Kwa Wamasai Ukimwi ni laana

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125
Kwa Wamasai Ukimwi ni laana
%5Cmasaitribe.jpg
Baadhi ya kinamama wa Kimasai wa Kijiji cha Pingo, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani. Jamii ya Kimasai inaamini kwamba Ukimwi ni laana na kupima au kuvaa kondomu ni kwenda kinyume cha mila na desturi.
Patricia Kimelemeta
KUMEKUWA na jitihada kubwa za kupambana na maambukizi ya Ukimwi zikihusisha elimu ya kujikinga na matumizi ya kondomu, alimradi kuwaepusha wananchi kuathiriwa na ugonjwa huo.

Takwimu za Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na taasisi mbalimbali zinaonyesha kuwa idadi ya watu wanaofariki dunia kutokana na ugonjwa huo imeshuka kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha mwaka 2008/09 ukilinganisha na mwaka 2007/2008. Kutoka asilimia 7.2 hadi asilimia 5.5.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa Mkoa wa Kigoma ndiyo wenye wagonjwa wachache kuliko mingine.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, kasi ya maambukizi kwa mwaka 2009/10 imepungua, jambo ambalo wadau hao wanaamini kuwa wamefanikiwa hasa katika suala zima la utoaji wa elimu ya kujikinga.

Lakini unaweza kudhani kwamba kwa jitihada na takwimu hizo, karibu wote wana uelewa wa hali ya juu juu ya maradhi hayo ambayo yaliingia nchini mwanzoni mwa miaka ya 1980. Ukiwa mmoja wao utakuwa unajidanganya. Kuna watu tena waishio karibu kabisa na maeneo ya mijini hivyo kuwa rahisi kwao kupata elimu ya ugonjwa huo lakini wala hawana habari.

Hawa ni watu wa jamii ya Kimasai waishio Mkoa wa Pwani ambao kwao Ukimwi ni ugonjwa unaotokana na dhambi anayofanya mwanadamu. Kwao, haijalishi kama dhambi hiyo ni ya ngono zembe au nyingine.

Ndiyo maana hawaamini katika kinga hizi zinazoelezwa na watalaamu wa afya hususan matumizi ya kondomu. Wanasema zinakwenda kinyume na mila na desturi zao. Wanaamini kwamba wanazo dawa zao walizorithishwa na mababu zao kwa ajili ya kujikinga na magonjwa ya kuambuliza ukiwemo wa ukimwi.

Wakizungumza katika Vijiji vya Pingo, Chamakweza na Chalinze Wamasai hao wanasema mila na desturi zao haziwaruhusu kutumia kondomu na wanaamini kwamba wanaofanya hivyo wanaweza kupata laana kutoka kwa mababu zao.

Wanasema wamekuwa wakifanya tendo la ndoa bila ya kutumia kinga yoyote na kuamini kuwa, mtu anayetumia kinga anakiuka mila na desturi yake.

“Suala la Wamasai kujitokeza kupima Virusi Vya Ukimwi (VVU) ni tatizo kubwa, jambo ambalo linafanya maambukizi ya ugonjwa huu kuongezeka, kwa sababu sasa kuna mabadiliko makubwa. Wanaume wa Kimasai wanaoa wanawake wa makabila mengine huku wakiwa na wake zao wa Kimasai, jambo ambalo linaongeza hatari ya maambukizi,” anasema Mwenyekiti wa Kijiji cha Pingo, Saimon Kondo.

Anasema wanawake wa kabila hilo nao wamekuwa wagumu kuamini kama kuna ugonjwa kama huo na wala hawana mpango wa kujitokeza kupima. Nao wanaamini kwamba kuendekeza mambo ya kupima Ukimwi ni kukiuka mila na desturi zao.

“Mmasai hawezi kuacha mila na desturi yake, kwa sababu tunaamini kuwa unaweza kupata mikosi katika maisha na kuishi kwa tabu na shida nyingi katika maisha yako yote. Hatuwezi kupima VVU kwa sababu hatujarithi hilo kutoka kwa mababu zetu. Hili suala limekuja sasa hivi,” anasema Neema Lazaro, mkazi wa Kijiji cha Pingo.

Anasema mila na desturi zao zinawaruhusu kutumia dawa za kienyeji ambazo zina kinga na uwezo wa kupambana magonjwa yote yanayoingia mwilini. Kwa imani yake na jamii yake, baada ya kuzitumia si rahisi kupata ugonjwa wowote ukiwemo Ukimwi.

"Si kazi rahisi kwa sababu mtoto wa Kimasai anapozaliwa anapatiwa dawa hizo mpaka anapokuwa au kufariki. Zinamkinga na magonjwa yote yawe ya kuambukiza au mengine."

Anasema ikiwa kuna Mmasai ambaye atabainika kwamba ameambukizwa Ukimwi, basi huyo atakuwa amefanya kosa kubwa ambalo mizimu yao itakuwa imempa adhabu kwa lengo la kumfunza adabu au kumkomesha kwa tendo alilofanya.

Mwanamke mwingine wa Kimasai, Maria Reuben anasema kuwa, ugonjwa wa ukimwi ni dhambi ambayo amefanya mwanadamu na kustahiri kupata maradhi ambayo hayana tiba ili aweze kubadilika.

Anasema wamasai hawana tabia ya kufanya dhambi hiyo, hivyo basi hawawezi kupata ugonjwa huo kwa sababu wanaendeleza mila na desturi walizoacha babu zao, jambo ambalo linawakinga na matatizo yote yakiwemo maradhi.

“Ukimwi ni dhambi ambayo mtu amefanya,mungu ameamua kumuadhibu kwa kumpa ugonjwa huu, lakini kama utaacha unaweza kupona na ukiendelea unaweza kufa, lakini sisi wamasai kinachotusaidia ni kuendeleza mila na desturi zetu, jambo ambalo linatukinga na mambo mengi ya kidunia,hivyo basi ninaamini kuwa ikiwa mmsai ataweza kuendeleza mila na desturi yake hawezi kufa na ugonjwa huo,anasema Reuben.

Kondo anasema kasi ya maambukizi katika vijiji hivyo inaongezeka, hasa kwa kwa watu wa kabila hilo, lakini hakuna dalili yoyote ya kuonyesha kuwa wameukubali ugonjwa huo na wanaendelea kudai kuwa kupima ni sawa na kukiuka mila na desturi zao..." Wanaamini kuwa kupima kunaweza kuwaleta matatizo katika maisha yao."

Anawataka wadau wa afya pamoja na vipngozi wa serikali na kisiasa kuitupia macho jamii hiyo ili ibadilishe mtazamo huo ambao ni hatari siyo kwao pekee bali wakazi wengi wa kijiji hicho na maeneo mengine.

Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ludamila Mgalula anakiri kwamba watu wa jamii hiyo wamekuwa wagumu kujitokeza kupima VVU jambo ambalo anaamini kwamba limechangia kuongezeka kwa kasi ya maambukizi.

Anasema kutokana na imani zao hizo, wamekuwa wakifanya tendo la ndoa bila ya kutumia kinga, jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa maambukizi kwani wamekuwa wakishirikiana katika tendo hilo na watu mbalimbali.

Anasema kutokana na hali hiyo wameamua kushirikisha taasisi mbalimbali zikiwemo za dini ili kutoa elimu kwao juu ya hatari ya ugonjwa huu na jinsi ya kuchukua tahadhari.

“Jamaa ni wagumu kuelewa. Tumekuwa tukikabiliwa na changamoto mbalimbali wakati wa kutoa mafunzo juu ya kutumia kinga na kujitokeza kupima VVU katika vituo vya afya. Wanakataa wanasema dawa za kienyeji zitawaponya. Jambo hili ni la hatari kwao na jamii kwa ujumla na ndilo tunalopingana nalo,” anasema Dk Mgalula.

Anasema kuwa vijana wengi wa Kimasai wamekuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanawake wa makabila mengine na kufanya nao ngono bila ya kutumia kinga huku wakiwa katika ndoa na wanawake wa kabila lao.

"Kutokana na hali hiyo, wanachukua virusi hivyo na kuvihamishia kwa wake zao. Kama wangeamua kuendelea na mila zao na kutoshiriki mapenzi na watu wengine, tungewaelewa lakini wanatoka nje ya ndoa zao."

Anasema kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo katika eneo hilo la Mkoa wa Pwani inaongezeka mwaka hadi mwaka kwa sababu ya mwingiliano wa kimapenzi baina ya wananchi, wakiwemo hao wa jamii ya Kimasai na makabila mengine.

Ndiyo maana anasema nguvu ya ziada zinahitajika kuwahamasisha wananchi hao wa kuangalia upya mila na desturi zao hasa katika suala hili la Ukimwi.


http://www.mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=18929
 
Back
Top Bottom