Mahabusu wafunga barabara kwa saa moja

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
266
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, zaidi ya mahabusu 30 wa gereza la wilaya mjini hapa, wamegoma kwenda mahakamani na badala yake kulala barabarani kwa zaidi ya saa moja, hali iliyosababisha msongamano wa magari yanayofanya safari za ndani na nje ya Tarime.

Tukio hilo lililowatoa jasho askari Polisi kwa muda, lilitokea jana saa nne asubuhi nje ya gereza hilo, baada ya kutolewa ndani ili kupelekwa mahakamani.

Wakati wakitoka gerezani, umbali usiozidi meta 100, lakini unaowalazimu mahabusu kuvuka barabara, walishikana na kutembea wawili wawili chini ya ulinzi wa polisi kutokana na kutofungwa pingu.

Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Ernest Kimora ambaye ndiye Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa, alisema: "Jeshi la Polisi tumefanikiwa kuzima mgomo huo uliodumu kwa muda nje ya gereza hilo na tumewapeleka mahabusu wote waliokuwa wanatakiwa kufika mahakamani leo (jana).”

Mgomo huo ulianza taratibu juzi, kwa watuhumiwa wa kesi mbalimbali zikiwamo za wizi wa kutumia silaha, mauaji na wa mifugo wanadai kuwa, wamesoteshwa rumande kwa muda mrefu, huku upelelezi wa kesi zao ukifanywa kwa mwendo wa kusuasua.

Kaimu Kamanda aliongeza kuwa, "viongozi wa migomo yote hiyo mitatu tutawafikisha mahakamani wakati wowote kuanzia sasa kujibu mashitaka ya kufanya vurugu na kutaka kutoroka wakiwa chini ya ulinzi, na baadhi yao kesi zao zimeanza kusikilizwa umebakia utetezi hali inayoonesha huenda walitenda makosa yanayowakabili."

Aliwataja baadhi ya mahabusu wanaotuhumiwa kuwa viongozi wa migomo hiyo ambao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kuwa ni Mageta Taminyo, Chacha Charwi, Werema Wambura, Seleman Matiko, Marwa Mhindi, Nindwa Machumu, Muhagachi James, Geofrey Anguti na Maiteka John.

Mwandishi wa habari hizi alifika eneo la tukio na kushuhudia msongamano wa magari, huku kukiwa na umati wa wananchi wengine ndugu za mahabusu hao waliofika kusikiliza kesi, na baada ya polisi kutumia mbinu ya kuwaondoa barabarani hapo, waliwapeleka katika mahakama ya wilaya lakini Hakimu wa Wilaya, Yusto Ruborogo hakuwapo kutokana na kuwa likizo hadi Januari 10.

Kutokana na mazingira hayo ilimlazimu Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo, Azizi Mzee aahirishe kesi hizo, huku ulinzi ukiimarishwa nje ya jengo, kwani lango la kuingia mahakamani hapo pia lilifungwa na kulindwa na polisi wenye silaha na kuzuia wananchi waliotaka kuwaona ndugu zao hao.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom