Madiwani Wengi Wao toka CCM wainunia Serikali; Watishia kutowapa ushirikiano wabunge, Rais 2015

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
*Watishia kutowapa ushirikiano wabunge, Rais 2015
*Wachukia kufananishwa na wenyeviti wa harusi
*Wamtuhumu Waziri Mkuu kukwepa kukutana nao

Na Mwandishi Wetu


MADIWANI nchini wamelalamikia kitendo cha Serikali kutowawezesha kutekeleza majukumu yao, tofauti na inavyofanya kwa wabunge.


Kilio hicho cha madiwani (wengi kutoka Chama Cha Mapinduzi) kimekuja wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka Umoja wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) uliomalizika Jumatatu wiki kwenye hoteli ya Kunduchi Beach jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo pamoja na mambo mengi, madiwani hao walijadili masuala mbalimbali ikiwamo ugumu wanaokabiliana nao katika shughuli za kuhamasisha na kusimamia maendeleo katika ngazi ya kata.


Akizungumza katika mahojiano maalumu, Katibu wa madiwani wa CCM kutoka moja ya mikoa nchini (jina linahifadhiwa) kwa niaba ya wenzake alisema; "Wakati wa kampeni za urais mwaka 2005, aliyekuwa mgombea wa CCM na baadaye kuukwaa urais, Jakaya Kikwete alitumia sana msemo wa mafiga matatu.


"Msemo huo ulikuwa na maana kuwaomba kura Watanzania wachague Rais kutoka CCM, Mbunge CCM na Diwani CCM, ili kutengeneza mafiga matatu ambayo juu yake kitakaa chungu cha maendeleo.


"Mafiga matatu wakati huo yalipatikana mengi tu katika maeneo mbali mbali nchini, ila suala kama baada ya hapo kiu ya maendeleo ya wananchi ilipata tiba au la tutalijadili siku nyingine.

"Rais kama kiongozi mkuu wa nchi ana majukumu yake ambayo zaidi ni kutoa maelekezo kwa watendaji, kufuatilia utekelezaji na kisha kupima mafanikio.


"Wabunge ni wawakilishi wa wananchi kutoka majimboni, na kwa kiasi kikubwa kazi yao ni kuhakikisha ahadi walizotoa wao wenye na zile zilitolewa kwenye Ilani ya uchaguzi zinatimizwa kwa ukamilifu wake.


"Kwa lugha rahisi, Rais na wabunge ni viongozi wa juu ambao si rahisi kushughulikia matatizo ya wananchi mmoja mmoja, au matatizo ya mtaa kwa mtaa, ingawaje wakati mwingine Mbunge anaweza kujikuta akilazimika kufanya hivyo.


"Lakini katika kuwatumikia wananchi, figa la tatu ambalo ni Diwani lina umuhimu mkubwa sana katika mustakabali wa maendeleo ya Watanzania kama kweli kuna nia ya dhati ya kuleta maendeleo.


"Kwa lugha rahisi, madiwani wetu ni watu wenye kazi nyingi mno kuzidi hata Rais na Mbunge katika suala la kuwahudumia na kutatua kero za wananchi.


"Lakini kitu cha ajabu na cha kushangaza madiwani hao hao ambao wanategemewa kwa kiasi kikubwa kusukuma mbele gurudumu la maendeleo, ni watu ambao Serikali imewasahau kabisa katika suala la uwezeshaji.


"Hawa ndio watu ambao wameshikilia (grassroots level) ya utawala, ndio watu ambao wanashughulikia kero ndogo ndogo ambazo mara nyingi ndizo huzaa uhasama katika ya wananchi Serikali.


"Pia tukumbuke hawa madiwani wapo ambao kata zao zipo kwenye miji mikubwa, miji midogo na wengine katika maeneo ya vijijini ambako hakuna miundombinu ya barabara huku maeneo yao ya kazi yakiwa makubwa mno.


"Miongoni mwa majukumu yao ni pamoja na kusimamia miradi ya maendeleo kama ujenzi wa barabara ndogondogo, utunzaji wa mazingira kwenye maeneo yao, kuhakikisha sheria ndogo zinafuatwa pamoja na mambo mengine mengi tu ambayo yanahusiana na maisha ya kila siku ya Mtanzania wa kawaida.


"Pia madiwani ndio wanapaswa kusimamia na kuendesha vikao vya kamati mbalimbali za maendeleo kwenye kata zao, vikao ambavyo havina posho yoyote wala hakuna fungu la kuviendesha, na kumlazimisha Diwani mara kwa mara atumie fedha zake ambazo hazirejeshwi.

"Hili halina ubishi, karibu kila Diwani unayekutana naye analalamika kutokana na kuzidiwa na majukumu bila kuwapo msaada wowote kutoka serikalini, lakini mwisho wa siku mambo yakionekana hayaendi, ni yeye huyo huyo anajikuta akiwa kikaangoni.

"Lakini inaelekea umuhimu wa madiwani bado hautambuliki, au kama unatambulika basi kuna wakubwa ambao hawalitakii mema Taifa letu na kwa makusudi wameamua kuwatosa viongozi hawa muhimu sana.


"Katika hali kama hiyo yenye mzigo wa majukumu, cha kushangaza katika Tanzania ya leo Diwani mwenye kuongoza kata nzima analipwa posho ya Sh 120,000 kwa mwezi, na hulipwa Sh 70,000 kila baada ya miezi mitatu kunapofanyika mkutano wa Baraza la Madiwani.


"Hata kodi nyingi zinazokusanywa na halmashauri zote nchini kwa kiasi kikubwa zinapatikana kutokana na utendaji na usimamizi wa madiwani, lakini wao huambulia patupu.


"Kuna falsafa moja ambayo imepitwa na wakati na haina mantiki kudai kuwa udiwani ni kazi ya kujitolea, lakini basi hata kama wanajitolea basi si wawezeshwe kutekeleza majukumu yao.


"Hata kazi za viongozi wa dini na mashirika mengine yanayotoa huduma za jamii ni za kujitolea, lakini kabla ya kutimiza majukumu yao huwa wanawezeshwa tena vizuri sana, sasa kwa nini kwa madiwani inakuwa kinyume wakati halmashauri zina pesa nyingi.


"Haitakuwa vibaya kusema kuwa, hata baadhi ya kashfa za uuzaji wa viwanja zinazowakumba madiwani mara kwa mara ni kutokana na kujikuta wakiwa na ukata huku majukumu yakiongezeka na hatimaye kushawishika kuuza maeneo.


"Kwa sababu kama Diwani anakuwa ametumikia wananchi wake kwa miaka mitano, hivi tujiulize atakuwa ametumia fedha kiasi kutoka mfukoni mwake, je fedha hizi atazirejeshaje?


"Matokeo yake ni madiwani wetu sasa kugeuka ombaomba, jambo ambalo linawafanya wanakuwa watumwa mbele ya watu wenye fedha na kujikuta wakiwapa upendeleo mwingi na kuzua malalamiko kutoka kwa wapiga kura.


"Serikali inapaswa kutambua kamwe haiwezi kufikia ndoto yake ya kuwaletea maendeleo Watanzania kama itaendelea kuwaacha watu muhimu kama madiwani wakiwa na njaa, tena njaa kali.


Diwani mwingine kutoka mkoani Mara alisema kutokana na kupuuzwa na Serikali, imefikia hatua baadhi ya wapiga kura kuwafananisha na wenyeviti wa kamati za harusi, ambapo umuhimu wao hukoma baada ya sherehe kumalizika, akifananisha uchaguzi na harusi.


"Sisi bwana unapokaribia uchaguzi ndipo umuhimu wetu unaonekana, uchaguzi ukiisha hakuna mtu ambaye anatukumbuka, kama hakutakuwa na mabadiliko, uchaguzi wa 2015 itabidi kila mtu apigane kivyake, Rais atafute kura zake, mbunge zake na diwani za kwake, kisha tuone hali itakuwaje," alisema kwa hisia kali.


Pia walieleza kusikitishwa na kitendo cha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kushindwa kufika kwenye ufunguzi ambapo alitarajiwa kuwa mgeni rasmi, na badala yake akamtuma Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), George Mkuchika.


Walisema Waziri Mkuu alipaswa kuja yeye mwenyewe na kusikia kilio chao, pamoja na kupata fursa ya kumuuliza maswali kadha wa kadha zikiwamo ahadi nyingi za kuboresha maslahi yao ambazo amewahi kuwaahidi, lakini hadi sasa hazijatekelezwa.
 
Back
Top Bottom