Lowassa aongea na vyombo vya habari; akataa kugusia suala la Richmond/DOWANS

Invisible

Robot
Feb 11, 2006
9,075
7,878
Wakuu,

Muda si mrefu tutaweza kwenda Live kutokea Monduli ambapo Mhe. Lowassa (Waziri Mkuu aliyejiuzulu) atakapoongea na vyombo vya habari. Tumefanikiwa kupenyeza mtu hivyo tutaweza kuwaletea alichoongea. Nita-update 1st post kulingana na atakavyokuwa anaongea.

Shukrani

* Soma updates hizi tokea chini:
=================

  • Mwandishi wetu kamsisitizia kuwa watu wamesisitiza wanataka kujua kauli yake juu ya Richmond/Dowans/Symbio na suala la kujivua gamba ndani ya CCM, vinginevyo mkutano huu hautakuwa na maana na watu wanahisi labda umetishwa. Kajibu kuwa masuala haya atayazungumzia lakini leo si wakati muafaka, kuna wakati atayazungumzia.
  • Mwandishi kamwuliza kama ametishwa, maana anaonekana kila la muhimu hataki kuongelea, kajibu kirahisi tu "SINTOJIBU MASWALI HAYO"
  • Mwandishi wetu pia kamwuliza juu ya 'Uvuaji Gamba', nalo kakataa katakata kuongelea, kasema si wakati muafaka.
  • Pamoja na mwandishi wetu kumweleza umuhimu wa yeye kuongelea suala la DOWANS/Richmond kakataa katakata na kusema ataliongelea wakati muafaka na si leo.
  • Wakuu... Kamaliza! Ila kamalizia na "I think this is enough for your stomach" sasa sijaelewa anamaanisha alichoongea au ......?
  • Juu ya DOWANS: Kaulizwa itakuwaje asihusishwe kwenye mjadala huo ilhali kuna watu ndani ya CCM wameshasema waliojiuzulu ndo walipe? Kasema SINA MUDA WA KUJIBU SWALI HILO!
  • Juu ya urais 2015: Hata mimi nashangaa, miaka bado sana, kwanini tuanze kuongelea urais wa 2015? Waandishi acheni propaganda, msipoandika chokochoko hizi hakuna atakayehangaika nazo.
  • Mitikisiko ndani ya CCM ni ya muda tu, tutapita katika hali hii.
  • MAJIBU: Si kama napuuza jitihada za serikali juu ya suala la ajira kwa vijana, lakini hali ni mbaya sana. Nashauri tuvunje kanuni, serikali ikope fedha na ijenge viwanda tuweze kuwaajiri watanzania wengi. Fedha zipo!
  • Moses Mashalo kauliza juu ya mustakabali wa CCM kwa siku zijazo kufuatia hali inayoendelea kwa sasa ndani ya CCM.
  • KAMALIZA... Maswali yanafuata
  • Uchumi wa dunia upo taabani, taifa letu linakabiliwa na hali mbaya. Shilingi yetu inazidi kuporomoka vibaya. Inflation inazidi kuelekea kubaya zaidi. Kuna tatizo kubwa la ajira kwa vijana, kubwa sana. Vijana wakiishi katika hali hii tutakuwa tumekalia bomu la muda na itapelekea kuvunjika kwa amani. Ni vyema tukatafuta suluhu ya mambo haya.
  • Naomba vyombo vya habari tusaidie nchi yetu. Tunapoandika propaganda za chuki kwa nia ya 'kulipuana' tujue tunalipeleka taifa kubaya.
  • Sasa niseme rasmi, IMETOSHA. Sintoendelea kuvumilia kuchafuliwa na vyombo vya habari. Nitachukua hatua kali dhidi ya magazeti yatakayonichafua na vyombo vya habari vyote vinavyonichafua. Ukinichafua nitakupeleka kwenye vyombo husika na niseme uhuru usio na nidhami ni fujo. Uhuru wa vyombo vya habari umekuwa 'abused' sana.
  • Vijana mara nyingi ni radical, wasibezwe na wasilaumiwe kwa wanachofanya bali waelekezwe. Anayekiuka sheria asifumbiwe macho.
  • Vijana wa UVCCM tusiwaingilie, ni taasisi muhimu kwa ajili ya chama chochote cha siasa.
  • Sheria ni sheria, hakuna aliye juu ya sheria. Kama kuna sheria inavunjwa hakuna anayetakiwa kuangaliwa tu.
  • Gazeti flani linaloniandama lilishafikia hatua ya kusema ndo nahusika na maasi ya vijana wa UVCCM, ni uwongo na wala sihusiki kwa namna yoyote na vijana wa Arusha. Nilikuwa nje kwa matibabu, ningejuaje nini wanapanga vijana?
  • Sijakutana na rais Kikwete barabarani, waache kunichonganisha naye na waache kunichafua mbele za watanzania. Walishasema eti nagombea urais mwaka 2010. Naamini hata rais Kikwete anajua kuwa huu ni uzushi tu.
  • Masuala ya Chama huwa yanaishia kwenye vikao, hii ya kubomoana nje ya vikao hayana maana. Siwezi kukihujumu chama changu mwenyewe.
  • Kuna waliofikia kudai eti namhujumu Mhe. Rais. Wengine eti nna mpango wa kumpindua kwenye Halmashauri kuu ijayo. Sina mpango wa hujuma na hata mabaya ya rais Kikwete siyafahamu.
  • Toka nilipojiuzulu uwaziri mkuu nilikaa kimya, kimya ni hekima toka kwa Mwenyezi Mungu
  • Anaomba kutoulizwa maswali ambayo ni nje ya hoja anayoongelea.
  • Anaanza kuongea sasa...
  • Alishakaa ili aanze kuongea, kaondoka na inaelekea kama kuna jambo anaenda kuliweka sawa kwanza.
  • Ilitarajiwa angeanza saa 4 kamili lakini inaelekea ataanza saa 4 unusu, waandishi wapo wengi. Atajivua gamba?
=============
UPDATE
=============
Full text ya alichozungumza Lowasa


17.jpg 18.jpg 19.jpg 20.jpg 21.jpg

===================================================================
HOTUBA YA MBUNGE WA MONDULI, EDWARD LOWASSA KWA WAANDISHI WA HABARI MONDULI, OKTOBA 19, 2011

Date: Wednesday, 19 October, 2011, 22:28

NDUGU wana habari nimewaita katika mkutano huu leo kwa sababu moja kubwa, kutoa ufafanuzi kuhusu matukio ambayo yamekuwa yakitokea huku yakinihusisha mimi binafsi kwa namna ambayo sasa yanatishia ustawi na mshikamano wa kimaadili, kihistoria na kikazi miongoni mwa viongozi na baina ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ndugu wana habari, naamini mmekuwa mkifuatilia kwa karibu habari zinazoripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari zinazolihusisha jina langu na harakati kadha wa kadha chafu ambazo hata mimi mwenyewe ninayehusishwa nazo huwa nazisikia na kuzijua baada ya kuwa zimesharipotiwa katika vyombo hivyo vya habari.

Uamuzi wangu wa kukutana nanyi leo hauna makusudi ya kuzozana na vyombo vya habari wala kwenda kinyume na utamaduni wa kimaadili wa ndani ya chama changu unaotutaka viongozi kujadili masuala yanayokihusu chama chetu ndani ya vikao vyetu rasmi vya kimaamuzi bali kutoa ufafanuzi na angalizo kwa pande zote hizo mbili ambazo zinaguswa na matukio yanayoendelea kutokea leo hii.

Moja ya mambo ambayo yameligusa jina langu kwa namna hiyo ni lile linalonihusisha eti na kundi moja la wanasiasa ambao wamekuwa na mikakati ya kumhujumu mwenyekiti wetu wa chama, Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete. Hakuna shaka ni madai ya kipuuzi, kizushi na yenye malengo machafu.

Hawakuishia hapo sasa wamefikia hatua ya kuvitumia vyombo hivyo hivyo vya habari na kufikia hatua ya kudai kwamba nimeanza kuandaa orodha ya kile wanachokiita madhambi ya Rais Kikwete ambayo wanadai nimepanga kuyasoma wakati wa kikao kijacho cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (CCM).

Ninaamini kwa dhati kabisa kwamba, waandishi wa habari wanaofuatilia kwa karibu na kwa umakini mwenendo wa masuala ya kisiasa nchini wanatambua kwamba, watu wanaopenyeza taarifa hizi katika vyombo vya habari wanafanya hivyo kwa malengo ya kufikirika ya kujisafishia njia kisiasa.

Ni jambo lisiloingia akilini kunihusisha na kile kinachoitwa mikakati ya kumhujumu rais au chama ambacho mimi ni kada wake wa muda mrefu, mbunge anayetokana na chama hicho hicho na mtu ninayeiongoza Kamati nyeti ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na zaidi ya yote kiongozi wa ngazi mbalimbali za kisiasa na kiserikali nilizowahi kushikilia.

Kuhusu hili napenda kusema kwa uwazi kwamba, mbali ya ukweli kuwa sijapata kufikiria hata mara moja kuhusu hicho wanachokiiita mabaya au madhambi ya rais, sina na wala siijui hiyo wanayoitaja kuwa ni orodha ya mabaya ya namna yoyote dhidi ya Rais Kikwete.

Mbali ya ukweli kwamba huo ni uongo wa wazi, silika yangu kama mwanasiasa na mtu mwenye dhamana kubwa kwa watu wa Monduli na kwa taifa langu haiwezi kamwe kunituma nianze kupanga mikakati ya kumhujumu kiongozi wetu mkuu au chama ambacho kimenilea na mimi mwenyewe nikakitumikia kwa uadilifu na kwa juhudi kubwa pengine kuliko ilivyo kwa hao wazushi.

Ndugu wana habari, nitakuwa ni mtu wa mwisho kufikiria au kupanga kumhujumu mwenyekiti wetu wa chama na rais ambaye nimemuunga mkono kwa dhati kwa muda mrefu na kushirikiana naye katika harakati nyingi za kifikra na za kiuongozi katika ngazi mbalimbali na kwa miaka mingi. Nilipata kulisema hili na leo nalirudia tena. Mimi na na Rais Kikwete hatukukutana barabarani.

Tangu serikali ya Awamu ya Nne iingie madarakani kuna kundi la watu limekuwa likifanya juhudi kubwa kunigombanisha na Rais wakitumia kila aina ya hoja za kupikwa.

Kundi hilo ambalo sasa limekuja na uzushi mpya, ndilo ambalo mwaka juzi lilipenyeza ndani ya chama chetu na katika jamii hoja kwamba nilikuwa nimejipanga kugombea urais kwa tiketi ya chama chetu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, likidai kwamba nilikuwa na malengo ya kumpinga Rais Kikwete ambaye wakati huo alikuwa ndiyo kwanza anaelekea kukamilisha ngwe yake ya kwanza madarakani.

Katika kuthibitisha kwamba watu hao walikuwa na hila, nilipohojiwa na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam miezi kadhaa kabla ya Uchaguzi Mkuu nilijibu kwa kifupi nikisema, hatutukutana na Rais Kikwete barabarani.

Nayasema haya na kurejea baadhi ya mambo huku nikiwa na imani ya dhati kabisa kwamba, viongozi wenzangu ndani ya CCM na wale walio na nia njema na chama chetu na taifa hili, akiwapo Mwenyekiti wetu wa Taifa, Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete hawawezi kamwe kuamini au kushawishiwa na propaganda chafu zinazoendeshwa na kikundi kidogo cha wanasiasa hao kwa zaidi ya miaka mitatu sasa ambao malengo yao ya kisiasa yako wazi na yanayojulikana.

Kama hiyo haitoshi, wanasiasa hao hao baada ya kulitumia jina langu kama ajenda yao ya uzushi wa kila namna, sasa wameanza kunihusisha hata na matukio ya kisiasa kama yale yaliyotokea majuzi tu hapa Arusha.

Ndugu wana habari baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu sasa, nimeamua kuanza kuchukua hatua mbalimbali za kisiasa na kisheria ambazo naamini zitatoa majibu sahihi dhidi ya wale wote walio nyuma ya ajenda hizi chafu kwa lengo la kuweka kumbukumbu sawia ndani ya chama changu na kwa jamii nzima ya Watanzania ambao kwa muda mrefu wamelishwa mambo mengi ya kizushi na wakati mwingine ya hatari dhidi yangu.

Tayari nimepanga kuanza kuwasiliana na kuwasilisha malalamiko yangu kwa mamlaka husika zinazosimamia mienendo ya kimaadili na weledi wa kitaaluma wa vyombo vya habari kama vile Msajili wa Magazeti na Baraza la Habari Tanzania.

Kama hiyo haitoshi, baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu nimeshaanza kufikiria na kujipanga kuanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waandishi wa habari na wahariri ambao kwa makusudi wameamua kutumia vibaya uhuru wa habari ambao serikali imeutoa. Naamini sote tunakubaliana kuwa; ‘UHURU USIO NA NIDHAMU NI FUJO.'

Ndugu zangu wana habari napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa viongozi wa chama na wale wa serikali kumsaidia rais na chama chetu kwa kutimiza ipasavyo wajibu wao badala ya baadhi yao tena wakiwamo wale wenye dhamana nyeti kuwa vinara wa kutunga mambo ya kufikirika kama haya wanayofanya leo.

Viongozi wenye mawazo ya namna hiyo wanapaswa kutambua kwamba, muda adhimu wanaoutumia kubuni na kuzusha uongo kila kukicha mbali ya kuwavunjia heshima wao wenyewe unavidhalilisha vyombo vya dola ambavyo vinafanya kazi kubwa kuhakikisha hujuma za namna yoyote dhidi ya viongozi na taifa zinadhibitiwa.

Nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ya Bunge na mtu aliyepata kuwa Waziri Mkuu ninatambua na kuiheshimu kwa dhati kazi hiyo kubwa inayofanywa kwa weledi mkubwa na taasisi mbalimbali za dola zenye wajibu wa kuhakikisha ulinzi na usalama wa viongozi wetu na taifa kwa ujumla.

Ndugu wanahabari nazungumza nanyi baada ya kurejea nikitokea katika nchi za Nigeria, Malaysia, Singapore, India, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani ambako nilipata fursa ya kujifunza mambo mengi lakini moja muhimu likiwa ni namna vyombo vya habari (kwa maana ya waandishi wa habari) na wanasiasa wanavyotumia muda wao mwingi kujadili masuala yanayogusa maisha na maendeleo ya watu wao.

Tofauti na kile wanachofanya wenzetu hapa nyumbani, ninyi wanahabari na sisi wanasiasa tumekuwa tukitumia muda wetu mwingi kujadili watu na propaganda za kisiasa zisizo na tija wakati tukitambua kwamba, taifa linakabiliwa na changamoto nyingi kama zile za kuhamasisha uwekezaji wa ndani na nje ya nchi, kuimarisha mifumo ya utawala bora, kuporomoka kwa thamani ya shilingi kila kukicha, mdororo wa uchumi, tatizo kubwa la ajira kwa vijana, kushuka kwa kiwango cha elimu na ugumu wa maisha kwa ujumla. TUNAPASWA KUJISAHIHISHA.

AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA
 
Tuesday, 18 October 2011 21:38
0diggsdigg

lowassa-top.jpg
MILLYA ACHAFUA HALI YA HEWA CCM, ASEMA MAISHA YAKE YAKO HATARINI
Waandishi Wetu
WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa leo anatarajiwa kuzungumza na vyombo vya habari katika mkutano ambao utazungumzia mambo makuu matatu likiwamo suala la Kampuni ya kufua umeme ya Richmond ambalo lilisababisha ajiuzulu wadhifa huo, Februari 2007. Mkutano huo wa Lowassa unafanyika siku moja tangu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Arusha, James Millya atoe matamshi makali akiwatuhumu aliowaita watoto wa vigogo kwamba wanavuruga umoja huo huku akilalamika kwamba: “Maisha yake yapo hatarini.” Habari zilizopatikana jana kupitia kwa watu walio karibu na Lowassa zinasema, katika mkutano huo, Mbunge huyo wa Monduli (CCM), pia atazungumzia taarifa zinazomhusu ambazo zimekuwa zikichapishwa katika baadhi ya vyombo vya habari nchini.

Suala jingine ambalo linatarajiwa kuzungumzwa na kiongozi huyo ni kuhusu mgogoro ndani ya CCM mkoani Arusha, ambao unatokana na mgawanyiko miongoni mwa makada na viongozi wa chama hicho. “Pia anasema kwamba ataanzia pale alipoishia, siku ile alipozungumza bungeni kuhusu Serikali kufanya uamuzi mgumu lakini hakutakuwa na kumshambulia mtu,” alisema mmoja wa watu hao na kuongeza:

“Anasema (Lowassa) kwamba lazima aweke kumbukumbu sahihi kwa baadhi ya mambo ambayo yametamkwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa na viongozi wengine kwani amebaini kuwa uongo ukisemwa sana na kwa muda mrefu hugeuka kuwa ukweli.”
Hii ni mara ya kwanza kwa Lowassa kuitisha mkutano wa vyombo vya habari tangu alipojiuzulu kuzungumzia sakata la Richmond ambalo halikuwahi kupata hitimisho la kisiasa wala kisheria.

Lowassa pamoja na mawaziri wawili waliowahi kuwa na dhamana katika Wizara ya Nishati na Madini kwa vipindi tofauti, Nazir Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha walijiuzulu nyadhifa zao kwa kuwajibika, baada ya matokeo ya uchunguzi wa Kamati Teule ya Bunge la Tisa, iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Ujenzi.

Uchunguzi huo ulihusu kampuni tata ya kufua umeme wa dharura ya Richmond, ambayo ilishindwa kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa mkataba baina yake na Tanesco, hivyo kuhamishia majukumu yake kwa kampuni Dowans.

Mkutano wa Millya
Mkutano wa Lowassa unafanyika katika kipindi ambacho CCM kinakabiliwa na misukosuko ambayo imedhihirisha kuwapo kwa mpasuko mkubwa huku kukiwa na tofauti za wazi miongoni mwa makada na viongozi wake ambao katika siku za karibuni wamekuwa wakirushiana maneno nje ya vikao rasmi vya chama.
Jana, Millya naye aliingia katika malumbano hayo pale alipowaambia waandishi wa habari kwamba: “Watoto wa viongozi wa CCM na Serikali wamejitwika madaraka ya wazazi wao kinyume cha sheria za nchi.”

“Ninaomba kuwaonya watoto wa vigogo wenye tabia ya kuingilia mambo ya UVCCM na uendeshaji wa nchi kwamba hatutaruhusu na hatutavumilia watumie mamlaka tuliyowapa wazazi wao ili kutuvurugia jumuiya yetu,” alisema Millya na kuongeza:

“Haki hufuatana na wajibu lakini amani huletwa na haki. Niwaombe viongozi wetu wasikubali kutumia mamlaka kunyima watu haki zao kwani kwa kufanya hivyo ni kuhatarisha amani na utulivu wa muda mrefu wa nchi yetu.” Millya alitoa kauli hizo akitokea polisi kuhojiwa kutokana na matamshi yake ya Oktoba 10, mwaka huu katika mkutano wa hadhara kwamba polisi walizuia maandamano ya UVCCM kutekeleza shinikizo la mtoto wa kigogo mmoja.
Akizungumzia kuhojiwa huko, Millya alisema: “Ni muhimu sana mfahamu kwamba sijayumba na sitayumba kwani tuna safari ndefu ya kujenga demokrasia ya kweli na Uhuru wa kweli wa mawazo na maoni.”

“Uhuru wa utashi wa kisiasa, Uhuru wa kusimamia misingi na kanuni za chama chetu, jumuiya yetu (UVCCM) bila woga, wala kuyumbishwa na mtu yeyote hata akijaribu kutumia vyombo vya dola au taasisi binafsi ili nitoke kwenye hoja ya msingi ya kuhakikisha Tanzania huru inawezekana.”
Alisema mkoa wa Arusha na Kanda ya Kaskazini wanahujumiwa na kikundi kidogo cha watu wenye uchu wa madaraka na wenye lengo la kulinda maslahi yao binafsi ya sasa na ya baadaye.

Alitoa mfano wa tamko lililotolewa na Baraza la UVCCM Mkoa wa Pwani kwamba Rais wa 2015, kamwe hawezi kutokea Kanda ya Kaskazini kuwa ni uthibitisho kwamba vijana hao walitumiwa.

“Mbali na kwamba hili ni tusi kwa watu wa kaskazini wenye haki yao kikatiba kuwania nafasi ya uongozi wa juu wa nchi yetu, ni tusi pia kwa wapiga kura wa Tanzania wanaoamini katika demokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa,” alisema.
Alisema cha kushangaza mpake leo hakuna chombo chochote cha Serikali ambacho kimewahi kutoa tamko la kukanusha taarifa hiyo iliyounganishwa na taasisi moja ya juu serikalini.

Millya alisema kwa hali falsafa ya kujivua gamba yenye waasisi wake, ni mbinu madhubuti na endelevu za kuwapunguza nguvu baadhi ya watu wenye ushawishi mkubwa ndani ya CCM ili kuwazuia kugombea urais 2015.Alidai kuwa hivi sasa maisha yake yapo hatarini kutokana na kutumiwa ujumbe wa vitisho kupitia simu yake ya mkononi na kwamba ametoa taarifa polisi kuhusu suala hilo.

Kama walivyofanya, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangoro na Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Benno Malisa, Millya naye alimtuhumu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kwamba ndiye chanzo cha mitafaruku yote ndani ya CCM.

Hata hivyo, Nape alipoulizwa kwa simu Jumamosi iliyopita kuhusu shutuma nyingi kuelekezwa kwake alisema: “Sijui kwa nini haya mageuzi ya kujivua gamba yanapotajwa yanahusishwa na urais, hili si sahihi hata kidogo.” Nape alikuwa akijibu tuhuma Ole Nangoro ambaye alimshambulia hadharani, akikosoa utekelezaji wa falsafa ya kujivua gamba inayosimamiwa na Sekretarieti inayoongozwa na Katibu Mkuu, Wilson Mukama.

Kujivua gamba Falsafa ya kujivua gamba ni moja ya maazimio 24 yaliyopitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM ikiwataka watuhumiwa wa ufisadi kupima kisha kuachia nafasi zao za uongozi ndani ya chama.

Mmoja wa watuhumiwa hao, Rostam Aziz alishajivua nyadhifa zake ambazo ni ujumbe wa NEC na ubunge wa Igunga ambalo CCM ilifanikiwa kulirejesha kupitia kwa Dk Dalaly Kafumu katika uchaguzi mdogo uliomalizika hivi karibuni.

Habari kutoka ndani ya CCM zinasema taarifa ya utekelezaji wa maazimio 24 ya NEC likiwamo la kujivua gamba, inaandaliwa ili iwasilishwe kwenye kikao cha NEC ambacho kinaweza kufanyika mwishoni mwa mwezi huu au mapema mwezi ujao, kikitanguliwa na Kamati Kuu (CC). Imeandikwa na Mwandishi
 
inawezekana mzee anaachia jimbo! Lets wait and see!! Mtuhabarishe!!!
 
Back
Top Bottom