Madaktari hubeba mizigo stahili?

Ozzie

JF-Expert Member
Oct 9, 2007
3,217
1,259
Ni kawaida kwa madaktari kulalamikiwa kila kuwapo na tatizo katika mfumo wa utoaji huduma za afya. Wakati mwingine daktari anaonwa kama malaika anayerejesha uhai. Muda mwingine akionwa kama mtu mbinafsi anayeua wagonjwa kwa makusudi au kutokukusudia ili kujaza pesa mifukoni mwake. Lakini je, madaktari wanapewa lawama stahili yao?

Bila shaka watu wanajua kwamba madaktari wa binadamu wamepata ujuvi wa tiba kwa kusoma, na si uganguzi. Tunajua maana tumesoma shule pamoja. Tulitumia madarasa yaleyale na vyuo vilevile ila mwingine wakachagua kumwita anafanya kazi ya wito na mwingine si wito japo karibu kila fani ina kiapo cha kufanya kazi kwa kufuata maadili yake.

Sote tunajua kuwa tiba ya kidaktari hutolewa kisayansi. Wagonjwa huponywa si kwa sababu wana uponyaji wa kimungu, au kufanyiwa maombi, lakini kwa sababu ya tiba zilizojaribiwa kisayansi na kugundulika zinafanya kazi. Bahati mbaya, mgonjwa akipata uponyaji huo daktari huishia kuonwa kama mtu mwenye nguvu za pekee za kimungu, japo huwa hawapewi sadaka.

Binafsi nimekuwa nakumbana na wagonjwa wengi ambao huishia kuniona mimi kama malaika. Kwa wagonjwa hawa ambao nimekuwa natumia dakika kumi na tano tu, kuwatoa maji kwenye moyo na yeye kuinuka akipumua vyema zaidi tofauti na dakika chache zilizopita. Jinsi wanavyokuangalia kwa hofu na heshima utaogopa. Lakini huhitaji kuwa Matunge; ni kiasi cha kujua moyo umejaa maji, niingize sindano katika nyuzi ngapi kuelekea upande wa mkao wa moyo na kisha natoa maji, na nikimaliza mgonjwa anainuka kwa furaha, moyo unaweza kujikunja na kutanuka vizuri tena. Kwa mgonjwa huo ni muujiza, ila haachi sadaka. Atasema Mungu akubariki, au ataishia kusema serikali inabidi iwakumbuke sana; hata kama yeye pia ni mtu muhimu mwenye kutoa maamuzi katika serikali.

Huduma ya utoaji afya, inafanana na huduma zozote zile za kijamii zisizohusiana na afya, lakini ajabu sana kwamba madaktari wanategemewa wafanye mambo makubwa sana hata ijapokuwa vitu vingine katika idara hii hii ya afya haviko sawa. Ili huduma ya afya itolewe sawia, lazima kuwepo na vitu vitatu; yaani daktari mwenye sifa, halafu kuwe na mwajiri (kwa Tanzania ni serikali kwa ukubwa) ambaye anahusika na majengo na kila kitendanishi kitakiwacho katika kituo cha afya na pia kuwe na mgonjwa (pamoja na ndugu wanaomzunguka) ambaye anahusika na kwenda hospitali katika muda muafaka na pia kufuata yale anayoambiwa na daktari kama timu ili aweze kupata tiba stahili. Hivi vitu vitatu lazima vifanye kazi sambamba ili mwisho wa siku jamii nzima iwe na afya bora na kuongeza uzalishaji wa taifa.

Utoaji huduma za afya ni biashara, ambapo wafanyakazi wanatakiwa walipwe vizuri, wagonjwa waridhike na jumuia zitoazo huduma husika pia zipate faida ya moja kwa moja kwa moja au zisizopimika kwa kuongeza kuzalisha kupitia kada nyingine. Katika utoaji huduma za afya kuna mapungufu mengi ambayo madaktari wamekuwa wakifanya kazi chini yake na ambayo yanasababisha iwe vigumu sana kupata matarajio yote mazuri yatokanayo na tiba za madaktari; lakini mwisho wa siku daktari atalaumiwa kwa ubaya wa mfumo wa afya.

Kuna vitu ambavyo daktari anapaswa kulaumiwa kwavo, mfano kuchelewa kufika kutoa huduma muda sahihi, na mengineyo. Lakini pia kuna vitu ambavyo vinachangiwa na watu wote watatu, kama vile mgonjwa kutopata tiba nzuri kutokana na uelewa mdogo wa daktari, daktari kuwa na msongo wa mawazo yatokanayo na ugumu wa pesa, kutokuwapo vifaa vya kutosha, mgonjwa kutosema ukweli au kutoweza mudu baadhi ya huduma, kutokuwa na vituo vizuri vya kutolea tiba n.k. Lakini bila kujua tatizo limetokea kwa nani, yote hayo huishia kuwa lawama kwa daktari.

Madaktari wanafanyishwa kazi kupita kiasi (kuwafanya wakose muda wa kutosha wa kupumzika na kufikiri, wakati mwingine hujifanyisha kazi nyingi wao wenyewe kupitia utoaji huduma katika vituo binafsi ili kuongeza mapato) na mara nyingi wamekuwa wakinyanyaswa na mahospitali, waajiri na viongozi na hivyo basi nao huishia kuwa wakali, waliopoteza furaha za maisha na wanaochukia kirahisi. Mwisho wa siku daktari huyu hawi na akili nzuri ya kutosha kumsaidia kufikia kujua hatima ya ugonjwa unaomsumbua mgonjwa aliyeko mbele yake.

Pia kumekuwa na lawama nyingi sana kwa madaktari, kwa matukio ambayo yametokea kwa nadra na mara chache. Matatizo ambayo ni ya kibinadamu, lakini kwa kuwa daktari anaonekana kama Mungu kwa jamii, huishiwa kusemwa vibaya. Bahati mbaya kosa moja tu kwa daktari yaweza kumuondolea sifa aliyojijengea kwa muda mrefu.

Daktari anaonwa anahusika na kila uchafu unaotokea kwenye mfumo wa afya. Mfano katika matatizo ya wizi wa madawa, na upungufu wa vitendanishi katika vituo vyao vya kazi. Madaktari hushangaa wakipimwa kwa mizani tofauti wakati serikali au wamiliki wa vituo vya afya na mgonjwa wajibu wao ukisahaulika kuwa sambamba naye katika utoaji wa huduma ya afya. Kama kifo kimetoa lazima hawa watatu wapimwe walivyoshiriki katika kusababishwa kifo. Lakini sivyo wafanyavyo. Wodi ya Mwaisela inasifika sana kwa kuwa na vifo vingi; lakini hakuna anayelaumu mgonjwa anayekuja kutafuta huduma kwa kuchelewa, shida iko kwa daktari.

Kuhudumia mgonjwa na kumfanya ajisikie vizuri ni jambo kubwa lenye kuleta ujira wa furaha na pia kuleta pesa. Lakini muda huwa hautoshi kufanya kazi kama hii, tena kwa ujira mdogo. Kama umepangiwa kuona wagonjwa 30 hadi 50 kwa siku katika kliniki, je ni akili ya binadamu gani inaweza kusikiliza hadithi nzima ya kila mgonjwa? Je, daktari hata akijua mgonjwa huyu anaumwa kitu fulani na kisha mgonjwa akashindwa kufanya vipimo fulani au kununua dawa alizoandikiwa na daktari kwa nini daktari alaumiwe? Daktari anapolalamika kwamba ujira wa kazi yake ni mdogo, na kwamba hata akienda dukani hapewi huduma bure kwa kuwa yeye ni daktari mwenye wito kwanini alaumiwe? Naamini wito unaishia kwa wale wenye magical healing na si kwa mtu aliyepata ujuvi sawa na engineer, mhasibu n.k. kupitia shule huyu akitumia darasa hili na yule akitumia darasa lingine.

Inapokuwa kazi ya daktari ni kutoa huduma nzuri, je, wajibu wa madaktari unaishiwa wapi mpaka akapata lawama?
 
Well said,

Matatizo ya madaktari Tz yanasababishwa na mfumo uliopo nchini wa kutothamini wataalam wa fan mbalimbal na badala yake kuwakumbatia wafanyabiashara na wanasiasa. Madai ya madaktari hayatofautian sana na ya wataaluma nyingine kama walimu, wahandisi na wengineo ambao kiukweli serikali na mfumo uliopo sasa umewasahau kiasi kwamba hata wakidai haki za msingi kama mazingira bora ya kazi,huchukiliwa juu juu na kupatiwa majibu mepesi mepesi...

Mgomo wa madaktari unatoa picha halisi ya hali mbaya inayowakabili wanataaluma wa kada mbali mbali nchini na kama serikali ya Tz ni sikivu, inapaswa kuutatua kwa busara wala si kwa mabavu na kwa kutoa kauli nyepesi nyepesi au za vitisho....Wakishindwa kufanya hivyo, sitashangaa migomo ikizidi kushamiri nchini....

Mungu amekwisha ibariki Tanzania....
 
Back
Top Bottom