Lowassa amtisha Kikwete kujiokoa

KIM KARDASH

JF-Expert Member
Sep 21, 2011
5,139
1,139
WAKATI Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, akimgeuzia kibao Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, imebainika kwamba watuhumiwa wa ufisadi walitumia nguvu kubwa kujilinda zikihusisha mchezo mchafu ulioratibiwa na familia ya mmoja wa watuhumiwa anayepaswa kujivua gamba, Raia Mwema, imeelezwa.
Lowassa, ambaye amekuwa akijinadi kwamba Kikwete ni rafiki yake ambaye "hawajakutana barabarani", alisimama ndani ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, kilichomalizika, wiki iliyopita, mjini Dodoma, na kumshambulia Rais Kikwete waziwazi, na kuaminisha umma kwamba kashfa zote zinazoelekezwa kwake Kikwete anazifahamu.


Lowassa azungumza NEC:

Akiwa mmoja wa viongozi ambaye muda wake wa kujiuzulu kwa ‘hiari' umekwisha, Lowassa alizungumza katika NEC na kulalamika kwamba anaonewa na si kweli yeye ni fisadi; huku akielekeza moja kwa moja mashambulizi kwa Kikwete kwa hasira.
Imeelezwa kwamba mashambulizi ya Lowassa kwa Kikwete, yalilenga kumtisha na kupotosha umma kuhusu dhana nzima ya ufisadi, hasa pale alipokumbushia mchakato wa kutafuta mgombea urais wa CCM mwaka 2005, ambako ilielezwa kwamba Mwenyekiti mstaafu Benjamin Mkapa ndiye aliyeokoa jahazi.
"Lowassa kumdhalilisha Rais mbele ya wajumbe wa NEC ni kosa linalohalalisha kuchukuliwa hatua, lakini pia wizi hauwezi kuhalalishwa kwa kumsema hakimu. Kikwete pale alikuwa hakimu, sasa unasema hakimu naye si msafi ili akusamehe ama akuhukumu?" alihoji mjumbe mmoja wa NEC ambaye yuko serikalini.
Mjumbe huyo amesema ukimya wa Kikwete unaweza kuwa na tafsiri nyingi, lakini kubwa ni ama amemuogopa Lowassa ama anajiandaa kuchukua hatua madhubuti kwa kutumia ushahidi uliokusanywa na vyombo vyake.

Simu zapigwa Lowassa akizungumza:

Hata hivyo, taarifa za kiuchunguzi kutoka vyanzo mbalimbali vya habari zinabainisha kuwa wakati wote ambao Lowassa alikuwa akizungumza, kulikuwa na simu zilizokuwa zimepigwa kwa watu maalumu nje ya kikao hicho ambazo watu hao walikuwa wakimsikiliza moja kwa moja kutoka kikaoni.
Baada ya Lowassa kumaliza kuzungumza, inaelezwa kuwa simu hizo ziliendelea ‘kubaki hewani' na alipoanza kuzungumza Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, naye alikuwa akisikika moja kwa moja kutoka kwenye kikao hicho cha NEC. Sumaye alikuwa ameketi jirani na Lowassa ndani ya kikao hicho cha NEC kilichoketi Novemba 23 na 24, 2011.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kwa ustadi mkubwa maelezo ya Sumaye yalipindishwa na waandishi wa habari maalumu waliopata taarifa kutoka kwa mtu maalumu aliyekuwa akisikiliza kikao cha NEC kupitia simu na ikaripotiwa kuwa "Sumaye amemtetea Lowassa."
Watu waliokaribu na Sumaye wanaeleza kuwa Waziri Mkuu huyo wa zamani hadi sasa hakufurahishwa na upotoshaji huo uliofanywa dhidi yake.

Sitta anyimwa nafasi kumjibu Lowassa:

Katika kile kinachoonyesha kushindwa kuvumilia kauli za Lowassa kuhusu kashfa ya Richmond ndani ya NEC, aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, aliomba nafasi ya kuzungumza akionekana kutaka kufichua zaidi yaliyofichwa kuhusu uhusika wa Lowassa na kashfa ya Richmond.
Hata hivyo, Sitta hakupewa nafasi hiyo na Kikwete ambaye alikuwa akiendesha kikao hicho na hivyo maelezo ya Lowassa kwamba hahusiki yakabaki salama. Inaelezwa kuwa ni Mkapa aliyemshawishi Kikwete kutowapa nafasi wengine kuzungumza baada ya Lowassa na Sumaye kuzungumza.
Wengine ambao kutokana na uamuzi huo walikosa nafasi ya kuzungumza ni pamoja na Kingunge Ngombale Mwiru, anayetajwa kuwa mtetezi mkubwa wa Lowassa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja
Katika kikao hicho, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, alielezwa kusimama baada ya Lowassa, kuonyesha hasira zake kwa Mwenyekiti Kikwete na wajumbe wa Sekretarieti, kuhusiana na kuyumba kwao katika kufanya maamuzi ya utekelezaji wa uvuaji gamba na kuruhusu mjadala wa hoja iliyokwisha kufanyiwa maamuzi na NEC.
Ni katika kikao hicho ambacho Sumaye anaelezwa kutaka ufafanuzi kuhusu kauli za wajumbe wa Sekretarieti, akiwamo Katibu wa Uenezi na Itikadi, Nape Nnauye, na Naibu Katibu Mkuu, John Chiligati ambao walizunguka nchi nzima kuelezea dhana ya uvuaji gamba kwa kuwataja majina baadhi.
"Sumaye alikua mkali kwa kuigeuzia kibao meza kuu kutokana na kuonyesha ugeugeu baada ya kumruhusu Lowassa. Alisema kama Nape na Chiligati walikosea, basi, wachukuliwe hatua na kama waliyosema ni maamuzi ya NEC, basi, yatekelezwe badala ya kuyumba. Kauli yake ilipotoshwa sana na nyie waandishi kwa maslahi yenu," anasema mjumbe mmoja wa NEC.
Viongozi wengine wastaafu ambao wameelezwa kuonyesha mshangao mkubwa wa hali ya mambo ni Rais Mstaafu Benjamin Mkapa ambaye amenukuliwa wiki hii na mmoja wa watu walio karibu naye akiwashangaa Lowassa na wenzake kushangilia ushindi, akisema, "huu ni ujinga kwa mtu kusema haya maazimio ya NEC yememsafisha Lowassa".
Hata hivyo, Mkapa anatajwa kuwa miongoni mwa wastaafu ambao wameonyesha kutopendelea dhana na uvuaji gamba, kwa maelezo kwamba ikitekelezwa kwa dhati, itawamaliza wanasiasa wengi akiwamo yeye binafsi ambaye amekuwa akiandamwa na tuhuma kadhaa za ufisadi, zinazohusishwa na uanzishaji wa kampuni ya ANBEM Limited, akiwa madarakani. Mkapa na mkewe Anna wameifilisi kampuni hiyo kwa hiari.

Makongoro Nyerere afichua msimamo:

Taarifa za kina zinaeleza kuwa Makongoro Nyerere, mtoto wa Baba wa Taifa, ambaye pia kwa sasa ni Mwenyekiti wa CCM, mkoani Mara, hakuwa akificha fikra zake kabla na wakati wote wa vikao vya NEC.
Makongoro anatajwa kueleza bayana kuwa kama akipewa nafasi ya kuzungumza ndani ya NEC na hasa kwa kuzingatia kuwa uamuzi wa kuvua gamba umeyumba, basi, angetamka: "Natoka mimi na kama mkiamua kuwatoa baadaye, nitarudi"; akiwa na maana ya kujiondoa kwenye wadhifa wake hadi wahusika wa ufisadi watakapong'olewa na yeye atakuwa tayari kurudi.
Makongoro ndiye katika kikao cha NEC kilichotangaza kujivua gamba alitoa mashambulizi makali dhidi ya wahusika ambao ni Edward Lowassa, Andrew Chenge na aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Azizi, ambaye alijiuzulu ndani ya muda wake wa hiari kama walivyopewa na CCM.
Makongoro kwenye kikao hicho cha NEC alinukuliwa akimwambia Kikwete kwamba japo yeye ni Mwenyekiti wa Taifa, yeye (Makongoro) naye ni Mwenyekiti wa Mara na kwamba NEC ndio waajiri wa Mwenyekiti Taifa.
"Akasema anapokaa Mwenyekiti wa Taifa ni mahala patakatifu na kwa ajili hiyo pasingeweza kusogelewa na shetani, hata kama siku moja Mungu alipata kukutana na shetani barabani.
Uvuaji gamba kwa lazima wasubiriwa
Msingi wa dhana ya kujivua gamba umejengwa katika azimio la NEC iliyofanyika Aprili 10 na 11, 2011, kwa lengo la kukipa chama hicho sura ya mageuzi na taswira mpya.
Azimio hilo la NEC linasema: "Viongozi wanaotuhumiwa na ufisadi watafakari, wajipime na kuchukua hatua wao wenyewe kwa maslahi ya chama, wasipofanya hivyo chama kiwawajibishe bila kuchelewa."
Taarifa zilizotolewa mara baada ya kikao cha NEC, wiki iliyopita, zinaeleza kuwa kazi ya kuwandoa wahusika sasa ipo chini ya Kamati Kuu, kupitia Kamati ya Maadili.
Kauli ya Kikwete kuhusu Lowassa
Kwenye kikao hiki cha NEC, Lowassa ambaye alijiuzulu uwaziri mkuu kwa kashfa ya zabuni iliyotolewa kwa kampuni ya kufua umeme ya Richmond, alijitetea.
Utetezi wa Lowassa ni pamoja na kujieleza kuwa alitaka kuvunja mkataba wa Richmond kwa kumpigia simu Rais Kikwete.
Ni kutokana na utetezi huo wa Lowassa na wajumbe wengine kutaka kumjibu papo hapo, taarifa zinaeleza kuwa Rais Kikwete alisikika akisema usiwe na haraka tutawaita kwenye Kamati ya Maadili ya chama chetu tukiwa na vielelezo vyote ili mtoe utetezi wenu. Tukishachukua hatua tutawaelezeni wajumbe wa NEC nyeupe na nyeusi. Safari hii tunataka "Natural Justice" ichukue nafasi yake.

Mchezo mchafu UVCCM Dodoma:

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, wabunge zaidi ya wanne akiwamo Saidi Mtanda wa Mchinga, mkoani Lindi na Dk. Hamis Kingwangala wa Nzega, mkoani Tabora, ni miongoni mwa waliokuwa tayari kufichua mchezo mchafu wa matumizi ya mamilioni ya fedha kuhonga baadhi ya vijana wa Umoja wa Vijana wa CCM.
Wakati mchezo huo unafanyika wabunge hao na wenzao walikuwapo Dodoma ambako kabla ya vikao vya CCM walikuwa wakishiriki shughuli za Bunge.
Inaelezwa ya kuwa hata hivyo, licha ya kuwa tayari wabunge hao walishindwa kupewa nafasi ya kufichua siri hiyo mbele ya NEC-CCM, inayotajwa kuhusisha familia ya kigogo huyo kupitia kwa mtoto wake mmoja.
Mtoto huyo ambaye kwa sasa jina lake tunalihifadhi kutokana na kushindwa kumpata kwenye simu yake ya mkononi, anatajwa kuwa mmoja wa walipaji posho kwa vijana wa CCM inayofikia hadi Sh milioni moja kwa mjumbe mmoja, fedha ambazo zinatajwa kutoka katika familia yake na watu wengine wasiojulikana.
Mtoto huyo pia anadaiwa kuwa kambi moja na Mwenyekiti wa UVCCM mkoani Arusha, James ole Millya, katika vurugu za mara kwa mara zilizokuwa zikiibuka UVCCM-Arusha ambazo hata hivyo, zilisuluhuhishwa na Steven Wassira, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.
Kwa mujibu wa taarifa za uhakika, alikuwa Nape Nnauye (Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM) aliyemtaka Mwenyekiti Rais Jakaya Kikwete kumpa mwongozo kuhusu kundi la vijana wa CCM kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania waliosafirishwa, kulipwa posho nono na gharama za malazi, wako Dodoma kwa shughuli gani na kwa sababu gani.
Nape anatajwa kueleza bayana kwamba ushahidi wa vijana hao kuwapo Dodoma kwa kuitwa na kundi la mafisadi upo, ushahidi ambao hata Kikwete anatajwa kuutambua na baada ya Nape kuhoji hivyo, Kikwete alimhoji Beno Malisa; fedha hizo wamezipata wapi.
Beno, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa UVCCM anatajwa pia kushambuliwa na mawaziri, William Lukuvi na Steven Wassira ambao hata hivyo walikuwa wakitoa lugha zenye mwelekeo wa kumuonya na si kutaka ashughulikiwe kwa mujibu wa kanuni za UVCCM au chama hicho.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa baada ya Malisa kupigwa mashambulizi ndani ya siku ya kwanza ya vikao hivyo, alifikisha taarifa hizo kwa wenzake waliosafirishwa "kwa kazi maalumu" Dodoma na baadhi yao walitishika na kuanza kufunga safari ya kurudi mikoa walikotoka.
"Vijana hawa walisafirishwa kuletwa hapa kwa kazi kubwa mbili. Kwanza kuna maneno waliambiwa uongozi wa UVCCM unavunjwa, lakini pili kuna hofu kwamba wale viongozi mafisadi watang'olewa katika kikao hicho cha NEC.
"Kwa hiyo walikuja kutibua masuala hayo mawili kwa vitisho kwamba kama ingekuwa hivyo wangehamia Chadema, lakini baada ya Rais Kikwete kusema kwenye kikao wasitutishe, waende hata kesho baadhi ya vijana waliogopa wakakimbia wengine usiku kurudi walikotoka," anaeleza mtoa habari wetu.
Katika mchakato huo wa mawasiliano, gazeti hili limeshuhudia ujumbe wa simu ya mkononi kutoka kwa mmoja wa viongozi wa vijana katika moja ya mikoa ya Kanda ya Juu Kusini, ambaye pia ni mwalimu katika moja ya vyuo vikuu nchini.
Kiongozi huyo ndiye aliyekuwa akisambaza ujumbe wa kuita vijana wafuasi wa viongozi wanaopaswa kujiuzulu ili wakusanyike Dodoma ambapo kwa mikoa ya mbali kama Kigoma, Raia Mwema imeelezwa kuwa tiketi za ndege kwa vijana waliokuwa tayari kuelekea Dodoma zilikuwa zikipatikana kwa masharti tu, ukifika Dodoma uungane na kundi hilo.
Taarifa zinabainisha kuwa bajeti ya mamilioni ya fedha ilitengwa na kutumika katika kugharimia vijana hao kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mpango huo pia ulikuwa ukiratibiwa na kijana mwingine ambaye ni mtumishi katika moja ya kampuni za aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Azizi.
Hujuma zilianza mapema
Taarifa za kiuchunguzi zinaelekeza kuwa mpango wa kuhakikisha mchakato wa kujivua gamba unahitimishwa kwenye kikao cha NEC uliandaliwa na kundi la watuhumiwa wa ufisadi, ukiratibiwa na mmoja wa wajumbe wa Sekretariati ya CCM (jina linahifadhiwa).
Kigogo huyo ndani ya sekretariati ndiye aliyepewa jukumu la kuandaa waraka maalumu kuhusu hali ya kisiasa ambamo ndimo masuala ya kujivua gamba na mengine yanapaswa kuhusishwa.
Kwa mujibu wa taarifa za uhakika kutoka kitengo cha maadili, jukumu la kuandaa waraka huo lililikuwa la kitengo hicho lakini baadaye lilikasimiwa na mjumbe huyo wa sekretariati, ambaye anadaiwa kufanya ‘uchakachuaji' ili kupenyeza matakwa ya mtandao wa kifisadi.
Hata hivyo, taarifa za kina zinabainisha kuwa waraka huo ulikataliwa mara kadhaa na Kikwete ambaye alikuwa anaukataa kupitia kwa Katibu Mkuu, Wilson Mukama.
Kutokana na kiongozi huyo kijana wa sekretariati kusumbuliwa kila mara kwa kurudishwa akatengeneze vizuri waraka huo; huku akishindwa kujua yalikuwa ni maagizo ya Kikwete na si Mukama, kuna wakati anatajwa kutishia kujiuzulu kutokana na kusumbuliwa akiamini ulikuwa ni usumbufu unaosababishwa na Mukama pekee.
Taarifa zinabainisha kuwa ingawa hatimaye alifuta maelezo yenye kuhujumu mpango wa kujivua gamba ndani ya waraka huo kama walivyotaka watuhumiwa wa ufisadi, lakini alikuwa akichomekea mawazo hayo wakati alipokuwa akifanya uwasilishaji kwenye vikao husika, vikiwamo vya Kamati ya Maadili iliyoketi kabla ya Kamati Kuu.
Mikakati ya kubadili upepo
Kumekua na juhudi kubwa za kubadili vita ya ufisadi kwa kuiwekea kinga ya kuwa chanzo chake ni vita ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015, ukihusisha watu wanaotajwa kuwania kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
Juhudi hizo zinazoendeshwa kwa gharama kubwa, zinalenga kuwasafishia njia watuhumiwa wa ufisadi ili kuweza kuingia katika mbio za urais na hatimaye kuingia madarakani baada ya Kikwete kwa gharama zozote zile.
Madai hayo yameanza kwa kujaribu kuuaminisha umma kwamba chimbuko la hali mbaya ya kisiasa ndani ya CCM ni wanamtandao walioshiriki kumpitisha mgombea Jakaya Kikwete mwaka 2005.
Katika kuuaminisha umma, watuhumiwa wa ufisadi wamefanikiwa kuwaaminisha watu kwamba tuhuma dhidi yao ni za kupikwa na kwamba baada ya kumpitisha Kikwete na baada ya kuwa na hakika ya ushindi dhidi ya Upinzani, wanamtandao mmoja mmoja walianza kujitathimini juu ya uwezekano wa wao wenyewe kuwania urais baada ya Kikwete.
Vinara wa kundi hilo walikuwa Edward Lowassa, Samuel Sitta, Rostam Aziz, Getrude Mongella, Zakia Meghji, Abdulrahman Kinana, Bernard Membe, Juma Jamaldin Akukweti (sasa marehemu), Kingunge Ngombale Mwiru, Philip Marmo, Emmanuel Nchimbi, Ali Karavina, Juma Mwapachu, Henry Shekifu, Ponsian Nyami, Makongoro Mahanga, Nazir Karamagi, Stephen Wassira na Sophia Simba.
Sasa maelezo ya watuhumiwa yanaanza kulikumbushia kundi hilo kwa kudai kwamba, kundi hilo lilikuwa pia likijipanga kwa ajili ya nafasi karibu zote za uongozi wa juu wa serikali na mihimili mingine baada ya uchaguzi wa mwaka 2005.
Pamoja na kuwa sababu hasa ya minyukano ndani ya CCM inapotoshwa, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma ya kuwa "hali ya siasa ndani ya chama ni shwari lakini si shwari sana".
Kwa mujibu wa Mukama, makundi kinzani yameshamri ndani ya chama hicho na sasa yanapangana safu za uongozi kwa kutumia fedha jambo ambalo alisema ni kansa ambayo inakitafuna chama hicho polepole.
Alisema kwa ajili hiyo chama kilikuwa kimeamua katika kikao cha NEC kutafuta dawa ya tatizo hilo na kwa kuanzia tuhuma zote za viongozi wote zitashughulikiwa kwa ngazi mbalimbali chini ya kamati za maadili husika na ambao tuhuma zao zitathibiti watachukuliwa hatua bila kuchelewa.
Akinukuu waraka wa NEC, Mukama alisema: "Kwa kutambua kuwa suala la ufisadi limekuwa mzigo mkubwa sana kwa Chama cha Mapinduzi licha ya juhudi kubwa ambazo Serikali ya CCM imezifanya katika kupambana na tatizo hilo, NEC iliamua kuwa viongozi wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi watafakari, wajipime na kuchukua hatua wenyewe kwa maslahi ya Chama. Wasipofanya hivyo Chama kiwawajibishe bila kuchelewa.
"Ni dhahiri kuwa azimio hili lililenga viongozi wote wa Chama, katika ngazi zote cha chama chetu, kuanzia ngazi ya Taifa hadi Tawi. Ni dhahiri pia azimio hilo lilikusudiwa liwe sehemu ya utamaduni wa kusimamia maadili ya viongozi na wanachama wa chama chetu, yaani kwamba viongozi au wanachama, wanavunja maadili watachukuliwa hatua zinazostahili bia kuchelewa.

"Hali ilivyo hadi sasa, takriban miezi saba baada ya azimio hilo kupitishwa hatujapata mwitiko wa kuridhisha kutoka kwa viongozi wa ngazi yoyote ambao ni walengwa wa azimio hilo. Bila shaka wakati sasa umefika kwa chama kutekeleza ile sehemu ya pili ya azimio husika kwa kuwawajibisha wahusika. Lakini utekelezaji wake utafanyika vipi ili haki ionekane inatendeka? Jibu ni kwamba utekelezaji huo hauna budi ufanyike kwa kufuata utaratibu uliowekwa na kanuni za CCM za uongozi na maadili."
Aliongeza Mukama: "NEC imeagiza kupitia Kamati za Usalama na Maadili zianze mara moja mchakato wa kutekeleza azimio hilo kwa mujibu wa kanuni na taratibu na vilevile kwamba zoezi hilo lifanyike bila kuchelewa." Kauli hiyo ya NEC ilikuja siku moja baada ya mmoja wa watu ambao wamekuwa wakituhumiwa kwa ufusadi Lowassa kuzungumza mkutanoni akisema alikuwa ametuhumiwa sana kwa kuitwa fisadi ili hali yeye si fisadi na kwamba alijiuzulu katika kashfa ya Richmond kulinda heshima ya CCM na serikali yake.
Aidha ilikuja baada ya NEC kutangaza ya kuwa ilikuwa imemvua madaraka Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kirumbe Ng'enda, ambaye alikuwa anatuhumiwa kuvuruga zoezi la kura za maoni katika chaguzi za wabunge na madiwani mkoani kiasi cha kuwashusha baadhi ya wagombea waliopata kura nyingi. Uamuzi huo umeelezwa kuwa ni, "kuchukulia hatua dagaa na kuacha mapapa."
Wakati tukienda mitamboni, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama, amekutana na waandishi wa habari na kusema hakuna aliyesafishwa katika vikao vya chama hicho mjini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mukama amesema baadhi ya vyombo vya habari vimepotosha maamuzi ya vikao vya juu vya CCM kwamba vimesafisha watuhumiwa wa ufisadi, wakati kinachoendelea ni mchakato wa kuwachukulia hatua.
Mukama amesema kwa sasa Kamati ya Maadili na Usalama Taifa, imepewa nguvu zaidi na kuwa Tume ambayo itakuwa na uwezo wa kuwachukulia watu hatua moja kwa moja bila kusubiri vikao vya juu.
Akirejea maamuzi ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) na hotuba ya Mwenyekiti wa chama hicho, Jakaya Kikwete, Mukama alisema Kamati ya Maadili na Usalama itawaita watuhumiwa na kuwataka wajitetee kabla ya kufanya uamuzi.
Alisema kamati hiyo inaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, ikiwa na wajumbe wengine wakiwamo wawili kutoka Zanzibar na wawili kutoka Bara na yeye akiwa mjumbe mpya aliyeingizwa katikia utaratibu mpya.
"Mhusika ataitwa na kuhojiwa, badala ya kumhoji kwenye NEC ambayo ina watu wengi ambao mtu asiye na kosa anaweza kuhukumiwa kwa hisia za kisiasa ama mhalifu anaweza kupona kwa hisia.
"Kuhusu maadili tumekubaliana kutokuwa na ajizi katika kupambana na rushwa, viongozi wajitafakari na kujiwabisha wenyewe, wasipofanya hivyo chama hakitasita kuchukua hatua. Katika kufanikisha hilo, tumemua kuiongezea nguvu kamati ya maadili na kuibadilisha na kuwa tume kamili yenye watu 14 kutoka 12 na kuipa mamlaka ya kuamua bila kusubiri vikao," alisema Mukama.
Alisema mabadiliko hayo yanalenga katika ngazi zote pamoja na kuwa Tume ya Maadili na Usalama itakuwa moja tu kitaifa na katika ngazi ya mikoa na wilaya zitaendelea kuwa Kamati ya Maadili na Usalama ambazo nazo zitakuwa na mamlaka ya kufanya maamuzi moja kwa moja.
Mukama alisema CCM haikukurupuka katika uamuzi wake wa kufanya mageuzi na kujisafisha, na kwamba kila jambo litafanyika kwa umakini wa hali ya juu, ikiwa ni pamoja na utafiti uliofanyika ndani na nje ya nchi.
 
Back
Top Bottom