Kwa nini kuna sheria moja kwa masponji na nyingine kwa masimenti?

X-PASTER

JF-Expert Member
Feb 12, 2007
11,610
1,810
Katika peruzi peruzi kwenye mtandao wa Raia mwema nimekutana na Makala hii amabao nikaona si vibaya nikashirikiana na wenzangu kuisoma.

Kichwa cha habari kinakwenda kwa jina ili:

Kwa nini kuna sheria moja kwa masponji na nyingine kwa masimenti?


Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.

VIPI mpenzi,

Unaendeleaje? Nimefurahi mno mno mno kusikia kwamba utakuja baada ya wiki moja. Yaani mpenzi. Nina furaha kuliko hata yule aliyeshinda kura za maoni bila kumulikwa ametoa rushwa teh teh teh. Njoo mshindi wangu nami nikupongeze na mahaba yote niliyo nayo.

Kwa kweli hapa mambo ni yaleyale tu. Uchaguzi … uchafuzi … uchaguzi … uchafuzi. Ila wiki hii ilibidi nicheke. Nilikuwa jikoni naandaa supu ya bosi nilipomsikia mlinzi anabishana na mtu getini. Kwa ushambenga wangu ilibidi nitoke na kusikiliza maana si kawaida kusikia mabishano vile maana ni wachache sana wanaothubutu kupenya maeneo ya miungu.

‘Hakuna kuingia.’

‘Sitaki kuingia. Nataka umpe kibosile wako hii barua tu.’

‘Hebu shika adabu. Hapa uko kwa Mheshimiwa Waziri wa Mikiki na Makeke, si kibosile.’

‘Ninajua. Ndiyo maana nipo hapa. Nimeleta barua kwa ajili yake. Ni muhimu sana.’

‘Barua muhimu haziji kwa njia hii.’

‘Sasa sikiliza kaka, unataka bosi wako ashinde uchaguzi au asishinde?’

Hapo mlinzi alilazimika kutafakari kidogo, asije akamwaga unga kwa kuwa mkali bila sababu. Hatimaye alichukua na kunipa mimi. Nikaichukua na kuweka mezani ili bosi aikute wakati anakuja kunywa supu. Kisha nikarudi jikoni.

Lo! Wakati namalizia kupakua supu, sauti iliyotoka, kidogo nidondoshe kila kitu.

‘Nani? Nani kaniletea huu upuuzi hapa. Nani!!!!’

Ilibidi niende japo kwa kutetemeka. Nikamkuta bosi ameshika ile barua huku akitweta kwa hasira.

‘We Hidaya, ni wewe umeleta?’

‘Ndiyo baba. Alisema ni muhimu sana ili uchaguliwe.’

‘Na wewe unaamini kila upuuzi unaoambiwa? Sasa kama ameweka bomu humu ndani?’

‘Samahani baba.’

‘Samahani ya nini. Sasa wanaona wanaweza kunitukana hadi nyumbani kwangu. Watanitambua.’

Na bosi akaamka na kujiondokea. Akasahau hata supu yake. Na ile barua pia. Baada ya kuhakisha kweli ametoka ilibidi niibeibe kujua mambo gani yamemkasirisha hivyo. Kumbe ilikuwa ni barua kutoka kwa wafungwa wa jela fulani. Siwezi kukumbuka maneno yote lakini barua ilisomeka kama hivi.

Mheshimiwa Waziri wa Mikiki na Makeke; Sisi wengi hapa tupo kwa ajili ya mikiki na makeke ya maisha ndiyo maana tumeona bora tukuandikie wewe baba yetu.

Kwanza kabisa tunapenda kukupongeza wewe na chama chako mnavyojitahidi sasa kuwakamata wakubwa badala ya sisi wadogowadogo. Wanaotoa rushwa wachaguliwe kweli wana uwezo sana ndiyo maana wana hela za kumwaga vile. Laiti wangetumwagia sisi. Kwa hiyo wale wachache waliokamatwa ni mwanzo mzuri sana na tunangoja wakamatwe wengine wengiwengiwengi maana tunao uhakika kwamba si wale tu. Na tunawakaribisha sana hapa petu waje wahonge mende na kunguni wasiwasumbue usiku.

Kwa ukarimu wetu, tuko tayari kuwagawia hawa mende na kunguni na wadudu wote wengine ili tuwe na haki sawa ndani ya jela, kulingana na sera zenu nzuri.

Mheshimiwa tunarudia kusema kwamba tumefurahi sana kuwaona hawa wakikamatwa. Hii kidogo imerudisha imani yetu kwa chama chenu kitukufu lakini tusipowaona hawa wakija kujiunga nasi, pamoja na wale wengine wengi waliovunja sheria kwa kuhonga vilevile imani yetu itapotea tena. Tunavyojua sisi, kuhonga ni kosa la jinai na kupokea hongo ni kosa la jinai pia ndiyo maana tunashangaa kwamba hawa wakosaji wote hawajajiunga nasi hadi sasa. Itakuwa ni heshima kubwa kwetu wakija tuweze kupangwa pamoja kwenye kundi rasmi la wahalifu.

Mheshimiwa tunafurahi pia kwa sababu hawa waliozoea masponji wakija kukaa na sisi tuna uhakika kwamba watapiga kelele kwa masponji wenzao kuhusu hali mbaya ya mazingira hapa jela. Hata wakikaa muda mfupi, watakuwa wameona na kuonja jinsi tunavyokula shida huku ndani.

Ingawa tunadhani wengi walikuwa wanasema eti tunastahili kula shida hivyo kwa sababu ni wahalifu, tunao uhakika kwamba wakishaonja pepo zetu hapa, watabadili msimamo. Kila mtu ana haki ya kuishi kama binadamu si kama tunavyoishi hapa.

Hivyo, tunao uhakika kwamba wakitoka hawatusahau sisi na watapigania kubadilika kwa hali zetu pia. Na hayo yatakuwa na mafanikio mengine mazuri ya sera yenu.

Ila, mheshimiwa, tuna wasiwasi mmoja na tunaomba utusaidie hapo. Wakikamatwa wote hao, na tunao uhakika kwamba kulingana na sera yenu ya kuchukia aina zote za uhalifu, mtawakamata wote, waliotoa na waliopokea hadi ziwatoke puani, nafasi zipo za kutosha kweli?

Si unajua mheshimiwa tayari tumebanana humu kiasi kwamba mnene anachukiwa maana anachukua nafasi ya watu wawili. Kidogo tushindwe kupumua kabisa. Sasa, kama wanaletwa wote hawa, utawaweka wapi? Au itabidi mgeuze majengo mengine kuwa jela za muda?

Ndiyo maana tunapendekeza kwamba sisi wahalifu wa hali ya chini, wahalifu wadogowadogo tuachiwe, ili tuwapishe hawa masponji. Tumeshaadhibiwa sisi ingawa tulio wengi makosa yetu yalitokana na umasikini unaonuka. Kwa hiyo, tuachiwe sisi tuwapishe hao ambao hawakuwa na shida kama sisi ila uchu wao umewaacha uchi.

Kwa njia hiyo tunajua kabisa kwamba chama chako kiko mstari wa mbele kukomesha uhalifu wote huo. Na msipowakamata wote, tuna wasiwasi kweli na hali ya baadaye ya nchi yetu, yaani sisi wadogo tuswekwe, wengine waachiwe, na tutazidi kutawaliwa na wahalifu ambao ndio waliostahili kuwa ndani ya jela.


Basi mpenzi naona barua iliendelea lakini nilishindwa kumaliza maana ghafla nilisikia mlango unabamizwa kwa nguvu. Nilikamata bakuli ya supu harakaharaka na kuanza kutoka.

‘We Hidaya unafanya nini hapa?’

‘Natoa bakuli ya supu baba, maana imeshapata ubaridi.’

Yaani mpenzi, kwa jinsi bosi alivyoniangalia kidogo nidondoshe bakuli, lakini nilijikaza huku nikiangalia chini kwa unyenyekevu.

‘Sina hamu na supu yako tena. Na ni mwiko, mwiko unasikia kupokea barua kutoka kwa mtu yeyote usiyemfahamu.’

‘Ndiyo baba.’

Basi bosi akachukua ile barua na kuweka mfukoni, kisha kageuka na kutoka tena, huku bado akitweta kwa hasira.

‘Haiwezekani wameandika wenyewe. Maadui … maadui wapo kila mahali … Lakini watanitambua …’

Kwa hiyo mpenzi, na mimi nilikunywa supu ya nguvu asubuhi asubuhi shauri ya wahalifu wa simenti wakiwakaribisha wahalifu wa sponji. Bila shaka bosi kawahurumia masponji wenzie ndiyo maana amekasirika vile.

Lakini unaona mpenzi. Msponji akivunja sheria, inapewa majina mengi ili ionekane hajavunja sheria, kisha apewe onyo au adhabu laini. Lakini msimenti atasota na hiyo simenti hadi akome. Kwa nini kuna sheria moja kwa masponji na nyingine kwa masimenti?

Akupendaye msimenti mwenzangu hata kama nadowea maisha ya masponji kidogokidogo.

Hidaya
 
Back
Top Bottom