Madereva wa daladala waibuka na mapya

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
Na Athman Hamza, jijini.

WAKATI fukuto la tishio la mgomo wa daladala jijini Dar es salaam likiwa bado halijapoa, Chama cha Madereva na Makondakta wa Daladala jijini (UWAMADAR) kimewageukia wamiliki wa daladala na kuwakumbusha ahadi yao ya kupewa mkataba kama Serikali ilivyoagiza.

Wamesema mpaka sasa zoezi la mkataba kwa watoa huduma hao wa daladala halijapatiwa ufumbuzi kwani licha ya kupewa madereva peke yao bado unapwaya na haulengi kumuokoa dereva katika maisha yake.

Akiongea na gazeti hili kwa njia ya simu, Katibu wa UWAMADAR , Shukuru Mlawa, amesema tatizo hilo limekuwa likilalamikiwa kwa muda mrefu sasa hali ambayo inaonyesha halitotatuliwa mpaka watangaze mgomo.

Mlawa amesema kwa sasa mikataba inatolewa kwa madereva peke yao na kutowahusisha makondakta wa daladala hali ambayo inaonyesha hakujawa na mkakati madhubuti ya kuboresha hali ya usafiri jijini.

“Unajua makondakta ni muhimu sana katika kuboresha huduma ya usafiri jijini sasa unaposhindwa kuwatambua na kuwapa mkataba unamaanisha wao hawana umuhimu na hawatambuliki hali ambayo inapelekea kushindwa kuwabana makondakta pindi wanapofanya makosa,” alisema Mlawa.

Mlawa ameongeza kuwa baada ya makubaliano na Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu, wamekubaliana kuwa kuanzia sasa kila mtu (dereva, makondakta au ubovu wa gari) watabeba mizigo yao wenyewe na hivyo kuonyesha kuwa kwa sasa mikataba inahitajiwa zaidi kuliko wakati wowote kwani mara baada ya gari kuonekana na makosa au derava na kondakta kufanya kosa wanaweza kufukuzwa kazi bila kuangalia haki zao.

“Kanuni zilizopo sasa hivi zinaonesha mikataba ni kati ya derava na mmiliki, sasa tunajiuliza makondakta watakapokosea watabanwa vipi? Amehoji Mlawa na kuongeza kuwa mikataba inayotolewa sasa hailengi kuwakomboa madereva kwani hutolewa pindi mmiliki anapotaka leseni ya usafirishaji na baada ya hapo inawekwa katika makabati.

Akiongelea kuhusu mgomo uliopangwa kufanyika leo, na kusitishwa baada ya waziri wa uchukuzi kuingilia kati, Mlawa amesema mgomo huo ulikuwa hauhusiani na ombi lao la kupandishwa nauli na kusema majadiliano bado yanaendelea kati yao na Serikali na kusema wakati muafaka ukifika wataliongelea suala hilo.
 
Back
Top Bottom