Madaktari Bingwa: Jamani tumezidiwa

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,316
33,125
headline_bullet.jpg
Waunga kamati kwenda kumuona Pinda
headline_bullet.jpg
UVCCM waionya serikali isifanye ubabe
headline_bullet.jpg
Wagonjwa walalamika kuishiwa fedha



Njelekela(8).jpg

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Dk. Marina Njelekela


Hali katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam, imezidi kuwa mbaya, kiasi cha madaktari bingwa kukiri kuelemewa na utoaji huduma kwa wagonjwa
Kutokana na hali hiyo, madaktari hao wameunda kamati ya watu watano kwa ajili ya kuonana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ili kuzungumza pamoja na mambo mengine mgogoro uliopo kati ya madaktari waliopo kwenye mgomo na serikali.
Akizungumza na waaandishi wa habari, Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa MNH, Aminieli Aligaesha, alisema uamuzi wa kuunda tume hiyo, umekuja baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Dk. Marina Njelekela, kujadiliana na madaktari bingwa baada ya kuona hali inaendelea kuwa mbaya.
Aligaesha alisema kamati hiyo itakwenda kuzungumza na Waziri Mkuu, jukumu kubwa ambalo wamepewa ni kuangalia namna ya kutatua mgogoro huo pamoja na kujadili madai ya hali bora kwa madaktari wote kwa jumla.
Alisema kuundwa kwa kamati hiyo kutatoa mwanga wa mgogoro huo ambao umesababisha hali ya utoaji huduma kuzorota kwa kiasi kikubwa kupita siku zote za nyuma tangu mgomo wa madaktari hao uanze.
“Toka Januari 25 huduma zimezorota sana, na kuna madhara makubwa, kwani wagonjwa wamepungua, kliniki zimefungwa,” alisema.
Hata hivyo, alisema licha ya madaktari wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupelekwa hospitalini hapo kusaidia kutoa huduma kwa wagonjwa wanaofikishwa katika kitengo cha magonjwa ya dharura, bado watu wanasita kwenda kupatiwa huduma ma kutoa mfano kuwa juzi ni wagonjwa 25 pekee ndio waliofikishwa hospitalini hapo.
“Ni kweli serikali imetuletea madaktari kutoka jeshini, lakini bado mwitikio wa watu umekuwa mdogo kutokana na kuwa na wasiwasi wa upatikanaji wa huduma,” alisema.
Ndani ya wodi namba nne, jengo la Mwaisela, inayofahamika kwa kuwa na wagonjwa wengi, jana ilikuwa tupu baada ya wagonjwa wengi kuondolewa na ndugu zao.
NIPASHE ilishuhudia vitanda vya wodi hiyo vikiwa vitupu, huku wagonjwa watatu pekee waliobaki kwenye wodi hiyo wakisubiri huruma ya madaktari hao kwenda kuwapatia matibabu.
Mmoja wa wagonjwa hao alisema, alishuhudia wagonjwa wakiondolewa kwenye wodi hiyo na ndugu zao na kuwapeleka sehemu nyingine kwa ajili ya kupewa matibabu.
“Ndani ya wodi tumebaki watatu tu ambao hatuna uwezo wa kwenda hospitali binafsi. Tumeamua kufia humu au kama madaktari wakiamua kurudi waweze kutupatia matibabu,” alisema mgonjwa huyo.

TUGHE WAUNGA MKONO MADAI YA MADAKTARI

Wakati huo huo, Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya Tanzania (Tughe), kimeunga mkono madai ya madaktari wanaoendelea na mgomo hivi sasa, na kuitaka serikali kufanya mazungumzo nao ili kupata suluhu.
Akitoa tamko kwa waandishi wa habari jana, Naibu Katibu Mkuu wa Tughe, John Sanjo, alisema madai ya madaktari hao ni haki yao ya msingi.
“Tughe inaunga mkono madai yote yaliyotolewa na madaktari kuwa ni haki yao, hivyo tunaitaka serikali ifanye mazungumzo nao haraka iwezekanavyo, ili wafikie suluhu waokoe maisha ya Watanzania,” alisema na kuongeza kuwa: “Tunaomba madaktari wote warudi kazini wakati mazungumzo yanaendelea.”

Kadhalika, aliitaka serikali kutekeleza madai ya wauguzi, kwa kuwapatia kurugenzi yao ambayo wamekuwa wakiidai muda mrefu.

CCK YAWASIHI MADAKTARI
Katika hatua nyingine, Chama Cha Kijamii (CCK) kimewashauri madaktari kufanya mazungumzo na serikali kutatua tofauti zao, ili kuokoa maisha ya Watanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Chama hicho, Renatus Muabhi, alisema wameamua kuingilia kati ili kunusuru maisha ya raia.

WAGONJWA WA MIKOANI WATAKA WAPEWE PESA

Kwa upande wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), hali ilikuwa bado ni tete, ambapo wagonjwa wanaotoka mikoani wameiomba serikali kuwapa fedha za chakula baada ya walizokuja nazo kwa ajili ya matibabu na matumizi kuwaishia.
Wakizungumza ndani ya wodi namba 17 ya Sewahaji, wagonjwa hao walisema tangu mgomo huo uanze wamejikuta wakitumia pesa zao kinyume cha walivyotarajia na sasa wameishiwa fedha.
Kepha Huzi, ambaye ni mkazi wa Singida alisema tangu afike hospitalini hapo kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa mguu hajapatiwa matibabu yoyote, huku kiasi cha fedha alichokuja nacho kikiwa kimemuishia kabisa.
“Sina la kufanya kwa sasa, sina pesa kabisa hata ile pesa ya gharama ya upasuaji nimemaliza. Naomba serikali ituangalie kwa kutupatia huduma kwa kipindi hiki ili kuokoa maisha yetu,” alisema Huzi.

UVCCM: SERIKALI IACHE UBABE
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umeitaka serikali kuacha ubabe na badala yake ishughulikie mgomo wa madaktari kwa njia ya mazungumzo kwa kuwa wapigakura walioiweka madarakani wanazidi kuangamia.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa UVCCM, Martine Shigela, alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Shigela alisema UVCCM ina wajibu wa kuiagiza serikali kumaliza mgomo huo wa madaktari kwa kuwa umoja huo mwaka 2010 ulihusika kuomba kura kwa Watanzania ambazo ziliiweka madarakani serikali ya sasa.
Alisema mgomo huo unaathiri afya za wapigakura walioichagua CCM kuongoza nchi na kwamba lazima hatua za haraka zichukuliwe ili kumaliza mgomo huo.
“Sisi tulihusika moja kwa moja kuitangaza CCM, katika uchaguzi wa mwaka 2010 na hivyo bado tuna wajibu wa kuiagiza serikali kumaliza mgomo huu,” alisema.
Hata hivyo, alisema UVCCM haiungi mkono upande wowote katika mgomo huo ambao umezidi kuathiri huduma za afya na kutaka pande zote kukaa chini na kuzungumza.
“Serikali irudi katika meza ya mazungumzo ili hatimaye imalize mgomo kwa kuwa maisha ya wananchi yanazidi kuteketea kutoka na mgomo wa madaktari,” alisema Shigela.


WAGONJWA WANENA

Abubakar Juma (32), mkazi wa Mafia:

“Nifikishwa hapa baada ya kupata ajali ya pikipiki, lakini tangu nilipofikishwa sijapata matibabu baada ya madaktari kugoma. Naomba Serikai ikae pamoja na madaktari kutatua mgogoro huu kwani tunaoathirika ni sisi wagonjwa ambao kwa kweli hatuna hatia na suala lao hilo. Kwa ajili ya kuokoa maisha yetu Serikali isitoe masharti ya kukutana nao kwani wanaokufa ni Watanzania wenzao.”


Kepha Huzi (49) Singida:

“Nawaomba madaktari wawe na moyo wa huruma kwani wakumbuke Mungu ndiye aliyewapatia ujuzi kwa ajili ya kuwaokoa binadamu wenzao, sasa wanapogoma wanakiuka kiapo chao walichokula wakati walipokabidhiwa majukumu. Kutokana na umuhimu wao si vizuri kugoma kwa ajili ya kudai haki, wangetumia njia ya majadiliano kwani Serikali haiwezi kudanganya tena juu ya madai yao ya msingi.”

Salum Mhando (42) Magomeni, Dar es Salaam:

“Nimefikishwa hapa tangu tarehe 15 Januari mwaka huu, nilikuwa napata matibabu vizuri, lakini baada ya madaktari kugoma hatujapata dawa mpaka sasa hivi wakati napata maumivu makali kutokana na kuvunjika mguu.

“Ninachopenda kuwaomba madaktari wasitishe mgomo wao ili waendelee kutusaidia sisi watu wanyonge ambao tunateseka kwa kukosa matibabu.”

Abdallah Selemani (26) Handeni-Tanga:

“Ninaomba Serikali na madaktari kukaa meza moja ili kutatua mgogoro wao ambao umetuathiri sisi wagonjwa. Nakumbuka nilipofika hapa nilikuta mgomo huu ndo unaanza, walitaka kunirudisha nyumbani lakini niliwagomea kutokana na mfupa wangu wa mguu umetoka nje.”

Tatu Hemed (22)-Rufiji:

“Nilipofikishwa hapa nilipatiwa matibabu mazuri, lakini hali ilibadilika mwishoni mwa mwezi uliopita, hakuna daktari anayeingia ndani kutuhudumia wote wamegoma. Ninachowasihi madaktari warudi kazini kwa ajili ya maisha ya Watanzania wakati wanaendelea na majadiliano yao na Serikali.”

Sikujua Chale (18)-Songea:

“Siwezi kusimulia adha tunayopata wodini kwa kukosa madaktari, lakini ninaishauri Serikali kukubaliana na matakwa ya madaktari ili warudi kazini haraka. Kinachotuogopesha zaidi pale tunaposikia kwamba hata manesi hawawataki madaktari wa jeshi, sasa sisi ambao tunaumwa tunazidi kukata tamaa kabisa.”

Mariam usinde, (80) Pangani-Tanga:

“Naomba wajukuu zangu madaktari warudi kazini, ona mimi pamoja na madaktari kuniona, lakini sifurahii kusikia wengine hawapati matibabu. Jamani wamuogope Mungu, watusaidie wote humu wodini.”

KCMC BADO TETE
Hali ya utoaji huduma katika hospitali ya rufaa ya KCMC si ya kuridisha, kutokana na madaktari kutokutoa huduma kwa wagonjwa waliokuwa wakifika hospitalini hapo.
Madaktari hao ambao wamekuwa na mgomo baridi wameripoti katika sehemu zao za kazi na kuandika majina, lakini hawakutoa tiba na badala yake waliamua kuondoka hospitalini hapo na kuwaacha wauguzi wakiendelea na utaratibu wa kupokea wagonjwa hususani wale waliokuwa na matatizo maalumu ambao madaktari bingwa peke yao ndio walikuwa wakiendelea na huduma.
Baadhi ya ndugu wa wagonjwa walionekana wakitumia njia za panya, ili wagonjwa wao waweze kupata huduma ambapo baadhi yao walielezea hali iliyokuwepo hospitalini hapo tangu waliporipoti wakiwa na wagonjwa wao.


Imeandikwa na Richard Makore, Elizabeth Zaya, Moshi Lusonzo, Samson Fridolin na Gwamaka Alipipi, Dar na Charles Lyimo, Moshi.




CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom