Maajabu ya kufikiri mambo makubwa na ni kwanini uweke malengo makubwa maishani.

Peter Agostino

Senior Member
Sep 23, 2016
105
226
Jamani mimi ninayeandika makala hii, ni mgeni humu Jamii forum, hii ni post yangu ya kwanza hivyo kama nitakuwa pengine nimekwenda kinyume na utaratibu, nadhani mtanisahihisha kwani badala ya kutumia jukwaa la kawaida la kujitambulisha mimi nimeona nijitambulishe hapahapa;

Majina yangu ni Peter Augustino, ni mwandishi wa vitabu vya ujasiriamali na pia mwanzilishi wa blogu ya Jifunzeujasiriamali. Napenda ujasiriamali na nimeona si vibaya nikajiunga na jukwaa hili katika juhudi za kupiga vita umasikini. Asanteni na karibuni.

Kabla ya kusoma makala niliyotayarisha hapa leo hii, Hebu kwanza jiulize mwenyewe, huwa malengo unayojiwekea yakoje? Ni malengo madogomadogo ambayo unapoyatekeleza yanakupa burudani au ni malengo makubwamakubwa yanayokupa tabu wakati wa kuyatekeleza? Na je, wakati ukijiwekea malengo hayo huwa unafikiriaje?, Unafikiri mambo makubwa au madogo?


Baada ya hapo sasa na hebu tuanze kuziangalia njia hizo za kivitendo zinazoelezea uwezo huu wa ajabu wa kufikiri mambo makubwa hata ikiwa ni ndoto tu ambazo bado hazijawa vitu halisi.


Ipo tabia moja, matajiri karibu wote duniani wanayo, akiwemo, Bill Gates, Warren Buffet, Said Salim Bakhresa, Mohamed Dewj, Mzee Reginald Mengi na wengineo wengi. Tabia hiyo siyo nyingine bali ni tabia ya “KUFIKIRI MAMBO MAKUBWA” Alhaji Aliko Dangote kwa kutumia mbinu hiyo ameweza kuanzisha viwanda vikubwa zaidi barani Afrika vya kuzalisha sementi na kufanikiwa kuwa tajiri namba 1 barani humo, Jeff Bezoz aliweza kuanzisha duka kubwa zaidi duniani la vitabu mtandaoni- Amazon,

Donald Trump anayegombea kiti cha uraisi wa Marekani sasa hivi kupitia Republican ameweza kuwa mjenzi wa majumba(Real estate Agent) mkubwa kabisa na anayeheshimika siyo Marekani tu bali na Duniani nzima kwa ujumla. Katika hotuba zake siku za nyuma, Trump mwenyewe aliwahi kusema hivi na hapa namnukuu; “Watu wengi hufikiria mambo madogo kwasababu wanayaogopa mafanikio, huogopa kufanya maamuzi na huogopa kushinda. Na hivyo kuwapa watu kama mimi faida kubwa”-Donald Trump.

Unapoyatazama maneno haya ya Trump utagundua kwamba hata anachokifanya sasa kwenye kinyanganyiro cha urais kule Marekani ni sawasawa ni hicho alichowahi kukitamka miaka zaidi ya mitano iliyopita. Trump hujiwekea malengo makubwa, Trump hufikiri mambo makubwa, Trump haogopi mtu hasa anapojua anafanya jambo ambalo havunji sheria ya nchi, Trump hana aibu linapokuja suala la maslahi yake iwe ni kisiasa au kiuchumi na Trump haogopi kabisa kufanya maamuzi hata ikiwa ni katikati ya hatari inayoweza kumgharimu kile anachokipigania.

Trump hapa anaendelea tena kusema hivi; “Napenda kufikiria mambo makubwa, ikiwa utaenda kufikiria kitu chochote, unaweza pia ukafikiria mambo makubwa”-Donald Trump


Sasa na sisi ndugu yangu tunasubiri kitu gani? Kwanini tusifikirie mambo makubwa na kujiwekea malengo makubwa maisha yetu yakabadilika? Hata kama hatutaweza kuwa kama Trump, lakini angalao tuweze kubadilisha tu mboga na watoto wetu wasome bila shida.

Baada ya utangulizi huo, hebu sasa tukayaone yale maajabu yenyewe 7 ya kufikiria mambo makubwa na sababu zinazokufanya ulazimike kujiwekea malemgo makubwa katika maisha yako ukiwa hapa Duniani.


1. Kufikiria mambo makubwa kunaisukuma akili yako, kuhoji misemo, kauli na desturi mbalimbali za jadi zilizozoeleka miongoni mwa jamii nyingi za kiafrika. Jamii nyingi pasipo hata kujua zimejijengea tamaduni mbalimbali na mitizamo ambapo jambo au kitu chochote kile kilichokuwa nje au kinyume na tamaduni hizo basi huchukuliwa kama ni jambo lisilowezekana au kitendo kiovu. Kauli hizo ni kama hizi zifuatazo, ni mifano tu zipo nyingine nyingi;

1) Soma sana ili baadae upate kazi nzuri yenye mshahara mnono.

2) Ridhika na kile upatacho.

3) Aliye juu mngoje chini.

4) Ili utajirike ni lazima kwanza uwe fisadi au uende kwa wataalamu wa jadi wakupe dawa za kuvuta utajiri nk.

Unapofikiri mambo makubwa, ni kwamba unailazimisha kabisa akili yako kupinga kauli kama hizo mbovu na ubongo wako kuanza mara moja kutafuta njia ya kujinasua na hali hiyo. Bill Gates angefuata kauli ya “Soma sana ili baadaye upate kazi nzuri” sidhani kama leo hii ungemsikia mtu akisema “Nipigie kompyuta yangu Window 7, au window 10” au karibu katika kila ofisi duniani kukuta programu za “Microsoft office” kwenye komputa zao.


Nakuomba unielewe vyema hapa, siyo kwamba natetea kila mwanafunzi au mwanachuo aache masomo yake akaanzishe ujasiriamali, HAPANA. Ila ninachotaka kukisisitiza hapa ni kuacha kuzifanya kauli za namna hiyo na misemo ya jadi kuwa kama sheria. Kwa mfano kwamba hakuna njia nyingine kabisa ya kufanikiwa maishani zaidi ya kusoma, inamaana hata wale wanaofeli basi huo ndio uwe mwisho wao wa maisha? Fikiria kwanza nje ya kauli hizo kabla haujazipa nafasi ya kwanza.

Wagunduzi wa ndege, Wright Brothers wangeliridhika tu hivihivi na kauli kwamba “Binadamu hawezi kabisa kuruka angani kwa vile hana mabawa ya kurukia kama ndege, hebu nieleze leo hii ungelizisikia wapi ‘Bombadier Q400’ za rais magufuli?


2. Hukupa changamoto ya kwenda hatua mbele zaidi kwa kukubali ukweli hata ikiwa ukweli wenyewe ni mchungu kiasi gani.
Unapojiwekea lengo kubwa maishani kiasi ambacho unahisi pengine lengo hilo ni gumu na halitawezekana, huwa unajisikia vibaya, lakini hapo unashauriwa ujisukume hivyohivyo tu kulitekeleza kwa kutumia mbinu hii ya kufikiri mambo makubwa, mwishowe utashangaa unafanikisha lengo lako kama ulivyolipanga.


3. Kufikiria mambo makubwa huunganisha pamoja hisia na shauku yako. Unavyojisikia wakati unapoweka lengo kubwa maishani mwako kunategemea sana jinsi utakavyovichanganya vitu hivyo viwili, hisia na shauku. Ikiwa utajisikia vibaya kuwa unalenga lengo kubwa basi inakubidi ujichunguze upya akilini mwako, lakini ikiwa utajisikia mchangamfu na uliyehamasika basi upo katika mstari mzuri. Lengo kubwa inamaanisha kuichangamsha shauku yako bila ya kujali lengo hilo lina changamoto kiasi gani.


4. Huiweka huru silka yako ya ubunifu.
Kufikiria mambo makubwa hiweka huru silka yako ya ubunifu na kukufanya ufunue mawazo yatakayokuwezesha kufikia malengo yako. Unapoweka lengo kubwa mwanzoni hupatwa na woga lakini baada ya akili kuanza kulizoea lengo lenyewe utaanza kuona uwezekano wa kulitekeleza lengo hilo kwa akili kuleta njia zitakazosaidia kulifanya lengo hilo kuwa kweli.


5. Hukupa changamoto ya kuongeza kipato chako, kuliko kuishi chini ya kipato unachopata.
Bila shaka umewahi kusikia kauli hii, “Ishi chini ya kipato chako”. Kauli hiyo ni mtazamo zaidi wa mtu mmoja mmoja kulingana na unavyoichukulia. Wanaofikiria mambo makubwa kamwe hawawzi kuishi chini ya vipato vyao. Wanachokifanya ni kutanua vipato vyao vilingane na mtindo wao wa maisha wanaoutamani. Hawaridhiki na matokeo ya wastani bali hulenga makubwa zaidi. Je, na wewe ndugu yangu ungependa uishi juu ya kipato ama chini ya kipato chako? Uamuzi ni wakwako.


6. Hukupa sababu ya kuliishi na kulifia lengo lako.
Kufikiria mambo makubwa na kujiwekea malengo makubwa hukupa kitu cha kushughulika nacho maisha yako yote. Christopher Columbus alipojiwekea lengo la kuizunguka dunia, pamoja na hatari yote iliyotokana na imani kwamba dunia ilikuwa na umbile tambarare lakini alilifanya kuwa lengo lake la maisha la kufa na kupona. Kila mtu hapa duniani analo lengo lake, lakini unaweza ukaligundua lengo lako tu endapo utafikiri mambo makubwa.


7. Huondoa yasiyowezekana.
Ajabu la mwisho la kufikiria mambo makubwa, ni uwezo wa kuvunja yale yote “yasiyowezekana” Hugeuza mambo yasiyowezekana kuwezekana. Kauli hii huwa kweli tu pale ambapo mtu unaanza kufikiria mambo makubwa na kuyatekeleza huku ukiwa na mtizamo wa kukubaliana na changamoto kubwa.


Peter Agostino ni mwandishi vitabu vya ujasiriamali na mwanzilishi wa blogu za Jifunzeujasiriamali na Smartbookstz
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom