Kumbe udini ndio ulitumika kumdhuru Lowassa kisiasa?

WATANABE

JF-Expert Member
Apr 13, 2011
1,092
466
CHANZO: RAIA MWEMA (Mei 25 - 31, 2011)

Kikwete na porojo za CCM kujivua gamba


- Ni ‘usanii' wa kusafisha njia kwa anayemtaka 2015

Itakumbukwa kwamba, Februari 5, mwaka huu, kwenye sherehe za miaka 34 ya CCM mjini Dodoma, Mwenyekiti wake ambaye pia ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, alieleza mengi huku akipiga chenga mengine na mwisho kuwaasa wana-CCM kwamba itabidi chama chao kivijue gamba.

Msemo huo wa Mwenyekiti Kikwete ulishabihiana na maneno ya aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Yusuf Makamba, ambaye aliwaambia Watanzania kwamba kazi ya TANU (chama mama cha CCM), kilikuwa kuleta uhuru na kazi ya CCM ni kushinda uchaguzi.


Ingawa maneno ya Makamba yalionekana kama mzaha lakini kiukweli yalikuwa na ujumbe mkuu wa CCM ya leo; kwamba kazi yake ni kutawala iwe kihalali au kiharamu. Alichokisema Kikwete kilikuwa ni dawa tu ambayo wao CCM wanaamini wanaihitaji ili waendelee kutawala.


Ingawa baadhi ya Watanzania waliamini kuwa kuna jambo kubwa na jipya litakalofanywa na CCM kwenye kujivua gamba, lakini wengine wenye kumbukumbu nzuri za maneno ya Kikwete na matukio ya CCM katika miaka ya karibuni, hawakutarajia chochote cha maana ama kipya.


Ikafika siku ya siku wakati wa vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM mjini Dodoma, Aprili mwaka huu. Baada ya hadithi ndefu, kuvunjiana heshima, kutishana, uongo, majungu na fitna, maamuzi ya kuchekesha kwa watu wazima yalifikiwa.


CCM ikawatangazia Watanzania imevunjilia mbali Kamati Kuu yake kwa kuwasihi wajumbe kujiuzulu, pia imeifutilia mbali Sekretarieti yake kwa kuwashinikiza wajumbe wake kujiuzulu. Ilielezwa kwamba sababu ya maamuzi haya ni kumpatia mtu mmoja tu, yaani Mwenyekiti wao, nafasi ya kuunda timu mpya.


Timu hizi mbili za Kamati Kuu na Sekretarieti za zamani zilishambuliwa kwamba eti hazikuwa zikimshauri Mwenyekiti wao vema; hivyo kusababisha chama kudhoofika vibaya. Kwa maajabu ya karne, Mwenyekiti yeye hakuonekana kwamba ni dhaifu, yaani ikawa hadithi ile ile ya "mkubwa hakosei."


Madai haya yalikuwa ni tofauti na utamaduni wa CCM wa kutegemea busara za Mwenyekiti wao na ikaonekana sasa Mwenyekiti ndiye anayetegemea busara za wanaomzunguka. Kimsingi, hii ilikuwa ni janja ya nyani tu ya kutafuta sababu ya kuunda timu mpya; kwani wanaomjua Kikwete wanasema hasikilizi ushauri, sasa iweje awalaumu watu kwa kutomshauri?


Mathalani, ilipofika kumchagua mgombea wa CCM wa kiti cha uspika Novemba mwaka jana, inaelezwa kwamba Mwenyekiti Kikwete aligoma kusikiliza ushauri wa mkongwe wa CCM, John Malecela, aliyemtahadharisha kwamba wakimtosa spika anayemaliza muda wake, Samuel Sitta, CCM itayumba.


"Unasemaje?", Kikwete alimhoji Malecela na kisha kujenga hoja kwamba chama si mtu, na kisha kutupilia mbali madai kwamba Sitta akiachwa CCM itayumba. Hatimaye Sitta aliachwa na CCM ikamsimamisha Anna Makinda ambaye ndiye Spika leo; huku wananchi na wapinzani wakiguna kila mara.


Tabia ya kutopenda ushauri kwa Mwenyekiti Kikwete ndio inayowavunja nguvu wasaidizi wake kwenye Chama na hata serikalini ambako mawaziri wake kila siku huonekana kama chipukizi wanaosubiri amri ya kucheza michezo ya halaiki uwanjani. Kikwete hasikilizi ushauri.


Kwa nini Kamati Kuu ilivunjwa


Kamati Kuu ya CCM ilivunjwa kwa sababu moja kubwa: Kuwaondoa watu wasiotakiwa na Mwenyekiti Kikwete na kuwaweka watu watakaomsikiliza, watakaounga mkono mipango yake ya kutafuta mrithi wake na wachache watakaochukua nafasi za madaraka baadaye.


Ingawa ilielezwa kwamba lengo ni kumpa fursa Mwenyekiti Kikwete kuunda timu mpya itakayoikomboa CCM, kiukweli ukiangalia uundwaji wa chombo hicho utaona janja ya nyani. Kwanza, ni vema kubaini kwamba sehemu kubwa ya wajumbe wa Kamati Kuu (zaidi ya nusu) ni wale wanaoingia kutokana na nafasi zao serikali, chamani na kwa heshima. Hawa ni lazima warejee.


Wajumbe wanaoingia kutokana na nafasi zao serikalini ni Rais wa Muungano, Rais wa Zanzibar, na Waziri Mkuu wa Muungano na wanaoingia kutokana na nafasi zao kwenye chama ni Makamu wa CCM Bara na wa Visiwani, Katibu Mkuu wa CCM, na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara na wa Visiwani.


Wengine ni wajumbe wa Sekretarieti ya CCM ambao baada ya kuundwa upya sasa ni Mhazini Mwigulu Mchemba, Katibu Mwenezi Nape Nnauye, na wakuu wa kamati mbili ambao ni January Makamba na Asha Abdallah.


Kundi jingine ni dogo; nalo linaundwa na wajumbe wa kudumu ambao ni marais wastaafu wa Muungano wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, na wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa; Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dkt. Salmin Amour; na Makamu Mwenyekiti Mstaafu, Mzee Malecela. Mpaka hapa idadi inakuwa wajumbe 16 kati ya 30.


Hata hivyo, inasemakana sasa wazee hawa wanne wastaafu wanaundiwa chombo chao kitakachoitwa Baraza la Wazee ili kuwaondoa ndani ya Kamati Kuu na kumwacha Kikwete akifanya atakalo bila bughudha.


Hivyo basi, wajumbe wa kuchaguliwa ambao kimsingi hutokana na mawazo ya Mwenyekiti na huku ikizingatiwa kuwa iliombwa hivyo, kuwa Mwenyekiti achague watu wapya, waliishia kuwa maswahiba wa Kikwete kwa kujali ajenda yake kuu: Kuunda CCM itakayomtii bila maswali.


Katika janja hiyo, Kikwete pia anadaiwa kufanya jitihada za kuhahakikisha kuwa Zanzibar inatoa wajumbe wengi kadri itakavyowezekana. Mbali ya kufuata katiba ya CCM lakini pia hii ni njia moja ya kupambana na malalamiko yaliyokithiri kutoka upande huo wa Muungano.


Sababu ya pili ni kunufaika na tabia ya Wazanzibari kupiga kura ya pamoja kwa makubaliano kuunga mkono jambo au kupinga; na mwisho ni kuhakikisha kuwa hapungikiwi waumini wa Kiislamu ambao kwa akili yake watamuunga mkono kwa vyovyote vile hasa pale atakaposema "ni zamu yetu," kama mwanae Ridhiwani anavyotamba vikaoni.


Wajumbe wapya saba walioteuliwa na Mwenyekiti kutoka Zanzibar ni: Dkt. Hussein Mwinyi, Dkt. Maua Daftari, Samia Suluhu, Omar Yusuf Mzee, Prof. Makame Mnyaa, Mohamed Seif Khatibu, na Shamsi Vuai Nahodha.


Wajumbe saba wa Kamati Kuu kutoka Bara: Abdulrahman Kinana, Dkt. Abdallah Kigoda, Pindi Chana, Steven Wassira, Constatine Buhie, William Lukuvi na Zakhia Meghji ambaye ni mzaliwa wa Zanzibar aliyehamia Bara.


Jumla ya wajumbe wa kuteuliwa ikafikia 14, hivyo kufanya Kamati Kuu nzima ya sasa kuwa na wajumbe 30.


Kwa nini Sekretarieti ilivunjwa


Sekretarieti ya CCM ilikuwa na tatizo moja kubwa kwa wanachama wa CCM na hata Watanzania - Katibu Mkuu Yusuf Makamba. Lakini pia huyu ndiye rafiki wa karibu zaidi wa Mwenyekiti Kikwete, na kwa hiyo kumtoa ilimuwia vigumu na inasemekana kwamba alishapuuza ushauri wa kumtoa siku nyingi zilizopita.


Urafiki wa Makamba na Kikwete unavuka mipaka ya kawaida na kuingia kwenye mambo ya kitamaduni yasiyotamkika magazetini. Kwa mujibu wa mashuhuda wa karibu wa utawala wa Kikwete, Makamba alikuwa mtu muhimu mno na bado ni muhimu mno ambaye ushauri wake hutengua ushauri mwingine wowote. Ushauri wa Makamba unaaminika kuwa huwa hauji hivi hivi tu.


Hata hivyo, kwa mujibu wa tathmini zote zilizofanywa, ikiwemo ya kikao cha makatibu wakuu wa mikoa na wilaya wa CCM, Makamba ilikuwa lazima atoke. Kutoka kwa Makamba ingawa kulikuwa ni maumivu makubwa kwa Mwenyekiti, lakini pia kulifungua mlango kwa Mwenyekiti kuweka watu wake watakaomsaidia kutimiza ndoto yake ya kurithisha utawala wake kwa watu wa "zamu yetu," msemo ambao familia yake imeuzoea.


Hivyo inadaiwa kuwa ulipangwa mchezo wa kuigiza, kwamba Makamba agome kujiuzulu halafu mwishoni aseme kwamba lazima Sekretarieti nzima ing'oke. Mbinu hii ilisaidia kumuondoa Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa anayeuota urais kama Kikwete alivyokuwa kabla ya 2005. Membe alikuwa akiongoza kamati ndogo ya mambo ya nje na siasa.


Lakini pia kuivunja Sekretarieti kutaondoa wababaishaji wengine kama Mhazini Amos Makalla na papo hapo kuacha nafasi wazi kwa watu wa Kikwete kuingia. Haikuwa ajabu kwamba January Makamba, mtoto wa Mzee Makamba, kuteuliwa na Kikwete kuingia kwenye Sekretarieti kuchukua nafasi ya Membe na Nape Nnauye kuwa Katibu wa Uenezi.


Itakumbukwa kuwa wakati wa sakata la Nape na Umoja wa Vijana, Mzee Makamba aliwahi kutamka kwamba Marehemu Moses Nnauye alimwomba yeye amtunze kijana wake, Nape. Marehemu Nnauye aliwahi kuwa Katibu Mwenezi wa CCM na baadaye kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara. Kimsingi, Nape amerithi kiti cha baba yake, lakini kubwa zaidi ni kwamba Makamba sasa ana "watoto wawili" kwenye Sekretarieti ya CCM!


Lakini pia nini maana ya kumbakiza John Chiligati kama Makamba alisema watoke wote? Chiligati anasifika kwa kitu kimoja: Utiifu. Chiligati si mbishi na hakatai amri yoyote ile hata kama ni ya hovyo, lakini pia kwa kuzingatia kuwa sasa si waziri, kwake itakuwa heri kuwa mtiifu ili, mbali ya ubunge, apate pia "ulaji" wa chama.


Kikwete na zoezi la udini


Kutokana na msimamo na mtindo wa Kikwete kutawala nchi kwa kufuata udini, pengine kutokana na uwezo wake mdogo wa kuona mbali na kujua nini cha kufanya kama mkuu wa nchi, kuna hesabu kwenye uteuzi wake wowote ule, iwe serikalini au kwenye CCM.


Mathalani; kwenye Kamati Kuu kwa upande wa Bara aliteua wajumbe saba jumla; Waislamu watatu na Wakristo wanne; huku akijua kuwa kutoka Zanzibar wote saba ni Waislamu. Kiujumla wake Kamati Kuu ina Waislamu 18 na Wakristo 12. Hii si bure kwa mujibu wa fikra za Kikwete, anajua anachokifanya.


Kwenye Sekretarieti mpya aliteua watu saba jumla, Katibu Mkuu Wilsom Mukama, Naibu Bara John Chiligati, Naibu Zanzibar Vuai Ali Vuai, Mhazini Mchambe, pamoja na Makamba mdogo na Bi Asha. Wakristo ni wanne na Waislamu ni watatu ikiwa ni janja ya kufunika kombe ili mwanaharamu apite; kwani tayari timu imeshapangika.


Pengine swali la msingi ni hili: Je, ni kwa nini Kikwete anajali sana idadi za watu kutokana na dini zao; huku Watanzania wakiwa hawajali kutokana na maadili ya kitaifa kwamba Watanzania wote ni ndugu wamoja?


Ndani ya serikali kwenye mahakama kuu na ya rufaa anatimiza ahadi yake kwa Waislamu kwamba atafanya uteuzi kwa kuwapa nafasi nyingi, lakini ndani ya CCM ni zaidi ya hapo. Kikwete anatafuta kura za kupitisha jina la mgombea urais wa CCM mwaka 2015 iwapo mpango wake wa kuteua jina la Mwislamu utafanikiwa.


Kwa taratibu za CCM Ili mtu apate tiketi ya CCM anahitaji kupitishwa na Kamati Kuu, kisha jina lake kwenda Halmashauri Kuu kwa ajili ya kuchuja na kubakiza majina matatu ya kwenda Mkutano Mkuu. Hivyo, iwapo hakuna udhibiti kuanzia juu, jina linalohitajiwa na bwana mkubwa linaweza kubaki nje.


Lakini jambo la kujiuliza ni hili: Kwamba kwa nini Kikwete asitafute Mtanzania mwadilifu, mwenye uwezo, safi na mzalendo bila kujali dini?


Jibu linalosemwa mitaani ambako Kikwete anaheshimika ni hili: Kwamba Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alitawala kwa miaka 23 na pia Rais Mkapa alitawala kwa miaka 10, hivyo kufanya jumla ya miaka ya marais Wakristo kuwa 33.


Kwa Waislamu, Rais Mwinyi alitawala miaka 10 na yeye Kikwete itakuwa miaka 10, hivyo kufanya jumla kuwa miaka 20. Kwa hiyo, ili kuleta "usawa" itabidi Mwislamu mwingine atawale baada ya Kikwete ili walau sasa Waislamu wafikishe miaka 30, na kukaribia miaka ya Wakristo.


Ni vigumu kuamini kwamba rais wa nchi anaweza kuhusika na mchezo mchafu kama huu wa kuwabagua wananchi wake kwa misingi ya dini zao, lakini matukio ya hivi karibuni yanathibitisha hilo.


Baada ya uchaguzi mwaka jana na hasa tukio la Arusha la Watanzania kupigwa na polisi kwenye maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), na kisha harufu ya udini kuibuka, Waislamu walianza kuzunguka nchi nzima wakitoa mahubiri ya chuki.


Mkutano wa kwanza wa Waislamu ulifanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam na wapambe wa mashehe wanadai kuwa uliungwa mkono na Kikwete. Mikutano hiyo ya chuki ilitamka maazimio mengi ya Waislamu ikiwemo kudai Mahakama ya Kadhi na Tanzania kuingia kwenye Jumuiya ya Kiislamu Duniani (OIC), na hata kuthubutu kusema kwamba Tanzania ikatwe vipande viwili, moja iwe ya Waislamu na nyingine ya Wakristo. Pendekezo la ajabu kabisa lisilofikirika.


Madai mengine yalihusu malalamiko kwamba Wakristo wamekuwa wakipendelewa tangu enzi za ukoloni na kwamba ingawa Waislamu ni "wengi zaidi" Tanzania, lakini hawana nafasi nyingi za madaraka. Walisema kwamba Wakristo wana shule na mahospitali lakini Waislamu hawana na kwamba serikali hutoa fedha kuzisaidia hospitali na Wakristo na walimu wa kufundisha shule za Wakristo lakini Waislamu wanaachwa hivi hivi tu.


Madai hayo yalifikia hatua ya kumlaani Mwalimu Nyerere na kusema kwamba hastahili kuitwa Baba wa Taifa bali anastahili kuitwa Baba wa Kanisa. Sasa ni wazi kuwa kiongozi Tanzania ambaye hamwiti Mwalimu Nyerere kwa hadhi yake iliyozoeleka ya Baba wa Taifa, ni Rais Kikwete peke yake pamoja na mashehe wanaohubiri chuki. Katika hotuba zake za hivi karibuni amekuwa akitumia jina "Mzee Nyerere." Watafiti wanahoji kwamba iwapo rais wa nchi anaweza kuungana na wahuni wanaotangaza chuki nchi nzima, basi, hawezi kushindwa kufanya vituko vya ajabu ndani ya chama chake na kwenye kusaka mrithi wake. Huyu ndiye Kikwete ambaye mambo yake kwa juu yako tofauti kabisa na yalivyo kwa ndani.


Geresha ya kujivua gamba


Pamoja na kubadili safu ya uongozi mjini Dodoma, CCM pia ilitangaza kwamba wanachama wake watatu wanaotuhumiwa kwa ufisadi wajiondoe wenyewe la sivyo wataondolewa kwa nguvu. Wanachama hao wanatajwa kuwa ni Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, na wabunge wawili, Andrew Chenge na Rostam Aziz. Ni kweli matajiri hawa hawapendwi na Watanzania wengi isipokuwa wa majimboni mwao tu.


Lakini pia watu hawa watatu wana sifa nyingine: kwamba ndio tishio pekee na la kweli dhidi ya mpango wa Kikwete wa kusaka Mwislamu wa kumrithi. Watu hawa nia yao kubwa si udini; bali ni ulaji. Wanataka kumweka Lowasa kwenye urais mwaka 2015, mtu ambaye pengine hatalazimika kumheshimu Kikwete na kumlinda. Lakini tatizo kwa Kikwete ni kwamba Lowassa si Mwislamu.


Kundi hili lina urafiki wa karibu na Makamba ambaye inadaiwa kuwa ndoto yake kubwa haikuwa udini kwa mwaka 2015, licha ya kuwa naye amesikika mara nyingi akijiingiza kwenye siasa za udini; bali anaota mwanae aje kuachiwa urais mwaka 2025 na kundi hili. Makamba hutamba kwamba mwanae anafaa kuwa kiongozi na hakuna ubishi kwamba alihakikisha mwanae anapata ubunge, uenyekiti wa kamati ya Bunge, na kisha kuingia kwenye Sekretarieti ya CCM.


Aidha, mtoto wa Makamba pia anaelezwa kuwemo kwenye kundi linalowaunga mkono watuhumiwa hawa wa ufisadi ambalo lina idadi kubwa ya wabunge na viongozi wa CCM wa ngazi za wilaya, mikoa na taifa. Hii ndiyo sababu tangu CCM ilipoanza kushambulia mafisadi hadharani, yeye amepotea jukwaani!


Kimsingi kuna kutofautiana kati ya Makamba na Kikwete kuhusiana na nani awe rais mwaka 2015 na hawa watuhumiwa wa ufisadi wafanyejwe. Hivyo, tangazo la kujivua gamba pamoja na kutajwa kwa watuhumiwa hao ambao Kikwete mwenyewe aliwapigia kampeni mwaka jana kwenye uchaguzi wa wabunge, ni geresha tu. Kikwete alikuwa anaunda timu itakayomrithi mwaka 2015.


Kimsingi, hadi sasa Kikwete ameshawaacha wabaya wake wote nje ya Kamati Kuu ambao ‘dhambi' yao kuu ni kuutaka urais wa mwaka 2015. Watu hawa ni Membe, na hili kundi la mafisadi pamoja na Prof. Mark Mwandosya ambaye licha ya kushindwa mwaka 2005 na umri kumtupa mkono, inadaiwa bado anataka kujaribu tena 2015.


Njama hizi za Mwenyekiti Kikwete ambazo zinaelezwa kwamba ni zoezi la CCM kujisafisha, ingawa upo ukweli pia kutokana na kuigopa CHADEMA, ndizo chanzo na mwisho wa zoezi la kujivua gamba. Hakuna cha zaidi.


Hivyo basi, hakuna ushujaa wala maamuzi magumu yaliyofanyika Dodoma. Ulikuwa ni ‘usanii' tu, na ndiyo sababu hakuna kiongozi wa CCM anayepigia kelele mafisadi zaidi ya kijana Nnauye ambaye anaganga njaa na kulipa fadhila za kupewa ukuu wa wilaya na cheo kwenye chama. Hata Chiligati aliyejitokeza mwanzoni sasa ameingia mitini.


Makamba mdogo naye amekaa mbali; kwani mafisadi hao ndiyo wafadhili wake wakuu kisiasa na maswahiba wa baba yake. Hofu yake ni kwamba, akiwachafua leo na wao watamwacha huko mbeleni au watamng'oa kwenye siasa.


Malalamiko ya Joseph Butiku hivi juzi kwamba viongozi wa CCM wamemwachia Mwenyekiti mzigo wa kupambana na mafisadi, yamekuja bila kujua ukweli wa mambo. CCM haiko kwenye mapambano na mafisadi; bali Mwenyekiti ndiye anapambana na maadui zake ila tu amepata bahati kwamba watu hao hao ndio wanaolalamikiwa kwa ufisadi. Ni bahati tu ya mtende iliyotoa nafasi ya fitna hii kuchezwa!


Aidha, kelele za CCM kupitia kwa Nnauye kwamba kuna vyombo vya habari, viongozi wa upinzani na viongozi wa dini ambao wamepangwa kuwatetea mafisadi na kuishambulia familia ya Kikwete, ni janja ya kuwatangulia mbele ili wakisema jambo wananchi waambiwe: "Si tulisema, mnaona sasa!?" Hata hivyo, inafahamika kuwa makundi haya matatu ndiyo yako mstari wa mbele kupinga ufisadi na udini unaosambazwa na Kikwete na watu wake, hivyo lolote litakalosemwa halitakuwa geni, bali ni muendelezo unaofahamika. Pengine CCM haijui kuwa wananchi wanajua kinachoendelea.


Wagombea wa Kikwete 2015


Kwa kufuatilia mambo ya kisiasa yanavyokwenda na jinsi Rais Kikwete anavyoendesha mambo yake, kuna majina mawili ya watu ambao angependa wachukue urais na umakamu wa rais wa Muungano mwaka 2015. Hii inatokana pia na imani yake kwamba Katiba mpya haitabadili mfumo wa sasa.


Sababu kubwa ni mbili: Kwanza, kutekeleza ahadi yake ya siri kwamba hawezi kuacha nchi kwa Mkristo; na pili, kuhakikisha uongozi mpya unamlinda yeye na familia yake na utajiri wao mkubwa wa ghafla walioupata katika miaka hii michache. Hatapenda kushambuliwa kama inavyotokea kwa Mkapa.


Ni wazi kwamba watu kama Membe, Lowassa na Mwandosya hawana sifa hizi hasa ikizingatiwa kuwa wote ni "makafiri", na pia Kikwete anaamini kwa dhati kabisa kwamba hata iweje, vyombo vya dola na CCM vina uwezo wa kupanga matokeo ya urais ya mwaka 2015 ili mtu wake awashinde wapinzani.


Ili watu hao wawili wakubalike, Kikwete atatumia mtindo ule ule wa funika kombe mwanaharamu apite. Atawapendekeza kwa kutumia vigezo vinavyoficha ukweli. Kutokana na hali ya kisiasa itakavyokuwa, anaweza kusema: "Jamani ni zamu ya wanawake sasa, tusitawale akina baba tu, nchi yetu wote." Iwapo wazo hili litakwama, basi Kikwete anaweza kusema hivi: "Jamani sasa wenzetu wa Zanzibar nao, miaka 20 imepita, tuwape nao nafasi jamani." Msemo huu hata hivyo hauna mashiko iwapo Katiba haitakuwa na agizo hilo; kwani wapinzani wote wanaweza kuweka watu wa Bara.


Mbinu hii ambayo ameshawahi kuitumia kwenye kuteua kwa amri yake binafsi kwenye nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana ambapo alimweka kijana wa Visiwani mwenye umri mkubwa uliopitiliza, na kwenye kupata jina la mgombea wa Uspika. Mbinu hii anaamini kuwa itafunika hoja yake ya udini kwani mwisho wa siku atataja jina la "mcha Mungu" na siyo "kafiri." Watanzania hawajali dini ya mtu ila yeye Kikwete ndiye mwenye tatizo.


Watafiti wa masuala ya kisiasa wanakubali kwamba hakuna ubaya nchi kutawaliwa na watu wa dini moja mfululizo kama wanafaa, hata kama itakuwa milele; bali wanacholalamikia ni mchezo wa kumchagua mtu kwa kuangalia kwanza dini yake halafu ndiyo yafuate mambo mengine; tena huku visingizio vikitumika.


Katika miaka ya karibuni Kikwete amekuwa na mahusiano ya karibu ya kikazi na mwanamama mmoja ambaye kila baada ya miezi michache hufika Ikulu, na kisha picha nyingi hupigwa kuonesha kwamba wawili hao wanaelewana na wanashirikiana kisiasa pia.


Huyu ni mwanamama ambaye ni mmoja wa wanasiasa wachanga waliofaidika na vyeo vya uwaziri wa Kikwete. Aidha, pale Tanzania ilipopewa mwanya wa kutoa jina la mwanamke wa kushika nafasi ya juu kimataifa, Kikwete hakusita kumtaja mwanamama huyu.


Nafasi hii ilikuwa baada ya Tanzania kufanya kampeni kubwa barani Afrika kuunga mkono jina la Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini, Ban ki-Moon, kwenye kugombea nafasi ya ukatibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.


Mwanamama huyo pia ana kisomo kinachoweza kuwaaminisha watu wanaotaka kuuliza maswali kuhusu uwezo wake.


Mwanamama huyo ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye hasikiki sana duniani zaidi ya anapokuja likizo Dar es Salaam. Huyu ni Dkt. Asha-Rose Migiro ambaye anaelezwa kuanza kujiandaa kurejea nyumbani Tanzania siku si nyingi.


Kwa upande wa Zanzibar ni waziri mmoja kijana ambaye urafiki wake na Kikwete huwashangaza viongozi wengine wa Zanzibar; mathalani jinsi wanavyosalimiana kama watoto wa mjini. Katika mtandao wa YouTube Watanzania waliweka picha ya video ya Kikwete akisalimiana na waziri huyu kwenye Uwanja wa Amani, Zanzibar siku ya Januari 12, mwaka huu. Ilitia aibu.


Hivi karibuni Waziri huyu alipokabiliwa na msukosuko wa kutakiwa na wananchi kwamba ajiuzulu ambao kimsingi ulisababishwa na utendaji dhaifu wa Jeshi la Wananchi uliochukua maisha ya watu kwenye milipuko ya maghala ya silaha, alikataa na Kikwete hakusema kitu. Huyu ni Dkt. Hussein Mwinyi.


Hitimisho langu


Rais Kikwete ana ajenda zake ambazo hazina uhusiano wowote na maslahi ya taifa la Tanzania na inaelekea ameamua kwa dhati kupambana ili kupata mrithi wake kwa njia safi na chafu kama alivyoingia madarakani. Mapambano yake haya yataleta balaa Tanzania iwapo Watanzania hawatabaini mawazo yake mapema na kujipanga kuyakataa, wote waliomo CCM na waliopo nje ya CCM.


Njia bora zaidi kwa wana-CCM ni kusafisha chama chao kwa uaminifu na werevu, na kisha kuachia demokrasia iamue nani awe mgombea wa CCM mwaka 2015. Lakini kwanza ni lazima uchafu uondolewe na siyo kuwaondoa watu wachache kwa hila binafsi na kuwaacha wengi.


Watanzania wana kazi rahisi zaidi: ni kukataa ‘usanii' wa Kikwete.Lakini pia kubwa ni hili: Kwamba juhudi za Kikwete za kutaka kuhakikisha kundi fulani kwa kutumia kofia ya udini fulani linashika madaraka ili lilinde familia yake, eti ni "zamu yao," ilihali wenzao wa dini hiyo wakitaabika na umaskini, ni unafiki mkubwa.


CCM na Kikwete wawe waangalifu ili Tanzania isitumbukie kwenye matatizo yanayosikika kwenye nchi zingine. Inawezekana Tanzania ikazama kwenye maachafuko kama mwendo wenyewe utakuwa hivi.


Watanzania wamechoka na CCM na wametosheka na Kikwete; hawatakubali kuburuzwa tena huku wakijua kuwa uchaguzi uliopita haukuwa wa haki na huru, na kwamba CCM inataka kufanya hila tena mwaka 2015. Watanzania wengi hawaamini matokeo ya uchaguzi uliopita.


Watanzania watakataa na hapo ndipo nchi itakapoingia kwenye machafuko; kwani CCM nayo itavimba. CCM na Kikwete wasiivunje nchi; waiache kama walivyoikuta, wairejeshe kwa Watanzania.
 
mhh! nimebaki speechless sa sijui nani wa kuaminiwa hivi ni nani ameandika hii makala duh hadi 2015 tutasikia na kuona mengi, sa sijui ka waz
tz tuna uwezo wa kudigest na kuelewa haya mambo na kujua mbinu chafu na dhamira ya kweli

Pukudu @Ilkiding'a, Arusha
 
iko kazi , kama ccm haitakuwa vipande viwili huko mbele basi itafuata nyayo za KANU. aheri ya wenzetu watu weupe, mtu akiisha jiuzuru kwa maslahi ya taifa ama kwa kashfa ni nadra sana kumsikia aking'ang'ania tena madaraka, ngozi nyeusi wacha mchezo.
 
Ni Bora Chadema ichukue 2015, CCM itatuondolea Amani

Ukiangalia Lowassa ni Mkristo Lutheran; Nyerere na Mkapa ni Wakristo Roman Catholics

Kwahiyo kama Kikwete ataanza kubagua kwa Udini lazima aangalia Udini ulivyo; Waislamu bahati wengi wa Bara ni Sunni kwahiyo rais atakayefuata awe Shiite Muislamu

Xoxo Count how many Christian Denominations they have to wait for presidency as well as Muslim's Denominations...

Atagawa Nchi kama alivyo shauriwa na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi... all these come from Mwinyi.
 
Give me a break

Mwandishi anataka kumharibia tu DR Asha Rose Migiro. Kwahiyo Mkapa aliyemuona mara ya kwanza alimteua kwa dini yake? Ban Ki Moon naye alimteua kwa dini yake?
 
nINDEFU SANA LAKINI INAUJUMBE TAFADHALI ISIPUUZWE, NA ZILE CD ZINAZOSAMBAZWA NCHI NZIMA NA VIJANA WA KIISLAM UKWELI UPO!
KUONDOKANA NA HILI NIMDA WA CCM KUKAA PEMBENI!
 
Huu ni moja kati ya uchambuzi makini,kwa kweli tusipoangalia nchi yetu ipo siku moja huyu Kikwete ataiingiza kwenye machafuko ya vita vya wenyewe kwa wenyewe au vya kidini,tunaomba kwa Mungu huu mpango wa Kikwete usije ukafanikiwa kwani utawagawa watanzania kidini.Mungu ibariki Tanzania tuendelee kudumisha amani na upendo,watu wa dini zote tuendelee kupendana.
 
Give me a break

Mwandishi anataka kumharibia tu DR Asha Rose Migiro. Kwahiyo Mkapa aliyemuona mara ya kwanza alimteua kwa dini yake? Ban Ki Moon naye alimteua kwa dini yake?
yULE MAMA UWEZO WAKE MDOGO JAMANI NDO YALEYALE TUKAWEKA MATUMAINI KIBAO KWA PROFF TIBAIJUKA AKABOMOA UKUTA MMOJA SAIZI YUPO TUU KAACHA MAISHA YAENDE!
 
Nimesoma habari hii kwa kina! Ila nilichoona hapa ni wale waliopata maumivu kutokana na maamuzi ya hivi karibuni ya ccm, hum ndani yameelezwa mengi, ya chama, ya serikali na watu kutajwa majina!

Kinachonishangaza kwa mwandishi ni pale anaposema ccm hananchi hawaitaki, then anazungumzia kikwete ataleta mtu wake wa kuongoza, sasa huyu mtu Kikwete atamtoa chama gani?kisha suala la kuteaua kwa kuangalia dini hilo c sahihi.

Aliyeandika makala anataka kupandikiza chuki ili tubaguane kwa dini zetu kwa maslahi yake binafsi ya kisiasa
 
Nimesoma habari hii kwa kina! Ila nilichoona hapa ni wale waliopata maumivu kutokana na maamuzi ya hivi karibuni ya ccm, hum ndani yameelezwa mengi, ya chama, ya serikali na watu kutajwa majina! Kinachonishangaza kwa mwandishi ni pale anaposema ccm hananchi hawaitaki, then anazungumzia kikwete ataleta mtu wake wa kuongoza, sasa huyu mtu Kikwete atamtoa chama gani?kisha suala la kuteaua kwa kuangalia dini hilo c sahihi. Aliyeandika makala anataka kupandikiza chuki ili tubaguane kwa dini zetu kwa maslahi yake binafsi ya kisiasa
Nyundo,
Soma tena kwa makini. Ndiyo, mwandishi kasema CCM wananchi hawaitaki tena. Lakini hapo hapo anasema Kikwete anaamini CCM itashinda kwa kutumia vyombo vya dola. Yaani hata kama ni kuiba kura CCM lazima ishinde. Sijaona contradiction hapo. Na huu ni ushahidi mwingine kuwa CCM haikushinda 2010.
 
Inatisha na kusikitisha.
Inaelekea kuna Kaukweli katika hii hoja.
Nimekuwa niki-idadavua kwa muda sasa.
 
Hii inatisha na ni kweli kabisa, hebu tujaribu waislamu kukosoana kama sio kuwashambulia viongozi wa imani ya kikristo? Lowasa leo kafiri lakini hakuwa kafiri alipomweka kikwete madarakani? au ndio koti sasa linabana livuliwe?

Kwa hiyo hatafutwi kiongozi mchapakazi na jasiri wa kupambano na mashindano ya dunia bali anaangaliwa jina?

angalia hiyo kamati kuu basi, 7 toka visiwani wote waislamu, 7 toka bara wanne waislamu 3 tu ndio wakristo katika kamati ya 14.
 
Ni busara kupitia kila neno,na kutolipuuza kwa kulitafakari...ila ni dhambi isiyosameheka kushawishi watu kwa kutengeneza dhana inayokaribiana/inayofanana na ukweli!...Haya maneno yanaozesha mioyo ya watu kwa chuki...nionavyo! Hatujafikia hapa!
 
Makala inaonekana Lowassa katoa hela ili iandikwe! Umalaya wa fedha tu vitu vilivyo andikwa havina maana yoyote kabisa! Njaa mbaya jamani leo hii hapa JF kuna watu wameanza kuwatetea Lowasa,Rostam na Chenge? Ni aibu!
 
Back
Top Bottom