Maaskofu, mashekhe, wanayumba - Wasomi

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Mkutano REDET waibua mpya


Mwandishi Wetu


udsm218.jpg



Chuo Kikuu cha Dar es Salaam


Vyama vya siasa vyakosa demokrasia, Serikali yatajwa legelege
Wanahabari wadaiwa kusaidia kulinda maslahi ya wanasiasa


WASOMI kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wameibua madai mazito dhidi ya baadhi ya viongozi wa dini na wanasiasanchini, wakisema kuna ushahidi wa vitendo na kauli kwamba vigogo hao wanatumia udini kujinufaisha kisiasa na zaidi, viongozi wa dini kutumia vibaya ushawishi wao kwenye jamii.

Katika hatua nyingine, wasomi hao wamevishambulia vyama vya siasa nchini kwa kukosa demokrasia ya ndani; huku wanahabari, kupitia vyombo wanavyofanyia kazi, wakilaumiwa kwa kusaidia njama za baadhi ya wanasiasa kuharibu demokrasia ndani ya vyama vyao na hatimaye demokrasia ya nchi kwa ujumla.


Hoja na lawama hizo zilijitokeza wakati wa mkutano wa 18 wa hali ya siasa nchini, uliondaliwa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala.


Katika mkutano huo wa 18 uliofanyika kwa siku mbili, Desemba 16 na 17, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, wasomi hao walijikuta wakiingia kwenye mvutano wa hoja kwamba je; wananchi na nchi imechanganyikiwa au ni wanasiasa na vyama vyao? Hata hivyo, walieleza baadaye kuwa wanasiasa na vyama vyao ndiyo wamechanganyikiwa.


Udhaifu vigogo wa siasa na dini

Wakiwasilisha mada maalumu kuhusu demokrasia na mageuzi ya kijamii Tanzania, Profesa Fredrick Kaijage na Mhadhiri mwenzake wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Bashiru Ally, walisema malalamiko dhidi ya viongozi wa dini kutumia vibaya ushawishi wao wa kijamii na rasilimali za taasisi za dini kwa maslahi ya wanasiasa na vyama vya siasa yameongezeka.

Wasomi hao wametoa madai hayo katika wakati ambao viongozi wa dini pia wamekuwa wakielekeza shutuma zao kwa wanasiasa na viongozi wa Serikali kama chanzo cha mambo kwenda kombo nchini.


"Ushahidi kuhusu kuwepo kwa vitendo na kauli za wanasiasa na viongozi wa dini kutumia udini kujinufaisha kisiasa upo ingawa wahusika wa vitendo hivyo hatari wanatumia hila na mbinu za kuzima mjadala huu muhimu kwa mustakabali wa taifa," walieleza wasomi hao na kuongeza kwamba;


"Ingawa malalamiko dhidi ya udini yamekuwapo kwa muda mrefu nchini, matukio ya mwaka 2010 wakati wa Uchaguzi Mkuu yalikuwa ya kusikitisha na kutisha zaidi."

Katika kuthibitisha hoja zao, walieleza kuwa Kigoma ni mkoa ulioathirika kwa siasa za udini, ikidaiwa kuwa wakati wa uchaguzi mkuu mwaka jana, vyombo vya habari hasa redio zinazomilikiwa na baadhi ya taasisi za dini za kikristo na kiislamu, baadhi ya viongozi wa dini na taasisi za kidini zilizokuwa na dhima ya kutoa elimu ya mpiga kura, vilitumika kisiasa.

Kwa mujibu wa wasomi hao, vyombo hivyo vilitumika kisiasa kuwanufaisha baadhi ya wagombea wa ubunge na urais na kwamba wilaya za Kibondo, Kasulu na Manispaa ya Kigoma ndizo zilizokumbwa zaidi na mikasa ya siasa za udini mwaka jana.

"Upo ushahidi wa nyaraka, ushuhuda wa wananchi, viongozi wa dini pamoja na taarifa za taasisi za dola kuhusiana na tatizo hili katika maeneo mbalimbali Mkoa wa Kigoma," walieleza katika makala yao hiyo.

Matumizi mabovu ya madaraka

Kwa upande wake, Profesa Athumani Liviga naye wa UDSM, pamoja na mambo mengine, alisema nyadhifa za kisiasa nchini ghafla zimekuwa chanzo cha madaraka na njia ya kujipatia utajiri.

"Kufungua uchumi chini ya utandawazi na ubinafsishaji kumezifanya nyadhifa za kisiasa kuwa chanzo kizuri cha madaraka na utajiri. Hali ya wanasiasa kuingia katika taasisi na vyombo vya mamlaka imevutia wataalamu kutoka maeneo mengine kama udaktari, uhandisi, sheria, uchumi, uandishi wa habari, taaluma na biashara," anasema.


Kwa mujibu wa mada ya Profesa Liviga, iliyowasilishwa na Profesa Ernest Mallya katika mkutano huo, hali ya wataalamu kukimbilia siasa ina athari hasi katika fani husika.


Profesa huyo anasisitiza akisema; "Mtu hahitaji kutumia nguvu nyingi kubaini athari za maprofesa 15 kuondoka chuo kikuu kimoja na kuingia katika siasa huku wakiacha pengo ambalo litachukua muda kuzibika."


Ingawa anajipa matumaini kwa kusema hali hiyo inaweza kupungua lakini pia anaeleza; "....kama hali hii ya sasa ambapo siasa zinalipa vizuri zaidi kuliko fani nyingine itaendelea, madhara yake yatakuwa mabaya mno.


"Hali hii ya watalaamu wa ndani kukimbilia katika siasa itasababisha mmomonyoko wa ufanisi na umadhubuti katika maeneo mengi ambako wananchi wa Tanzania wanastahili uongozi na huduma bora."


Ni watawala na si viongozi

Dk. Mohammed Bakari wa UDSM kuhusu kuyeyuka kwa matarajio ya nchi kuwa na viongozi wa umma badala ya watawala anasema; "Haikutegemea kwamba Mahakama zingetawaliwa na rushwa. Mategemeo yaliyokuwapo wakati wa vuguvugu la kupigania Uhuru ni kupata viongozi ambao wangekuwa watumishi wa umma (public leaders) na si watala (rulers).

"Kwa matendo na kauli katika mfumo tulionao wa dola hatuna viongozi wa umma kwa maana halisi ya neno hilo. Unapomsikia kiongozi kwa mfano anasema hata kama watu watakula majani, ndege ya Rais lazima inunuliwe."


"..au wapiga kelele juu ya ufisadi uliokithiri katika sekta ya umma tena kwa ushahidi ambao si wa kupuuzwa lakini anasema..ah waache wapige kelele; kelele za mpita njia hazimnyimi mwenye nyumba yake usingizi, kauli hizi haziwezi kutolewa na viongozi wa umma, zinaweza kutolewa na watawala."


Alivigeukia vyama vya siasa akisema havionekani kama taasisi zilizo na mifumo rasmi na kwamba baya zaidi, vinaongozwa chini ya mifumo ya kiimla na kihafidhina iliyojengeka zaidi kwa taswira ya kiongozi au viongozi wachache wa juu (oligarchic personality culture).


"Kutokana na hali hiyo, demokrasia ya ndani ya vyama imekubwa na migogoro mikubwa nchini. Kwa mfano, kubadilisha viongozi huwa ni jambo gumu sana na huweza kuwa sababu ya migogoro na hata kusambaratisha vyama."


Anashauri akisema; "Ili vyama viweze kusimamia kwa dhati ajenda ya mabadiliko ya jamii havna budi kujengwa na kuendeshwa kama taasisi za jamii badala ya kuwa vilabu vya watu wateule (elite clubs).


Kwa upande wake, Dk. Benson Bana anasema; "Ipo haja vyama vya siasa kujitazama upya na kujipanga upya ili kutimiza wajibu wake kwa wanachama na wapenzi wake na taifa kwa ujumla.


Vyama vya siasa vilinde na kudumisha misingi ya tunu za taifa badala ya kupandikiza mbegu za uhasama na chuki miongoni mwa wananchi. Vitumie mbinu na mikakati muafaka ya kisiasa na kisheria katika kudai haki, na vitambue kuwa vina waibu wa kujenga taifa na kudumisha tunu za taifa.


Vijitahidi kumaliza migongani hasi na kusuluhisha migogoro kwa mujibu wa Katiba na kanuni za vyama hivyo ili viweze kutegemewa na kuaminiwa na wapiga kura.


"Vihamasishe wanachama na wapenzi wake kujenga, kuimarisha a kuendeleza utamaduni wa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili taifa na wananchi wake waondakane na tabia ya utegemezi."


Serikali imekuwa legelege

Dk. Godfrey Sansa wa UDSM kwa niaba ya Profesa Ernest Mallya, aliwasilisha mada kuhusu demorasia, utamaduni na mageuzi ya kijamii akisema, Serikali imekaa legelege kuhusu mashirika yake nyeti, kama Shirika la Ndege (ATC).

"Serikali nayo imekaa legelege kuhusu mashirika haya kama ATC, Tanesco na Shirika la Reli. ATC ambalo kwa muda mrefu halina ndege hata moja lakini lina wafanyakazi wanaolipwa mishahara. Wataalamu wa raslimali watu watatuambia kuwa kuna likizo zisizokuwa na malipo, lakini mkondo huo wa maamuzi haujatazamwa na Serikali kuhusu ATC.


"Sasa hivi tunasikia suala la Shirika la UDA (Usafirishaji Dar es Salaam) linadaiwa kuuzwa kinyemela, bila aibu. Bodi ya Wakurugenzi ipo na menejimenti ya shirika hilo ipo lakini mambo yanayofanyika ndiyo hayo. Kwani watatufanya nini? Huu ndiyo utamaduni unaojengeka sasa," alisema Dk. Sansa.


Anasema; "Kuna suala la kupeleka mafisadi mahakamani, kuvalia njuga suala la dawa za kulevya, kubomoa majengo yaliyojengwa kinyume cha sheria, kutovumilia rushwa na kuipigia kelele.


"Dhana ya CCM kujivua gamba ni mojawapo ya mikakati ya kujisafisha kwa wapiga kura. Hata hivyo, masuala mengine yanayohitaji uamuzi mgumu yamekuwa yakiwasumbua wafanya uamuzi. Suala la rushwa, kwa mfano, limekuwa gumu na wananchi wanaamini halifanyiwa juhudi za kutosha."


Kwa upande wake, Profesa wa Uchumi, Samuel Wangwe alisema ingawa umebuniwa mpango wa miaka mitano wa mwaka 2011 hadi 2015 ambao ni wa kwanza wa aina yake katika miongo mitatu iliyopita, utekelezaji wake ni changamoto kubwa.


"Utekelezaji umekuwa changamoto kubwa katika juhudi nyingi za awali kuelekea mabadiliko ya kiuchumi. Kimsingi, ufanisi katika ngazi ya utekelezaji ni mchakato wa kisiasa. Mafanikio ya sera katika kufanikisha mabadiliko ya kiuchumi yataamuliwa na kutegemea sana mikabala ya mabadiliko ya kisiasa na kijamii. Hii itaamua jinsi gani sera za kiuchumi kuelekea mageuzi ya kiuchumi zitaingiliana na siasa na ni jinsi gani itikadi inayoongoza itaandaliwa.


Profesa wake anasema suala la aina ya siasa na uongozi wa kisiasa unaoweza kuleta mabadiliko ya kiuchumi linaendelea kubaki juu katika dondoo za ajenda ya maendeleo.


Anasema; "Kimsingi, kama uzoefu wa mabadiliko ya kiuchumi yaliyofanikiwa unavyoonesha, mabadiliko ya kiuchumi ni mradi wa kisiasa kwa maana kwamba kwa kiwango kikubwa yanaamuliwa na aina ya siasa na uongozi wa kisiasa."








 
Back
Top Bottom