Liyumba akwama Mahakama Kuu

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
MKURUGENZI wa zamani wa Utawala na Utumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, ataendelea kutumikia kifungo cha miaka miwili jela kama alivyohukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali rufaa yake.

Akisoma hukumu hiyo iliyochukua zaidi ya saa mbili katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana, Jaji Emilian Mushi alisema amezingatia maelezo ya pande zote husika, ambazo ni Jamhuri na utetezi wa mrufani na kujiridhisha bila wasiwasi wowote kuwa rufaa ya Liyumba iliyo mbele yake haina msingi wowote.

Aidha, jaji alisema kipengele cha adhabu ya kifungo badala ya faini kilichoelezwa na mawakili waandamizi wa Liyumba; Onesmo Kyauke na Majura Magafu, kama msingi mmojawapo wa rufaa hiyo, hakina nguvu ya kuifanya mahakama ibadilishe hukumu ya kifungo iliyopo kwa kuwa ndiyo ya juu iliyostahili.

Jaji Mushi alisema, “Kwa kuzingatia hoja za upande wa Jamhuri na zile za utetezi, bila wasiwasi wowote wa kisheria, ninaiona rufaa hii kuwa haina msingi wowote na hivyo kuifunga kwa kusimamia hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyotolewa kwa kufuata uamuzi wa Mahakimu Waandamizi wawili kati ya watatu, uliomtia mrufani hatiani”.

“Hata hivyo, pamoja na Mahakama ya Kisutu kumtia Liyumba hatiani, nimejiridhisha pia kuwa hukumu ya kutumikia kifungo cha miaka miwili jela badala ya ile ya kulipa faini ndiyo inayomfaa kutokana na unyeti wa shitaka alilohukumiwa.

“Kwa maana hiyo, ninasisitiza kifungo hicho kiendelee kwa kuwa ndiyo adhabu ya juu inayomstahili kisheria kutokana na uhalisia wa kosa lake, ikiwa ni pamoja na madhara ambayo ameyasababisha kwenye uchumi wa taifa hili na jamii kwa ujumla.”

Akitoa ufafanuzi kuhusu hukumu yake hiyo ambayo wakati wote alisisitiza kuwa imezingatia maslahi ya taifa na ya Liyumba mwenyewe, Jaji Mushi alisema, kisheria na kwa kufuata ukweli kwamba alistahili adhabu kali sana kati ya mbili zilizokuwa zikimkabili, hana uwezo wa kuiingilia wala kuibadili na kwamba suala linalomstahili mrufani huyo kwa sasa ni kuendelea kutumikia kifungo hicho. “Ni vema ikaeleweka kwamba mahakama yoyote hailazimishwi na mtu ye yote wala sheria yenyewe kumwamuru mshitakiwa ye yote wa makosa kama haya alipe faini badala ya kumfunga, eti kwa sababu adhabu inayompasa ina mbadala,” alisema Jaji Mushi na kuongeza:

“Na kama kosa ni kama hilo la Liyumba la kutumia madaraka na ofisi ya umma vibaya, sheria inaelekeza adhabu iliyojuu kuliko nyingine kati ya zile zinazopendekezwa, ambapo kwa suala hili ni ya kifungo.”

Hata hivyo, Jaji Mushi, kama ilivyokuwa kwa mahakimu wa Kisutu, alitupilia mbali utetezi wa Liyumba kuwa alikuwa anatekeleza maagizo ya aliyekuwa Gavana Dk. Daud Ballali wakati wa kusimamia mradi huo.

Jaji alisema Liyumba ndiye aliyekuwa kiungo mkuu katika mradi huo na alipaswa kumshauri gavana kufuata taratibu na sheria za benki ambazo ziliwataka wote kwa pamoja kupata kibali cha Bodi ya Wakurugenzi kabla ya kufanya mabadiliko waliyoyafanya.

Alisema amejiridhisha bila kubaki na shaka yoyote kwamba Mahakama ya Kisutu ilisikiliza ushahidi uliotolewa na pande zote mbili; ya Jamhuri na utetezi na hivyo kufanya uamuzi wake kwa kuzingatia sheria iliyokuwa ikiwaongoza hadi kutoa hukumu husika, ambayo yeye kama Jaji msikiliza rufaa anaiona sahihi.

Vigezo vikuu vya rufaa hiyo iliyowasilishwa na mawakili Kyauke na Magafu ni pamoja na kilichodai kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haikuzingatia wala kupitia vizuri ushahidi uliotolewa na upande wa utetezi na hivyo kukosea kisheria kumtia hatiani Liyumba pamoja na kumhukumu kifungo gerezani.

Kigezo kingine ni cha adhabu iliyochaguliwa na mahakimu husika ya kumwamuru akae gerezani kwa miaka miwili badala ya kumtoza faini.

Hata hivyo, baada ya hukumu hiyo kutolewa, wakili Kyauke alisema anakubaliana nayo na hana ubishi mwingine wa kisheria juu ya maamuzi hayo.
 
It is a good precedent kwamba wakili anatambua tatizo katika kuframe rufaa yake na kutotaka kuendelea na malumbano yasiyo na tija.
 
Back
Top Bottom