Kwa haya tanzania yenyewe yafaa kuwa moja ya maajabu saba ya dunia

Kurunzi

JF-Expert Member
Jul 31, 2009
9,271
9,900
RAFIKI yangu Dk. Lupembe alinipa wazo.
Daktari Lupembe anasema badala ya watu
kuhamasishwa wapigie vivutio vya utalii
viingizwe kwenye maajabu saba ya dunia, ni
afadhali tuipigie Tanzania kura iingie kwenye
maajabu hayo.
Kwa hakika hatutatoka haba maana Tanzania
kwa yenyewe ni moja ya maajabu kutokana na
yanayoendelea na yatakayoendela. Unabisha?
Ni wapi kwingine isipokuwa Tanzania utamsikia
waziri wa Nishati na Madini akijiapiza kwa
miungu yake kwamba hakuna mgawo wa
umeme wakati ukiwa njiani kwenda kibaruani
lakini unafika kibaruani unakuta umeme
umekatika na unapoulizia sehemu nyinginezo
unaambiwa huko nako hakuna umeme!
Kweli inaingia akilini kuambiwa eti
wanarekebisha miundombinu wakati kwa akili
ya kitoto tu huo ni mgawo wa umeme? Isitoshe
kwetu mgawo ni mgawo tu. Iwe ni kwamba
wameshindwa kuilipa Dowans au iwe ni
ukarabati wa miundombinu au iwe hitilafu ya
mitambo au kushuka kwa kina cha maji. Hayo
hayatuhusu.
Sisi tunataka umeme na katizo lolote la
umeme kwa sababu yoyote huo ni mgawo wa
umeme. Full stop. Ni wapi kwingine mgawo
huo unakuja kinyume cha ahadi ya serikali na
watu wakakaa kimya kama waliowekewa gundi
mdomoni? Tanzania ni moja ya maajabu ya
dunia.
Hayo ya umeme na porojo wanazopewa
Watanzania weka kando. Hebu rejea kwenye
elimu. Tuna wizara na taasisi za elimu
zinazohusika na elimu hiyo hiyo lakini ni kama
watu tunaopaka hewa rangi au tunaotwanga
maji kwenye kinu. Kelele nyingi na ahadi kibao.
Ni Tanzania pekee ambako utakuwa wanafunzi
hawana madawati wanakaa chini na wengine
kwenye vyumba visivyostahili kuitwa vyumba
kwa ubovu na uchakavu wake lakini ukasikia
ahadi ya kila mwanafunzi kupewa kompyuta ya
majani a.k.a laptop. Hiyo huwezi kuikuta
popote na bado hamuamini Tanzania ni ajabu la
dunia?
Unatoa ahadi ya kompyuta kwa kila mwanafunzi
huku hawana dawati wala vitabu? Hapo
hujazungumzia hoja ya umeme. Bado hamuoni
haja ya kuishangaa Tizedi?
Na kama hiyo haitoshi haijawahi kusikika
popote ulimwenguni kwamba kuna mhitimu
aliyefaulu mtihani wake tena mtihani wa
kufanywa kwa njia ya maandishi huku yeye
mwenyewe akiwa hajui kusoma wala kuandika.
Ni wapi ulimwenguni kwenye data za kuonesha
hilo la kufaulu mtihani wa maandishi bila
aliyefaulu kujua kusoma na kuandika? Hakika
hili lipo Tanzania peke yake na linafaa kuifanya
Tanzania moja ya majabu ya ulimwengu huu na
watalii wakaribishwe waje kujionea maajabu
haya.
Kama bado unashangaa, hayo machache
jiandae kushangaa zaidi. Ni wapi kwingine
kiongozi wa chama tawala atawaambia watu
kwamba hajui chanzo cha umaskini wa watu
wake kisha akarudi katika uchaguzi kwa
kaulimbiu ya maisha bora kwa kila mtu halafu
akapeta pia kwenye huo uchaguzi? Hii ipo
Tanzania peke yake ambapo watu wanakichagua
chama hicho hicho kwa miaka hamsini licha ya
ukweli kwamba chama hicho hakijajua sababu
ya umaskini wao licha ya kuimba mapambio ya
neema kwa watu wote. Ni wapi kwingine
utapata maajabu haya?
Hakuna sehemu yenye maajabu kama Tanzania
ambako watu kusahahu ni sehemu ya maisha
yao. Ni Tanzania tu ambako yanaweza
yakatokea kama yaliyomkuta Dk. Ulimboka
watu wakajidai kupata kiwewe halafu ndani ya
mwezi mmoja watu wameshasahau kabisa
kilichotokea na si ajabu wengine wakisoma
sehemu hii wanajiuliza hivi Dk. Ulimboka ni
nani?
Hii ipo Tanzania tu ndugu zangu. Ni Tanzania hii
hii anaweza kuibuka babu akwaambia
nazungumza na Mwenyezi Mungu na amempa
dawa na watu wakapanga foleni kama wasio na
akili kwenda kupata muujiza wa Mungu
unaouzwa shilingi mia tano. Mungu wa wapi
anafanya biashara zama hizi na nyie hata
hamjiulizi?
Hii miujiza utaipata Tanzania tu maana hata
wataalamu wa teolojia walinaswa katika mtego
huu ambao ulipaswa kuchukuliwa kama
sinema.
Na hayupo anayeulizia babu yule kaishia wapi
na wala hakuna anayefanya utafiti ni madhara
kiasi gani yamepatikana. Na hata watu wa
mamlaka ya kodi hawakuthubutu kwenda
kukusanya kodi licha ya biashara ile ya dawa
kutangazwa kila kona. Labda waliogopa kumtoza
Mungu kodi maana babu alituambia
anawasiliana na Mungu ana kwa ana! Haya
yanatosha kuifanya Tanzania iwe moja ya
maajabu ya dunia.
Kama unadhani ni hayo tu yanaifanya Tanzania
istahili kupigiwa kura kuwa kwenye moja ya
maajabu saba ya ulimwengu bado umekosea,
yapo mengi sana.
Ni wapi tena ulimwenguni linapokuja suala la
barabara unakujta barabara iliyotengenezwa
kwa minajili ya njia mbili yaani ya kwenda na ya
kurudi lakini serikali inaamua zigeuzwe ziwe
njia tatu, mbili za kwenda na moja ya kurudi
bila upanuzi wa barabara hiyo.
Kama wadhani haya ninayoyasema ni hadithi ya
kufikirika nakushauri ukaitembelee Barabara ya
Ali Hasaan Mwinyi huko Dar es Salaam ujionee
siasa zinavyoweza kufanya kazi ya kitaalamu.
Hakuna anayeshangaa licha ya ugumu wa
magari kupishana njia ya katikati.
Nauliza ni wapi kwingine utakakokuta njia rahisi
na salama inayokubalika na askari wa usalama
barabarani kuruhusu magari yapipte njia zote
mbili kuelekea upande mmoja?
Kwa utimamu wa akili kabisa polisi wanazuia
magari upande mmoja kwa muda na kuruhusu
magari yanayoelekea upande mmoja kupita
sehemu zote za kulia na kushoto kwa barabara.
Ulishawahi kufikiria katika mtindo huo nini
kitatokea iwapo kuna dharura mathalani ya
moto au mgonjwa na njia zote mbili zimezibwa
kuelekea upande unaohitaji gari kufika? Hiyo ni
ajabu tosha kwa nchi yetu. Na hata kutanua,
yaani kupita kando kando ya barabara imekuwa
kama halali vile.
Asiyejua hili apite njia ya Old Bagamoyo hasa
maeneo ya Kawe ndipo atajua kwamba Tanzania
hata watu binafsi wana uwezo wa kubadili
sheria ya Bunge tena machoni mwa askari
polisi.
Kwenye barabara hiyo ule utaratibu wa magari
yanayokwenda mwelekeo mmoja kupita kulia
na uelekeo mwingine kupita kushoto
ulishasahaulika. Kama wewe ni dereva unapita
popote unapoona upenyo! Hiyo bado haiwezi
kutuweka katika moja ya maajabu saba ya
dunia?
Maajabu ni mengi. Daktari Lupembe anasema
hapa kwetu utakuta tuna wizara ya viwanda
lakini uliza hiyo serikali ina viwanda vingapi.
Utakuta kuna wizara inayohusika na maji, lakini
jiulize shida ya maji kwa nini haimaliziki licha
ya vyanzo vyote tulivyo navyo.
Yapo mengi tena sana ya kushangaa na hivyo
kustahili kuifanya Bongo kuwa moja ya vivutio
vya utalii ili watu waje washangae
yanayoshangaza.
Haya ni machache bado hujazungumzia chenji
ya rada, twiga kupakia ndege na kwenda
ughaibuni, polisi kutuhumiwa kuua kisha
wenyewe kuunda tume kuchunguza na wakati
tume inachunguza mtuhumiwa yuko
mahakamani!
Bado yapo mengi ya kushangaza kama vile
waziri kuunda tume, halafu anaambiwa hana
mamlaka, anasema ameunda kamati na
vyombo vya habari viko kwenye usingizi wa
pono, biashara inaendelea kama hakuna
lililotokea! Hii ni Tanzania na Tanzania ni zaidi
ya uijuavyo.
 
Naunga hoja, unakuta nchi ina mari kibao lakini ndio inayoongoza kwa kuomba msaada ulimwenguni
 
maelezo ya Lupembe yanaelezwa kwa maneno mawili tu "Lawless Country!!"
 
Back
Top Bottom