Kupanda kwa umeme kwazua kilio

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,011
Posted Date::12/29/2007
Kupanda kwa umeme kwazua kilio
Na Tausi Mbowe
Mwananchi

SIKU moja baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Nchini (Ewura), kubariki ombi la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kutaka kupandisha viwango vya matumizi ya umeme, wadau mbalimbali wamepinga hatua hiyo na kusema itazidi kuwaongezea makali ya maisha wananchi.

Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustino Mrema amesema hatua ya kuongeza gharama za umeme itaendelea kumgandamiza mwananchi wa kawaida.

Mrema alisema asilimia 21.7 waliyokubaliwa Tanesco kuongeza ni kubwa hasa ikizingatiwa kuwa wananchi wengi wana kipato kidogo kiasi cha kushindia mlo mmoja.

Alisema hatua hiyo itazidi kuweka matabaka na kufanya umeme kuonekana ni jambo la anasa kwani ni wananchi wachache pekee wataweza kumudu gharama hizo na kuacha wananchi wengi wakitumia vibatari.

Alisema Mtanzania amekuwa ni mtu wa kupata maumivu kila kukicha na kutoa mfano wa mfumuko wa bei katika baadhi ya bidhaa kama mafuta na chakula na sasa hata bei ya umeme inapanda.

Mrema alisema inachofanya serikali ni kuwalagahali wananchi wake na kutoa mfano kupandisha mishahara kisha kuongeza bei za bidhaa.

"Hivi karibuni serikali imetangaza kuongeza mishahara kwa sekta binafsi ifikapo Januari Mosi lakini kabla ya siku hiyo kufika tayari Mtanzania huyo anaongezewa bei katika vitu muhimu huu ni ulaghai mkubwa kwa wananchi," alisisitiza Mrema.

Nalo Shirikisho la Wenye Viwanda Nchi (CTI), lilisema kuwa kuwa ongezeko hilo ni kubwa sana ikilinganishwa na hali ya halisi ya Mtanzania wa kawaida.

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini kwa madai yeye si msemaji kutokana na viongozi wa shirikisho hilo kuwa likizo, mmoja wa viongozi wa Shirikisho hilo alisema ongezeko hilo litasababisha ongezeko la bei kwa kiasi kikubwa hivyo kusababisha maisha kuwa magumu zaidi.

Alisema viwanda vingi vimekuwa vikitumia nishati ya umeme katika kuzalisha bidhaa zao hivyo kupandisha gharama za umeme ni sawa na kuongeza bei za bdhaa hizo.

Alisema kuwa hali hiyo pia inachangia kwa kiasi kikubwa Tanzania kushindwa kuingia katika ushindani wa kibiashara duniani kwani itawalazimu kutumia gharama kubwa katika uzalishaji wa bidhaa zao hivyo kulazimika kuziuza bidhaa hizo kwa gharama ya juu ili kupata faida wakati nchi nyingine wanamikakati ya kupunguza bei.

CTI ni miongoni mwa wadau mbalimbali nchini waliokuwa wakipinga ongezeko la viwango vya gharama za umeme kwa asilimia 40 ambapo shirikisho hilo lilitoa maoni yake na kupendekeza ongezeko la asilimia 10 kila baada ya miaka mitatu.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Nchini (Ewura), juzi ilibariki ombi la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kutaka kupandisha viwango vya matumizi ya umeme nchini kwa wastani wa asilimia 21.7 pekee badala ya asilimia 40 iliyoombwa na shirika hilo awali.

Agizo hilo lililotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Haruna Masebu na kuanza kutumika rasmi kuanzia Januari Mosi mwakani liliwataka Tanesco kuongezeka kwa asilimia 21.7 kulingana na bei za sasa huku gharama za maunganisho kwa wateja wapya zitaongezeka kwa kati ya asilimia 66 hadi 215.

Kwa mujibu wa Ewura ombi Tanesco la nyongeza ya bei za gharama ya umeme lina mantiki na ni halali ukiondoa makosa kwenye takwimu zilizowasilishwa.

Kutokana na ongezeko hilo gharama za umeme kwa sasa zitapanda kutoka Sh128 hadi Sh156 kwa wati moja kwa wateja wa matumizi makubwa ya kaya na bei ya kila wati moja kwa wateja wa matumizi ya kawaida (general supply) itakuwa Sh129 kutoka Sh106 za awali.

Kwa upande wa msongo mdogo itakuwa Sh79 kwa kila wati moja badala ya Sh65 ilioyokuwa ikitozwa awali.Hata hivyo, kwa upande wa visiwa vya Zanzibar hali imekuwa mbaya zaidi kutokana na Mamlaka hiyo kubariki ongezeko la asilimia 168 katika bei zake za awali kutokana na visiwa hivyo kulipa viwango vidogo kwa muda mrefu na hakukuwapo upandishaji wa gharama hizo kwa muda mrefu.

Kwa upande wa gharama za maunganisho kwa wateja wapya pia zimeongezeka ambapo umbali wa mita 30 'single phase' bei hiyo imepanda mpaka Sh342,619 kutoka Sh140,000 na kwa upande wa matumizi ya kawaida wenye dira za LUKU sasa watalipia Sh385,682 badala ya Sh200,000 za awali.

Jackson Odoyo na Kuruthum Ahmed wanaripoti kuwa wananachi wamesema hatua ya Tanesco kupandisha garama za umeme kwa asilimia 21.7 inazidi kupandisha garama za maisha kwa watanzania wa hali ya chini.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti walisema kiwango hicho ni kikubwa kiasi kwamba mwananchi wa hali ya chini hawezi kukimudu katika katumizi yake.

Victoria Riza alisema hali ni mbaya kwani hata kiwango cha zamani baadhi yao walishindwa kukimudu leo hii wamepandisha zaidi ya kile cha zamani,kwa hali hiyo wengi watashindwa kabisa kutumia nishati hiyo.

Riza alisema kiwango hicho kitaongeza wizi wa umeme kwani kuna watu wanaolipa bili zao kwa mlango wa nyuma ambapo ni hatari kwa serikali na shirika kwa sababu fedha nyingi zinapotea.

Naye John Kijumbe alisema Serikali iangalie hali hiyo ya bei kupanda kwa sababu hali ya maisha kwa ujumla ni magumu Wananchi watashindwa kulipa bili zao kuwani hata mishahara wanayolipwa haiwezi kukidhi maisha.

Mtu mwingine aliyezungumzia gharama hizo ni Shy-Rose Bhanji ambaye alisema hali ni ngumu lakini inadibi serikali iangaliye namna ya kupandisha gharama hizo japokuwa wananchi wanahitaji maendeleo na Tanesco pia inahitaji kujiendasha kwa faida.

Seleman Said alisema mafuta yalivyo panda watu wachache ndio walioadhirika tofauti na kupanda kwa umeme ni kitendo ambacho kinawaadhiri watu wengi ambacho kitapelekea watu kushindwa kulipia gharama za umeme.
 
Bei mpya za umeme TANESCO kupinga?

na Waadishi Wetu
Tanzania Daima

SIKU moja baada ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Matumizi ya Nishati (EWURA) kuridhia ongezeko la bei ya umeme kwa asilimia 21.7, kuna taarifa kuwa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) halijaridhika na ongezeko hilo na lina mpango wa kukata rufaa.

Habari kutoka ndani ya shirika hilo zilieleza kuwa, viongozi wa shirika hilo walifanya vikao mbalimbali jana, wakijadili maamuzi ya EWURA kabla ya kufikia hatua madhubuti za kuchukua.

Habari zilieleza kuwa TANESCO halijaridhiswa na ongezeko hilo kwa maelezo kwamba halitaweza kukidhi uendeshaji wa shirika hilo ambalo kadiri siku zinavyokwenda hali ya kifedha inakuwa mbaya.

Awali, TANESCO waliwasilisha maombi EWURA ikitaka bei ya umeme iongezwe kwa asilimia 40, ili iweze kumudu gharama za uendeshaji ambazo zinazidi kupanda siku hadi siku.

"Hivi sasa ofisi zetu zinawaka moto, kwani viongozi wameonekana kutoridhika na kiwango cha bei kilichotangazwa na EWURA," kilibainisha chanzo chetu cha habari.

Chanzo hicho kilieleza kuwa vikao hivyo vipo chini ya Kaimu Mkurugenzi, Godfrey Mhando, kutokana na Mkurugenzi Mkuu, Dk. Idrisa Rashid kuwa likizo.

Kilieleza iwapo rufaa hiyo haitakubaliwa, kuna hatari ya shirika hilo kushindwa kujiendesha, hali itakayosababisha kupunguzwa kwa wafanyakazi pamoja na kutotoa huduma kwa uhakika.

Wakati hayo yakijiri TANESCO, wananchi wameelezea kusikitishwa na ongezeko hilo la gharama za umeme, na kusema hali hiyo itasababisha mfumuko wa bei katika bidhaa mbalimbali na hali ya maisha kuzidi kuwa mbaya.

Wakizungumza na Tanzania Daima jana kwa nyakati tofauti, walisema ongezeko hilo litasababisha baadhi ya viwanda vinavyotumia huduma hiyo vinavyozalisha bidhaa mbalimbali navyo kuongeza bei ya bidhaa wanazozalisha.

"Kwa mantiki hiyo, maisha yatazidi kuwa magumu sana, kwani kila kitu kitapanda kwa sababu ya ongezeko hilo, naamini hata wanaouza soda au bia nao watapandisha," alisema James Paulo, mkazi wa Vingunguti.

Hata hivyo, mtu mwingine, akizungumza kwa njia ya simu kutoka Iringa, Hans Kiwele, alisema kupanda kwa gharama si tatizo kama huduma itapatikana kwa wakati na uhakika.

Alisema kuwa gharama zilizopandishwa lazima ziendane na thamani ya huduma ambazo TANESCO itazitoa kwa wateja wake.

"Gharama lazima ziendane na tija… huduma tupate kwa wakati, si twende TANESCO tuambiwe kuwa mita hakuna tusubiri," alisema Kiwele.

Aidha, alipinga upandaji wa gharama hizo kwa sababu hali za wananchi bado ni ngumu, hususani kwenye upande wa kipato.

Kwa upande mwingine, aliilaumu EWURA na kudai kuwa haifanyi kazi yake ya kudhibiti kama ambavyo majukumu yake yanavyoeleza na kwamba chombo hicho kimekuwa ni cha kisiasa.

"Maoni ya watu wengi walisema wasipandishe, EWURA wamejidai kukusanya maoni na wamepita katika baadhi ya mikoa kukusanya maoni, hii ni danganya toto, wanatumia hela za serikali bure," alisema.

Mwananchi mwingine alisema serikali ilipaswa kuwaangalia wananchi wake, kwani maisha bora inayoahidi wananchi wake bado hayaonekani.

"Sasa hayo maisha bora iliyokuwa imeahidi serikali yako wapi? Mbona tunaona ni bora maisha… hivi kweli maendeleo yatapatikana kweli kwa maisha haya? Tunazidi kuumia kila kukicha, serikali haina msaada wowote katika kudhibiti suala hili," alisema John Mwambapa.

"Hii inasikitisha sana na ongezeko hilo litachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza hali ngumu ya uchumi kutokana shughuli nyingi za kiuchumi kutegemea zaidi nishati hii ya umeme, na hali hii inapunguza na kuogopesha wawekezaji ambao wanakuja kuwekeza nchini," alisema Jumanne Hassan, mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam.

Semeni Hassan, mkazi wa Mwananyamala, alisema kutokana na kupanda kwa gharama za umeme, watu wengi hawataweza kumudu gharama hizo, hivyo kutumia nishati mbadala ambazo ni adui wa mazingira, hali itakayosababisha kuongeza kwa uharibifu wa mazingira.

Joyce Gogadi, mkazi wa Sinza, alisema kupanda kwa gharama hizo kutasababisha kuongeza matabaka katika jamii, kwani wenye uwezo tu ndio wataweza kumudu gharama za umeme.

Naye David Charles, alisema kuwa hatua ya EWURA kupandisha gharama za umeme haitasaidia TANESCO kumudu gharama za uendeshaji kwa kuwa wafanyakazi wa shirika hilo ni wababaishaji na wala rushwa.

Aidha, Mwazani Ally, alisema serikali inaelekea kubaya kwa kuwa inaonekana wazi inajali zaidi maslahi ya watu wachache wenye fedha na kuwasahau wengi ambao ni maskini, kwani hakuna maskini yeyote atakayeweza kumudu gharama za kuingiza umeme.

Mkazi wa Sinza, aliyejitambulisha kwa jina la Mama Salome, alisema kutokana na hali hiyo, enzi za ujima za kutumia taa za vibatari zinarudi.

Kwa maelezo ya mama huyo, serikali isipokuwa makini nyumba nyingi zitaungua kutokana na utumiaji wa taa hizo za vibatari, na kuongeza kuwa hata bei ya awali ilikuwa ni shida kwa wananchi wengi kuimudu.

Mkazi mwingine, Freddy Raymond, aliiomba serikali kufikiria upya gharama hizo, ili kumpunguzia mwananchi wa kawaida mzigo.

Taarifa hii imeandaliwa na Ratifa Baranyikwa, Skola Athanas, Salehe Mohamed, Lucy Ngowi, Editha Msaki na Jamila Khalfan.
 
Mungu ibariki Tanzania...
hope serikali yetu ina wahsauri wengi wanaoujua uchumi kiasi kwamba wanajua how umeme na mafuta yakipandishwa bei yanavyojibiwa mapigo na gharama za maisha ya mtanzania wa hali ya chini!!!!!
shame on them leaders up there
 
Kwa upande wa gharama za maunganisho kwa wateja wapya pia zimeongezeka ambapo umbali wa mita 30 'single phase' bei hiyo imepanda mpaka Sh342,619 kutoka Sh140,000 na kwa upande wa matumizi ya kawaida wenye dira za LUKU sasa watalipia Sh385,682 badala ya Sh200,000 za awali.

Sasa wale ambao waliishalipia kuunganishiwa kitambo kitambo na hawajaunganishiwa itakuwaje? Kama hawana (au wanaona heri wanunue panel za sola) hizo laki mbili za ziada Tanesco itawarudishia pesa yao pamoja na riba? Mimi naona badala ya huu mchezo wa mazingaombwe wangeachiwa waongeze kiasi walichokiomba halafu tuone hayo mapato yakiongezeka! Hawa jamaa wanaongozwa na msomi basi wapewe nafasi ya kutuonyesha vitu vyao bila kupata sababu ya kukimbilia.
 
Back
Top Bottom