Kupanda miti siku ya wajinga

Ngalikihinja

JF-Expert Member
Sep 1, 2009
31,244
31,354
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII


TAARIFA KWA UMMA.
MABADILIKO YA SIKU YA TAIFA KUPANDA MITI
Serikali imebadilisha Siku ya Taifa ya Kupanda Miti kutoka Januari Mosi ya kila mwaka na kuwa Aprili Mosi. Mabadiliko hayo yametokanana Waraka wa Waziri Mkuu Na 1 wa mwaka 2009 kuhusu kubadili Siku ya Taifa ya Kupanda Miti kutoka Januari Mosi na kuwa Aprili Mosi ya Kila mwaka.

Kwa mujibu wa waraka huo, kuanzia mwaka 2010 Siku ya Taifa ya Kupanda Miti itaadhimishwa Aprili Mosi ya kila mwaka. Waraka huo unaanza kutumika rasmi tarehe 01 Juni, 2009 na unafuta waraka wa Waziri Mkuu Namba 1 wa Oktoba, 2000.
Uamuzi wa kubadilisha siku hiyo unatokana na mapendekezo yaliyotolewa na Mhe. Jakaya Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Januari Mosi 2008 aliposhiriki maadhimisho ya Siku ya Taifa ya Kupanda Miti na kutaka maadhimisho hayo yahamishiwe kipindi ambacho sehemu nyingi za nchi zitakuwa zinapata mvua.

Kwa mujibu wa waraka huo, Aprili Mosi itakuwa ni siku ya Taifa kuhamasisha upandaji miti huku kila mkoa ukiendelea kujipangia Siku ya Kupanda Miti kutokana na majira ya mvua yatakavyoruhusu. Ili kazi ya kupanda miti iwe inatekelezwa na wadau wote, Waraka huo umeagiza Wizara, Mikoa, Wilaya, Viongozi wa wilaya, Halmashauri za Jiji, Manispaa na Mamlaka za Miji midogo, Tarafa, Kata, Vijiji na mitaa kuandaa programu za utekelezaji mapema iwezekanavyo.

Maafisa Misitu walioko mijini, mikoani, wilayani na vijijini wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu aina ya mbegu na miche inayofaa katika eneo husika na kushauri utayarishaji wa vitalu vya miche kwa wakati unaofaa.

Waraka umemtaka kila kiongozi ahakikishe zoezi la upandaji miti linatekelezwa na kusimamiwa ipasavyo kwenye eneo lake. Aidha, pamoja na masuala mengine kiongozi atapimwa kutokana na juhudi zake za kuhamasisha, kutekeleza na kusimamia wananchi kupanda miti. Halmashauri zote kwa kushirikiana na mamlaka husika, zihakikishe kuwa upandaji miti ni pamoja na kupanda kando kando ya barabara zote nchini.

Waraka huo umetahadharisha kuwa kupanda miti pekee hakutoshi kukabiliana na jangwa kama hatua za makusudi za kutunza na kulinda uoto wa asili hazitachukuliwa. Siku ya Taifa ya Kupanda Miti iliadhimishwa kitaifa kwa mara ya kwanza mwaka 2001 katika eneo la Jangwani mkoani Dar es Salaam.
Ezekiel Maige (Mb)
NAIBU WAZIRI

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
 
Back
Top Bottom