Shairi: Leo nimejishindia!

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,475
39,991
Leo ninashangalia, mimi tena siyo duni,
Kwani nimejipatia, furaha nyingi moyoni,
Na nimekoma kulia, imenitoka huzuni,
Binti niliyekutaka, leo nimejishindia!!

Ilikuwa kazi ngumu, miye kukufuatilia,
Ilizidi yangu hamu, ninapokuandikia,
Nimeupata utamu, leo ninajisikia,
Wewe niliyekutaka, leo nimejishindia!!

Wewe binti wa kibongo, miye ninakusifia,
Sitausema uongo, moyoni umeingia,
Umenitoa usongo, pale uliponijia,
Wa ubani binti wewe, leo nimejishindia!!

Picha uliyoituma, wiki jana ilifika,
Hakika wewe ni chuma, na tena umepambika,
Nami nikaona vyema, ujumbe nitaandika,
Mbalamwezi sura yako, Leo nimejishindia!!

Nije kukutembelea, miye nikajialika,
Ndipo ukachelekea, ukasema njoo kaka,
Haraka nikatokea, bila haya nikafika,
Habiba nakuimbia, leo nimejishindia!!

Kifuani kukuweka, nilipokukumbatia,
Ndipo niliweweseka, busu ulinipatia,
Bwana mdogo karuka, joto aliposikia,
Furaha imenijaa, leo nimejishindia!!

Pale uliponigusa, moyo wangu ulidunda,
Na sitofanya makosa, huyu dada nampenda,
Ndipo nilipojitosa, ukanipa hilo denda,
Wewe binti wa kibongo, leo nimejishindia.

Leo wanitembelea, nyumbani hapa nilipo,
Mola ameniletea, huyo wangu wa upepo,
Furaha imerejea, huyu binti kweli yupo,
Miye ninajivunia, leo nimejishindia.

Lahi lahi subihana, shukurani wa taala,
Umenitoa utwana, ewe Mola uso hila,
Kwa yako yote mapana, umejibu zangu swala,
Moyo wangu umetekwa, leo nimejishindia!!
 
Mkuu, Mwanakijiji,

Taratibu, one thing at a time.

Nachambua kuhusu mbuzi isokuna nazi kwanza.
 
Duu!! hii kali kwa kweli. Mkuu MKJJ- yaani wee siku ukijishindia unatangazia ulimwengu? Inaonekana ulikuwa na kiu cha muda mreeeefu sana.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom