BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,005
Maoni ya Mhariri
Lukuvi ujasiri huu uwe endelevu
Imeandikwa na Mhariri; Tarehe: 22nd May 2009
Lukuvi ujasiri huu uwe endelevu
Imeandikwa na Mhariri; Tarehe: 22nd May 2009
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, anaonekana 'kutema cheche' hasa kutokana na kukerwa na mambo kadhaa aliyoyakuta mkoani Dar es Salaam, alikohamishiwa hivi karibuni akitokea Dodoma ambako anasema ameacha huruma aliyokuwa nayo.
Kauli ya Lukuvi inaonyesha ujasiri fulani kwa dhamira yake ya kutaka kuweka mambo sawa katika mkoa huu wenye mambo mengi na wakazi wengi wa rangi, tabia, itikadi, makabila na dini tofauti; hali inayosababisha uangalifu mkubwa katika kukabiliana na matatizo yaliyopo.
Mkuu wa Mkoa anaona wazi kero ya wafanyabiashara wa kigeni kuvamia biashara za wenyeji, ambazo hazistahili utaalamu kutoka nje kuziendesha, ikiwa ni pamoja na uuzaji wa karanga na hata maua tena katikati ya Jiji.
Anasema waziwazi kuwa atapambana na watendaji wake wabovu, kwani hakuja Dar es Salaam kujenga urafiki usio na tija kwa wananchi anaowaongoza, hivyo amedhamiria kubanana nao katika kazi za kupambana na kero za wananchi.
Kero nyingine anayosema inamchefua pia ni ya uchafu ambao unaanza kukithiri katika kona mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam licha ya kuwapo magari mengi ya kusomba taka ingawa nayo yanaonekana kuwa taka kutokana na ubovu na uchafu wao.
Tunasema kauli ya Lukuvi ni ya kijasiri kwa kuzingatia waliomtangulia ambao nao walikuwa wakiingia Dar es Salaam, kwa 'gia' kama yake lakini baada ya muda gia hiyo imekuwa ikishindwa kuliwezesha 'gari la maendeleo' kupanda kilima hata kidogo.
Tulishasema huko nyuma, kuwa Dar es Salaam ndio uso wa nchi, ambapo wageni wengi kama si wote waingiao nchini, huanzia kabla ya kwenda mikoani, hivyo hakuna namna yoyote ya kukwepa kuiona Dar es Salaam na uchafu na miundombinu yake duni.
Kwa kuzingatia hilo, Rais anapomteua Mkuu wa Mkoa wa kuiongoza Dar es Salaam, anatarajia kuwa na kiongozi atakayeweza kuuosha uso wa nchi kwa maji na sabuni ukatakata. Mwosha uso wa sasa ni Lukuvi.
Tunamwamini kuwa ni mchapakazi ambaye ameshawahi kuishi Dar es Salaam na kuongoza wizara kwa nafasi ya unaibu ambako pia alifanya vizuri lakini baadaye akaondolewa na kuwa mkuu wa mkoa, hivyo ni wazo ana uchungu na watu wa Dar es Salaam na mkoa wenyewe.
Anaelewa pia kuwa Dar es Salaam haina miundombinu mizuri hususan ya barabara na hivyo anahitaji kuja na mikakati itakayosaidia kuboresha miundombinu hiyo huku akichelea kutoa ahadi za takwimu ambazo hatimaye kwa mwaka wake huu mmoja, atashindwa kuzitekeleza.
Kama walivyo wananchi wa Dar es Salaam, sisi tunaahidi kumpa ushirikiano kama kweli ataonyesha dhamira ya vitendo ya kulisaidia Jiji hili kuondokana na kero hizo na hasa atakapopambana na viongozi 'Waswahili' wenye visingizio na wanaotanguliza posho kwa kila kitu.
Kwa kuwa kupanga ni kuchagua, Lukuvi ana changamoto kubwa ya kutoa kipaumbele kwa miradi muhimu ambayo itakuwa ndiyo inayolenga kukabiliana na kero za wananchi na kuzimaliza, ili Dar es Salaam ianze kuonekana kama miji mingine yenye hadhi yake Afrika, kwa kuanzia.
Ingawa hajabainisha staili yake ya kuongoza, tuamini tu kuwa anaongoza kwa vitendo virefu na si maneno, hivyo tuna matumaini makubwa kuwa yaliyoshindikana kwa Abbas Kandoro yatawezekana kwa Lukuvi.