Mafisadi papa: Si ubaguzi ni masilahi ya taifa

Magezi

JF-Expert Member
Oct 26, 2008
3,359
692
Mafisadi papa: Si ubaguzi ni masilahi ya taifa
Padri Privatus Karugendo
Raia Mwema – Muungwana ni Vitendo Mei 6, 2009

SIKUSUDII katika makala hii kumtetea Reginald Mengi, na wala siandiki kumlaumu na kumlaani.

Kama ningeamua kuandika kumtetea ningefanya hivyo kwa uhuru na si kwa kushawishiwa na msimamo wake; pia kama ningeamua kuandika kumlaumu na kumlaani ningefanya hivyo kwa uhuru wangu bila shinikizo wala kupokea bahasha.

Wiki hii nilikutana na mtu (jina nalitunza) aliyenishawishi nichukue upande katika swala hili ili niupige kisogo umasikini; hanifahamu vizuri – fedha za kununua uhuru wangu hakuna tajiri wa kuzipata!

Hakuna utajiri mkubwa kama wa mtu kuwa huru. Hivyo ninaandika makala hii kutetea masilahi ya Taifa. Naandika kuwakumbusha Watanzania wenzangu ule msemo wa "Wajinga ndio waliwao".

Ingawa sifahamu kwa hakika malengo na nia ya Mengi kutangaza mafisadi papa, ninaelewa vizuri hasira aliyo nayo. Hasira hii iko mioyoni mwa Watanzania wengi.

Bahati nzuri au mbaya Mengi, ana vyombo vya habari; anaweza kuvitumia vizuri au vibaya. Lakini kuna Watanzania wasiokuwa na jukwaa la kutoa hasira zao; siku wakisema imetosha, patakuwa padogo!

Hata hivyo, alichokifanya Mengi hakikuwa kipya. Labda ni kwa vile Watanzania tuna ugonjwa wa kusahau au tunaendeleza ule ugonjwa wa "Wajinga ndio waliwao". Majina matano aliyoyatangaza yamekuwa kwenye vyombo vya habari kwa muda mrefu; yametajwa kwenye Richmond, EPA, Ununuzi wa Ndege ya Rais na mengine mengi ya kuhujumu na kupora rasilimali za Taifa.

Alichokifanya Mengi ni kuchambua kwenye vyombo vya habari na kutangaza. Kama kuna mtu anayetaka kumshitaki, asianzie kwake – aende mbali kwanza kuvifikisha mbele ya sheria vyombo vyote vya habari vilivyotangaza majina hayo.

Sipendi kumtetea Mengi, lakini ninashawishika kuamini kwamba nia na lengo lake ni jema. Binafsi simfahamu kwa karibu. Jitihada zangu za kutaka kumfahamu kwa karibu ziligonga Mwamba. Mwaka 2002, nilipojitokeza kuunga mkono matumizi ya kondomu kwenye Mkutano wa Ukimwi kitaifa kule Arusha; nilishawishika kumtafuta Mengi, ili tuungane na kuwa na sauti mmoja, yeye pia wakati huo alikuwa akigombana na maaskofu kuhusu swala la kondomu.

Nilifunga safari kutoka Karagwe kwenda Dar es Salaam. Ile picha niliyokuwa nikiona kwenye vyombo vya habari kwamba yeye ni mtu wa watu ilinifanya niamini kwamba isingekuwa vigumu kukutana naye.

Ofisini kwake, wasaidizi walinishauri niandike barua ya kujieleza na kuomba kukutana naye. Niliandika barua na kuwapatia wasaidizi wake. Nilishauriwa nirudi Karagwe, ili Yeye, Mengi, akipata nafasi aniite. Mwaka mzima wa 2003 ulikatika.

Mwaka 2004 nilikwenda ofisini kwake tena, wasaidizi wakaniambia barua yangu ilifika, nisubiri kuitwa. Mwaka mzima wa 2004 nao ulikatika. Nilifunga tena safari mwaka 2005 kutoka Karagwe, hadi ofisini kwa Mzee Mengi,lakini sikufanikiwa kuonana naye. Nilikikata tamaa; hivyo hadi leo hii sijafanikiwa kukutana naye. Hivyo simfahamu kwa karibu!

Nakumbuka siku ya mwisho nilipokata tamaa nilikutana na mlemavu aliyeniambia siku hiyo kwake ilikuwa ni mara ya 99 akijaribu kukutana na Mengi, bila ya mafanikio! Wasaidizi wa Mengi, kama nilivyojaribu kuwasoma, wanafikiri kila mtu anayekwenda pale, anataka msaada; hivyo wanamkwepesha bosi wao asikutane na waomba misaada. Nafikiri hata mimi niliwekwa kwenye kapu la kuomba msaada!

Sikutaka kabisa kujiingiza kwenye swala hili la mafisadi papa na sasa fisadi nyangumi. Taifa limekumbwa na siasa za makundi. Jambo likitokea, linaangaliwa kimakundi. Ninajua hata sasa hivi kuna wanaofuatilia kwa makini kuona ni nani anaandika nini, ni nani anamuunga mkono Mengi, au ni nani anampinga.

Hata vyombo vya habari vimegawanyika kimakundi. Ukisoma magazeti unaweza kuona wazi ni gazeti gani liko upande upi. Maadili na utaalam wa uandishi wa habari umewekwa kando; hata waandishi wanaoaminika wameanza kuyaangalia matumbo yao na familia zao, na kusahau kabisa kazi ya kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha.

Nimeamua kuandika baada ya kuona baadhi ya Watanzania (hata na wale ninaowaheshimu) wanataka kupotosha swala zima la mafisadi papa. Wanataka kuingiza ubaguzi. Wanafikiri kuwataja wahindi ni kuwabagua. Hili si kweli! Na kama nilivyosema hapo juu ni kwamba hasira ya Mengi, ni ya Watanzania wengi; ikitokea wakasema inatosha – ni kweli hapatatosha! Si kweli kwamba hoja ya ubaguzi ikitumika basi watetezi wa haki za binadamu watafunga midomo juu ya swala hili la mafisadi papa. Wamepotea njia!tutasema!

Maoni yangu binafsi ni kwamba mtu anayehujumu uchumi, mtu anayepora rasilimali za Taifa, awe mweusi, awe mzungu, mhindi, mwekundu, mweupe, kijani au rangi yoyote ile ni adui wa umma! Ni lazima umma umchukie, ni lazima umma umtenge na ikibidi upambane naye! Tusitumie hoja ya rangi kuendeleza mshikamano wa kihalifu.

Kwa upande mwingine mimi siwalaumu hawa wahindi; ni wajanja, wanajua jinsi ya kuishi kiujanja ujanja ili kuendeleza kizazi chao na kulinda mshikamano wao. Ni wajanja sana katika biashara; wanakuhitaji na kukupenda wakijua una faida kwao; wakisha kukutumia wanasahau sura yako na jina lako.

Wameishi zaidi ya miaka 100 hapa lakini hadi leo ni jamii iliyoshikamana, hawakujichanganya na weusi kama walivyofanya waarabu na baadhi ya wazungu. Wametunza lugha yao, wametunza mila zao, wametunza dini yao na wala hawakutaka kuieneza miongoni mwetu kama walivyofanya wazungu na waarabu; wanatawanya ndugu na jamaa kwenye nchi mbali mbali duniani, ili kesho na keshokutwa yakitokea matatizo eneo moja wapate pa kukimbilia.

Hata wale tulioamini ni Watanzania wazalendo, waliolitumikia Taifa hili kwa uaminifu mkubwa wamezikwa nje ya nchi. Hivyo hawa watu wanaishi kwa malengo na kwa mshikamano.

Tujilaumu sisi wenyewe; tumebaki kuwa wajinga ndio waliwao. Tumeshindwa kuwa wapole kama njiwa na wajanja kama nyoka. Kwa vile wahindi ni wajanja, tulipaswa kuwa wajanja vilevile. Tunawaruhusu kufanya biashara, lakini tuwabane kwenye ushuru na masharti mengine ya kuchangia shughuli za maendeleo. Sisi tuna wasomi wengi katika serikali yetu; kusema kweli walio wengi wamesoma sana kuwazidi hawa wahindi wanaoliyumbisha taifa.
Inakuwa vipi, wasomi wetu wanayumbishwa na wajanja, inakuwa vipi wasomi wetu ambao ndio wenye mali, wanawapigia magoti wageni? Inakuwa vipi tenda zote wanazipata wahindi? Inakuwa vipi wahindi ndio wanasamehewa kodi? Inakuwa vipi wahindi ndio wanaendesha uchumi wa taifa? Inakuwa vipi tunasimama na kuwatetea? Kwa vile wanatoa misaada mikubwa kwenye vyama vyetu vya siasa? Kwa vile wanatoa misaada kwenye timu za mpira? Hizo fedha wanazitoa wapi? Huo utajiri wameutoa wapi kama si hapa hapa kwetu? Si kwamba wanatoa msaada, bali wanarudisha walichokipora!

Wanaoendesha magari mazuri na ya kisasa ni wahindi, wanaoendesha biashara kubwa ni wahindi, wanaougua na kwenda kutibiwa nje ya nchi ni wahindi, wanaosafiri kwa wingi nje ya nchi ni wahindi. Ukienda uwanja wa ndege wa Dar es Salaam, unashangaa jinsi ndugu zetu wanavyotoka na kuingia. Watanzania weusi wanaozea Ubungo, Tabata na Kigogo.
Kama wanafanya biashara halali, hakuna neno, maana sisi tumesinzia. Ila kama wanahujumu, kama wako kwenye ufisadi wa EPA,RICHMOND na kashifa nyingine zilizoibuka katika uongozi wa awamu ya nne, ni lazima tusimame na kusema. Na hili lisitafsiriwe kama ubaguzi; ni kutetea masilahi ya Taifa.

Kama ni ubaguzi kwanini asibaguliwe Profesa Issa Shivji? Au kwanini wasibaguliwe makamaradi wengine wa kihindi tunaowafahamu vizuri katika taifa letu? Mbona kuna wazungu Watanzania na wazalendo, hawabaguliwi? Suala si rangi, suala ni uzalendo; suala ni unalifanyia nini taifa la Tanzania. Tusitumie hoja ya rangi kuvuruga jitihada za kupambana na ufisadi.
Tunaweza kuiga mifano ya nchi nyingine. Nigeria, hawakugombana na wahindi wala hawakuwafukuza kama alivyofanya Idi Amin wa Uganda. Wao walikuwa wapole kama njiwa na wajanja kama nyoka. Walifanya uamuzi wa kuyasusia maduka na biashara zote za wahindi; kwa vile wahindi wana mtandao mkali katika nchi mbali mbali na kwa vile hawakuwa Nigeria kama wazalendo waliamua kutimuka kutoka Nigeria, na kuhamia nchi nyingine.
Tunaweza kufanya hivyo kwa wale wanaoendesha biashara na kukwepa kodi, lakini kwa mapapa, ni lazima wabanwe, warudishe fedha na rasilimali walizoficha nje ya nchi. Ni lazima wabanwe ili wawataje wale wanaoshirikiana nao ndani ya serikali.
Hatuwezi kuendelea kuimba wimbo wa ufisadi wakati tunawalea mafisadi; hatuwezi kupambana na ufisadi wakati tunawatetea mafisadi na kuwakingia kifua.

Wale wanaompinga Mengi na kuwatetea mapapa, ninawaomba wasimame na kuwaelezea Watanzania undani wa familia za hawa ndugu zetu wahindi: Je, familia zao ziko wapi? Wajomba, shangazi, watoto na ndugu zao wengine wako wapi? Mtu anayefanya biashara hapa wakati familia yake iko Marekani hawezi kufanya biashara kwa moyo wa kizalendo. Mtu anayefanya biashara hapa wakati watoto wake wanaishi India, hawezi kufanya biashara kwa moyo wa kizalendo.

Rafiki yangu msukuma, anayefanya biashara ya samaki, alinielezea alivyoshangaa alipokwenda India kumtembelea rafiki yake aliye na kiwanda cha kusindika samaki pale Mwanza. Anasema, mhindi huyu akiwa Mwanza, anajifanya ana maisha ya chini na kuishi kwenye nyumba ya msajili; lakini kule India amejenga jumba la kifahari na ndugu zake kule India wanaishi kwenye ufahari wa hali ya juu.

Rafiki yangu mwingine Mhindi wa Bukoba, tulishibana kweli kweli, maana nilikuwa nikimuuzia dola, wakati huo tunaziuza kama bangi; nilikuwa nikikaribishwa hadi nyumbani na kula chakula; nilifahamiana na ndugu zake wote na kila wakati alinielezea mipango yake yote.
Nilipoishiwa zile dola na maisha yakabadilika, alisahau sura yangu na jina langu! Hata nikikutana naye leo hii, kwa vile sina zile dola tena na sina faida yoyote kwake, mimi ni mtu ambaye sikuwahi kuishi!
Siandiki haya kupandikiza chuki, na wala mimi si mbaguzi! Lengo langu ni kutaka kuwaamsha Watanzania wenzangu kutoka kwenye ndoto za "wajinga ndio waliwao".

Ni lazima tuwe wapole kama njiwa na wajanja kama nyoka. Ni lazima na sisi tuishi kwa malengo, ni lazima na sisi tuishi kwa mshikamano; si mshikamano wa kihalifu bali mshikamano wa kujenga Taifa letu.
Nampongeza Mengi kwa ujasiri wa kusema; na nawapongeza wengine wote wanaopambana na ufisadi kwa malengo ya kizalendo; wale wanaopambana na ufisadi bila kulenga kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu wa 2010, wale wanaopambana na ufisadi bila kulenga kuwania urais wa 2010; wale wanaopambana na ufisadi bila kuwa na nia na lengo la kuwania tenda ama kuvuruga biashara ya watu wengine.
Nawaunga mkono wale wote wanaopambana na ufisadi kwa moyo wa kizalendo. Tanzania ni yetu sote na ni lazima tuilinde kwa gharama yoyote ile!
 
Unapandikiza chuki tu ,huna zaidi ya hilo ,hivi huwajui wanaomiliki mabasi huko mikoani ,hivi huwajui wanaojivunia maliasili ya nchi hii,hivi huwajui wanaoimaliza nchi hii ,wewe muandishi wa habari hiyo hapo juu ukiwa mmoja wa, kwani dola ulitakiwa uzibadilishe kwenye benki yako na badala yake ikawa unazipeleka kwa Mhindi sasa nani ni fisadi hapo wewe au huyo mhindi ?
 
Back
Top Bottom