Let's talk about the truth; CCM imetapika tu, bado haijajivua gamba!

KAMBOTA

Senior Member
Mar 21, 2011
176
103
mz6.jpg



Na Nova Kambota,


Binafsi nimeshtushwa sana na kauli za baadhi ya wana CCM kuwa chama chao kimeshajivua gamba , wanatumia mabadiliko ya safu ya uongozi ndani ya chama hiko yaliyofanyika hivi karibuni huko Dodoma, wakiwa na furaha kubwa wanadai kuwa hatua ya sekretarieti ya chama chao kujiuzulu huku ikimtupa nje katibu mkuu Yusuph Makamba na kumwingiza katibu mkuu mpya Willison Mkama na pia hatua ya kamati kuu ya chama hiko kuvunjika kwa maana nyingine imewatupa nje wajumbe mbalimbali lakini kati ya hao wapo wanasiasa wawili waliotawala vichwa vya magazeti hawa ni Andrew Chenge na Rostam Aziz lakini kujipa matumaini wanaccm wanadai kuwa kuingia kwa sura mpya tena za vijana kama Nappe Nauye na January Makamba ni ushahidi kuwa chama chao kimejivua gamba na sasa kipo safi .

Hata hivyo miezi michache tu baada ya safu mpya ndani ya chama hiko kutangazwa dalili za wazi kabisa zimeonekana kuwa CCM ilikuwa imeshiba sana kiasi kwamba ilikuwa vigumu kwake kupenya kwenye tundu jembamba sana hivyo ilipaswa kujivua gamba ili ipite lakini kwavile gamba la CCM limeshikamana na ngozi basi kikao cha Dodoma kimehofia maumivu ya kuvua gamba na badala yake CCM imejidanganya yenyewe kama sio kufanya mchezo wa kitoto wa kutapika ikidhani kuwa kwa kupunguza ukubwa wa tumbo itaweza kupenya hapo lakini sivyo inapaswa kujivua gamba! Lakini kwanini nasema CCM imetapika tu na sio kujivua gamba kama wengi wadhaniavyo?

Kwanza kabisa wanabiolojia au wataalamu wa elimu ya viumbe wanafahamu kuwa nyoka hajivui gamba kwa lazima la hasha! Bali gamba lenyewe huelegea na kujivua au hulegea sana na wakati nyoka akipita kwenye upenyo Fulani basi gamba huvuka hata pasipo nyoka mwenyewe kufahamu huu ni ukweli wa kisayansi kabisa lakini cha ajabu sana ni kile kinachoitwa kujivua gamba kwa ccm ni kwa kujilazimisha ,hakika nyoka hawezi kujivua gamba kwa kujilazimisha hivyo hata CCM haiwezi kujivua gamba kwa kujilazimisha badala yake inaweza kutapika kwa kujilazimisha labda kwa kuingiza vidole kwenye koromeo au kula kitu Fulani kitakachopelekea tumbo kuvurugika kisha kutapika hivyo kwa mantiki hii ni dhahiri kabisa ilichofanya CCM ni kutapika tu lakini sio kujivua gamba kama wanavyotaka kuuaminisha umma wa watanzania.

Pili ni jinsi CCM ilivyoshindwa kufanya mabadiliko ya kimchakato ndan ya mioyo ya makada wake nasema hivi kwasababu naona kabisa kile kinachoitwa migawanyiko au minyukano ndani ya CCM itaendelea kwa maana mpaka sasa CCM haijafanikiwa kujipambanua kiitikadi na kiimani iwapo ipo pamoja na wafanyabiashara ambao ni wafadhili wa chama hiko huku wengi wao wakihusishwa na tuhuma za ufisadi au wapo pamoja na wakulima na wafanyakazi ambao ndio wenye chama chao lakini sasa wameporwa kiasi kwamba sasa wenye fedha ndio wenye nguvu na ndio wenye uwezo wa kugombea na kushinda ndani ya chama hiko kiasi kwamba katibu mkuu wa zamani wa chama hiko Philip Mangula aliwahi kutamka kuwa CCM itangaze tenda kwenye kuwania uongozi! Hivyo ni wazi kuwa CCM haijaweza kuwaleta meza moja Harrison Mwakyembe na Edward Lowassa, pia haijafaulu kuwakutanisha kimtazamo Samwel Sitta na Rostam Aziz au kuwaimbisha wimbo mmoja Andrew Chenge na Anne Kilango Malecela wala mabadiliko haya hayawezi kuwasemesha lugha moja Yusuph Makamba na Shy-Rose Bhanji, CCM ingejivua gamba haya yasingekuwepo lakini kwavile imejidanganya kwa kutapika tu siiombei mabaya ila nasema isubiri ione nini kitafuata.

Tatu CCM ingejia gamba kweli isingejitosa kwenye maji ya moto tena yanayochemka nasema hivi kwasababu mpaka sasa dalili za wazi zinaonyesha kuwa CCM haiamini kuwa ipo ndani ya mfumo wa vyama vingi chukulia mfano wa hoja ya katiba mpya , naona kabisa ukimtoa Prince Bagenda nadhani wanaccm wengine wote licha ya kutamka kuwa katiba ni hoja ya wananchi ila mioyoni mwao wanaamini katiba ni hoja ya CHADEMA, CUF, NCCR na baadhi ya wanaharakati tu kwasababu iwapo kweli CCM inaamini kuwa ipo kwenye ushindani wa kisiasa kwenye mfumo wa vyama vingi basi kujijenga kwake kungetegemea katika kuipenda na kuikuza demokrasia badala yake inategemea nguvu zake , mimi naamini CCM ilipaswa kuwa ya kwanza kuipinga rasimu ya marekebisho ya katiba kwa jinsi ilivyojaa mapungufu badala yake inaunga mkono licha ya mapungufu hayo hii inatafsiri gani? Je CCM inataka kuvikomoa vyama vya upinzani au uhafidhina unaisumbua CCM? Je CCM ingejivua gamba ingeendeleza uhafidhina wa jinsi hii? au na yenyewe ingepinga rasimu hiyo? Jibu rahisi ingejivua gamba isingekuwa na uchafu wa aina hii ila kwavile imetapika tu ndio maana sasa ina njaa ya kuwakomoa wapinzani lakini niwakumbushe kuwa katiba mpya ni hitaji la watanzania sio CHADEMA wala CUF.

Nne CCM walipaswa kufanya mapinduzi ya kimfumo sio watu kama ilivyofanya, kwangu mimi nilitegemea CCM ingekuja na maazimio ya kukomesha mfumo wa wafanyabiashara kukimbilia ndani ya chamma hiko na vilevile kukomesha mfumo wa viongozi wa chama hiko kupendaz kusifia na kusifiwa tu , mimi nilitegemea kuwa sasa CCM inaandaa mkakati rasmi wa kuwa na tabia ya kujikosoa ili kulinda staha, tunu na falsafa ya mapinduzi ya chama hiko lakini sijaliona hili amini nakwambia ndani ya CCM bado ukiwa msemakweli kama Samwel Sitta,Harrison Mwakyembe na John Magufuli utajikuta unaongeza maadui kuliko marafiki, mambo haya hayawezi kubadilishwa kwa kumwondoa Makamba na kumweka Mkama bali kubadili mfumo wa CCM ndio maana nasisitiza kuwa ilichofanya CCM imetapika tu haijajivua gamba kwa kuhofia maumivu kwa maana gamba limeshikamana na ngozi.

Tano nilitegemea CCM ijisafishe kwa dhati kabisa kwenye kila ngazi na jumuiya zake tena kwa kuwapiga chini viongozi wale wanaoonekana ni mzigo lakini siamini kama hili litafanyika , hapa sidhani kama UVCCM , UWT na Jumuiya ya wazazi zitaguswa, labda nitumie wasaa huu kumpa siri Jakaya Kikwete kuwa hayo anayoita makundi na minyukano ya vigogo wa chama hiko kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015 chanzo chake haswa ni huko kwenye jumuia hizi na endapo hatazigusa wala kuzitikisa walau kidogo basi hicho kinachoitwa kujivua gamba litakuwa ni jambo la kufikirika tu kuliko uhalisia ndani ya chama chake hiko.

Mwishowe nihitimishe makala haya kwa kuwaasa wanaaccm kuwa bado wana safari ndefu ya kujivua gamba sio kirahisirahisi hivi kama wanavyodhani tena hakuna ubishi kuwa kwa gamba lilliloshikamana na ngozi kazi kubwa inahitajika kulivua, kwa upande wa vijana wa chama hiko wasishangilie kuingia kwa vijana wenzao January Makamba na Nappe Nauye bali wanapaswa wajikite zaidi katika mapambano ya ndani ya chama yatakayowawezesha kukibadili chama hiko kutoka wazee oriented kuwa vijana oriented kisha wapindue mfumo wa wafanyabiashara na wakirudishe chama mikononi mwa wakulima na wafanyakazi vinginevyo hiko wanachoita kujivua gamba si lolote bali ni kutapika tu na hivyo CCM yao haiwezi kupenya kwenye mioyo miyembamba ya watanzania masikini kwa kujitapisha tu bali inapaswa ijivue gamba hata kama itapata maumivu makali…Tafakari!


Nova Kambota,
+255717 709618
novakambota@gmail.com
www.novakambota.com
Tanzania, East Africa
Jumamosi, 2 julai 2011

Naomba kura yako kwenye tuzo za blog Tanzania kwenye vipengele vya best collaboration/group blog, best informative political blog na best political blog kunipigia kura nenda www.tanzanianblogawards.com

 
Back
Top Bottom