili domo
langu, sitaki kuwaudhi wakubwa
miye. Simo kabisa tena simo
watu wangu.
Unajua wanadamu ni watu wa
ajabu sana. Wakiamua kuona
dosari watatafuta kila mahali. Si
umewasikia wakosaji wa JK huko
mitaani? Nasikia wanasema
waliokuwa wanagoma ni
wafanyakazi, sasa ikawaje tena
wanaoitwa kuzungumza na
mwajiri mkuu ni wastaafu?
Wakosoaji wanasema hata kama
itakubaliwa kwamba ujumbe ni
sahihi bado ulikuwa ukitolewa
kwa hadhira isiyo sahihi. Wazee
wa Dar es Salaam kwani ndio
waliopanga kugoma?
Kama mkuu alitaka kumjibu
Mgaya, mbona ingependeza zaidi
Mgaya mwenyewe akawepo?
Angesaidia sana kumkumbusha
rais kuhusu baadhi ya hoja
ambazo inaelekea wasaidizi wa
Mkuu wa Kaya hawakumpa
vielelezo sahihi.
Si mmeona TUCTA wakitoa
barua inayosema mkutano wa
hazina waliambiwa waende saa
nane mchana wakati Mkuu wa
Kaya katuambia waliitwa saa
nne?
Ningekuwa Mkuu wa Kaya
ningekuwa nimeshawafuta kazi
wale wote waliotoa taarifa isiyo
sahihi kwa kiwango kile. Mimi
simo lakini kama angewapa
nafasi wale aliokuwa anawapa
ujumbe bila shaka baadhi ya
kumbukumbu zingesahihishwa.
Lakini hawa wazee wa Dar es
Salaam huwa wanapewa
mwaliko kwa njia ipi? Na
inawezezekana hakuna wazee
walio katika vyama vya upinzani?
Pale niliona mashati, fulana na
kapero za chama chetu kigumu
kinachodumu! Kigumu Chama
Cha Mapinduzi! Hivi CUF,
CHADEMA, PONA, TLP na
wengineo hawana wazee kwenye
vyama vyao? Au vyama vyao
havina sare?
Naapa kuna wakati nilihisi wale
ni wazee wa CCM wa Mkoa wa
Dar es Salaam. Tena na
wenyewe hawakuwepo wote.
Mzee wa Kujitoa miye wala
mwaliko sikupewa mtu wangu.
Simo! Niliangaza macho pale
sikumuona pia Mzee Ali Hasan
Mwinyi. Nikafikicha macho pia
sikumuona mtu wangu Salim
Ahmed Salim.
Nadhani hata Joseph Sinde
Warioba hakuwepo. Hivi kuna
uanachama ili uweze kuwa Mzee
wa Dar es Salaam?
Nasema simo ila sijui hii mialiko
ya wazee kukutana na rais sijui
kwa nini haitangazwi ili wazee
wote twende bila kujali itikadi
zetu kisiasa. Nasema tena simo
huko, tena simo kabisa.
Hivi kumbe wazee ni kisima cha
hekima ndiyo maana mtukufu
akawaita ili awasemee TUCTA
kwao eh? Sasa mbona wale
wastaafu wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki nao ni wazee lakini
sijaona wakiitwa na kuteta na
mkuu wa nchi?
Mmesahahu hawa wazee
walivyofika mahali wakaanza
kumwaga radhi? Nasema wakati
wengine wakishangilia kwamba
watu wapewe vidonge vyao,
kuna “mapacha” wao walishalala
barabarani wakiulizia lini
watapewa kile wanadai.
Huko nasema simo, ukitaka
kujua zaidi kamtafuteni mzee
wangu Mlaki. Narudia tena kwa
sauti kubwa kwamba katika hayo
yote mtoto wa mama miye
najitoa kabisa.
Ila nimeamini wabongo ni
wachokozi kwa asili. Eti mijitu
mingine inasema mbona rais
hajawahi kuwa mkali hivyo kwa
wakosaji wengine kama
itaamuliwa kwamba wafanyakazi
ni wakosaji!
Hayo ni ya walimwengu wala si
yangu jamani! Eti mbona mkuu
alipotoa hotuba kuhusu mafisadi
hakuonyesha hasira kali kama ile
ya siku ile alipokuwa
akiichachafya TUCTA.
Nasikia hotuba ile imemfanya
kaka yangu Mgaya awe matawi
ya juu. Miye simo ila wanahabari
wametupasha hayo.
Wabongo wanasema kama rais
angekuwa mkali kwa mafisadi
ungekuta tumeshamaliza
kitambo hadithi za Richmond,
IPTL, dege la rais, rada, EPA na
ufisadi mwingine wowote
unaoufahamu.
Eti mbona rais wetu kipenzi
hajawahi kuwa mkali kwa kiasi
hicho anapozungumzia haya
mambo ya rushwa?
Baba Kikwete maadam uliongea
kwa ukali na kuwafahamisha
wana wema walio wafanyakazi
wa nchi hii kwamba wakigoma
kuna FFU, tunaomba kwa ukali
uleule uwaambie watu wa
Kigoda kwamba kuna mahakama
na jela.
Baba tunakuomba kwa ukali ule
ule uwaagize wahusika
wakamate wale waliotafuna
rushwa kwenye sakata la rada,
nasikia wakoloni wetu wa zamani
wameshatutafunia kila kitu
imebaki kumeza tu.
Tunaomba uwe mkali kwa
mafisadi walau kama ulivyokuwa
mkali kwa wafanyakazi na
ikiwezekana uwe mkali zaidi
baba.
Baba tunakusihi kwa
unyenyekevu kabisa
wakumbushe wale wote
wanaotufanya tushindwe
kuwalipa baadhi ya wafanyakazi
wetu mishahara walau ya
kutosha milo yenye hadhi kwa
mwezi mzima kuwa ufisadi ni jinai
na kuna vyombo vya dola. Kuwa
mkali kwa wote baba, ili nyota
yako iendelee kung ’aa kama
walivyotuambia REDET! Jamni
REDET nao wee acha tu. Mimi
simo huko.
Kati ya masomo ambayo Mzee
wa Kujitoa hajawahi kuanguka
darasani ni pamoja na hisabati.
Enzi zake akiwa darasani mambo
kama magazijuto, milinganyo,
aljebra na vitu kama hivyo
vilikuwa havimpi tabu sana.
Sasa kwenye ile hotuba ya
mheshimiwa kuna kitu kina
mchanganya Mzee wa Kujitoa.
Hivi laki tatu ukizidisha na laki
tatu unusu unapata trilioni sita?
Nasema sijui labda kama
mwalimu wangu wa hesabu
marehemu Kiko alinidanganya.
Lakini mbona mimi napata kitu
kama trilioni moja na ziada
kidogo? Sasa zile takwimu
mbona hazikuainisha inakuwaje
tunapata trilioni sita nukta
kadhaa?
Hapana, mimi kwenye hili
nawaachia wanazuoni wanifanyie
mahesabu. Narudia tena simo,
sitaki kuchonganisha watu miye.
Wacha tu nifunge kazi niondoke
niwahi misafara ya weldi
ikonomik foram. Si mliona
Watanzania tulivyo na akili za
ziada? Kusikia wageni wanakuja
nasikia mlipanda miti iliyokomaa
kule kwenye Barabara ya Sam
Nujoma.
Mungu mkubwa, mvua zilinyesha
hivyo wageni wakajua siku zote
barabara zenu zilikuwa
zimepambwa na hizo palm za
dhahabu. Inawezekana ulikuwa
ni mpango wa jiji kufanya hivyo?
Hivi ni sahihi kupanda miti ya
gharama vile kwa ajili ya urembo
wakati tuna barabara hazipitiki?
Mbona huku ni sawa na kuuza
kiatu ili ununue soksi?
Nikiwaambia wakati mwingine
mnachomekea makoti kwenye
suruali kama asemavyo kaka
yangu Meku mnabisha!
Najitoa jumla jumla. Simo
kwenye haya yote mjukuu wa
babu miye!
 
Nikiikumbuka siku mkwere alipotutukana,kutudhalilisha,kutudhihaki na kutuchonganisha na watz wengine huwa naumia sana nafsini mwangu.Alituambia wazi hata tugome miaka 8 laki tatu unusu haziwezekani,leo tena anasema hawezi kumaliza matatizo ya watanzania(kwani hata mzee Nyerere alishindwa!).Maisha yanazidi kuwa magumu,kila kukicha afadhali ya jana,lakini wafanyakazi watz tuko kimya,tunanung'unikia chinichini...TUCTA nao weshachakachuliwa,wamesahau kutetea maslahi yetu....Ni lini uvumilivu utatuishia(kama Pinda alivyomsemea jk),na kuvaa ujasiri na kudai maslahi bora?Shime wafanyakazi wenzangu tulianzishe!
 
Ni kweli kuna haja ya kuamua kudai haki zetu, tusitegemee hata siku moja kama tutakuja kuzipata kwa kusubiri serikali ya huyu Kiwete itukumbuke, nami amfunge paka kengele, Mgaya keshachakachuliwa.
 
Ni kweli kuna haja ya kuamua kudai haki zetu, tusitegemee hata siku moja kama tutakuja kuzipata kwa kusubiri serikali ya huyu Kiwete itukumbuke, nami amfunge paka kengele, Mgaya keshachakachuliwa.

kama na mgaya kachakachuliwa kilichobaki ni sisi wenyewe wafanyakazi kuingia mabarabarani tu na kudai chetu.
 
Back
Top Bottom