Kitabu : Kiu ya uzalendo

Shayu

Platinum Member
May 24, 2011
608
1,653
MOJA YA KURASA YA KITABU CHA KIU YA UZALENDO AMBACHO NILIANDIKA MWAKA 2013

Lakini kwanza ni kwa jamii zetu kuwa na nidhamu, mpangilio na utaratibu. Maendeleo kama maendeleo ni matokeo ya kazi na hakuna maendeleo pasipo kufanya kazi. Kama tutawapanga watu wetu vizuri katika kila nyanja nina uhakika tutapata maendeleo kwa haraka zaidi.


Hatutaweza kuzungumzia maji vijijini, umeme na udhibiti wa maliasili zetu bila kuzungumzia mambo ya msingi niliyoyazungumzia. Ambayo kwa uhakika ndio yatakayoleta haya mengine na ambayo yatakayojenga jamii iliyostaarabika. Pasipo kujitambua kwa watu wetu hawatoweza kudhibiti maliasili zao.

Bila dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko kwa upande wa wananchi na kwa serikali taifa letu halitopiga hatua kimaendeleo.

Bila kujitambua kwetu safari yetu ya kuleta maendeleo itakuwa mbali sana. Lakini chombo pekee kitakacholeta mabadiliko kwa haraka ni elimu. Iliyotengenezwa katika ubora na ambayo lengo lake ni kunufaisha jamii kwa ujumla na sio mtu mmoja mmoja. Kama jamii yote ikielimika ni lazima tutapiga hatua kimaendeleo kwasababu kila mtu atakuwa anajitambua.


Kwa hali iliyopo sasa hivi, Taifa letu linahitaji kiongozi ambaye yuko makini sana katika ukuaji na maendeleo ya kijamii kutokana na huu utandawazi. Udhibiti unahitajika ili ukuaji wa watoto wetu ujenge maadili na nidhamu itakayochangia kuimarisha taifa letu.


Kama nilivyosema nidhamu hii ni muhimu sana kwa taifa letu. Bila nidhamu hii hatutaweza kupiga hatua yeyote kubwa ya kimaendeleo. Nidhamu hii inahitajika nyumbani, shuleni, kazini na katika serikali yetu. Hili dhahiri kabisa kuna tatizo hili la nidhamu katika taifa letu.


Ni lazima taifa letu tulirudishe katika nidhamu na utaratibu ili kuleta heshima katika taifa. Ili kuleta umoja na mshikamano kwa watu wetu wote. Bila nidhamu hii taifa letu halitaweza kuendelea kuwa moja.


Hili ni jambo la msingi sana kwakuwa bila ya familia zetu kuwa imara ambazo ni sehemu mdogo inayojenga taifa hakika hatutafika mbali kwakuwa malezi ya vijana wetu na mahusiano yao na jamii yanaanzia huko. Na mahusiano yetu ndio msingi mkuu wa maendeleo yetu kama taifa. Ndio msingi mkuu wa umoja wetu.


Hatutaweza kufanikiwa kama huku chini sio wamoja katika ngazi ya familia na mahusiano yake na jamii inayomzunguka. Kufikiwa kwa malengo yetu na mahitaji yetu katika ngazi za chini kunategemea sana mahusiano yetu na umoja wetu katika malengo. Bila kujipanga na kuwa na nidhamu na utaratibu hatutaweza kufanikiwa.


Kwahiyo kuvurugika kwa jamii yeyote au taifa lolote uanzia kwenye familia na mahusiano yake na jamii inayomzunguka. Ambayo inayoundwa na majirani kadhaa ambao pengine wana mahitaji sawa kama jamii ili wasonge mbele. Iwe kwenye masuala ya elimu ya watoto wao ambayo itajenga misingi ya nidhamu na maadili vitu ambavyo kwa hakika hujenga mahusiano ya mtu kwa jamii yake, maji, umeme au miundo mbinu ni mambo yanayatugusa wote kama jamii na bila nguvu ya pamoja hatutaweza kufanikiwa. Kwahiyo ni muhimu tujitambua na kujua kwamba mahusiano yetu ni kila kitu na pasipo mahusiano bora hatutaweza kulinyanyua hili taifa. Na dhamira yetu ni lazima iwe kunyanyua maisha ya kila mmoja wetu kama taifa. Na kujenga taifa lenye furaha na lenye familia imara na jamii zilizo bora. Ni lazima tujenge moyo wa kujitolea kwa taifa letu ambalo kwa hakika naamini wote tunalipenda. Umoja wetu ndio nguvu yetu.


Migawanyiko mingi katika jamii inatokana na watu kuangalia maslahi binafsi badala ya maslahi mapana ya kijamii. Huu ni msingi ambao ni lazima tuujenge. Kabla ya kufanya kitu chochote ni lazima tuangalie maslahi ya jamii na kuyalinda. Kutokuangalia maslahi ya jamii kwanza na kuweka ubinafsi mbele ni sawasawa na kukata mti tulioukalia, tutaanguka wote.


Mataifa mengi yameharibiwa kwa uchu huu unapoingia, na kusahau jamii bali kufikiria kujiingizia pesa tu hata kama njia hizo zitakuwa na madhara kwa jamii na kwa taifa.


Matatizo yote haya ya ufisadi na rushwa yana madhara makubwa kwa jamii na mwisho wake ule umoja na mshikamano wa watu hutoweka na mwisho kabisa watu huingia katika vita


Ni muhimu watu wetu kujizuia na ndio maana nasema nidhamu hii ni ya msingi sana ili tujenge taifa ambalo ni la amani na endelevu.

Ili mambo haya yaimarike ni lazima kila mtu amwangalie mwezake kabla ya kujiangalia yeye, aingalie jamii kwanza kabla hajaangalia maslahi yake binafsi.

Kwa kufanya hivi tutajenga jamii imara na endelevu na ndipo tutapata amani ya kweli. Kwa mtazamo huu wa kumwangalia mwenzako kwanza na jamii kabla hujajiangalia mwenyewe, tutafanikiwa kuwa na utulivu na amani ya kweli. Hii ni sheria ambayo ipo na ambayo itatupunguzia uovu katika nchi yetu. Ni katika mazingira haya ya ujenzi wa taifa letu katika haki na nidhamu tutapiga hatua na kuheshimiana.

Hatutaweza kujenga taifa hili katika matazamo wa ubinafsi alafu tukaendelea na kuwa na amani. Kwa huu wajibu wa kila mmoja kwa mwezake ni muhimu sana katika ujenzi wa taifa bora na imara lakini pia lenye furaha.

Mivutano yote katika jamii inatokana na haya mambo. Ni muhimu sana kujiangalia upya. Kwasababu kwetu sisi ni muhimu kujenga jamii yenye furaha. Na furaha hii haitokuwepo pasipo upendo miongoni mwetu.

Umaskini wa taifa hili utaondoka pale tu tutakapofanya kazi kwa pamoja na kwa kuangalia maslahi ya jamii na ya taifa badala ya kuangalia yale ya kibinafsi kwanza.


Makala hii ni sehemu ya Kitabu changu ambacho nilikiandikia kinachoitwa KIU YA UZALENDO. Natumaini mtakuwa mmeelemika vya kutosha kwa yote niliyoandika humu. Ni mambo ninayoamini kwa dhati yana uwezo wa kulibadili taifa letu.
 
Back
Top Bottom