Lukuvi akataa ripoti ya mabomu

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,007
Lukuvi akataa ripoti ya mabomu
Thursday, 04 June 2009 07:36

*Mengine 11 kulipuliwa tena Jumamosi
*Nyumba zote kurudishiwa zilimokuwa

Peter Masangwa na Salum Pazzy

Majira

KAMATI ya Kutathmini Maafa yaliyosababishwa na milipuko ya mabomu katika kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Mbagala, 'imemkoroga' Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. William Lukuvi kwa kukabidhi taarifa yenye upungufu licha ya kuongezewa muda wa kufanya kazi hiyo.

Kutokana na upungufu wa taarifa hiyo, Bw.Lukuvi ameiagiza Kamati hiyo kurudi tena Mbagala ili kukamilisha sehemu ambazo hazikujitosheleza kiasi cha kumpa wasiwasi.

Hatua hiyo ilifikiwa jana Dar es salaam wakati Kamati hiyo ilipokabidhi taarifa ya tathmini hiyo kwa Mkuu huyo wa Mkoa ayetoa siku tatu kukamilishwa taarifa hiyo na maeneo mengine kufanyiwa marekebisho.

"Nimeipa Kamati siku tatu kukamilisha sehemu nilizoagiza na Jumapili wiki hii watanikabidhi tena ili nielewe vizuri sehemu ambazo sikuzielewa leo," alisema Bw. Lukuvi


Upungufu wa taarifa hiyo umemfanya, Bw. Lukuvi kukataa kutaja jumla ya kiasi cha fedha watakazo fidiwa waathirika hao kama alivyoahidi hapo awali kwani alisema mabadiliko yanaweza kutokea baada ya marekebisho hayo ya kamati hiyo.

''Najua jumla ya gharama ya maafa lakini sitaki kusema kwa sasa kwani kuna upungufu hivyo nasubiri maofisa taathmini warudi tena site (eneo la tukio) ili wakajiridhishe kuhusu zile nyumba 286 zilizoharibika kabisa na wale wenye mali zilizoharibika na hawakupigwa picha," alisema Bw. Lukuvi.

Alisema Serikali haitamhamisha mtu yeyote eneo la Mbagala hivyo kila atakayelipwa fidia atatakiwa kujenga eneo lake la awali mbali licha ya eneo hilo kuwa jirani na kambi hiyo,vinginevyo yatolewe maelekezo mengine na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Bw.Lukuvi aliwashukuru wakazi wa Mbagala kwa uvumilivu wao kwa mwezi mzima tangu milipuko hiyo ilipotokea, Aprili 29 mwaka huu, maafa ambayo yamewafanya kusitisha shughuli zao.

"Kwa sasa wakazi wa Mbagala wanaweza kuendelea na shughuli zao kwani Serikali imemaliza kazi yake ya kutathmini na kazi iliyobaki sasa ni kuwalipa fidia zao jambo ambalo haliwazuii wao kufanya kazi," alisema.

Katika tukio la jana lililohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mkoa, madaktari walisema jumla ya wagonjwa 681 walitibiwa kutokana na milipuko hiyo, 531 kati yao walipatiwa matibabu na kuruhusiwa kurudi, 99 walilazwa na 26 walipoteza maisha.

Huduma iliyotolewa na madaktari hao mashuleni baada ya kubainika idadi kubwa ya wanafunzi kuwa na matatizo ya macho na masikio, ilibaini kuwa zaidi ya watu 1,221 walifanyiwa uchunguzi, 507 walidai kusumbuliwa masikio, 552 macho, 210 walibainika kuwa na matatizo ya masikio kuziba kwa nta na wengine matatizo tofauti

Kuhusu mwathirika aliyepoteza mkono, Bw. Lukuvi alisema atawekewa mkono na wenye matatizo ya macho watanunuliwa miwani.

Kamati hiyo iliyokuwa chini ya Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza (ACP) Cleophace Rweye, ilihusisha wataalamu wengine mbalimbali kutoka Mikoa ya Tanga, Morogoro na Pwani.

Wakati huo huo JWTZ limetangaza kuwa litafanya uteketezaji wa mabomu mengine 11 Jumamosi ijayo saa nne asubuhi.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya JWTZ jana ilieleza kuwa wakazi wa Mbagala watapewa tahadhari kabla na baada ya milipuko hiyo.

Imewataka wakazi hao kuwa watulivu kwani zoezi hilo litafanywa kitaalamu na halitakuwa na madhara hata hivyo wametakiwa kuwa mbali na eneo hilo.
 
Back
Top Bottom