Kitanzi cha Magufuli

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125
Sasa ashitakiwa kwa Waziri Mkuu
headline_bullet.jpg
Ni kuhusu kusitisha nauli za kivuko
headline_bullet.jpg
JK naye ajulishwa kuhusu mashitaka



Magufulii(8).jpg

Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli


Upinzani dhidi ya nauli mpya za huduma za vivuko vya serikali, umezidi kupamba moto, ambapo sasa Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk. Faustine Ndugulile, amelifikisha suala hilo kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akimuomba pamoja na mambo mengine,

amtake Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kusitisha mara moja utozaji wa nauli hizo na kuomba radhi kwa madai ya kuwatukana na kuwadhalilisha wananchi.

Kauli inayodaiwa kuwaudhi wananchi hao ni ile iliyotolewa na Waziri Magufuli Januari Mosi, mwaka huu, alipozungumza na wananchi wa Kigamboni kuhusu nauli hiyo mpya na kuwaambia kuwa asiyetaka kulipa nauli hiyo apige mbizi baharini kuzunguka Kongowe kuingia katikati ya jiji au arudi kijijini akalime.

Pia baadaye siku hiyo hiyo, akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za wizara hiyo, alisema yeyote asiyetaka nauli hiyo mpya kutozwa, anunue kivuko chake na akitaka akipe jina la chama chake cha siasa kisha atoe huduma hiyo kwa Sh. 100 au bure ilimradi aende kwake (waziri) kupata kibali cha kutoa huduma hiyo.

Dk. Ndugulile ‘amemshtaki’ Waziri Magufuli kupitia barua yake yenye Kumbukumbu Namba: KIG/KVK/VOL.1/6 ya Januari 3, mwaka huu, aliyomwandikia Waziri Mkuu, jijini Dar es Salaam jana.
Nakala ya barua hiyo yenye kichwa cha habari “Ongezeko la viwango vya nauli katika kivuko cha Magogoni”, imepelekwa kwa

Rais Jakaya Kikwete, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama, Kamati ya Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam na madiwani wote wa Jimbo la Kigamboni.
Mbali na mambo hayo, katika barua hiyo, ambayo NIPASHE inayo nakala yake, Dk. Ndugulile pia anataka utaratibu ufanyike

kuhakiki mapato na matumizi ikiwa ni pamoja na kuangalia maeneo ya kupunguza gharama akisema yapo maeneo mengi yanayoweza kutumika katika kupunguza gharama.
Pia anataka mchakato kuongeza viwango vya nauli hizo, uanze upya kwa kushirikisha wadau wa huduma hizo.

Anasema anasitishwa kwa nauli mpya kutawezesha kubaini uhalali wake kisheria na vigezo vilivyotumika.
“Aidha, wananchi wa Kigamboni wametiwa simanzi na kuongezewa machungu na kitendo cha tarehe 1/1/2012 kilichofanywa na Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa John Pombe Magufuli cha kuwatukana na kuwadhalilisha. Wananchi wa Kigamboni wanamtaka

waziri huyu awaombe radhi,” anasema Dk. Ndugulile katika barua yake hiyo.
Anaongeza: “Naomba umshauri Waziri Magufuli afanye hivyo. Ni jambo la kiustaarabu na kiungwana na litalinda heshima ya serikali.”

Dk. Ndugulile alimuomba Waziri Mkuu kulipa suala hilo umuhimu wa pekee kutokana na hali iliyopo Kigamboni hivi sasa.
“Kumekuwapo na utulivu wa muda kwa kuwa niliwaomba wanaKigamboni wanipe mbunge wao nafasi ya kulifanyia kazi suala hili. Kwa kuchelewa kutoa maamuzi serikali inajiweka katika mazingira magumu,” anasema Dk. Ndugulile.

Anasema wananchi wa Kigamboni wanapinga ongezeko la nauli hizo kwa sababu mbalimbali, ikiwamo vivuko na nauli zake kutawaliwa na sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini Nchini (Sumatra).
Pia masuala ya nauli yanatawaliwa na kanuni ambazo zilichapishwa kwenye Gazeti la Serikali namba 92 la Februari 26, mwaka juzi.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, wanaKigamboni wangependa kujua: Je nauli hizi mpya zimepitishwa na Sumatra? Kama ni ndiyo. Lini? Ni Lini mapendekezo ya nauli mpya yalitolewa kwa umma? Serikali ilitumia magazeti gani? Matangazo yalitoka tarehe zipi? Ni lini na wapi mikutano ya wadau kuchangia kuhusu nauli mpya ilifanyika?” anahoji.

Anasema wana Kigamboni pamoja na naye kama mbunge, hawajapata kuona tangazo lolote na wala kushirikishwa katika kujadili bei mpya.
Dk. Ndugulile anasema katika barua hiyo kuwa katika barua yake ya Januari 19, mwaka jana yenye Kumbukumbu Namba KIG/KVK/VOL.1/1 kwenda kwa Mkurugenzi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), aliomba na kusisitiza wanaKigamboni wahusishwe na kushirikishwa katika mchakato wowote wa kuongeza nauli, lakini jambo hilo halikufanyika.

Anasema vilevile, wanaKigamboni wanahoji vigezo vilivyotumika kufikia bei mpya za kivuko.
Dk. Ndugulile idadi ya vijana nchini ni takriban asilimia 60-70 na kwamba, wengi wao kwa sasa wanajiajiri kwa kuendesha maguta, pikipiki, Bajaj na kusukuma mikokoteni.

Kutokana na hilo, anamuomba Waziri Mkuu kujua vigezo vilivyotumika kuongeza nauli ya guta kutoka Sh. 200 hadi Sh. 1,800 (sawa na asilimia 800), ambayo anasema ni kubwa kuliko gari dogo.
Pia anamuomba anataka kujua vigezo vilivyotumika kuongeza nauli ya Bajaj kutoka Sh. 300 hadi Sh. 1,300 (sawa na asilimia 333) na nauli ya mikokoteni kuongezeka kutoka Sh. 200 hadi Sh. 1,500 (sawa na asilimia 650).

“Isitoshe mizigo inayopakiwa nayo inatozwa nauli,” anasema Dk. Ndugulile.
Anasema wafanyabiashara wengi wa Kigamboni wanatumia maguta, Bajaj a mikokoteni kusafirisha bidhaa na kutokana na ongezeko la nauli ya kivuko, bei ya bidhaa zimepanda maradufu, hali ambayo anasema inazidi kuwatia umaskini wananchi wa eneo hilo.

Dk. Ndugulile anasema wana Kigamboni wanaamini kuwa hakuna haja ya kuongeza nauli ikiwa mapato yatadhibitiwa vizuri.
Anasema kivuko cha Magogoni-Kigamboni eneo la Feri, kinakusanya kiasi cha wastani wa Sh. milioni nane kila siku na kwamba makusanyo maalum yakifanyika, mapato hufika hadi Sh. milioni 13 na kwamba, upotevu wa Sh. milioni tano kila siku ni nyingi.

“Wananchi hawaoni kwanini wabebeshwe mzigo wa serikali kushindwa kusimamia na kudhibiti mapato,” anasema Dk. Ndugulile.
Hatua hiyo imechukuliwa na Dk. Ndugulile, baada ya juzi wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, kutoa tamko la pamoja wakitaka nauli hiyo mpya isitishwe mara moja na Waziri Magufuli aombe radhi kwa sababu hizo.

Wabunge hao pia waliomba wapewe wiki mbili kusimamia mapato yanayotokana na huduma za kivuko cha Magogoni-Kigamboni ili kuithibitishia serikali kiasi cha mapato yanayopotea kwa njia za kifisadi katika kivuko hicho badala ya kuwabana wananchi wanyonge.

Tamko hilo lilitolewa na wabunge hao, wakiwamo wa majimbo na wa viti maalum wa mkoa huo, wakiongozwa na Mwenyekiti, Abbas Mtemvu (Temeke-CCM) na Katibu wao, John Mnyika (Ubungo-Chadema), walipozungumza na waandishi wa habari, katika ofisi ya Mbunge wa Ilala, jijini Dar es Salaam juzi.

Lilitolewa na wabunge hao baada ya Waziri Magufuli kutangaza rasmi nauli hiyo mpya ya huduma za vivuko vyote vya serikali nchini, ambazo zilianza kutumika Januari Mosi, mwaka huu.

Dk. Magufuli alisema kuanzia tarehe hiyo, wizara kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), imeongeza viwango vya nauli katika vivuko vyote vya serikali nchini na kwamba, kutokana na mabadiliko hayo, nauli ya kivuko cha Magogoni-Kigamboni imeongezwa kutoka Sh. 100 iliyokuwa ikitozwa zamani hadi Sh. 200 kwa mtu mzima.

Pia alisema watoto wa umri mpaka miaka 14 watalipa Sh. 50 kutoka bure na kwamba, atakayeruhusiwa kutumia huduma hiyo bure ni mwanafunzi tu atakayekuwa amevaa sare na kubeba kitambulisho cha shule.
Vilevile, nauli ya baiskeli imeongezwa kutoka Sh. 200 hadi Sh. 300; pikipiki (kutoka Sh. 200 hadi Sh. 500); mizigo chini ya uzito wa

kilo 50 (kutoka bure hadi Sh. 200); mzigo unaozidi kilo 50 (kutoka Sh. 300 hadi Sh. 500); mkokoteni (kutoka Sh. 200 hadi Sh. 1,500).
Pia guta (kutoka Sh. 200 hadi Sh. 1,800); Bajaj (kutoka Sh. 300 hadi Sh. 1,300); wanyama kama ng’ombe (kutoka Sh. 500 hadi Sh. 2,000); wanyama wadogowadogo kama mbuzi na kondoo (kutoka Sh. 500 hadi Sh. 1,000); gari dogo (kutoka Sh. 800 hadi Sh. 1,500); gari la mizigo hadi tani 1.5 (kutoka Sh. 1,000 hadi Sh. 2,000); na station wagon (kutoka Sh. 1,000 hadi Sh. 2,000).

Vilevile, basi dogo lenye uwezo wa kuchukua abiria mpaka 15 (kutoka Sh. 2,500 hadi Sh. 3,500); gari zaidi ya tani 2 hadi tani 3.5 (kutoka Sh. 5,000 hadi Sh. 7,500); basi lenye uwezo wa kuchukua abiria zaidi ya 15 mpaka 29 (kutoka Sh. 5,000 hadi Sh. 7,500) trekta bila trailer (Sh. 7,500); trekta na trailer (haliruhusiwi) na gari lenye uzito wa zaidi ya tani 3.5 (haliruhusiwi).

CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom