Kunyamazisha viongozi wa dini ni tambiko la ombwe la uongozi

Halisi

JF-Expert Member
Jan 16, 2007
2,802
613
Kunyamazisha viongozi wa dini ni tambiko la ombwe la uongozi

lC.gif
Mwandishi Maalumu
Septemba 16, 2009
rC.jpg

RAIS Jakaya Kikwete aliingia madarakani kwa ridhaa ya Watanzania wengi, mtaji wake ulikuwa mkubwa ukijumuisha wanazuoni, wana habari, viongozi wa dini, bunge, na hata baadhi ya vyama vya upinzani.
Kile kilichoitwa ushindi wa tsunami, kilikumba na kusomba kila aina ya upinzani uliokuwa njiani kujaribu kuchelewesha azma ya Kikwete kuingia Ikulu. Mhanga wa kwanza wa nguvu ya tsunami alikuwa Rais Benjamin Mkapa aliyeondoka kwenda Dodoma kushuhudia anguko la Kikwete akaishia kumtawaza madarakani huku roho ikimuuma.
Kwa kuwa ushindi wa Kikwete ulishadidiwa na mikakati ya ushindi kuliko ya kuongoza, katika miaka minne ya uongozi wake, tumeshuhudia mambo makuu mawili. Kwanza, ni ombwe la uongozi linaloonekana kwa njia ya yeye binafsi kutokuwa na maamuzi kwa hofu ya kuwaudhi marafiki zake waliowezesha ushindi.
Msimamo wake maarufu anaowaambia wanaomwendea kumshauri juu ya kufanya maamuzi umekuwa ni “ukiona mtu anajimaliza, usihangaike naye”. Hii pia ndiyo aliyoiita “ajali ya kisiasa” pale swahiba wake alipokumbwa na kashfa ya Richmond.
Pili, Serikali yake na chama chake vimegubikwa na makundi ya kimaslahi. Makundi haya yalianza wakati wa kampeni na yameendelea mpaka sasa na kuifanya Serikali yake itumie muda mwingi na rasilimali nyingi kutatua migogoro badala ya kuongoza.
Nyufa hizi mbili, zimemfanya Rais Kikwete hivi karibuni kufanya jambo la kihistoria pale alipozuia viongozi wa dini kutoa miongozo kwa waumini wao kwa hofu ya kuwa wanaigawa nchi. Napenda katika makala hii, nijadili zuio hili la kihistoria.
Hapana shaka sasa kuwa pale Kingunge Ngombale Mwiru alipolikemea Kanisa Katoliki kwa kutoa waraka au mwongozo wa elimu ya uraia alikuwa ametumwa. Kingunge, mshauri wa siasa wa Rais Kikwete alikuwa anakariri yale aliyokuwa ametumwa. Alipopuuzwa ndipo Rais kaja na zuio. Lakini huyu ni Rais aliyeungwa mkono na viongozi wa dini wakati wa kampeni na baadaye kiasi cha kuitwa “chaguo la Mungu”.
Wakati huo hakuona kuwa wanaigawa nchi, lakini sasa wanapotoa elimu ya uraia ili lipatikane “chaguo la Mungu” jingine ya hili la sasa liendelee kuongoza, Rais anaona nongwa.
Katika hali ambayo imekuwa ikitafsiriwa kuwa viongozi wa dini wanaziba ombwe la uongozi katika nchi, ni rahisi mtu kudhani kuwa Rais ametambua ombwe hilo la kuamua kuwanyamazisha ili aonekane kuwa bado anaongoza nchi. Njia hii ya kuongoza kwa kunyamazisha haina tija, inaweza kunyamazisha hata sauti za kumwambia yeye mwenyewe hatari inayomkabili.
Katika kipindi cha maswali na majibu ya papo kwa papo kwa njia ya televisheni wiki iliyopita, Rais kwa namna ya pekee amegusia mazuio kwa makundi makuu matatu. Magazeti ya Serikali kwa umakini mkubwa yaliripoti mazuio hayo huku magazeti yasiyo ya Serikali yakipuuza mazuio hayo. Kundi la kwanza ni la viongozi wa dini pale Rais aliposema madhehebu ambayo hayajatoa matamko yasifanye hivyo.
Hii ina maana yale matamko yaliyo tayari kwenye mzunguko ama hayana maana au ndiyo pekee yaruhusiwe kutumika. Kundi la pili, ni la wabunge wapinga ufisadi. Rais alishindwa kushawishi wasikilizaji kuwa Halmashauri Kuu ya CCM haikuwazuia wabunge hao kuendelea na harakati zakupinga ufisadi. Zuio la Rais kuhusu wabunge hao ni pale anapowataka wabunge kuangalia maslahi ya chama badala ya maslahi ya nchi.
Kwa kuwa ni wazi sasa kuwa minyukano iliyo ndani ya CCM si ya kiitikadi bali ya kimaslahi, zuio la NEC na Mwenyekiti kwa wabunge linasimika rasmi ufisadi ndani ya CCM. Kinachogombaniwa ndani ya CCM si kama CCM ni chama cha kijamaa au kibepari, bali ni mgongano wa nani kala nini na wapi? Kama wabunge wote wangepata mgawo wao sawasawa tusingeona minyukano inayoendelea ndani ya chama hicho kikongwe.
Kundi la tatu lililoguswa na zuio la Rais ni la wana habari. Akijibu swali kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, Rais kwa uswahili na kwa mizaha ya hapa na pale kama ilivyo kawaida yake aliwatisha waandishi wachokonozi kuwa “wakidiriki” kuchokonoa na kutikisa mustakabali wa nchi na maslahi ya watendaji wake watakiona cha mtema kuni.
Kwa mtu yeyote anayeitakia mema nchi hii, hawezi kupuuza mazuio haya ya Rais kwa makundi tajwa kwa sababu yakitekelezwa hata Rais mwenyewe hawezi kuwa salama. Usalama na ustawi wa Rais kama taasisi, ni pale uhuru wa kutoa maoni unaposhamiri, si unapofinywa kama ambavyo Rais anaelekea kuelekeza.
Nikirejea tena katika zuio la Rais kwa viongozi wa dini, napenda nisajiri masikitiko yangu juu ya sababu aliyoitoa Rais kuhusu zuio hilo. Alisema kuna hatari kuwa Watanzania wataenda kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwakani kufanya uchaguzi wa maelekezo ya dini zao.
Mtu aweza kufikiri Mheshimiwa Rais alisoma nyaraka hizo na kubaini hatari hiyo ndipo akaweka zuio la nyaraka zaidi kutoka madhehebu mengine. Na dawa ya hatari hii, Rais anaona ni kuwaita viongozi wa dini na kukutana nao ili “kuwafundisha” namna nzuri ya kutoa nyaraka zao au “kuwafundisha’ wasiwafundishe waumini wao namna ya kupiga kura.
Ikiwa hili ndilo kusudi la Rais kuwaita viongozi wa dini, tukubaliane mambo machache kabla ya mkutano huo unaosubiriwa na wachache. Jambo la kwanza, upo uwezekano Rais hajasoma nyaraka hizo na hivyo kutegemea maelezo ya wasaidizi wake. Hili si jambo la ajabu kwa sababu si mara ya kwanza kumwona Rais akizungumzia mambo anayoonekana hayaelewi sawasawa.
Mathalani katika kujibu swali la makundi ya CCM, Rais anakataa kuwa hakuna makundi bali uhasama uliopindukia. Kutokujua kuwa kuna makundi ndani ya CCM ni hatari kuliko makundi yenyewe; hali hii ikiendelea uhai wa CCM u shakani.
Jambo la pili, yawezekana Rais ameusoma waraka wa Kanisa Katoliki ambao umehaririwa na vijana wake wanaopenda usomeke kama Rais alivyousemea mbele ya Watanzania usiku ule. Kwamba, kuna njama za makusudi kumpotosha Rais kwa makusudi ya kumchonganisha na viongozi wa dini, maana waraka ule tumeusoma na hakuna mahali unasema Wakatoliki wachague Wakatoliki au Wakiristo.
Je, Rais kweli amechukia waraka unaoelekeza watu wasichague mafisadi? Na je, mafisadi wako CCM tu? Mbona ni CCM inayoonekana kuupigia kelele waraka huu? Jambo la tatu, Rais anafikiri kimya cha viongozi wa dini kuhusu hali ya nchi kinaweza kuongeza udhibiti wake katika hatamu za nchi- yaani kelele za viongozi wa dini zinapunguza mamlaka na madaraka yake kwa nchi?
Kwa Mheshimiwa Rais, madaraka na mamlaka ni bidhaa adimu ambayo hataki kuigawana na viongozi wa dini kwa kuhofia itaisha? Madaraka na nguvu ya ushawishi katika nchi hii ni kwa mgawo kama umeme wa Tanesco! Rais hana mshauri au muonaji wa kumjulisha kuwa kuongoza Taifa lenye viongozi wa dini walio kimya ni mzigo mzito usiobebeka?
Hata Bwana Yesu (Nabii Issa) aliwahi kuwaambia Wayahudi waliokerwa na kelele za wafuasi wake, kuwa “hawa wakinyamaza, mawe yatapiga kelele”. Siku za karibuni tumeona wanafunzi wakipiga kelele, walimu wakipiga kelele, watumishi wa reli, madaktari, watoto wa shule za msingi, wamasai wa Loliondo, wana habari, viongozi wa dini, na wabunge wa kweli. Taifa lililo hai ni lile linalopiga kelele. Zuio la Rais kwa viongozi wa dini ni la hatari sana na halina wema ndani yake.
Mheshimiwa Rais anapaswa ajue kuwa Tanzania ni kubwa sana na hatari ya Watanzania wengi kutotendewa haki ni wazi. Uwezo wa Rais kujua kila mara nini kinaendelea pembezoni mwa nchi achilia mbali hata katika baadhi ya maeneo yaliyo ndani ya Dar es Salaam si mpana kiasi hicho.
Rushwa na ufisadi ni mtindo wa maisha ya kila siku katika maeneo mengi. Taasisi za kiserikali na hata vyombo vya dola na vya utoaji haki vimevuka viwango kwa vitendo vya rushwa na hali ya kukata tamaa miongoni mwa Watanzania wengi inaongezeka kila siku.
Mtindo wa kushughulikia matatizo ya watu kwa njia ya operesheni haukidhi mahitaji. Matokeo yake ni misururu ya watu kuelekea Ikulu kueleza matatizo yao moja kwa moja kwa Rais kana kwamba watendaji wengine wa ngazi za chini ya Rais hawapo.
Mtu masikini wa kipato na asiye na jina hana uwezekano wa kupata haki. Tumeona wenyewe siku za karibuni kuwa ili kesi yako isikilizwe haraka inabidi uwe na fedha au uwe unajulikana. Mifano ni mingi: Ditopile Mzuzuri (marehemu) Abdallah Zombe, Costa Mahalu, Basil Mramba, Daniel Yona, na Grey Mgonja.
Tumesikia pia habari ya Mbunge mmoja mkoani Morogoro anayetuhumiwa kumpiga mtumishi wa Idara ya Maji jalada la uhalifu wake likipelekwa kwa DCI Robert Manumba badala ya Polisi kumpeleka mahakamani moja kwa moja.
Ni kana kwamba tuna mifumo miwili ya kisheria katika nchi moja. Mfumo mmoja kwa watu wanaopelekwa mahakamani bila kibali cha DCI na wale ambao wakifanya uhalifu inabidi kwanza iombwe ruhusa kabla ya kuwafikisha mahakamani.
Kutokuwa na haki sawa mbele ya sheria kunaleta mbinyo na msongo wa mawazo kwa Watanzania wengi. Mbinyo huu unapoendelea kwa muda mrefu, ndio unaowapa viongozi wa dini jukwaa la kusemea, ndio unaowapa wana habari uwanja mpana wa kuchambua jamii na ndio unaowapa wabunge nguvu ya dhamiri kusemea kile kisichopendwa na chama chao.
Masikini wa Tanzania husemewa na viongozi wa dini, wana habari na wabunge wenye dhamiri safi. Kwa zuio la mheshimiwa Rais, masikini wa Tanzania wasiwe na msemaji wala mtetezi maana kufanya hivyo ni kuhatarisha umoja wa kitaifa.
Umoja wa kitaifa ni ule wa kutowasumbua mafisadi na kuwachagua kila baada ya miaka mitano bila kuwadai uwajibikaji. Mpaka hapa natamani Mheshimiwa Rais aondoe zuio lake kwa viongozi wa dini, wana habari na wabunge wapingao ufisadi, na badala yake ajiunge nao kutetea wanyonge hawa na kuwarudishia heshima yao.
Kinachoendelea ndani ya Taifa ni zaidi uwepo wa ombwe la uongozi kama ambavyo imenukuliwa mara kwa mara na watu mbalimbali. Kwangu mimi, ombwe linakuwapo pale ambapo kwa sababu za kimfumo, uongozi uliochaguliwa unakosa haiba na ujasiri wa kuongoza taifa kutokana na mazingira yanayounyima uongozi huo fursa ya kufanya hivyo.
Ombwe la namna hiyo huzibwa ama pale uongozi huo unaposema “sasa basi” na kujikomboa kikweli kweli kutoka katika makucha ya wale waliouweka rehani au kelele zinapojitokeza za kuutaka usome alama za nyakati.
Kinachoonekana katika taifa letu kwa sasa, ni uongozi unaohofia kisichokuwapo bado huku ukipuuza kilichopo tayari. Mathalani, Serikali kupitia kwa Rais inahofia viongozi wa dini kujihusisha na utoaji elimu ya uraia kuwa watahatarisha umoja wa kitaifa, huku Serikali hiyo hiyo ikipuuza hatari ya ujinga wa wananchi wengi kuhusu elimu ya uraia.
Kwa maana hiyo, tunajivumia mamilioni ya Watanzania wanaobaki gizani bila kujua haki zao katika kushiriki michakato mbali mbali ya kidemokrasia. Lakini ujinga unaoshangiliwa sasa kesho unaweza kugeuka kuwa silaha ya maangamizi ya taifa.
Kule bungeni aliyetangaza zuio kwa viongozi wa dini kutokutoa nyaraka au kuondoa zile zilizo katika mzunguko alikuwa mzee Kingunge. Mzee huyu baadaye alisikika akisema kwamba wakati wa Mwalimu Julius Nyerere, hali hii isingeruhusiwa kuendelea. Sijaona popote mzee huyu alipokosolewa juu ya tamko lake hili lisilo na ukweli wote.
Mwalimu Nyerere aliipenda Tanzania na hata maadui wake walimheshimu kwa hilo. Walimsema mengi yasiyopendeza, lakini hawakutilia shaka uzalendo wake kwa taifa hili wala upendo wake kwa Watanzania.
Nadiriki kusema kuwa Mwalimu Nyerere aliipenda Tanzania kuliko familia yake, dini yake na hata chama chake. Tulimwona akiwatosa marafiki zake walipopingana na msimamo wa kujenga jamii ya Kitanzania isiyovumilia aina yoyote ya ufisadi.
Wakati fulani tulishuhudia hata Mwalimu Nyerere akitofautiana na Mama Maria pale alipobaini au kuhisi masuala ya familia yanaanza kuingilia masuala ya kitaifa. Kwa hiyo, kama ilitokea Mwalimu akawakaripia viongozi wa dini (kama aliwahi kufanya hivyo), alifanya hivyo ili kulinda maslahi ya Taifa na si pungufu ya hilo.
Sasa tujiulize, zuio la Rais kwa viongozi wa dini kutokutoa tena nyaraka za kuelimisha waumini juu ya elimu ya uraia lina manufaa kwa Taifa? Je, umoja anaodai kuulinda Rais bado upo?
Siwezi kudai kujibu maswali haya mawili kwa usahihi, lakini itoshe kusema ya kuwa zuio hili linawanufaisha mafisadi na viongozi miungu-watu. Linawanufaisha watu wachache waliozoea kupata uongozi wa kuchaguliwa kwa njia ya kununua kura na kulaghai wananchi wasioelewa.
Zuio hili linalenga kuimarisha tabaka la watawala (CCM) dhidi ya watawaliwa (Watanzania masikini wa vijijini). Ni hawa watawaliwa waliolengwa kuelimishwa na nyaraka za viongozi wao wa dini na elimu hii ilikuwa ni ukombozi kwao. Rais wao waliyemchagua kwa kura nyingi amezuia wasipate elimu hii wasije wakaasi na kuanza kuhoji.
Kuhusu ikiwa umoja anaoulinda Rais kwa kuweka zuio la kutokutoa nyaraka nyingine, nachelea kusema haupo kwa sasa. Tanzania ya sasa imegawanyika katika matabaka makubwa manne ya kiuchumi, kijamii na kimaeneo.
Tabaka la kwanza ni la watu wa mijini dhidi ya watu wa vijijini. Ukikutana na Mtanzania siku hizi ni rahisi kujua huyu wa mjini na yule wa kijijini kwa jinsi anavyofikiri, anavyoamua na hata kutembea. Mgawanyiko huu ni mtaji mkubwa wa wanasiasa kwa sababu tofauti yake kubwa iko katika uelewa (knowledge).
Tabaka la pili ni la kipato, yaani kati ya walio nacho na wasio nacho. Umasikini wa kipato umeigawa Tanzania katika makundi haya mawili, moja likizidi kuwa dogo kueleka juu, na jingine likiongezeka kwa kasi kuelekea chini. Sihitaji kulisemea sana hili maana Mwalimu Nyerere alilisemea katika uhai wake, na hivi karibuni mzee mmoja mashuhuri, mfuasi wa Mwalimu Nyerere, Ibrahimu Kaduma ameliandikia kitabu.
Tabaka la tatu ni lile la wanawake na wanaume. Haishangazi sana kuona kuna mafisadi wanawake wachache, na pia kuona kuwa mafisadi huwakimbilia sana akina mama wakati wa uchaguzi wowote. Kundi la akina mama lina masikini wengi wa kila sura na pia kwa wingi wao hugeuka kuwa mtaji wa kisiasa.
Katika hali ambayo tumeruhusu rushwa iamue nani achaguliwe, tabaka hili ni nguzo muhimu katika kuleta mabadiliko ya kweli.
Tabaka la mwisho kwa mtizamo wangu, ni lile linaloibuka kwa kasi kati ya vijana wanaosoma Shule za Kata na wale wanaosoma shule binafsi za watakatifu. Shule aliyosoma mtu inaanza kuamua aina gani ya kazi apate na shirika gani afanyie kazi.
Sijatoka nje ya mada yangu kwa kuchambua matabaka haya nikijaribu kueleza kuwa umoja wa kitaifa anaodai kuulinda Rais kwa kuwaziba midomo viongozi wa dini, wana habari na wabunge wapinga ufisadi haupo kabisa.
Kilichopo kwa sasa ni harakati za matabaka na minyukano ya kimaslahi iliyosababishwa na tabia ya tabaka moja kula bila kunawa. Baada ya miongo kadhaa ya matabaka haya kusigana kimya kimya kama alivyobaini Profesa Issa Shivji (Silent Class Struggle), kwa sasa matabaka haya yananyukana waziwazi ili kunyakua kombe moja la thamani.
Kombe hilo linaloshindaniwa si jingine bali Mheshimiwa Rais mwenyewe. Kila tabaka linadai Rais yuko upande wake huku naye akipata kigugumizi kujitambulisha na kundi lolote na hali hii kwa maoni yangu ndiyo inayotishia umoja wa kitaifa – si nyaraka za viongozi wa dini.
Mzee mmoja ninayemheshimu sana ndani ya Serikali, baada Rais kutamka kuwa hakuna makundi ndani ya CCM ameniambia kuwa “Rais asiye na kundi kwa sasa hatufai”.
Viongozi wa dini wanaozuiwa kutoa nyaraka nyingine walikuwa wanajaribu kusemea na kutetea maslahi ya tabaka la wanyonge. Uamuzi huu haukumpendeza Rais na akaamua kuwazuia. Kwa kuwa madaraka (mandate) ya viongozi wa dini haitokani na Rais, nabakia kuamini kuwa viongozi hawa hawatakaa kimya na kuusaliti utii wao kwa Mungu.
Sasa tumeanza na kuzuia nyaraka za kichungaji, kesho tutataka mahubiri ya viongozi wa dini yapelekwe Ikulu kabla hayajasomwa, keshokutwa tutataka viongozi waongezewe idadi ya nadhiri wanazoweka kwa kumtii Rais wa Jamhuri.
Hatimaye siku moja mtu anaweza kutaka kichwa cha kiongozi kwenye sahani. Mnashangaa? Hii haitakuwa mara ya kwanza, Herode alikwisha kutangulia!
Ukiona kuwa ilani mbalimbali za vyama vya siasa, tena zilizo tofauti kabisa, hazigawi watu, lakini ukaona miongozo ya dini ni ya hatari, wewe ni wa hatari kuliko hatari yenyewe.
Namheshimu sana Rais Kikwete lakini kwa hili natamani kabisa avunje kabisa mpango wake wa kukutana na viongozi wa dini kuwafundisha wajibu wao. Kama ana la kusema, atoe mwongozo ulioandikwa kama viongozi wenyewe walivyofanya, na awaachie wananchi waamue lililo jema kwa mustakabali wa Taifa. Mkutano wa Rais na viongozi wa dini utamvunjia heshima yake iliyobaki.
hs3.gif

Mwandishi wa makala hii amejitambulisha kuwa ni msomaji mzuri wa Raia Mwema na mmoja kati ya viongozi wa Ukiristo nchini. Barua Pepe: msomajiraia@yahoo.co.uk, Simu: 0712881704


http://www.raiamwema.co.tz/news.php?d=1696
 
Last edited:

Similar Discussions

Back
Top Bottom