Mabilioni yetu wameiba, adhabu yao kigugumizi

Tuandamane

JF-Expert Member
Feb 2, 2008
1,220
52
Nimeguswa sana na uchambuzi wa Gervas nikaona nivizuri niulete hapa


Na Gervas Zombwe wa Tanzania Daima



WANANCHI wanachangishwa michango ya ujenzi wa shule kwa nguvu. Na kutokana na umaskini wao wanaamua kuuza kuku, mazao yao, na hata baadhi ya vitu ili watoe michango ya kujenga shule. Wakati wananchi wanachangishwa, kodi zao zinachotwa na mafisadi wachache waliojiundia ka mtandao ka kulindana.


Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mabilioni yamechotwa, na ili kuwahadaa wananchi, wezi hao wakajiita ‘makampuni hewa' Hewa ikapenya dirishani ikachota mabilioni Benki kuu. Na leo tunaambiwa hewa inaanza kurudisha pesa hewa! Kweli Tanzania?

Mjadala wa kihistoria bungeni uliotokana na ripoti ya uchunguzi wa zabuni ya kampuni hewa ya Richmond umefichua mengi na kutufundisha mengi. Kamati hiyo imejenga Tanzania mpya japo ni kwa siku chache.

Tunaipongeza sana kamati kwa kuwafahamisha watanzania ukweli, ambao kwa muda mwingi taarifa nyingi nyeti kama za mikataba ilikuwa ni ndoto kuzijua.

Michango ya wabunge na mapendekezo ya kamati ni muhimu sana kwa mustakabali wa taifa letu.

Na bahati nzuri mapendekezo yote yamepitishwa na wabunge wote kwa karibu asilimia 99.05. Kweli haya ni mapinduzi chanya kwa Tanzania.

Pamoja na ukweli kwamba kamati hii imefanya kazi kubwa, suala la mapendekezo kufanyiwa kazi, hasa wahusika wa ubadhirifu kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, ndilo linalosubiriwa na wengi. Kamati nyingi zimeundwa hapa Tanzania na zinataoa ripoti nzuri zenye kujali maslahi ya taifa lakini inawezekana kuchelea kuchukua hatua kwa wahusika ndiyo imekuwa changamoto kubwa.

Mathalan, Tume ya Jaji Warioba iliyochunguza hali ya rushwa hapa Tanzania, hatua zingechukuliwa ingetoa dira tosha ya kutupa mwelekeo sahihi. Nadhani tusingefika kwa kina Richmond, maana yaliyosemwa humo yamejirudia. Mchakato mzima tuliouona juzi, hautakuwa na maana iwapo hatua zaidi hazitachukuliwa hasa kwa viongozi waliophusishwa na kashfa.

Naamini maamuzi yakitolewa kwa kuzingatia hali za wananchi na maisha yao hakuna atakayeonewa aibu.

Maana wananchi wengi ndio wanaoishi maisha magumu huko vijijini na kuzigusa tabu, dhiki na shida si viongozi.

Mathalani, kiongozi haathiriki panapokosekana huduma muhimu kama vile shule, zahanati, barabara na umeme huko vijijini. Maana viongozi waandamizi na familia zao wanatibiwa hospitali za daraja la kwanza au nje ya nchi.

Hivyo ubadhirifu wowote wa pesa ya umma unaumiza wanyonge ambao ni zaidi ya asilimia 80 ya waliomchagua Rais wetu.

Ubadhirifu wa fedha za umma unatisha sana. Tukiangalia maeneo yafuatayo tunakosa sababu za msamaha kwa watu waliohusika;

Moja, taarifa ya upotevu wa sh bilioni 133 BoT inatisha. Wakati huo huo Rais Kikwete alipotembelea Rukwa mapema 2007 alipewa taarifa ya kufungwa kwa zahanati 12 kwa kukosa dawa na waganga. Fikiria; sh bilioni 133 zilizochotwa na wajanja BoT zingeweza kujenga Zahanati kila kijiji mkoa wa Rukwa, na kusomesha zaidi ya madaktari 200 ambao wangeokoa maisha ya akina mama na watoto.

Pia fedha hizo zingeweza kununua vyandarua 5,000 vikawakinga watoto malaria. Wagonjwa na watu wengine wanakosa dawa wanakufa, zahanati zinafungwa, madaktari wanafunzi wanakosa mikopo Chuo Kikuu, pesa ziko mikononi mwa mafisadi. Moyo wa nani utawasamehe wahujumu uchumi wa namna hii?

Pili, ripoti ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2005/2006 ilibainisha kiasi cha sh bilioni 273 hazikujulikana ziliko.

Mabilioni haya yangeweza kujenga madarasa ya sekondari elfu tano. yangeweza kununulia vitabu elfu kumi na kulipa madai ya walimu bilioni nane, na wananchi wa kigamboni wangeweza kupata kifuko kipya na pesa nyingine zikabaki.

Lakini cha kushangaza mabilioni yanapotelea mikononi mwa wajanja, na badala ya viongozi wanaohusika washitakiwe kwa uhujumu uchumi, wanaadhibiwa wananchi kwa kufungiwa zahanati, kuchangishwa michango ya ujenzi wa madarasa tena kwa shurba kama ilivyoripotiwa huko Bukoba.

Mama mmoja aliwekwa kizuizini kisa hana mchango. Hadi akalazimika kujifungulia ofisi ya serikali ya kijiji.

Je, hii si uonevu kwa wananchi? Katiba ya nchi inawataka viongozi wawajibike kwa wananchi si kwa matumbo yao na majirani zao.

Tatu, rasirimali zetu zinavunwa kiholela na wajanja wachache wakiwemo viongozi. Wakati haya yanafanyika wananchi ambao ndio wamiliki wa rasilimali hizo wanapigwa marufuku kukata miti, kuua wanyama na maeneo mengine hawatakiwi kuishi.

Wanaambiwa ni kwa manufaa yao lakini manufaa hayaonekani.

Kuthibitisha haya, utafiti wa Wizara ya Maliasili na Utalii uliofanywa kwa niaba ya wizara na shirika lisilo la kiserikali linaloshughulika na ufuatilia wa bisahara ya wanyamapori na mazao ya misitu, lijulikanao kama TRAFFIC 2007, lilibainisha upotevu mkubwa wa mapato kwenye uvunaji wa magogo. Ambapo serikali inapoteza karibu bilioni 58 kila mwaka kutokana kuwepo kwa makampuni haramu yanayovuna magogo kiharamu, na kukwepa kodi..

Ripoti ya TRAFFIC inaenda zaidi kueleza kwamba miongoni wa makampuni 35 yaliyokuwa yanavuna magogo na kupeleka nje kinyemela, makampuni 28 yalikuwa ya viongozi wa serikali au jammaa zao.

Je, hatua gani zilichukuliwa dhidi ya hawa watu? Wakazi wa maeneo hayo wanakatazwa kukata miti.

Nne, Richomnd, IPTL nazo zaendelea kuvuna kodi za watanzania, huku machungu ya wananchi na taabu zao zikiongezeka.

Wanaolipa kodi hizo za kuwanufaisha akina Richmond, IPTL na wingi wa makampuni hewa ya Benki Kuu ni Watanzania maskini.

Wanauza karanga wanalipa kodi, wanavua samaki wanalipa ushuru, wanauza kuku wanachangia ujenzi wa shule. Huu sio uonevu? Kuna haja ya kuendelea kuwachangisa wananchi michango wakati kodi zao zinachotwa tu na watu wajanja wachache?

Karibu kila ubadhirifu wa fedha nyingi za umma unahusisha viongozi, ina maana madaraka yanageuzwa kuwa tiketi ya ufisadi? Hadi lini Tanzania?

Tunaamini dhamira ya Rais wetu kushughulikia suala hili ni kubwa na watanzania wanatarajia maamuzi yenye neema kwao. Mwalimu Nyerere alishawahi kusema msomi anapoisaliti jamii iliyomsomesha hafai hata kuwapo.

Namnukuu: "Kama msomi mwenye elimu ana majivuno kwa sababu ya ujuzi wake au yuko mbali sana na wananchi wengine ama wamwogope ingekuwa bora zaidi kama msomi huyo asingelikuwapo." (Nyerere: 1968). Kama tunamuenzi Mwalimu, kwa nini mafisadi wasifikishwe mahakamani au kufungwa maana hawafai hata kuwapo.

Inashangaza hata kamati ya Benki Kuu bado inakigugumizi hata cha jinsi fedha zinavyorudishwa, na hapa kuna maswali mengi magumu kutokana na mwenyekiti wa tume kutoa kauli zenye mkanganyiko. Ipo siku ukweli utajulikana kwa nguvu za umma na wasaliti wa nchi hii watalia na kusaga meno.

Mungu ibariki Tanzania
 
Back
Top Bottom