Mahakama yazuia mkataba wa TANESCO, DOWANS!

Dowans rushwa tupu

Na Saed Kubenea - Imechapwa 02 March 2011

Siri za mawakili wao zavuja

Wahofia TANESCO kushinda

Taarifa zinasema hoja ya kuwapo rushwa katika mkataba kati ya Dowans na TANESCO zilitosha kuishawishi Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC), kutupilia mbali madai ya kampuni hiyo.
Kwa mujibu wa hukumu ya ICC, hoja ya rushwa ilijitokeza wakati wa kusikiliza shauri hilo. Haikuwa katika hati ya kiapo ya mjibu madai. Katika hali hii mahakama isingefanya rushwa kuwa hoja kuu.

Kwa maelezo haya, ama mawakili wa TANESCO hawakuona, hawakujua, hawakuthamini hoja ya rushwa; au waliipuuza kwa makusudi. TANESCO iliwakilishwa na Rex Attoneys ya Dar es Salaam.

Surtees ndiye ICC ilisema alitumwa na Rostam Aziz nchini Marekani, 7 Oktoba 2006, kusaini mkataba kati ya Richmond na Dowans, huku akiwa na nyaraka zote muhimu za mkataba kati ya TANESCO na kampuni hiyo.

Taarifa zinasema serikali, mbali na kumpatia Surtees mkataba kati ya Richmond na TANESCO, ilimpatia muhtsari wa kikao cha kamati ya majadiliano kati ya TANESCO na serikali na nyaraka nyingine muhimu ili kurahisisha kazi yake, jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Usalama wa Taifa (TIS) ya mwaka 1976.

MwanaHALISI lilimhoji wakili wa Mahakama Kuu, Tundu Lissu juu ya uwezekano huo na kushindwa au kupuuzwa kwa hoja kuu ya rushwa. Katika mahojiano hayo, Lissu anasema hatua ya mawakili wa TANESCO kushindwa kueleza kuwepo rushwa ndani ya kesi ya msingi, ndiko kulikochangia TANESCO kushindwa.

Lissu ambaye pia ni mbunge wa CHADEMA (Singida Mashariki) anasema, "Kuna ushahidi usiopingika kwamba, mawakili wetu waliolipwa zaidi ya dola 2.4 milioni (sawa na Sh. 3.6 bilioni), hawakufanya kazi yao kama inavyotakiwa."

"Hatua ya mfanyakazi wa Rostam, Bw. Henry Surtees kupata nyaraka za serikali bila kibali cha katibu mkuu kiongozi, ni rushwa ya madaraka. Hata mahakama imeelezwa urahisi huu wa mambo ulitokana na Rostam Aziz kuwa na nguvu kubwa ya ushawishi katika wizara ya nishati na madini," ameeleza Lissu.

Lissu ambaye alishiriki katika kesi ya kampuni ya City Water dhidi ya serikali na kushinda anasema, "Kwa maoni yangu, kazi waliyofanya mawakili wa TANESCO siyo ya kitalaamu. Siamini kuwa hawajui kazi yao. Haya mambo ya rushwa yamejitokeza sana wakati wa kuhoji mashahidi, lakini hayakuwamo katika hati ya utetezi; jambo ambalo limelifanya suala hilo kutopewa uzito wakati wa hukumu."

Anasema kesi ya Dowans dhidi ya TANESCO ilikuwa rahisi kushinda kwa kuwa ilifanyika kwa kutumia sheria za Tanzania. Anasema, "Ni vigumu kuamini kwamba ushiriki huu wa Rostam Aziz, Edward Lowassa, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha ulikuwa na lengo zuri la kulisaidia taifa kumaliza tatizo sugu la umeme."

Lissu anasema "kuna uwezekano mkubwa kwamba viongozi hawa walitumia tatizo la umeme kama kisingizio cha kuliingiza taifa katika mikataba ya kinyonyaji ambayo imeligharimu fedha nyingi na kuwatajirisha wao na maswahiba wao wa kibiashara."

Ni katika mazingira haya, Lissu anasema, watetezi wa TANESCO wangeshinda kama wangetumia sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini ya mwaka 2007. Sheria hiyo inakataza vitendo vya rushwa katika mikataba na manunuzi ya umma, kujipatia manufaa kwa kutumia nafasi za utumishi wa umma na matumizi mabaya ya madaraka ya umma.

Lissu anasema, "Hata kula njama tu kufanya matendo yaliyokatazwa na sheria hii, ni kosa.

Zaidi ya hayo, adhabu ya makosa sio tu ni faini na, au kifungo jela; bali kutaifishwa; na au kufilisiwa kwa mali iliyopatikana kwa njia ya rushwa."Tarehe 28 Novemba 2006, akiwa nchini Canada, Karamagi aliwasiliana na mwenyekiti wa bodi ya TANESCO, Balozi Fulgence Kazaura akimfahamisha Richmond imehamishia mkataba wake kwa kampuni nyingine na kumtaka kuangalia uhalali wa hatua hiyo chini ya makubaliano kati ya TANESCO na Richmond.

Naye Balozi Kazaula akitekeleza maagizo ya Karamagi, alimwandikia Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Adriaan van Der Melwe wakati huo, akitaka kufanya kazi aliyotumwa na Karamagi. Adriaan van Der Melwe, akitekeleza maagizo ya Balozi Kazaula, alimwandikia katibu wa shirika, Subira Wandiba ili aeleza kama taratibu zimekiukwa au hapana.
Siku hiyohiyo Wandiba alijibu barua ya mkurugenzi wake kwa kusema, "…kufuatana na mkataba wa 23 Juni 2006, Richmond hairuhusiwi kuhamisha mkataba wao kwenda kampuni nyingine yeyote."

Kuhusu hilo, Lissu anasema, "Hawa watatu wa kwanza walikuwa wanashikilia nafasi za uongozi wa kuchaguliwa na wananchi kama ubunge na uwaziri. Kamishna Mrindoko anashikilia nafasi ya kuteuliwa.
"Kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995, wahusika wote hawa walikuwa ni ‘viongozi wa umma' kwa tafsiri ya kisheria ya maneno hayo. Hivyo ilitosha kujenga hoja mahakamani kuwa hapa kuna rushwa," ameeleza.

Akiongea kwa kujiamini Lissu alisema, "Hatua ya Lowassa kuipa kazi Richmond wakati akijua kwamba haikuwa na sifa, ni rushwa. Hata kuandaa mazingira ili mtu mwingine aweze kulipwa kupitia mgongo wa Dowans, ni rushwa."
Anasema, "Haiwezekani waziri mkuu na waziri wa nishati wavunje taratibu na sheria zilizowekwa na serikali yenyewe, ikiwamo sheria ya manunuzi ya umma, halafu useme hapa hakuna rushwa. Inawezekana mawakili waliogopa kusimamia hoja hii, kwa sababu mwisho wa siku wangewataja akina Lowassa, Karamagi na Msabaha."

Wakati hayo yakiachwa tangu mwanzo wa shauri, mawasiliano yaliyonaswa na gazeti hili kati ya mawakili wa Dowans, Kennedy Fungamtama na John M. Miles, ambayo yamenakiriwa kwa wakili mwenzao Elizabeth Karanja, wamiliki wa Dowans wamepatwa na kiwewe wakihofia kutopata tuzo ya Sh. 94 bilioni waliyopewa na ICC.

Katika mawasiliano hayo, wakili Fungamtama anasema, "Nionavyo, TANESCO wanaweza kupinga hukumu hii kwa kutumia vipengele vya sheria ya usuluhishi ya Tanzania ambavyo vinazungumzia maslahi ya umma na mambo yaliyo kinyume cha sheria."

Mawasiliano hayo ya 9 Desemba 2010, saa 3:47 asubuhi, yamechukuliwa na wachunguzi wa mambo ya sheria kueleza kile walichoita "mawakili wa Dowans kupata kiwewe." Fungamtama ambaye pia ni wakili wa Rostam Aziz, alikuwa akijibu baruapepe ya Miles ya tarehe 7 Desemba 2010 saa 8:41 usiku. Miles alitaka ufafanuzi kutoka kwa Fungamtama iwapo kuna uwezekano wa sheria za Tanzania kuzuia malipo kwa Dowans.

Ijumaa ya 17 Desemba 2010, saa 2:58 asubuhi, mmoja wa wanaotajwa kuwa wamiliki wa Dowans, Guy Picard, kutoka Canada, alipeleka baruapepe kwa wahusika wa Dowans katika kesi hiyo, akitaka kujua iwapo ni kweli Mahakama Kuu ya Tanzania imefungwa hadi Februari kama anavyosikia.

Baruapepe hiyo iliandikwa kwa Elizabeth W. Karanja, Stanley Munai, Henry Surtees na mkurugenzi mtendaji wa Dowans ambaye hakutajwa jina (md@dowans.com). Picard pia alituma nakala kwa Miles, Amish Shah na Fungamtama.
Siku hiyohiyo usiku wa manane, Miles alimjibu Picard kwa kukiri kwamba ni kweli Mahakama Kuu itafungwa na hilo litachelewesha tuzo yao kusajiliwa lakini hilo litawaruhusu waende London, kuisajili.

Mawasiliano mengine kati ya Fungamtama, Amish Shah, Elizabeth W. Karanja, Stanley Munai, Henry Surtees yalifanyika 21 Januari 2011, saa 2:09 asubuhi na tarehe 23, 24, 27 na 9 Februari 2011. Katika moja ya mawasiliano hayo, Fungamtama anasema, "…niko imara kupambana na wanasheria wa TANESCO katika hoja yoyote watakayoileta kupinga hukumu hii.

chanzo Mwanahalisi
 
Back
Top Bottom