Maaskofu Wakemea wanasiasa kutumia matusi majukwaani; Wasema usikivu, umakini wapungua kwa viongozi

kipindupindu

JF-Expert Member
Dec 16, 2010
1,053
170
Wakemea wanasiasa kutumia matusi majukwaani
headline_bullet.jpg
Wasema usikivu, umakini wapungua kwa viongozi



Askofu%20Nzigirwa(1).jpg

Askofu Msaidizi Eusebius Nzigirwa wa Kanisa katoliki la St Joseph, jijini Dar es Salaam, akitoa mahubiri wakati wa ibada ya Pasaka jana.


Maaskofu wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo nchini wameitahadharisha serikali juu ya uwezekano wa nchi kuingia katika machafuko iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa kudhibiti ubaguzi wa misingi ya dini, kabila, ukanda, majimbo na jinsia ulioanza kuibuka miongoni mwa Watanzania.

Maaskofu hao; Godfrey Sehaba (Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Morogoro) na Thelesphori Mkude (Kanisa Katoliki, Jimbo la Morogoro) walitoa tahadhari hiyo kwa nyakati tofauti wakati misa za Ibada ya Sikukuu ya Pasaka jana, kuadhimisha kumbukumbu kufufuka kwa Yesu Kristo zaidi ya

miaka 2,000 iliyopita, mjini Morogoro na kusema iwapo hali hiyo itaachwa iendelee taifa linaweza kuangamia.
Katika mahubiri yake kwenye ibada hiyo iliyofanyika kitaifa katika Kanisa la Utatu Mtakatifu la Anglikana, Askofu Sehaba, alisema tayari kumeanza kuzuka udini, ukabila na ukanda, huku vikidekezwa na serikali pasipo kuanza kuchukuliwa hatua zozote.

Alisema karibu miongo mitano taifa limejengwa katika misingi ya utu, uhuru, maendeleo, usawa, haki, kujitegemea, uzalendo na maadili, lakini kumeanza kutokea matukio nchini yanayoashiria kutikisa misingi hiyo na kuleta nyufa.

Askofu huyo alisema iwapo hatua za dhati hazitachukuliwa mapema nchi inaweza kuingia katika machafuko.
Alisema hali hiyo imeanza kuleta ufa katika umoja wa taifa ambao ni tunu iliyoachwa na waasisi wa taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume.

MAADILI KATIKA TAIFA


Alisema kwa sasa maadili yameporomoka kuanzia kwa wakubwa hadi wadogo, huku watoto wakiacha kuheshimu wazazi na waajiri kuacha kuheshimu waajiriwa na hivyo kusababisha maandamano na fujo na kuweka ufa mkubwa katika taifa.
Aliwataka viongozi wa dini kuendelea kuwahubiria watu habari njema ili watubu na kupata msamaha wa dhabi zao na kuacha uovu.

TOFAUTI YA KIPATO

Alisema pia tofauti kati ya wenye nacho na wasio na kitu imekuwa kubwa na kwamba wapo maelfu wanaoshinda na kulala bila mlo wa maana wakati wenye nacho wanasaza na kumwaga chakula.
Askofu Sehaba alisema kuna watoto wengi wa wasio na uwezo wanashindwa kusoma katika hata shule za kawaida wakati wenye uwezo wanasomeshwa katika shule nzuri za kulipia hapa nchini na nje ya nchi, ikiwamo Ulaya.
Alisema wasio na uwezo wamekuwa wakikosa matibabu na kupoteza maisha wakati wale wenye uwezo hata wakiugua mafua wanapelekwa India na Ulaya kwa gharama kubwa zinazolipiwa kodi za wavuja jasho maskini.

MFUMUKO WA BEI

Askofu Sehaba alisema hivi sasa maisha yamekuwa magumu na kuleta maumivu makali katika jamii kutokana na pato la Taifa kutogawiwa kwa haki.
Alisema hali hiyo imesababisha hivi sasa wananchi kukata tamaa na kujiingiza katika vitendo viovu vya kutaka kujipatia utajiri kwa njia ya ushirikina badala ya kufanya kazi za halali.
Askofu huyo alisema mauaji ya albino na yale ya vikongwe hapa nchini ni kiashiria cha tatizo hilo.

UMAKINI, USIKIVU WAPUNGUA KWA VIONGOZI

Alisema umakini na usikivu kwa viongozi katika taifa hivi sasa umepungua sana na kusababisha maslahi ya madaktari kuachwa kushughulikiwa mapema hata kusababisha migomo na hatimaye wananchi wasio na hatia kupoteza maisha.
Alisema hali hiyo ni dalili kwamba kuna viongozi wasiojali wajibu wao, kiasi kwamba mauaji yamekuwa yakifanyika nchini, lakini hakuna anayetoa kauli ya kukemea na kusema hiyo ni dalili ya kutojali ulinzi na usalama wa wananchi.
Aliitaka serikali na viongozi wa ngazi zote hasa za juu kujenga tabia ya kushughulikia kwa karibu na kina migogoro kabla ya haijaleta madhara.

KUHUSU KATIBA

Askofu Sehaba alisema taifa katika siku chache zijazo litaanza mchakato wa katiba mpya, hivyo alitaka wnasiasa kuacha kuwatisha wananchi hasa wa vijijini waweze kutoa maoni yao ili yasikike na hatimaye kupatikana kwa katiba mpya ya Watanzania wote.

WANAWAKE WATAKIWA KUCHUKUA NAFASI ZAO

Naye Askofu Mkude, akihubiri katika maadhimisho ya misa takatifu ya Sikukuu ya Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Patriki, aliwataka wanawake nchini kuchukua nafasi zao kikamilifu katika malezi ya familia na kusema katika imani za Kikristo mwanamke amepewa umuhimu wa pekee kutokana na kushirikiana katika wokovu wa mwanadamu.

Alisema katika Biblia Takatifu mwanamke alikuwa wa kwanza kupashwa habari juu ya kuzaliwa kwa mwokozi wa watu ambaye ni Yesu Kristo.
Askofu Mkude alisema fumbo la kuzaliwa kwa Yesu Kristo lilimtokea mwanamke aliyejulikana kwa jina la Maria ambaye alichukuwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwa mujibu wa maandiko ya Biblia Takatifu na kisha kumzaa mkombozi wao huyo.

Alisema ni wanawake pia waliokuwa wa kwanza kujulishwa habari ya ufufuko wa Yesu Kristo na Malaika baada ya siku ya tatu ya juma kwenda kaburini ambako mwili wa Yesu ulilazwa kufuatia kifo chake msalabani, jambo ambalo alisema kuwa kufufuka kwake ndiyo sababu ya Wakristo kote duniani kusherehekea Sikukuu ya Pasaka.

Askofu Mkude alisema tukio la Pasaka ndilo lilikuwa la kwanza kufahamika duniani kabla ya Krismasi ambayo huadhimishwa kila mwaka kama siku ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo kwa vile tokea ufufuko wa Yesu Kristo ndipo waandishi wa vitabu vitakatifu walipoona umuhimu wa mtu huyo na kuanza kufuatilia kujua chimbuko lake.

“Mimi sisemi kuwa sikukuu ya Krismas haina maana ispokuwa nataka kusisitiza chimbuko la imani ya Wakristo ilikuwa ni kufa na kufufuka kwaYesu Kristo, kwa vile baada tu ya kufufuka ndipo wanadamu walipokumbuka yale yote aliyozungumza wakati wa mafundisho yake,” alisema.
Alisema kutokana na umuhimu wao, kulingana na historia, wanawake bado wanayo nafasi ya kutosha kuzijenga familia zao na kwamba familia ambayo mama haisimamii kikamilifu ni ya wasiwasi.

Aliwakumbusha Watanzania juu ya kupendana na kukumbusha juu ya maandiko matakatifu kama yalivyo katika Biblia Takatifu ambako suala la upendo limesisitizwa.
Alisema kulingana na maandiko hayo Yesu Kristo hakuja dunia kutengua torati ambayo ilisisitiza juu ya upendo, lakini alichokuja kukifanya ni kuikamilisha kwa kuwataka wanadamu kupendana kama mwenyewe alivyowapenda.

WATANZANIA WATAKIWA KUFANYA MAOMBI KUKEMEA UFISADI


Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji Dk. Leonard Mtaita, akiwasilisha salamu za jumuiya katika ibada hiyo, alisema Watanzania wanapaswa kufanya maombi kwa ajili ya kukemea nguvu za kifisadi ambazo zimeanza kuisumbua nchi.

Alisema hivi sasa nchi inasumbuliwa na tatizo la wizi kuliko rushwa kutokana na baadhi ya viongozi wa juu kujiingiza katika wizi badala ya kuwatumikia wananchi.

“Ningeshauri ile Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ingeitwa ya ‘kuzuia wizi’ maana hali ni mbaya. Viongozi ambao wanategemewa ndio wamekuwa wakijichotea fedha hizo,” alisema Mchungaji Mtaita.

Alisema viongozi hao wamekuwa wakifanya wizi huo, ikiwamo kuiingiza nchi katika mikataba mibovu ili kujinufaisha na kuonya iwapo serikali haitachukua hatua za makusudi kudhibiti hali hiyo, nchi inaweza kuteketea.
“Nani anaweza kuliondoa jiwe la mikataba mibovu? Nani anaweza kuliondoa jiwe la wezi wa fedha za nchi hapa Tanzania? Nani anaweza kuliondoa jiwe la kuikomboa nchi hii? Lazima tufunge na kuomba kwa Mwenyezi Mungu” alisema.

ASKOFU MALASUSA: TUMEFIKA MAHALI PABAYA


Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa, amesema taifa limefika mahali pabaya kutokana na Watanzania wengi kutawaliwa na dhana kwamba, mambo mbalimbali, kama vile amani, maadili mema na kutoishi kwa ujanjaujanja, hayawezekani kuwapo nchini.

Alisema hayo katika mahubiri yake ya Sikukuu ya Pasaka ya kuadhimisha kumbukumbu kufufuka kwa Yesu Kristo zaidi ya miaka 2,000 iliyopita, kwenye Kanisa la Azania Front, jijini Dar es Salaam jana.

Alisema Wakristo na Watanzania kwa jumla wanapaswa kujifunza kutoka kwa Mariamu Magdalena, Mariamu wa Yakobo na Salome waliokwenda kwenye kaburi alimozikwa Yesu kwa nia ya kuupaka mwili wake mafuta.

Dk. Malasusa alisema licha ya kukuta kaburi hilo likiwa limefunikwa na jiwe kubwa, kinamama hao waliendelea kuwa na matumaini ya kuufikia mwili wa Yesu na kutimiza walilokusudia, kwa kuwa waliamini inawezekana.

“Lakini watu wengi tumeweka mapingamizi mengi katika maisha yetu. Wengi wanadhani amani katika nchi haiwezekani, wanadhani maadili mema hayawezekani, kutoishi kwa ujanjaujanja haiwezekani,” alisema Dk. Malasusa.

Alisema kutoweka kwa amani na kuzuka ugomvi katika chaguzi hivi sasa kunachangiwa na watu, wakiwamo wale walioaminika kutokuwa na matumaini ya kuwezekana kwa mambo.

“Tumefika mahali pabaya tukidhani haiwezekani. Tunatakiwa kuishi kwa matumaini,” alisema Dk. Malasusa.
Alisema kitendo cha kinamama hao watatu kuamka alfajiri kwenda kuupaka mwili wa Yesu mafuta kunaonyesha namna walivyokuwa na upande kwake tofauti na siku hizi, ambapo watu wengi wanapenda kuokoa nafsi zao kuliko za watu wengi wengine.

Alisema haitoshi kwa Wakristo kuzungumzia ufufuo wa Yesu au kuimba Yesu amekufa miaka 2000 iliyopita, bali lililo muhimu kwao ni kuzingatia ujumbe wa Pasaka kwamba: “Kaburi li wazi”.

Aliwataka Wakristo na Watanzania kwa jumla kujizuia na tabia ya kuringa kila wanapopata kitu kipya akisema daima mwenye tabia hiyo ni yule tu asiyekuwa na hekima.

Alisema hivi sasa baadhi ya watu wamekuwa wakikubaliana na dini za ajabu ajabu zinazozuka kila uchao nchini, nyingine zikijiita za ufufuo na kusema hakuna sababu inayowafanya watu hao kukimbilia kwenye dini hizo isipokuwa kutokuwa sawasawa kiakili.
Hata hivyo, Dk. Malasusa, alisema hawawezi kuyumbishwa na watu hao kwa vile wanaamini ufufuo ni wa Yesu peke yake na imani hiyo (ufufuo) haimaanishi miili waliyonayo wanadamu.

WANASIASA WAEPUKE MATUSI MAJUKWAANI


Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika, Godfrey Mhogolo, aliwaasa wanasiasa nchini kufuata maadili na kuepuka tabia ya kutoa lugha ya matusi majukwaani.

Aliyasema hayo jana katika ibada ya Sikukuu ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu mjini Dodoma.
Aliwataka wanasiasa kuelezea sera zao na namna watakavyowakomboa maskini nchini, ikiwa ni pamoja na kuwa waadilifu katika namna zote na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kuinusuru nchi.

Alisema baadhi yao wanaonekana kukengeuka na kuondoka katika mstari wa maadili.
Alisema vilio vya wananchi vimekuwa vikisikika kila kona ya nchi kutokana na uwapo wa kundi kubwa la watu wasiokuwa na maadili hasa wanasiasa

wanaotoa lugha chafu hadharani, rushwa na ubinafsi uliowajaa mioyoni mwao.
“Sasa hivi nchi ina hali mbaya kuliko miaka 15 iliyopita. Wanasiasa wamejaa matusi. Wanapanda majukuani na kuanza kutoa matusi…Wasomi wamekuwa sio msaada kwa nchi kwa sababu wamekuwa wanatumia fursa ya elimu yao kuibia nchi badala ya kukomboa nchi, hata katika kanisa,” alisema.

Alisema licha ya kutumia kodi za wananchi kusoma, wamekuwa sio kielelezo cha maisha mazuri badala yake wamegeuka kuwa mafisadi.
Askofu Mhogolo alisema katiba mpya inayotazamiwa kubadili sura ya nchi haiwezi kuwa mkombozi kama maadili mema yenye sura ya Uafrika wenye

kujaa upendano, kuheshimiana, amani na mshikamano pamoja staha havitahuishwa kwa kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anakuwa na kujengeka katika uzalendo wa kweli kwa nchi yake.

Alitaka kuwapo kwa haki, upendo, amani na ushirikiano wa kitaifa.
Alisema vijiji vingi havina hatimiliki ndio maana migogoro ya ardhi imekuwa haiishi.

Mhogolo alisema vijiji vimekuwa vikiporwa ardhi kutokana na kutokuwa na hatimiliki na kwamba hiyo inatokana na wawekezaji kupewa kipaumbele kuliko wanakijiji.

Alisema hata Wakristo ambao wamekuwa wakiimba na kuhubiri wamekombolewa na Yesu, wamekuwa sio kielelezo chema kwa kuwa ndio wanaojihusisha na rushwa na wizi, huku wakijifariji kwa kufika makanisani na kutoa zaka.
Naye Askofu wa Kanisa la International Evengelism la Ipagala mjini hapa, Silvester Thadey, aliwataka waumini kusherehekea Pasaka kwa upendo na amani na kutaka sikukuu hiyo iwe kila siku katika maisha ya Wakristo badala ya kuishia makanisani.

WATANZANIA WAPINGE UTOAJI MIMBA


Askofu Mstaafu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Dodoma, Mhashamu Mathias Isuja Joseph, akihubiri katika ibada ya misa takatifu ya kusherekeha kufufuka kwa Yesu Kristu, kwenye Kanisa la Kiaskofu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, mjini Dodoma jana, aliwataka Watanzania kupinga vikali suala

la utoaji mimba kwani ni kinyume cha maadili na pia ni chukizo mbele ya Mungu.
Alisema Watanzania wanatakiwa kusimama kidete kuhakikisha wanakataa sera za utoaji mimba ambazo kwa sasa zimeenea katika baadhi ya nchi zilizoendelea.

Alisema uhai ni zawadi kutoka kwa Mungu na unaanza pale mtoto anapotunga mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomkuta.
“Lakini kwa siku za hivi karibuni baadhi ya watu wamekuwa wakikataa zawadi hiyo kwa kuamua kutoa mimba na kuua watoto wasiokuwa na hatia.

Yaani ni ajabu sana ni sawa sawa na wewe baba unamletea mtoto wako…halafu unampa zawadi ya Pasaka yeye anakurushia usoni. Sasa hii ni sawa na wewe unayepewa zawadi ya mtoto na Mungu halafu unatoa mimba,” alisema.
Aliwataka Watanzania kujiandaa kikamilifu ili kushiriki katika sensa ya watu na makazi kwa kuwa inatoa picha halisi kwa serikali katika kuhudumia watu wake na mahitaji mengine.

KATIBA MPYA IKOMESHE UBINAFSI, UFISADI, ULAFI, UPENDELEO


Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi, Isaack Aman, amewataka Watanzania kushirikiana na serikali kikamilifu katika kuandaa Katiba mpya itakayokomesha ubinafsi, ufisadi, ulafi na upendeleo.

Katika salamu zake za Pasaka kwa waumini wa kanisa hilo, ambapo katika Parokia ya Korongoni mjini
Moshi, zilisomwa na Paroko wa Parokia hiyo, Severini Mafikiri, alisema ni haki ya wananchi kushirikiana na serikali katika upatikanaji wa Katiba mpya, ambayo itahimiza utumishi bora na wenye uadilifu kuliko utumishi wa heshima.

Alisema kwa kufanya hivyo Pasaka itakuwa imeiangazia Katiba ili itumikie haki, upatinisho na haki katika amani kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
“Kila raia anayo haki ya kutoa maoni na kushirikiana na maandalizi ya Katiba mpya, kwani siku zote chumvi hukoleza chakula pale inapoyeyuka kwenye chakula, vivyo hivyo jamii itakolezwa na waumini walio tayari
kujitoa nafsi kwa faida ya umma,”alisema.

Alisema kila mwanajamii analo jukumu la kuweka utaratibu wa kuwatendea watu wote kwa haki katika sekta zote, kwaani tabia ya kujichukulia sheria mikononi inajitokeza katika mauaji ya vibaka na watuhumiwa wengine hata kwenye michezo.

Aliwataka viongozi wa jamii kuzingatia maadili ya utumishi na sio kuwapotosha watu, kuwatumia au kuwadhalilisha na kwamba taifa linapoingia katika mchakato wa Katiba mpya lilenge katika maendeleo ya wote na hasa wanyonge.

Alisema uzazi wa mpango umesababisha mamilioni ya watoto wachanga kuteketea, hususan katika
nchi zinazoendelea na kwamba makaburi ya watoto hao yanadhihirisha ukatili wa binadamu wasiomjali Mungu wala uhai na kwamba vilio vyao ni laana na kisasi kwa jamii husika.
Aliwataka waumini kuacha kujiunga wala kusikiliza mahubiri ya dini ambazo zinajiendesha kibiashara zaidi
ambazo zimeshamiri kila mahali kwa sasa.

MAZINGIRA YATHAMINIWE NA KUTUNZWA


Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT, Dk.Martin Shao, amewataka Watanzania kuthamini na kutunza mazingira kwani upo uwezekanao mkubwa wa kutoweka kwa miti na kusababisha watu kukosa mahala pa kuzikiwa na kuzikwa kwenye maplastiki na hatimaye kuchomwa moto kutokana na kukosekana kwa majeneza ya mbao.
Aliwataka Watanzani kutumia wakati huu kuotesha miti kwa ajili ya kurudisha hali iliyo kwani upo uwezekanao mkubwa wa kutoweka kwa miti nchini.

WATANZANIA WASIMAMIE UKWELI


Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki Songea, Mhashamu Norbetha Mtega, akihubiri katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Mathias Mulumba Kalemba mjini Songea kwenye ibada ya mkesha wa pasaka, amewataka Watanzania kusimamia ukweli kwa kila kitu ili kuonyesha uadilifu kwa kila jambo linalofanywa nao.

Alisema hakuna jambo linalofanywa ambalo halijatoka kwa Mwenyezi Mungu, hivyo watendaji na viongozi wa nchi katika ngazi zote wanapaswa kusimamia ukweli kwa kila jambo na kupiga vita ufisadi.

Askofu Mtega alisema kitendo hicho kinapaswa kikumbukwe kwa moyo wa ukweli kwa sababu aliyekufa alikufa kwa ajili ya ukweli.
Alisema viongozi na wananchi wakisimamama kwenye ukweli, uadilifu na hofu ya Mungu kauli mbiu ya amani, utulivu na upendo wa taifa, itakuwa na maana kubwa kwa ajili ya maendeleo ya taifa ambalo litakuwa limesimama kwenye ukweli.

Alisema kama ukweli na uadilifu hautakuwapo, kamwe kauli hiyo haiwezi kuwa na maana kama ambavyo Mwenyezi Mungu aliyoagiza kwa wanadamu na uongo ukipewa nafasi amani itatoweka.

Aliwataka viongozi kuwa waadilifu na kuheshimu maamuzi ya walio wengi badala ya kulazimimisha matakwa yao hata kama walio wengi hawataki na wamewakataa kwa kura wao huamua kutumia nguvu na hata wakati mwingine kusababisha madhara na vifo ili mradi tu malengo yao yatimie.
Alisema mchakato wa kupata katiba mpya usipozingatia ukweli, hata ikiandikwa kwa kibao cha dhahabu haitakuwa na maana kwani uongo ukiruhusiwa katika katiba hiyo upo uwezekano wa kuharibu amani na utulivu vilivyoasisiwa na waasisi wa taifa hili ambao walisimamia ukweli wakati wote wa maisha yao.

WAKRISTO WATAKIWA KUWA MFANO BORA


Mchungaji wa Kanisa la KKKT, Dayosisi ya Kati, Shadrack Langu, akihubiri kwenye ibada ya Pasaka, iliyofanyika katika Usharika wa Amani, mjini Singida jana, aliwataka Wakristo kuwa mfano bora, kufuata mafundisho yenye maadili mema na kujenga moyo wa upendo na huruma miongoni mwao.

Alisema kutokana na kazi njema aliyoifanya Yesu duniani wakati wa uhai wake, ni vyema ikaungwa mkono kwa jamii kupendana na kufuata matendo mema, kuamini na kujenga umoja wa kweli miongoni mwa Wakristo.
Alisema kuna baadhi ya watu ni wagumu kuamini kadri wanavyofundishwa na kuwataka wajitahidi kufuata imani na kujenga umoja miongoni mwao na jamii inayowazunguka.

WATANZANIA WATAKIWA KUJIEPUSHA NA PROPAGANDA ZA MAUAJI


Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa, akihubiri katika ibada ya pasaka jana, aliwataka Watanzania kuacha kushabikia propaganda za mauaji, kwa kuwa kuna watu wengi wanauliwa na ndugu zao bila makosa ili kujipatia mali kitu ambacho alisema ni chukizo kwa Mwenyezi Mungu.

Alisema uzima na mauti ukishindanishwa, unatakiwa kupigania uzima ili kuibuka mshindi badala ya kifo kama Yesu alivyoibuka mshindi kwa kufufuka kwake.

Askofu Nzigilwa alisema kuna watu wanaonewa, wanagandamizwa na kunyanyaswa katika mazingira magumu na watu wengine na kuwataka wamtumainie Mungu.
Alisema katika dunia ya sasa watu wengi wamekuwa na kiburi na majivuno, uhasama, chuki, kisirani na watu wengine hawaelewani katika sehemu zao za kazi na kusema hayo yote ni machukizo kwa Mungu yanapaswa kuwa na toba.

KATIBA MPYA UWE DAWA KUMALIZA UFISADI


Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Augistine Shao, akihubiri katika ibada ya pasaka kwenye Kanisa la St Joseph, Shangani, mjini Zanzibar juzi, alisema mabadiliko ya katiba ya Muungano lazima yazingatie mambo yatakayosaidia kuondoa ufisadi na rushwa kwa viongozi na watendaji serikali.

Alisema marekebisho ya katiba ya Muungano yana umuhimu mkubwa kwa kuhakikisha katiba mpya inaondoa ufisadi, ikiwamo tabia ya viongozi kufunga mikataba bila ya kuzingatia maslahi ya taifa.
Hata hivyo, alisema katiba bora itapatikana Tanzania kama wananchi watajiepusha na kutoa kauli za kejeli, matusi na fujo wakati wa kutoa maoni ya kusaidia kupata katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Tunataka katiba itakayokuwa na uwezo wa kuondoa ufisadi na kuzuia matumizi mabaya ya madaraka, kuweka aina ya serikali tunayotaka kuamua aina ya Muungano tunaotaka Tanzania,” alisema Askofu Shao, huku waumini wengi wakitikisa kichwa.

Alisema Watanzania lazima wapewe nafasi ya kuamua juu ya ukubwa wa Baraza la Mawaziri ili kuwa na muundo wa serikali unaofanana na hali halisi ya uchumi wa nchi.

Askofu Shao alisema baadhi ya viongozi wamekosa moyo wa uzalendo na upendo wa nchi yao na kuweka vipaumbele vya mikataba ya biashara kwa wawekezaji wa nje na kutumia vibaya raslimali za nchi, ikiwamo ardhi.

Alisema Watanzania hawawezi kukataa utandawazi unaozungumzwa, lakini utandawazi unaonyag’anya rasilimali sawa na kutegeneza mazingira ya kuwa mtumwa katika nchi yako.
Askofu huyo alisema kumeibuka vitendo vya ubaguzi Zanzibar vinavyokwenda kinyume cha misingi ya haki za binadamu na utawala wa sheria.

Alisema imefika wakati Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kukemea na kulaani biashara zinazoendeshwa kwa misingi ya ukabila, mahali alipotoka mtu, dini au itikadi ya kisiasa kwa vile ni kinyume cha misingi ya haki za binadamu na utawala bora.

Askofu Shao alisema magari ya mizigo Zanzibar yamekuwa yakitoa huduma kwa ubaguzi kwa kuwanyima huduma hiyo jamii nyingine kitendo ambacho ni kinyume cha mashariti ya leseni ya biashara wanayopewa wafanyabiashara kila mwaka.

Alisema serikali lazima ichukue hatua za kukemea vitendo vilivyoibuka kwa baadhi ya viongozi wa dini Zanzibar kutumia sehemu za dini na viwanja vya kisiasa kukashifu imani za watu wengine na kutoa vitisho vya kuharibu mali kinyume cha ibara ya 19 ya katiba ya Tanzania juu ya uhuru wa kuabudu.

Naye Mchungaji wa Kanisa la Anglikana Doyosisi ya Zanzibar, Staley Lichinga, alisema Zanzibar itapiga hatua kubwa ya maendeleo iwapo wananchi wataendelea kudumisha amani na umoja wa kitaifa.
Akihutubia waumini wa kanisa hilo Mkunazini katika ibada ya pasaka, alisema mataifa mengi yaliyoendelea yalifikia lengo kutokana na wananchi wake kudumisha amani na mshikamano.

Aliwataka waumini kusaidia watu wasiojiweza katika kipindi hiki cha kusherehekea Sikukuu ya Pasaka kutokana na kuwapo na makundi yanayoishi katika mazingira magumu.
Hata hivyo, sikukuu hiyo inaendelea kufanyika Zanzibar huku soko la ndani likikabiliwa na mfumko mkubwa wa bei na kusababisha kilio kwa wananchi wanyonge kufuatia kupanda kwa ukali wa maisha na kusababisha sherehe za pasaka kuzorota kutokan na tatizo la ukata wa fedha.

ASKOFU AWAPA WAUMINI MAMBO MATATU KUJIPIMA


Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati wa Kanisa la KKKT, Dk. Thomas Laiser, amewapa waumini wa kanisa hilo mambo matatu wajipime wenyewe na kuamua wapo kundi gani.

“Je, wewe ndugu yangu upo katika kundi lipi? Upo katika kundi la wanaompenda Yesu kama Maria Magdalena ama lile la wasiompenda? Ama la wale Wayahudi waliomsulubisha au kama Yuda aliyemsaliti?” alihoji Askofu Laizer katika mahubiri yake katika ibada ya kukumbuka kufufuka kwa Yesu Kristo, kwenye Usharika wa Arusha mjini na Moshono jana.

Alisema kama kuna watu waliompenda Yesu, Maria Magdalena alikuwa mmoja wao na hiyo ilijidhihirisha kwa yeye kwenda kwenye kariburi la Yesu alfajiri.

Askofu huyo alisema Yesu alimponya Maria kwa kumwondolea pepo saba na hivyo kubadilisha maisha yake kwa kumsamehe na kumtakasa dhambi, hivyo Maria hakuweza kusahau tukio hilo kamwe.

“Maria hakuwa na kingine cha kumpa Yesu ila kumpenda sana hata kaburi, hata mauti, akasukumwa na upendo huo kuwa wa kwanza kufika kaburini alfajiri sana siku ya kwanza ya juma,” alisema.
Aliwataka waamini kupima iwapo wapo kwenye kundi lipi kati ya lile la wale ambao baada ya kushindwa katika kumtetea Yesu, wanashindwa kabisa na kumwacha, ama katika kundi lile la akina Simon Petro ambao ingawa kuna kushindwa lakini wanaamka na kumtafuta alipo Mwokozi Yesu aliyefufuka.

Petro ndiye yule aliyeagizwa na Yesu kulisha na kuchunga kondoo zake, ndiye aliyeahidi kwenda na Yesu po pote aendapo, ndiye yule ambaye katika purukushani za Wayahudi kumkamata Yesu alimkata mtu sikio, ndiye yule ambaye mambo yalipowaka na kuwa magumu akamkana Yesu mara tatu.

Askofu Laiser alisema Petro alipofika kaburini hakusimama kando na kuchungulia tu, bali aliingia ndani ya kaburi na akahakikisha kuwa kutokuwepo mwili wake kaburini humo sio kuwa umeibiwa bali alikuwa amefufuka.

Pia aliwahoji wapo katika kundi lipi katika kundi la vijana wenye nguvu ambao hutumia nguvu zao, wakati wao na wepesi wao kuyakimbilia maovu ame wapo katika kundi la vijana wale wa Kristo akina Yohana wanaopendwa na Yesu, ambao hukimbia mbele ya wazee kuona na kuthibitisha ya kuwa hakika Yesu amefufuka?

Alisema Biblia inasema Yohana ni mwanafunzi aliyependwa na Yesu na kwamba ndiye aliyepata habari ya mwili wa Yesu kutokuwepo kaburini naye alichukua uamuzi wa haraka kufika kaburini kuona kimetokea nini.
Alisema alizitumia vizuri nguvu zake za ujana kukimbia haraka kumtangilia Mzee Petro kuona yaliyotokea.

Imeandaliwa na Muhibu Said na Jimmy Mfuru (Dar), Ashton Balaigwa (Morogoro), Sharon Sauwa, Peter Mkwavilla na Jacqueline Massano (Dodoma), John Ngunge (Arusha), Salome Kitomari na Upendo Mosha (Moshi), Gideon Mwakanosya (Songea), Elisante John (Singida), na Mwinyi Sadallah (Zanzibar).





CHANZO: NIPASHE

 
Hivi hakunaga mambo ya kiroho huko kanisani?

Hivi hakunaga mambo ya kanisa yanayohitaji maelezo?
 
Hivi hakunaga mambo ya kiroho huko kanisani?

Hivi hakunaga mambo ya kanisa yanayohitaji maelezo?
Ya kaizari muachieni kaizari na ya mungu mwachieni mungu, tutawatafutia uwanja wakwenda kupambana huko siku moja, lakini tuachieni matatizo yetu watanzania bila ya miungu yenu.
 
Back
Top Bottom