Kuuzwa mitambo Dowans balaa

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,005
Kuuzwa mitambo Dowans balaa



*Yadaiwa ni kitendo cha kudharau mahakama

Na Rabia Bakari
Majira

KUUZWA kwa mitambo ya Dowans kwa kampuni ya Kimarekani ya symbion Power kumezua balaa jipya baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuombwa iwakamate wahusika wa mitambo huyo kukamatwa na kupelekwa gerezani kwa kudharau mahakama.

Aliyetoa maombi hayo ni Mwandishi wa habari mwandamizi anayepinga Tuzo ya Dowans iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) kusajiliwe na Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Timoth Kahoho.

Bw. Kahoho aliwasilisha ombi hilo jana mchana akiwataka wakurugenzi wa Dowans Holdings SA na Dowans Tanzania Limited kukamatwa baada ya kudaiwa kuuza mitambo ya Dowans kinyume na kauli ya mahakama iliyotaka kampuni hiyo kutoa taarifa mahakamani kwa chochote ikatakachotaka kufanya.

Mnamo Machi 3, mwaka huu, Jaji Emilian Mushi anayesikiliza kesi ya kuomba kusajiliwa kwa tuzo ya Dowans alitoa amri ya kutaka pande zote mbili katika kesi hiyo 'kuacha mambo yote kama yalivyo' na endapo watataka kufanya jambo lolote wangepaswa kuomba kibali cha mahakama.

Katika ombi lake la dharura, Bw. Kahoho anadai kuwa wakurugenzi wa Dowans wamekwenda kinyume na agizo hilo baada ya kudaiwa kuuza mitambo ya kampuni hiyo bila kuomba kibali cha mahakama.

Katika maombi hayo, Bw. Kahoho alidai kuwa taarifa za madai ya kuuzwa mitambo ya Dowans ziliandikwa na gazeti la The African la Mei 21 mwaka huu, lilichapisha habari mitambo ya Dowans imeuzwa kwa kampuni ya Symbion Power ya Marekani kwa thamani ya dola za Marekani 120.

Sambamba na ombi hilo, pia Bw. Kahoho ambapo kwa mujibu wa hati yake ya maombi, anaiomba mahakama itoe amri ya kuwataka wadaiwa hao waweke dhamana dola la Marekani 120 kama dhamana, na walimpe gharama za kesi hiyo aliyoifungua jana.

Hata hivyo ombi hilo ambalo limewasilishwa chini ya hati ya dharura bado haijapangiwa jaji wa kuanza kuisikiliza.

Katika kesi ya msingi ya kupinga kusajiliwa tuzo ya Dowans itatajwa Julai 28, mwaka huu mbele ya Jaji Mushi, mbali na Bw. Kahoho wengine wanaopinga tuzo hiyo ni Kituo cha Kutetea Haki za Binadamu (LHRC), Shirika la Umeme (TANESCO), ambao wanapinga tuzo ya Dowans isisajiliwe.

Mapema Januari 25 mwaka huu, Dowans iliwasilisha ombi lake la kutaka Mahakama Kuu ya Tanzania isajili tuzo waliyopewa na ICC na siku chache baadaye Tanesco, LHCR, Kahoho wakawasilisha hati ya nia ya kupinga ombi hilo la kutaka tuzo hiyo isajiliwe kwa kuwa mahakama hiyo ya kimataifa haikuzingatia sheria za nchi katika hukumu yake.

Mahakama ya ICC, ilitoa hukumu ya kesi ya Dowans dhidi ya TANESCO, Novemba 15 mwaka jana, na kuitia hatiani Tanesco kwa kosa la kuvunja mkataba na Dowans na ikaimuru iilipe fidia ya sh. bilioni 94.
 
Back
Top Bottom