Maalim Seif: Ataka kiti cha Z'bar UN Kirudishwe.

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,883
1,482
maalim_mwanakwerekwe_c-564x272.jpg

Na Mwinyi Sadallah

14th August 2012

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kuna haja kwa Zanzibar kurejeshewa kiti chake katika Umoja wa Mataifa (UN). Alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na viongozi wa wilaya na majimbo wa Chama cha Wananchi (CUF) katika ukumbi wa Benjamin Mkapa, kisiwani Pemba jana. Alisema Zanzibar kabla ya Muungano ilikuwa nchi huru iliyokuwa na kiti chake UN na kuelezea haja ya kuwepo kwa mamlaka kamili ya Zanzibar ili iweze kurejesha kiti chake kwenye umoja huo.

Maalim Seif alisema hoja kubwa ambayo Wazanzibari wanatakiwa kujadili katika mchakato wa maoni ya Katiba mpya ni muundo na mfumo wa Muungano.

"Zanzibar tunayo Katiba yetu ya mwaka 1984 ambayo imejitosheleza kwa mambo yetu ya Zanzibar, lakini suala kubwa kwenye mabadiliko hayo kwetu sisi litakuwa ni la Muungano na hili haliwezi kuepukwa," alisema Maalim Seif. Maalim Seif aliwataka wananchi kuangalia maslahi ya nchi yao kwanza katika mchakato wa kukusanya maoni ya mabadiliko ya katiba na kuacha tabia ya kutetea misimamo ya vyama badala ya maslahi ya nchi na wananchi wake.

"Katiba ya nchi ni mali ya wananchi siyo ya chama chochote, lakini najua kila chama kina katiba yake na hiyo ndiyo itabakia kuwa katiba na mwongozo wa chama husika, kwa hivyo ndugu zangu naomba tulifahamu hili na tuangalie maslahi ya nchi yetu kwanza," alisema Maalim na kupigiwa makofi na wanachama.

"Mimi najua wapo wanaotaka serikali moja, wengine mbili, tatu, nne, na muungano wa mkataba, lakini wengine wanataka waachiwe wapumue…Yote hayo ni maoni na kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake bila ya kulazimishwa, kwa hivyo wakati wenu ukifika nendeni mkatoe maoni hayo kwa uwazi," alisema Maalim Seif.

"Wakati wenu ukifika nendeni mkatoe maoni yenu kwa uwazi bila ya hofu hiyo ni haki yenu ya kikatiba," aliongeza.

Alisema serikali ya Tanzania tayari imepanga ifikapo Aprili 2014, Tanzania iwe na katiba mpya ambayo inatokana na matakwa ya wananchi wake wa pande mbili za Muungano huo. Ingawa Maalim Seif hakufafanua kauli yake ya Zanzibar kuwa na kiti chake katika UN, lakini anamaanisha kwamba Zanzibar inapaswa kuwa na mamlaka yake kamili.

Kwa maana hiyo ikiwa Zanzibar itarejeshewa kiti chake katika UN hapatakuwepo na Muungano tena kwa kuwa itakuwa ni nchi kamili ambayo inatambuliwa na UN na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla. Tangu Tume ya kukusanya maoni ya Katiba mpya kuanza kazi hiyo, kumeibuka kikundi kinachofanya kampeni misikitini (Uamsho) kutaka Zanzibar kujitenga katika Muungano huku wengine wakitetea kuwepo kwa Muungano wa mkataba.

Vile vile, baadhi ya Wazanzibari wakiwemo mawaziri na makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamesema kuwa kuna haja ya kuwa na Muungano wa mkataba kwa lengo la kumaliza kero zinazolalamikiwa. Baadhi ya makada wa CCM waliotaka Muungano wa mkataba ni Waziri asiye na Wizara Maalum, Mansour Yusuf Himid na mmoja wa waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, Ali Nassoro Moyo.
Hata hivyo, baadhi ya makada wamewashambulia na kuwatisha wanachama wa chama hicho wanaotoa maoni tofauti na sera ya CCM ambayo ni muundo na mfumo wa serikali mbili.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, wiki iliyopita wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Jimbo lake la Kitope, alisema wanaopingana na sera ya CCM kuhusu muungano warejeshe kadi zao za uanachama badala ya kusubiri kufukuzwa. Naye Mbunge wa Uzini (CCM), Dk. Mohammed Seif Khatib, Alhamisi iliyopita akizungumza na waaandishi wa habari mjini Dodoma akiwa na wabunge zaidi ya 30 kutoka Zanzibar alieleza kushangazwa na wanachama wanaotoa maoni ya kuvunja Muungano.

Khatib ambaye ni Mwenyekiti wa wabunge wa CCM Zanzibar, alisema chama hicho kinapaswa kuwachukulia hatua kwa maelezo kuwa walipata nyadhifa zao kwa kutumia ilani ya CCM inayoeleza wazi kuwa sera yake ni ya Muungano wa serikali mbili.

CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom