Kwaresma itumike kuombea upendo, umoja, amani nchini

mzambia

JF-Expert Member
Dec 31, 2010
885
60
LEO Wakristo wa Tanzania wameungana na wenzao duniani kote kuanza kipindi cha Kwaresma ambacho ni cha kuelekea mateso ya Bwana Yesu Kristo kwa ajili ya kuwakomboa wanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi.

Kwa Wakristo, kipindi hiki ni cha kutafakari upendo wa Mungu na Yesu Kristo alivyojitoa kufa kwa ajili ya dhambi na matatizo mengine yanayoikabili duinia. Ni wakati ambao hutawaliwa zaidi na maombi yanayoambatana na kufunga siku 40 kwa baadhi ya madhehebu, au siku kadhaa kadiri mtu anavyoona.

Kimsingi, kufunga na maombi hayo yanaelekeza kujitakasa, kuombea kanisa, taifa na jamii ili iondokane na matatizo yanayosababisha mateso, mahangaiko, haki kutotendeka, amani kutoweka na hatimaye faraka, utengano na ugomvi kutokea katika jamii.

Hii ni kutokana ukweli kwamba, kipindi hiki, BwanaYesu alidumu katika kuwaombea watu wa taifa lake na dunia nzima ili pawe mahali salama pa kuishi. Ndiyo maana leo tumeamua kuungana na Wakristo wa Tanzania, kwa kuwakumbusha umuhimu wa kanisa na jamii ya Kikristo kushiriki kikamilifu katika Kwaresma hii, si tu kufunga na kufanya sala ndefu zenye maneno mengi bila matendo.

Ni wajibu wa Kanisa la Tanzania na Wakristo wote wanaomcha Mungu kutafakari kwa kina nafasi yao katika jamii na kuona kwa jinsi gani watasaidia kujenga umoja na mshikamano wa taifa hili, hasa kipindi hiki ambacho nchi yetu inapita katika wakati mgumu.

Tunajua nafasi ya kanisa, wajibu na mchango wake kwa jamii na taifa letu katika kudumisha amani na kutoa huduma za kijamii kwa watu wenye matatizo mbalimabli, ikiwemo kutoa misaada ya kiutu na kiroho kwa waliokata tamaa kutokana na matatizo yanayowakabili kiafya, kiuchumi na kiroho.

Pia tunajua mchango wa kanisa katika kudumisha umoja wa kiimani na ushirikiano na dini nyingine katika kudumisha amani, jambo ambalo limesaidia nchi yetu kufikia hapa tulipo sasa, licha ya kuwepo dini na madhehebu mbalimbali ya dini.

Tumeliona kanisa la Tanzania linavyoshughulikia upatanishi katika mafarakano na migongano kisiasa na hasa jinsi linavyojitoa kuombea amani ya nchi yetu. Kutokana na wajibu huo, ambao Wakristo wamekuwa wakiufanya siku zote, wakati huu wanatakiwa kufanya hivyo mara dufu kwa maombi na vitendo vinavyoashiria mshikamano na upendo wa kweli kwa watu wote na nchi yetu.

Ni kweli kwamba, Tanzania sasa hivi inapita katika kipindi kigumu. Kisiasa mambo hayajakaa sawa, kama tunavyosikia matamshi ya wanasiasa yanayotishia amani ya nchi yetu kutokana kushindwa kuvumiliana. Na kwa kuwa siasa ndiyo inayotawala, uvumilivu unapokosekana miongoni mwa wanasiasa na vyama vya siasa, ni dhahiri tunalipeleka taifa letu mahali pabaya, hivyo kanisa linatakiwa kukaa katikati kwa njia ya maombi na roho ya upendo ili kujenga umoja kwa msaada wa Mungu.

Tanzania hivi sasa ina hali mbaya kiuchumi na kusababisha maisha ya Watanzania kuendelea kuwa mabaya kila kukicha kutokana na mfumuko wa bei ambao umesabisha bidhaa zote zikiwemo muhimu kunda kwa kasi, hivyo kusababisha malalamiko na vilio kutoka pande zote za nchi.

Kama wananchi wanakosa chakula kutokana na bei kuwa juu, kama wanashindwa kupeleka watoto shule kwa sababu ya hali ngumu, kama hakuna umeme na uzalishaji viwandani, ni dhahiri kuwa watu watakosa matumini na hatimaye kuamua vinginevyo jambo ambalo ni hatari kwa taifa na wananchi wake.

Hapo ndipo unapoonekana wajibu wa kanisa na waumumini wake kuingilia kati kwa maombi na kujitoa kutetea haki na kulinda amani na umoja wa taifa letu.

Kwa hiyo basi, tunawaomba Wakristo wa madhehebu yote nchi kukitumia kipindi hiki cha Kwaresma kuombea amani na umoja wa Taifa letu, kama Yesu Kristo alivyoombea umoja na mshikamano wa ndugu katika Yohana malango wa 17.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom