Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,316
- 33,125
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba Waandishi Wetu SIKU moja baada ya Mahakama Kuu kusajili tuzo ya malipo ya Sh111 bilioni kwa kampuni ya Dowans, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, amemshauri Rais Jakaya Kikwete kumwajibisha Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na watendaji wake kwa kuisababishia nchi hasara hiyo. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Profesa Lipumba alisema kwamba Ngeleja na watendaji walioko chini yake ndio waliosababisha hasara hiyo ambayo sasa Serikali inapaswa kulipa hivyo ni lazima wawajibishwe mara moja. Wakati huu ambao Serikali imeshindwa kutatua tatizo la umeme, tunaongezewa gharama za kesi. Hili ni ombwe la uongozi ndani ya Serikali ya CCM, tangu Rais, mawaziri na watendaji wake. Nashangaa bado viongozi waliosababisha yote haya wako madarakani, alisema Profesa Lipumba.Juzi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilibariki malipo kwa Dowans baada ya kusajili tuzo iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC), dhidi ya Tanesco na kampuni hiyo ya kufua umeme.Kwa uamuzi huo, Tanesco sasa inatakiwa iilipe Dowans kiasi cha Sh 111 bilioni badala ya Sh 94 bilioni za awali kwani inatakiwa kuilipa fidia hiyo na riba ya asilimia 7.5. Profesa Lipumba alisema tukio hilo ni matokeo ya ufisadi ndani ya Serikali kwa sababu Dowans ilitokana na mkataba wa Richmond ambao tangu mwanzo, Tanesco waliupinga, lakini baadhi ya viongozi wa Serikali wakashinikiza. .. Aishukia kampuni ya Rex Attorney Vilevile, Profesa Lipumba aliilaumu kampuni ya uwakili ya Rex Attorney ya jijini Dar es Salaam kwa kile alichoeleza kuwa ilicheza mchezo wa kimaslahi pale ilipoishauri Tanesco kuvunja mkataba na Dowans kwa madai kuwa haukuwa halali huku ikiisaidia kampuni hiyo kupata mkopo katika benki ya Stanbic. Tanesco waliitumia Rex Attorney kupata ushauri wa kuvunja mkataba wa Dowans na Tanesco, lakini Rex hao wakaandika tena barua kwa Benki ya Stanbic ikitaka Dowans ikopeshwe Dola 20 Milioni za Marekani. Hawa ndiyo waliosababisha tushindwe kesi, alisema Profesa Lipumba. Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema hatma ya Tanzania sasa iko mikononi mwa wananchi hivyo, wanapaswa kutambua kuwa nchi inanyonywa na watu wachache. Haya ni matokeo ya ubinafsi wa viongozi, wanafanya mambo kwa manufaa yao wenyewe na wala sio kwa faida ya taifa, alisema Makulilo.Alisema kama wananchi wataamua kusimamia rasilimali za taifa, viongozi wataongoza kwa umakini katika kusaini mikataba ya kibiashara.Profesa Peter Maina alisema hakuna haja ya Dowans kulipwa fedha hiyo kwani tangu mwanzo, mkataba wa Tanesco na Richmond, ulikuwa wa mashaka. Alisema uzoefu umeonyesha kuwa kumekuwapo na mikataba mingi mibovu nchini hivyo, kukubali kuilipa Dowans, ni kuingia gharama zisizokuwa za lazima. Mvungi ataka Dowans wasilipwe Naye kiongozi wa wanaharakati walioishitaki Dowans isilipwe na kushindwa kesi, Dk Sengondo Mvungi, alisema kitendo cha Mahakama Kuu kukubali kusajili tuzo iliyotolewa na ICC ni kukubali kulipa deni, jambo ambalo mtandao huo ulipinga.Alisema malipo hayo ni ufisadi wa waziwazi na yakitekelezwa, maana yake Serikali imehalalisha dhuluma dhidi ya wananchi wake. Kitendo cha Mahakama Kuu kukubali kusajili tuzo hiyo kimetuangusha sana, kwa sababu walijua wazi kuwa mwisho wa kesi hiyo ni kuilipa Dowans. Huu ni ufisadi na ni sawa na kuhalalisha rushwa ndani ya Serikali. Tunawaomba wananchi wapinge kwa nguvu zote malipo hayo, alisema Dk Mvungi. Kwa mujibu wa Dk Mvungi, mkataba tata ulioingiwa kati ya Richmond na Tanesco, bado unaendelea kulitafuna taifa kwani ndio uliorithiwa na Dowans na sasa kampuni ya Symbion.Symbion ni mrithi wa Richmond na Dowans, hivyo mwisho wake ni mahakamani tena. Wananchi wanapaswa kuwa makini na wakemee dhuluma hiyo,aliongeza. Novemba 15, 2010, ICC iliiamuru Tanesco iilipe Dowans fidia ya Sh 94 bilioni kwa kuvunja mkataba baina yake na kampuni hiyo kinyume cha sheria. Kufuatia uamuzi huo wa ICC, Januari 25, 2011 Dowans iliwasilisha maombi mahakamani hapo ikiomba tuzo yake hiyo isajiliwe ili utaratibu wa ulipwaji wake uwe na nguvu ya kisheria . Katika kesi hiyo, Tanesco kupitia kwa mawakili wake, Rex Attorneys kwa kushirikiana na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Februari 9, 2011, waliwasilisha mahakamani hapo pingamizi la usajili wa tuzo hiyo. Tanesco waliwasilisha hoja 11 za kupinga tuzo hiyo ya ICC wakieleza kuwa mahakama hiyo ya kimataifa ilijipotoka kisheria katika kutoa tuzo hiyo kwa Dowans na hivyo kuiomba Mahakama hiyo iitupilie mbali tuzo hiyo. Hata hivyo, hoja zao zilitupiliwa mbali na Mahakama Kuu kusajili tuzo ya Dowans. Habari hii imeandaliwa Elias Msuya, Patricia Kimelemeta, Ellen Manyangu na Elizabeth Edward |
chanzo: Gazeti la Mwananchi
whttp://mwananchi.sekenke.com/aambie Ukweli tunataka viongozi kama nyie Msiogopa kitu katika nchi yetu masikini.........