Madaktari waelezea machungu

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125
headline_bullet.jpg
Wagonjwa waelezea masikitiko yao
headline_bullet.jpg
Wataka Watanzania wasiwahukumu



Muhimbili%2815%29.jpg

Hospitali ya Taifa Muhimbili


Madaktari waliorejea kazini baada ya mgomo uliotikisa takriban wiki tatu wameelezea machungu kwamba kipindi kile cha mgomo kiliwaweka katika wakati mgumu kisaikolojia, hasa waliposhuhudia wagonjwa wakipoteza maisha.
Hata hivyo, wakasema ilibidi wawe nje ya wigo wa kutoa huduma ikiwa ni uwajibikaji wa pamoja uliolenga kuwasilisha madai yao ambayo serikali iliyafumbia macho kwa muda mrefu.
“Tulikuwa na wakati mgumu, tuligundua nafasi yetu katika kuokoa maisha ya ndugu zetu, lakini hatukuwa na jinsi kwa maana tulihitaji serikali itutendee haki,” anasema mmoja wa madaktari hao.
Hata hivyo madaktari hao, hawakutaka kutajwa majina yao gazetini kwa kile kilichobainika kuwa ni makubaliano yaliyofikiwa baada ya kuhitimisha mgomo huo.
Wakizungumza na NIPASHE Jumapili kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya madaktari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na ile ya manispaa ya Ilala walisema ulikuwa wakati mgumu kwao kuwaona wagonjwa wakipata taabu kwa kukosa huduma za matibabu hospitalini.
“Wakati wa mgomo tulikuwa na wakati mgumu sana tunaposikia na kuwaona wagonjwa kupitia luninga jinsi wanavyopata mateso kwa kukosa huduma…Watanzania wasituhukumu kwa yaliyotokea kwani serikali ndiyo ibebeshwe lawama,”alisema Daktari mmoja wa MNH aliyekutwa katika wodi ya Kibasila.
Daktari mwingine wa hospitali ya Amana iliyopo Ilala, alisema suala la huduma za afya ni nyeti hivyo serikali inapoona wafanyakazi wake wanagoma, isitumie mabavu kuzima mgomo na badala yake itafute namna bora ya kufikia muafaka.
Kwa upande wao, wagonjwa waliokuwa wamelazwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili na ile ya manispaa ya Ilala, walisema mgomo huo uliwaweka katika mazingira magumu mbali kutokana na kuhitaji huduma za haraka wakati madaktari hawapo.
Walisema wakati wa mgomo kila kitu kilikuwa hovyo, mazingira ya ndani na nje ya wodi yalikuwa machafu na hakuwepo wa kuwabadilishia shuka.
“Kwa waliokuwa na ndugu wa karibu walifanikiwa kuletewa lakini wapo waliotoka nje ya Dar es Salaam walilazimika kuvumilia,” alisema mmoja wa wagonjwa hao.
Yusuna Said ambaye alikutwa akimhudumia mgonjwa Amina Ramadhani, aliyelazwa wodi ya Mwaisela, alisema wakati wa mgomo wauguzi na madaktari walikuwa hawataki kuulizwa kitu chochote wala kugawa vifaa kama shuka.
“Kipindi cha mgomo ukimfuata muuguzi na kutaka shuka kwa ajili ya mgonjwa wako walikuwa wanakataa na kutoa lugha chafu, kwa hiyo tukawa tunalazimika kuwafunika shuka za majumbani,” alisema Said.
Mgonjwa mwingine, Tekra Mnyeti mkazi wa Ubungo aliyelazwa katika wodi namba tano ya Mwaisela, alisema baada ya siku mbili za mgomo kuanza, alichukuliwa na ndugu zake kupelekwa nyumbani alikokuwa akiendelea na matibabu kama kawaida.
Naye Jelard Mbuso wakati wa mgomo alilazimika kutumia fedha zake kununulia dawa za kujitibu ingawa alikuwa hajaandikiwa na daktari ili kutuliza maumivu kutokana na ugonjwa unaomsumbua.
Mbuso alisema kutokana na kero walizopata wagonjwa ikiwemo kuingia gharama kununua dawa katika hospitali za watu binafsi, serikali ifanye utaratibu wa kuwarejesha wagonjwa fedha walizotumia kwa kununua dawa kwa bei ghali katika hospitali na maduka ya watu binafsi.
John Pandura alisema nyakati za usiku wagonjwa ambao hali zao zilikuwa mbaya walikuwa wakiangua vilio kutokana na maumivu makali na wale wenye nafuu walilazimika kuwapatia dawa za kutuliza maumivu.
WANAHARAKATI WAKOMALIA WAZIRI, NAIBU KUNG’OKA
Wakati huo huo, wanaharakati nchini wamezidi kuweka shinikizo la kujiuzulu kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda na Naibu wake Dk. Lucy Nkya.
Wamesema hawategemei kuona mawaziri hao wanampa Rais Jakaya Kikwete majaribu kwa kukataa kujiuzulu.
Wakizungumza na NIPASHE Jumapili, wanaharakati hao kutoka Chama cha Waandishi Wanawake (Tamwa) na Kituo cha Haki za Binadamu (LHCR) walisema si vyema kwa mawaziri hao kufanya ujanja ili kuepuka kuchukua hatua hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Ananilea Nkya, alisema wanaharakati wataendelea kupigana hadi wahusika wa sakata la mgomo wa madaktari watakapowajibishwa.
"Tumesema mara kadhaa juu ya umuhimu wa uwajibikaji kwa viongozi, leo tunaona viongozi hawa wanavyosita kuchukua maamuzi ya kuwajibika, tunavyotaka Dk. Mponda na Naibu wake wajiuzulu nafasi zao haraka," alisema Nkya.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHCR), Helen Kijo-Bisimba alisema suala la kujiuzulu wa mawaziri hao halina mjadala, kwani itakuwa ni moja ya kuonyesha jinsi gani wanavyoonyesha hisia zao kwa wananchi.
Alisema mgomo wa madaktari umeonyesha ukweli wa madai yao, kwani katika kipindi walichogoma wananchi wamefahamu nini hasa madaktari hao wanachokitaka kwa serikali.



CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
 
Back
Top Bottom