Kwa nini tusivutie wawekezaji wa kuendesha serikali

Njowepo

JF-Expert Member
Feb 26, 2008
9,710
2,226

NIMEMALIZA kujadili na kudadisi suala ambalo nimepokea mrejesho kidogo sana kutoka kwa wasomaji. Naamini kwamba huenda masuala ya kudadisi vitu visivyoonekana moja kwa moja na kuelezeka kirahisi hukosa mvuto kwa wasomaji wengi. Yupo mmoja alidiriki kunieleza kwamba hiyo ‘superstructure’ ninayohubiri ni kazi bure kwa sababu huenda viongozi hawasomi makala zetu.
Viongozi wasome wasisome, hilo si tatizo la wanaoandika. Wanaosoma historia vizuri wanajua sheria ya asili inasema nini kuhusu hatma ya viongozi na watawala waliodharau sauti na fikra mbadala. Mke wa Mfalme Louis wa Ufaransa aliyefikia jeuri ya kushauri kwamba wananchi wa Ufaransa waliokuwa wanaandamana kwa kukosa mikate kwa nini wasile keki alifanya hivyo kwa sababu alikuwa hataki kusoma yale yanayomuudhi. Akina Caesescu wa Romania walizoea kusoma makala zilizowapamba na kuwasifia hadi siku waliposhangaa kilichotokea.
Na kama nilivyoeleza katika makala zangu zilizopita, tunaweza kujenga mazoea ya kuwa tunarukia tatizo moja baada ya jingine na kulijadili kana kwamba linajitegemea na halina uhusiano na mlolongo wa matatizo mengine yaliyopita na yanayokuja. Tunajadili. Tunafokeana. Tunawindana. Tunapanga kuondoana duniani. Lakini kama hatujabaini chanzo au kiini cha matatizo yetu yanayotupa huo wazimu, hatuwezi kamwe kutoka hapa tulipo.
Nilieleza katika makala yangu iliyopita kwamba wapo watu hawaelewi ni kwa nini wapo waandishi, wanazuoni, watafiti, wanasiasa, na hata wapiga ramli wanaozungumza kwamba mambo hayaendi vizuri nchini.
Lakini pia wapo watu wanaodhani leo hii Rais Jakaya Kikwete akiamka na kuamuru wote tunaowashuku au ambao ni dhahiri kwamba ni mafisadi wafungiliwe mbali katika jela iliyo kisiwani basi Tanzania itaanza kupata maendeleo kwa njia ya osmosis. Wapo watu wanaamini kabisa kwamba leo hii Chama cha Mapinduzi (CCM) wakiondolewa tu madarakani basi matatizo yote ya nchi hii yataondoka automatically na chama hicho kikongwe barani Afrika. Na kwamba baada ya hapo, eti mara moja wananchi wataanza kuishi kwa neema na furaha ya maisha bora. Hizo ni ndoto tu. Na kila mtu ana haki ya kuota.
Na hii ndiyo aina nyingine ya upotofu ambao hatuna budi kuushughulikia kwanza kabla hatujaenda mbali kuzungumzia mabadiliko ya aina yoyote tunayohitaji kama jamii na kama Taifa. Tunao ushahidi wa kutosha kuthibitisha kwamba tunaweza kuwaondoa CCM madarakani kesho, tukaruka ruka, tukashangilia lakini baadaye tukarejea kule kule. Tukawa bado hatujatatua kiini cha matatizo yetu.
Kama nilivyodokeza katika makala zilizopita, ni dhahiri kwamba wapo watu, wakiwamo wanasiasa na watendaji, ambao hushangaa sana wanaposikia baadhi yetu tukiandika na kueleza kutokuridhishwa kwetu na mambo yalivyo au yanavyoendeshwa. Wapo Watanzania wenzetu ambao wao wakiwa ndani ya ofisi nzuri zenye viyoyozi, na baada ya hapo wanakuwa ndani ya magari mazuri ya kifahari yanayonunuliwa kwa fedha za walipa kodi; huku wakisafiri kila leo nchi za nje kwa posho nono, na wanapata mapato ya kuwafanya waishi kama wako Ulaya; hawa ukiwaambia kuna matatizo nchi hii hawakuelewi!
Lakini ni dhahiri kwamba haihitaji aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini wakati wa ukaburu, Peter Botha, au Professor James Watson wa Marekani watumie akili nyingi kuhitimisha kwamba watu weusi wana matatizo ya kufikiri.
Hivi kwa mfano, leo hii Jenerali Kinjekitile Ngwale, Mfalme Mkwawa wa Iringa na hata Mfalme Mirambo wa Tabora wakifufuka na kukuta Mkuu wa Wilaya (mweusi) wa Tanganyika huru anaongoza juhudi za kuwaswaga wananchi masikini weusi ili ardhi yao wakabidhiwe wale wale ambao wazee wetu walijitoa mhanga kuwafukuza, watatuelewaje? Tutawajibu kuwa ndiyo utandawazi? Tutawaambia wamepitwa na wakati?
Hivi tuchukulie kwamba miaka takriban 50 ya uhuru tumeshindwa kulima na tukajitosheleza kwa chakula. Tuchukulie pia kwamba wananchi wetu wenyewe ni wavivu au wajinga au chochote kile kiasi kwamba wameshindwa kabisa kujitegemea!
Hivyo basi, kwa vile hivyo ndivyo ilivyo, inabidi watafutwe wawekezaji (tena kutoka kule kule), wabembelezwe, waje waulizwe wanataka wafanyiwe nini, halafu baada ya hapo wale kapuku watakaokuwa katika ardhi anayotaka mwekezaji watimuliwe wote, wakafie mbali ili mpendwa mwekezaji awekeze kwa raha zake.
Tumeshuhudia juhudi kubwa sana, hasa kipindi cha miaka ya 1990 na kuendelea, wakitafutwa wawekezaji kwa udi na uvumba na wakiuziwa mashirika yetu ya umma na viwanda huku vingine katika hivyo vilivyouzwa vikibadilishwa kuwa mahanga ya kutunzia mitumba kutoka ng’ambo!
Na viongozi wetu walikuwa wakitoa maelezo kwamba Waswahili wetu sisi walikuwa wameshindwa kuendesha mashirika ya umma na kwa vile yalikuwa yakijiendesha kwa hasara ilibidi yauzwe kwa wawekezaji kutoka nje (soma wenye akili zaidi). Na kulikuwa na lugha inazungumzwa na viongozi ‘weusi’ kwamba “hawa Waswahili wetu” wasingeweza kuwekeza katika mengi ya mashirika yaliyokuwa yakiuzwa.
Lakini watawala hao hao ambao ndio waliokuwa wakiwasimamia hao walioshindwa kuendesha mashirika wakaendelea kubaki madarakani kuendesha nchi. Hapa mantiki ina jam. Kama ni hoja kwa Kiingereza inaitwa falacy. Kwamba “Waswahili wetu” wanashindwa tu kuendesha shirika la watu mia moja lakini eti wana uwezo wa kuendesha nchi yenye mashirika lukuki na raia milioni 30!
Lakini mzaha wenye mantiki zaidi huenda ungehusu umuhimu wa wale wale walioshindwa kusimamia uendeshaji wa mashirika ya umma hadi yakafa nao watangaze ubinafsishaji wa serikali ili waje wawekezaji waendeshe nchi.
Mantiki yake ni rahisi. Kwamba inawezekanaje viongozi au watawala waliotokana na jamii ya watu wavivu ambao hata kulima chakula cha kutosheleza mahitaji yao wanashindwa; jamii ya mameneja wanaoshindwa kuendesha mashirika ya umma hadi yanakufa kutokana na hasara; jamii ya aina hiyo inawezaje tena kutoa viongozi wenye uwezo wa kubuni, kupanga na kusimamia uchumi unaoendeshwa na wawekezaji tuliowavuta kutoka nje?
Ifanyike hivi: Vyama vyetu viendelee kushiriki katika chaguzi. Kwanza vyama vyote kwa ujumla wake hapa nchini havina hata zaidi ya wanachama milioni tano. Kwa hiyo hata uhalali wa vyama hivyo bado ni mdogo. Ushauri wa kimantiki ni kwamba chama kitakachoshinda uchaguzi ujao kijaribu tu fikra mpya. Kitangaze tenda ya kimataifa kuvutia kampuni au kikundi cha consultants, kutoka nchi zilizoendelea wanaoweza kuja kuongoza nchi kwa kipindi cha miaka mitano. Halafu wao viongozi wetu (weusi wenzetu) wakae pembeni kabisa, wakila kuku na starehe nyingine watakazoona zinawafaa ili wawaachie wawekezaji wapya waongoze serikali kwa ufanisi ule ule wanaouonyesha katika kuendesha mashirika yaliyokuwa yamefilisika au wanavyolima mashamba tunayowapa kwa maelfu ya ekari baada ya kuwafukuzilia mbali wananchi wetu kapuku. Ni wazo tu.

 
Back
Top Bottom