Kwa nini Wazanzibari tuikatae katiba ya wasakatonge?

Kifoi

JF-Expert Member
May 12, 2007
1,226
531
Tuisomeni vizuri na kuichambua katiba iliyopendekezwa kabla ya kuikataa au kuikubali. Kuikataa tu kwa sababu ya muundo wa muungano itakuwa tunakosea. Tuisome hasa mambo yanayoihusu Zanzibar na kero zetu za muda mrefu je zimepatiwa ufumbuzi?

Mimi nnavokumbuka kero za muungano zilikuwa ni:-
1-Zanzibar kuweza kujiunga na mashirika ya kikanda na kimataifa
2-Zanzibar kuweza kukopa kutoka katika taasisi za ndani na za nje.
3-Mafuta na gesi asilia kutolewa katika mambo ya muungano.
4-Uvuvi wa bahari kuu isiwe mambo ya muungano
5-Rais wa zanzibar awe makamo wa pili wa Rais wa Tanzania
6-Mfuko wa pamoja wa Muungano
7-Uwiano katika ajira za muungano
8-Mambo ya muungano yapunguzwe kutoka 22 mpk 11 kama zamani
9-nk
Hayo ndio malalamiko yetu makuu waznz ilikuwa, sasa tuisomeni na kuichambua km haya mambo bado yamo tuipigieni HAPANA lkn km yametolewa tuipigieni YES.

Kama tunavyoona katika maelezo yake, ndugu yetu huyu anahisi kwamba walio na wazo la kuipinga Katiba wameguswa zaidi na suala la muundo wa Muungano. Yaani kwa kuwa walitaka uwe wa Serikali Tatu, na kwa vile takwa hilo limetupiliwa mbali (ingawa ndilo takwa la Watanganyika walio wengi, wakati Wazanzibari walio wengi hata hilo silo takwa lao la asili bali walichotaka ni pande zote mbili za Muungano ziwe na mamlaka yao kamili na kuanzisha Muungano wa Mkataba) na kurejeshwa mfumo ule ule wa Serikali Mbili, ndio maana wanataka Wazanzibari waipigie kura ya ‘HAPANA' katiba pendekezwa.

Lakini badala yake, yeye anahisi kwa kuwa Wazanzibari tulikuwa na orodha ya mambo kadhaa (ambayo ili kuyahafifisha yamekuwa yakiitwa ‘Kero za Muungano') tuliyokuwa tukiyadai na kuyalalamikia; na kwa kuwa sasa, kama alivyoyataja mwenyewe tutayapata katika hiyo itakayoitwa Katiba Mpya, kuna sababu gani ya sisi kuipigia kura ya ‘Hapana' Katiba iliyopendekezwa?

Kabla ya kujibu hoja yako ndugu yangu Mzanzibari naomba kukuuliza wewe na wale wote wenye mtazamo kama wako maswali yafuatayo:
1. Sisi Zanzibar tulipoungana na Tanganyika mwaka 1964 hatukuwa sote, Tanganyika na Zanzibar, na hadhi sawa kimataifa kama nchi na mataifa huru? Kiasi kwamba ndani ya kipindi kifupi tu tangu tulipopata uhuru wetu tuliweza pia kuomba, tukakubaliwa na tukawa nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa yenye kiti chake katika umoja huo?

2. Wakati tunaungana na Tanganyika, nchi yetu haikuwa mbele zaidi kuliko jirani yetu huyu katika vipimo mbalimbali vya maendeleo vikiwemo vya elimu, afya na hata miundomsingi? Na je sisi na wao leo hii baada ya miaka 50 nani aliye mbele zaidi kimaendeleo? Unaijua sababu yake?
3. Ikiwa Zanzibar na Tanganyika zilipoungana zilikuwa na hadhi sawa kama nchi, wewe au nyinyi mlio na mtazamo wa kuunga mkono rasimu ya katiba ya Wasakatonge, mnaamini kwamba Tanganyika ina HAKI ya kuwa na mamlaka zaidi katika muungano huu kuliko Zanzibar? Kama ndiyo, kwa sababu gani?

Ndugu yangu Mzanzibari uliyeandika hayo na Wazanzibari wengine wote wenye mawazo kama yako ni muhimu ujue kwamba suala la MUUNDO wa Muungano ndilo suala la msingi kabisa na ndilo tatizo sugu kwa Wazanzibari; kwa sababu lina uhusiano na fungamano la moja kwa moja na MAMLAKA yetu katika Muungano ambacho ndicho kilio chetu kikuu. Hiki ndicho kilichomfanya Mzee Karume asusiane na Nyerere na kupoteza subira ya kuuvumilia Muungano huu wa Serikali Mbili kabla haujatumiza hata miaka 10, sio 50; na ndicho kilichomfanya Mzee Aboud Jumbe, Rais aliyechaguliwa kwa kura za Wazanzibari aondolewe madarakani na Nyerere kwa kutumia rungu la chama tu. Kupunguzwa orodha tu ya mambo ya Muungano ndugu yangu sio dawa maadamu hatutokuwa na ‘mamlaka ya kinchi' ya kuyafanyia kazi mambo hayo.

Hali yetu ya sasa Zanzibar ni sawa na ya mtu ambaye amekuwa na samani au fanicha chache za ndani ya nyumba, akalilia aongezwe nyengine kubwa na za thamani zaidi kama friji, kuka, vitanda na makabati ambavyo vyote hivyo hakuwa navyo kabla. Lakini kioja ni kwamba mtu huyu hana nyumba ya kuwekea vitu hivyo. Hebu nikuulize, hata akipatiwa vyote hivyo, mtu huyo atakuwa amepata kweli au amepatikana? Nyumba hapa ndugu yangu ni MAMLAKA ya kufanyia kazi. Labda nikuulize tu, kwani hivi sasa masuala ya Afya, Elimu isiyo ya Juu, Kilimo, Uvuvi, Biashara na mengine mengi si yako nje ya Muungano? Je Wazanzibari tuna mamlaka nayo kama walivyo wenzetu Watanganyika? Kwa asiyejua, anaweza kujibu ndiyo. Na huenda nikawa nimekukanganya kukuuliza hivi, lakini acha nikuthibitishie kwamba Muundo wa Muungano wa Serikali Mbili ni muundo wa kinyonyaji, wa kighilba, wa kidhalimu, kandamizi na wa kikoloni. Kwa nini natoa tuhuma zote hizi?

Zingatia mfano huu mmoja tu. Kilimo si suala la Muungano. Zanzibar tuna Waziri wa Kilimo, na Tanganyika ina Waziri wa Kilimo. Kisheria, kwa kuwa hili si suala la Muungano mawaziri wawili hawa inapasa wawe na hadhi sawa kitaifa na kimataifa; swali, ni kweli wako hivyo? Kwanza kabisa sote tunajua kwamba japokuwa tunavyodai, muungano wetu huu ni wa nchi mbili zilizokuwa na hadhi na mamlaka sawa, lakini ajabu ni kwamba mambo yote yanayohusu Muungano iwe ni katika misingi ya kitaifa au kimataifa yako Tanganyika. Mfano mzuri ni balozi zote kuu za kigeni pamoja na ofisi za mashirika ya kimataifa. Sasa tuangalie hadhi na mamlaka ya mawaziri wetu wawili wa masuala yasiyo ya muungano.

Wakati Waziri wa Kilimo wa Tanganyika (ambaye amevaa koti la Muungano na kujulikana kimataifa kama Waziri wa Kilimo wa Tanzania) anapotaka kufanya safari nje ya nchi, ikiwa ni ya ziara katika nchi nyengine au kushiriki mikutano ya kimataifa, yeye huomba idhini kwa nani? Jibu, haombi idhini kwa yeyote, kwa sababu kama alivyo Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania wa Muungano na yeye pia ni Waziri wa Kilimo wa Tanzania hivyo analivaa kwa njia haramu koti la Muungano japokuwa Kilimo si suala la Muungano! Na anapokwenda huko nje huwa anawakilisha nchi gani? Tanganyika? Jibu, hapana. Anawakilisha, kama cheo chake kinavyojieleza, nchi ijulikanayo kimataifa kama Tanzania! Swali, huo ndio ukweli halisi? Na je waziri huyo ana mamlaka mengine ya ziada kisheria ghairi ya kuwa Waziri wa Kilimo wa Tanganyika tu?

Sasa tuje upande wetu. Waziri wetu wa Kilimo anapotaka kufanya safari kama hizo inamlazimu afanye nini? Anapokwenda nje ya nchi, anawakilisha nchi gani? Na ikiwa waziri wa kilimo wa Tanganyika anataka kufunga mikataba huko nje analitumia koti alilovaa la Muungano kujifanyia hayo, muulize waziri wetu wa kilimo wa Zanzibar hulazimika kupitia ngazi ngapi za urasimu wa Wizara ya Mambo ya Nje kwa ajili ya mambo hayo? Ndugu yangu Mzanzibari, nilikuuliza awali, Tanganyika ina haki ya kuwa na mamlaka zaidi katika muungano kuliko Zanzibar? Jibu lako litowe kwa kuzingatia maelezo hayo.
Swali jengine. Ikiwa Waziri wa Kilimo wa Tanzania (kama anavyoitwa) na Waziri wa Kilimo wa SMZ na sio Zanzibar kama tunavyojihashua, watafikisha kwa wakati mmoja ombi la kutaka kuonana na balozi wa Marekani, Denmark au Uturuki Dar es Salaam, unadhani nani atapewa kipaumbele, na kwa nini? Swali jengine. Ikiwa kuna kongamano la kimataifa la kilimo katika nchi fulani, barua ya mwaliko inayotolewa kwa Tanzania hufikishwa kwa Wizara gani ya Kilimo; ya Tanzania (Tanganyika) au Zanzibar?

Ndugu yangu Mzanzibari, huo ni mfano mmoja tu na wa wizara moja tu. Kaa utafakari hali hiyo kwa wizara nyengine zote, ujue hivyo ndivyo Muungano wa Serikali Mbili unavyotunyonya na unavyotukandamiza Wazanzibari.
Niliwahi kuandika, na nakushauri na wewe ulichunguze hilo. Leo hii ukitembelea mitandao ya kijamii ya habari ya Tanzania, kama blogi ya Issa Michuzi na Hakingowi, kutaja michache tu, utaona kila siku yanafanyika makongamano, semina na hafla za utoaji misaada kimataifa inayofaidisha wizara zote za Tanganyika zisizo za Muungano kwa kutumia jina la Tanzania, huku sisi Zanzibar tukibaki kughani wimbo wa Mapinduzi Daima.

Sasa hebu jiulize, kwa nini Wazanzibari tulikuwa na kila sababu ya kupigania angalau kuwa na muundo wa Muungano wa Serikali Tatu? Jibu nadhani liko wazi kabisa. Ni kwamba kwa kuwa na mfumo huo, Tanganyika haitoweza tena kujipa mamlaka ya kulitumia jina la Tanzania kwa maslahi yake. Rasimu ya Warioba iliweka wazi kisheria jinsi nchi zote mbili washirika wa Muungano, yaani Tanganyika na Zanzibar, na si Tanzania Bara na Zanzibar, zitakavyoweza kujifanyia mambo yao yasiyo ya Muungano kimataifa kwa uwazi kabisa na kwa haki sawa.

Yaani, ima zote mbili zitapitia Wizara ya Mambo ya Nje kufatilia masuala yao, kama inavyodhalilishwa Zanzibar hivi sasa, au zote mbili zitapewa mamlaka kamili na yenye hadhi sawa ya kujifanyia mambo hayo. Na kutokana na kuwepo uwazi (transparency) wa mamlaka , na si ghilba, ujanja na ulaghai kama ilivyo sasa, ina maana endapo kutakuwa na kongamano la kimataifa la kilimo, na mwaliko ukaletwa kwa Tanzania, nchi hii itawakilishwa kwa uzito sawa na mawaziri wa Kilimo wa Tanganyika na Zanzibar, au pande husika huko nje, kama ni nchi au shirika la kimataifa zitajulishwa kuwa, kuanzia sasa zitapaswa kuamiliana na Tanganyika na Zanzibar ‘independently' na ‘separately' katika mahusiano ya kimataifa, kama pande mbili zenye hadhi sawa katika Jamhuri ya Shirikisho la Tanzania.

Kama ndugu yangu Mzanzibari umeulewa barabara mfano huu mwepesi niliokupa utaweza kuelewa kwamba hata mafuta na gesi kutolewa katika mambo ya Muungano ni upuuzi mtupu katika mfumo uliopo hivi sasa. Maana Waziri wa Nishati wa Tanganyika ndiye atakayeendelea kushika mpini, na kila ambalo Zanzibar itataka kufanya itaendelea kuwa na hali ile ile ya kudhalilishwa na kuomba huruma ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Muungano.
Huenda ukajipa moyo kwa kusema, tutaruhusiwa pia kujiunga na mashirika ya kimataifa. Ujue kwamba huo ni usanii tu. Hali itabaki kuwa ile ile. Maadamu Zanzibar si nchi (ingawa hata tulivyojipa mamlaka hayo katika marekebisho ya 10 ya Katiba hakutusaidii vyovyote kimataifa, na hilo pia Mkoloni Tanganyika hawezi kulivumilia) hakuna tutakachoweza kufanya.

Maana tutaendelea kusubiri kupata huruma na ridhaa ya bwana mkubwa Tanganyika aliyejipa mamlaka ya Tanzania; na kila pale itakapohisika na yeye kuwa hatua yetu inakiuka katiba, inatishia umoja wa Watanzania, inaweza kusababisha magaidi na Uislamu wa siasa kali kuingia Zanzibar, na uzandiki mwengineo unaoweza kutolewa na bwana mkubwa Dodoma huko, kama alivyoeleza pia Lukuvi, tutakwamishwa tu tusiweze kufanya chochote.
Mimi si mwanasheria na wala si mtaalamu wa masuala ya Katiba, na naamini utakuja kujionea mengi ya kukuweka kinywa wazi wakati wataalamu wetu wa sheria watakapoisasambua rasimu ya kina Sitta kwa kuilinganisha na ya asili ya Warioba, lakini natumia fursa hii kukudondolea rasimu mbili hizi za Warioba na ya kina Sitta uone uhalisia wa haya niliyokueleza.

Kwa faida ya maudhui yetu, yaani MUUNDO WA MUUNGANO na kukuonyesha jinsi Zanzibar tutakavyoendelea kuburuzwa, kunyonywa na kudhalilishwa na Tanganyika nitadondoa baadhi tu ya nukta katika vifungu vya rasimu hizo; kwa faida kamili rejea mwenyewe rasimu mbili hizo.
Rasimu ya Warioba inasema:

SURA YA SITA
MUUNDO WA JAMHURI YA MUUNGANO
(60) (1) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa na muundo wa shirikisho lenye serikali tatu ambazo ni :
(a) Serikali ya Jamhuri ya Muungano
(b) Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; na
(c) Serikali ya Tanganyika.
Nchi Washirika: (64) (1) Kwa mujibu wa Katiba hii, Nchi Washirika ni Tanganyika na Zanzibar
(2) Serikali ya Tanganyika itakuwa na mamlaka juu ya mambo yote yasiyo ya Muungano yanayohusu Tanganyika.
(3) Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa na mamlaka juu ya mambo yote yasiyo ya Muungano yanayohusu Zanzibar.
….(5)***** Msisitizo ni wangu: Nchi Washirika zitakuwa na hadhi na haki sawa ndani ya Jamhuri ya Muungano na zitatekeleza majukumu yao kwa mambo yote yasiyo ya Muungano katika mamlaka ya Nchi Washirika kwa mujibu wa masharti yatakayowekwa na Katiba za Nchi Washirika.
Mamlaka ya Nchi Washirika 65. ***** msisitizo ni wangu: (2) Bila ya kuathiri mipaka iliyowekwa na Katiba hii, kila Nchi Mshirika wa Muungano itakuwa na uwezo na uhuru wa kuanzisha mashusiano au ushirikiano na jumuiya au taasisi yoyote ya kikanda au kimataifa kwa mambo yaliyo chini ya mamlaka yake kwa mujibu wa Katiba ya Nchi Mshirika wa Muungano.
(3) Nchi Mshirika wa Muungano inaweza, wakati wa kutekeleza majukumu yake chini ya ibara ndogo ya (2), kuomba mashirikiano kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kufanikisha mahusiano na jumuiya au taasisi ya kimataifa au kikanda, na Serikali ya Jamhuri ya Muungano inaweza kutoa ushirikiano kwa Nchi Mshirika wa Muungano kwa namna itakavyohitajika….mwisho wa kunukuu.
Sasa tuje kwenye rasimu ya Sitta, Chenge na Wasakatonge:

SURA YA SABA
MUUNDO WA JAMHURI YA MUUNGANO
70. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa na muundo wa Serikali mbili ambazo ni :
(a) Serikali ya Jamhuri ya Muungano; na
(b) Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
73. (2) Bila kuathiri mipaka iliyowekwa na Katiba hii, katika kutekeleza mamlaka yake chini ya ibara ndogo ya (1), Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa na uwezo na uhuru wa kuanzisha uhusiano na ushirikiano na jumuiya au taasisi yoyote ya kikanda au kimataifa. (3) Endapo, katika kutekeleza mamlaka na majukumu yake kwa mujibu wa ibara hii, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahitaji kupata ushirikiano kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kufanikisha uhusiano au ushirikiano na jumuiya au taasisi ya kikanda au kimataifa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano yaweza kufanikisha uhusiano au ushirikiano huo KWA KUZINGATIA MASHARTI YA KATIBA HII NA SHERIA ITAKAYOTUNGWA NA BUNGE. (Msisitizo ni wangu).
Linganisha kipengele hicho na namna rasimu ya Warioba inavyoeleza kuhusu nukta hiyo. Na kama vile haitoshi rasimu iliyokatiwa na viuno na Wasakatonge inasema:

(4) Kwa madhumuni ya ibara hii, Bunge litatunga sheria itakayoainisha na kufafanua:
(a) Majukumu na mipaka ya utekelezaji wa mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu uhusiano au ushirikiano wa kikanda au kimataifa;
(b) Utaratibu wa kushughulikia athari zinazotokana na uhusiano au ushirikiano wa kikanda au kimataifa;
(c) Utaratibu wa utafutaji na upatikanaji wa mikopo na misaada kutokana na uhusiano na ushirikiano huo;
(d) Utaratibu au masharti ya kuvunja au kuimarisha uhusiano au ushirikiano huo;
(e) Utaratibu wa mawasiliano na mashauriano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu uhusiano au ushirikiano wa kikanda au kimataifa;

(f) Utaratibu wa utekelezaji wa masharti ya ibara hii; na
(g) Mambo mengine yatakayohusu uhusiano au ushirikiano wa kikanda au kimataifa chini ya ibara hii.

Ndugu yangu Mzanzibari unaiona rasimu hiyo iliyokatiwa viuno na Wasakatonge? Yaani hata katika kuvunja au kuendeleza mahusiano hayo tutakuwa chini ya udhibiti wa bwana mkubwa. Yako wapi mamlaka ya Zanzibar?

Unaviona vigingi vya ujanja, ulaghai na ghilba hivyo vya kuidhibiti Zanzibar katika suala hilo moja tu la kujiunga au kuwa na uhusiano na jumuiya au taasisi za kimataifa? Wakati rasimu ya Warioba inaeleza sisi na Tanganyika ni NCHI WASHIRIKA, katika rasimu hii ya kidhalimu Zanzibar ni kitu gani? Mkoa, jimbo, wilaya au kata ya Tanzania?

Umeona na umeshaelewa sasa tunakotoka kwenye rasimu ya Warioba ni wapi na walipoifikisha Zanzibar Wasakatonge ni wapi? Kama wewe ni Mzanzibari mwenye akili timamu na mwenye uchungu wa nchi yako, ikiwa utawekewa rasimu mbili hizi utakubali kweli kuipigia kura ya ‘ndiyo' rasimu ya kina Sitta, Chenge na Wasakatonge?

Wakati sisi Zanzibar tunawekewa masharti yote hayo na Tanganyika inayojiita Tanzania, wao anawadhibiti nani katika kufanya mambo hayo? Ndo nilipokuuliza ndugu yangu, Tanganyika ina haki zaidi kuliko Zanzibar katika Muungano huu?
Mfano niliokupa ndugu yangu ni mmoja tu wa UOZA wa hii katiba pendekezwa juu ya muundo wa Muungano. Lakini utakapoisoma katiba yenyewe utakuta mengi zaidi na ya msingi, na utajua kwamba kilichofanywa na kundi la wasakata tonge kutoka Zanzibar (ingawa ni kwa mizengwe; kwa sasabu theluthi mbili hawakuzipata, si kiharamu wala kihalali) waliposhangiria Dodoma huku wakikata viuno, ilikuwa ni kuipiga mnada na kuizamisha Zanzibar iliyokuwa tayari maji shingoni kutumbukia kwenye tumbo la chewa Tanganyika.

Lakini mwisho kabisa napenda nikueleze jambo moja ndugu yangu.
Katiba iliyotungwa, kwa asilimia zaidi ya 90 inahusu masuala ya Tanganyika tu. Na kama alivyosema Warioba mwenyewe, kwa kazi waliyofanya, ilikuwa tayari wamesharahisisha pia utungaji wa katiba ya Tanganyika katika mfumo wa Muungano wa Serikali Tatu. Sasa basi, kwetu sisi Wazanzibari suala la MUUNDO WA MUUNGANO ndilo lililokuwa muhimu na la msingi katika utungaji wa katiba mpya ya Tanzania na ndilo lililohitaji kazi ya umakini kama ilivyofanywa na Tume ya Warioba. Ulikuwa ni ujinga mtupu, kupoteza wakati na baya zaidi, mabilioni kwa mabilioni ya shilingi, ikiwa Wazanzibari tulitaka kupigania mambo kadhaa tu yatolewe kwenye orodha ya mambo ya Muungano.

Kwa sababu, kwanza kabisa, yote hayakuhitaji kutungiwa katiba mpya, bali yangewezekana kufanywa kupitia marekebisho tu ya katiba hii ya sasa ya mwaka 1977 katika bunge la Jamhuri. Kwani kuondolewa cheo cha Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, ambalo ni suala la msingi la makubaliano ya Muungano kulifanywa kwa kutunga katiba mpya? Au kupitisha yale mambo yote ambayo awali hayakuwa ya muungano, lakini yakapenyezwa kidogo kidogo kuwa ya Muungano kulifanywa kwa kutunga katiba mpya au marekebisho ya katiba tu?

Lakini la pili jiulize ndugu yangu Mzanzibari, hiyo kazi ya kuondoa mambo hayo yakiwemo ya mafuta na gesi na kujiunga na jumuiya za kimataifa, yamefanywa na nani? Kwa muda wa miaka 50 CCM na serikali yake ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshindwa kuyashughulikia na kuyapatia ufumbuzi mambo hayo. Hata hilo la gesi na mafuta, Zanzibar, kupitia Baraza la Wawakilishi imeshalipigia kelele kwa miaka mingapi sasa? Je serikali ya Tanganyika inayojiita ya Tanzania imejali na kusikiliza kilio hicho cha Wazanzibari? Ni Tume ya Warioba, ndiyo iliyokuwa na ujasiri wa kuyashughulikia mambo hayo kama ilivyoonyesha ujasiri wa kutaka kumaliza enzi za ukoloni na unyonyaji wa Tanganyika kwa Zanzibar kupitia mfumo wa Serikali Mbili kwa kupendekeza mfumo wa Serikali Tatu. Kilichofanywa na Mafia wa Muundo Kandamizi wa Muungano wa Serikali Mbili kule Dodoma wakiongozwa na Samuel Sitta kwa ushirikiano na Andrew Chenge, kilikuwa ni kupandia mawimbi ya kazi nzuri ya Tume ya Warioba, kwa kunyofoa waliyohisi yana maslahi na wao na watakayoweza kuyatumia kuwahadaa wananchi, na kuyatia kapuni yale ya msingi kabisa yanayotokana na matakwa halisi ya Watanganyika na Wazanzibari.

Kwa hivyo kama umeyaelewa barabara maelezo haya ndugu yangu Mzanzibari, na kama una uchungu wa kweli wa NCHI yako, naamini utaungana nami kuhakikisha sio tu tunainyima theluthi mbili katiba pendekezwa, bali kuirarua rarua na kuipiga na chini kwa theluthi mbili za kura za HAPANA, rasimu hiyo ya kina Chenge, Sitta, pamoja na Wasaliti na Wasakatonge wa Zanzibar, ambayo hakika yake hasa ni katiba ile ile ya sasa iliyotiwa viraka tu na tena vilivyoraruka; na badala yake kuhakikisha rasimu halisi ya Warioba, ambayo ndiyo rasimu halali na iliyofanyiwa kazi na kupendekezwa kwa nia njema na kwa maslahi ya Watanzania wa pande zote mbili za Muungano inarejeshwa na kupitishwa rasmi.

Tafadhali kwanza ufikishe ujumbe huu kwa Wazanzibari wote na pili, piga kura ya HAPANA kwa katiba bandia pendekezwa na ungana na wazalendo wenzako, bega kwa bega na mkono kwa mkono hadi Zanzibar yenye haki sawa na Tanganyika katika Shirikisho la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania! Daima Zanzibar Kwanza.

Chanzo:Mzalendo
 
Back
Top Bottom