Kutoka London:Harusi za majuu ghali, lakini hakuna kadi za michango

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,315
33,111
Na Freddy Macha

KILA mtu anajua kuwa harusi ni tukio muhimu katika maisha ya mwanadamu na ni tukio ghali zaidi kuzidi yote. Lakini kwa ‘Majuu,’ gharama za harusi hazisemeki. Si ajabu kuona watu wanaoana kimya kimya maana utamwalika nani akuchangie?

Gharama za vyumba, vinywaji, maakuli si mchezo. Huku uzunguni huwezi ukaitisha mkutano au kutoa kadi kutaka wafanyakazi wenzako au marafiki wakuchangie.

Harusi, huwa shughuli za bwana na mkewe tu basi. Mara nyingi wazazi huelezwa tu badala ya kuwa waamuzi wakuu wa shughuli. Hivyo sishangai ninavyoalikwa harusi hii Uswisi nikashuhudia ugomvi kati ya wazazi na binti yao.

Rafiki yangu kanilalamikia:
“Mwanangu si yule mwali wa kinyumbani niliyemlea. Ingekuwa kwetu Afrika angefuata tu masharti. Nilipomuuliza mtoto vipi huyo bwana atanipa mahari, nikaangaliwa kama nimesema punda hula nyama.”

Rafiki yangu alifurahia sana binti yake alipokuja nchi hizi kusoma. Msichana alikuwa na heshima. Akamaliza shahada ya kwanza. Wakati anaanza shahada ya Uzamili, akakutana na kijana mwenzake wa huko huko Afrika. Wakavaana. Kuna wakati wazazi walipowatembelea wakafurahia namna vijana walivyopendana. Baada ya mwaka mambo yakaharibika. Binti akadai yule mmatumbi mwenzie alikuwa mwingi wa mabibi. Baadaye akasheheni mwingine.

Mambo yakawa siafu zaidi, wakaachana- sababu eti alikuwa na mke nyumbani, Afrika na watoto. Vibaya zaidi alimwacha mjamzito na kutokana na ugumu wa maisha ya kusoma na kufanya kazi, dada wa watu akaamua kuitoa mimba.

Mama mtu ananieleza: “Kuanzia hapo binti kawa mwingine. Kaapa hatokwenda tena na wanaume wa Kiafrika. Sisi hatukupenda hata kidogo. Kufumba na kufumbua tumeambiwa wameshachumbiana na kijana wa Kizungu. Kugeuka mwaka umekwisha; tunaalikwa harusini.”
Wazee wakanitafadhalisha nijaribu kuongea na binti.

Vijana wa huku Uzunguni nadra kumsikiliza mtu mzima. Akili zao hufuata wakitakacho. Wazee hawastahiwi. Zamani tukikua, tulihofia laana za wazee. Vijana wa leo huku Majuu, hawayajui hayo. Husema : “Wazee wanatakiwa watuheshimu sisi, ndiyo na sisi tutawaheshimu.”

Basi nikamfuata msichana wa watu.
“Vipi anko, yamekuleta nini huku?”
Nikamweleza wazee wake wameniomba nichunguze mahusiano yake na Dieter(jina bandia), Mswisi aliyeamua kuoana naye.

“Yaani wamekufanya polisi wakunichunguza.”
Si uaskari, bali mila za kikwetu, nkajitetea. Tendo...la kuhakikisha mtoto hapatwi na matatizo baadaye.
Baada ya malumbano ya moto, binti akanipeleka kwake. Nikakutana na Dieter kijana wa Kizungu mpole, mrefu, mweupe, dada wa kwetu maji ya kunde. Uzuri uliowakubali yale mapenzi yao.

Binti akapiga yowe: “Wazee wana wasiwasi. Si unajua watoto wa kichotara wanavyopata shida? Hata kwetu watoto wa mchanganyiko bado hutaniwa. Bado watu nyumbani hutumia maneno ya kizamani kama hafkasti (“Half-caste”). neno la ubaguzi ambalo limeshapigwa marufuku huku Uzunguni lakini nyumbani bado linatumika kumwita mwanadamu nusu mtu.”

Binti kanijuza Dieter kaanza kujifunza Kiswahili na kupika ugali. Kapania lazima siku moja si kutembee Afrika, bali akaishi. Anapenda Afrika, kasoma habari za Mandela, Nyerere na Nkrumah. Baada ya harusi wamepania wakafunge fungate kwa kupanda Mlima Kilimanjaro.

“Miye siwezi kuupanda huo mlima lakini Dieter na wenzake wawili wamesema wataukwea tu.” Hayo kwangu yalinitosha.
Miaka ya karibuni takwimu zimeonyesha kuwa mahusiano ya ndoa kati ya wanawake weusi na wanaume wa Kizungu hudumu na kunufaika kuliko kati ya wanaume weusi na wanawake wa Kizungu. Kwa wanaume weusi na wanawake wa Kizungu mizozo huwa mingi, kila mmoja anataka kumtawala mwenzake ilhali kwa kina dada weusi maelewano ni rahisi zaidi.

Basi yakaisha kwa kuwapa habari wazee wa msichana kuwa mambo si mabaya.
Huyu ni kijana anayeheshimu utamaduni wa mkewe anayeipenda asili ya mpenziwe. Wanapendana. La zaidi nini?
Wazee wakaheshimu kauli.
Harusi ikapangwa. Harusi ikafanyika.
Harusi kama tulivyosema awali aghali sana Uzunguni.
Wazee wanataka ndugu wahudhurie. Wajomba, shangazi, binamu, kaka na dada. Watoto bado wanasoma na hata kama wangekuwa wamemaliza masomo hawangeweza kugharamia nauli za ndege kwa ndugu wote hao ambao wazazi walitaka waje.

Nauli kutoka Afrika Mashariki hadi Ulaya ni wastani wa dola 1,000 (Sh 1.5 milioni ) Si pesa kidogo. Nusu ya pesa hizi ni kodi na bima ya kusafiri ambavyo hutozwa na mashirika makubwa ya ndege. Nusu iliyobakia ndiyo nauli. Kifupi nauli si kubwa kodi, ushuru na bima ndivyo vinavyoongeza uchungu wa pilipili.

Kwetu Afrika ukisafiri na basi likapinduka, ukaumia, si kawaida mwenye basi kulipa gharama za tiba. Je nauli unayolipia inayo sehemu ya bima yako ya maisha? Sidhani. Maana ingekuwa abiria wanaojeruhiwa au kufariki kutokana na ajali za usafiri Bongo zinazotokea kila mwezi wanalipiwa fidia tungesema mengine.

Hiyo ndiyo moja ya sababu nauli za ndege kuwa kubwa ndani ya safari hizi za kimataifa.

Ugomvi wa nani aalikwe ulikuwa mkubwa. Watoto Majuu wamesema watawaalika marafiki zao wanaowajali. Watafanya karamu ndogo inayowafaa wao. Wazazi wa pande zote wataalikwa kwa heshima yao. Watapewa sehemu ya kulala pia watalishwa lakini zaidi yao hakuna wengine.
Ili kupunguza gharama ukumbi ambao watoto waliamua kufanyia harusi ndipo pia yote yalipomalizwa. Ulikodishwa tangu saa sita mchana hadi saa sita usiku. Akaalikwa ofisa wa kufunga harusi toka halmashauri ya jiji, akaja na makatarasi yake.

Idadi ya wageni ilikuwa 40 wengi vijana wenzao. Baada ya shughuli kufanywa maharusi wakatoka nje katika bustani za ukumbi kupiga picha.

Baada ya picha wageni tukapewa kinywaji cha kwanza ambacho kwa Kizungu huitwa “Champagne.” Watu sasa tukalegea, tuna nishai kidogo.
Saa moja baadaye mmoja wa wale mashoga zake binti akatangaza waiingie ndani kula keki kwa chai na kahawa. Pale pale kwenye ukumbi. Wageni tukaambiwa tutawanyike tutembee kidogo kunyoosha miguu. Karibu na pale lilikuwepo jumba la makumbusho ya historia ya mji. Tukatembezwa. Saa kumi na mbili jioni tukarudi tena ndani kupata msosi.

Wakati wa chakula zikatolewa zawadi na hotuba za wazazi, ndugu na marafiki. Tofauti kubwa kati ya harusi Bongo na Majuu ni suala la zawadi. Maharusi huandika orodha ya vitu wanavyotaka wapewe.

Wapo wanaosema wanataka tu pesa. Wengine huandika vitu wanavyohitaji kama bidhaa za kupika, shuka, nk. Ndiyo hivyo. Ikabaki rumba, disko na Ndombolo hadi saa sita usiku juu ya alama. Tusingepitisha mida zaidi maana malipo hayakuruhusu.



-London, 21 Mei, 2012
-Barua pepe: kilimanjaro1967@hotmail.com
-Tovuti: Freddy Macha
 
Back
Top Bottom