Kisa cha Ngoswe!!!!NGOSWE KITOVU CHA UZEMBE na EDWIN SEMZABA

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
MOJA ya tamthiliya zilizopendwa na zenye mafunzo makubwa kwa jamii ni ile iliyotungwa na Mwalimu Edwin Semzaba ya “Ngoswe: Penzi kitovu cha uzembe”.

Ilichapwa kama kitabu mwaka 1992 na kufanywa kuwa mchezo wa radio na RTD, inatosha sana kutufanya tufikirie jinsi gani watu wenye madaraka wanaweza kujisahau katika madaraka yao na kujikuta wakiyatumia vibaya.

Niseme mapema kuwa kama hujawahi kusoma tamthiliya hii au kuisikiliza au kama umekwisha isahau nashauri ujipatie nakala yako popote kitabu hicho kinakopatikana na mnaweza kujisomea kwenye familia (kama waigizaji – role playing) au na washirika wako kazini au hata kijiweni! Na kama ningekuwa na uwezo kidogo ningehakikisha wabunge wote wanapata nakala yake, na wale mawaziri ningewataka wakisome kwenye semina yetu Ngurdoto!

Tunapoendelea na vita dhidi ya ufisadi tunaweza kuona mfanano mkubwa kati ya yale aliyokuwa akiyafanya Ngoswe (mhusika mkuu katika tamthiliya hiyo) na yale ambayo baadhi ya watawala wetu wanayafanya leo. Ingawa katika tamthiliya hiyo kuna migogoro mingi, mgogoro mkubwa ni ule uliotokea kati ya Ngoswe (afisa wa Sensa) na Mzee Mitomingi na familia yake hasa baada ya Ngoswe kumdondokea Binti wa Mitomingi aitwaye Mazoea.

Katika tamthiliya hiyo tunaweza kuona jinsi gani Ngoswe alivyokolewa na penzi la Mazoea hadi kuwa mzembe kazini. Kwangu mimi nataka niende hatua moja mbele, kuonyesha kuwa ufisadi leo katika jamii yetu na hasa katika utumishi wa umma umetokana, kulelewa na kukuzwa si na mapenzi kazini (hilo lawezekana) lakini zaidi kutokana na kundi la watu wachache waliolewa na kujilewesha kwa mvinyo wa madaraka.

Kwamba, leo hii kwa kiasi kikubwa madaraka yasiyosimamiwa vyema (unchecked power) ndiyo hasa kiini cha uzembe ambao umezaa ufisadi! Ufisadi ambao ndicho kiini cha Taifa kutopiga hatua kubwa ya maendeleo jinsi ambavyo ingepasa.

Mwaka huu tumeshuhudia mambo mengi ambayo yamedhihirisha ukweli kuwa kiini cha ufisadi nchini si ukosefu wa sheria nzuri (hilo laweza kuwa lipo pia) lakini hasa ni jinsi wale walio madaraka wanavyofanya mambo kana kwamba hakuna sheria nchini au vyombo vya kusimamia sheria.

Tunachokiona mwaka huu ni jinsi gani baadhi ya wale waliodhaminiwa uongozi wa taifa au baadhi ya taasisi na idara zake wamefikia mahali pa kuamini na kujiaminisha katika upotofu wao kuwa wao ndio nchi, na ya kuwa bila wao hakuna kitakachofanyika.

Mfano mzuri ni pale tuliposhuhudia jinsi waliopewa dhamana ya kulisaidia taifa kujinasua na tatizo la nishati walivyotumia nafasi zao na matatizo ya nchi yetu kujinufaisha wao na marafiki zao. Kama tusingepata ripoti ya Kamati Teule ya Bunge tusingejua ni jinsi gani kuna watu ambao kwa hakika wamelewa madaraka. Watu ambao waliweza kuingilia utaratibu wa manunuzi ya serikali na kwa kutumia nguvu za vyeo vyao wakalazimisha washirika wao wasio na uwezo wapewe tenda ya kuleta majenereta ya umeme.

Licha ya kugundua kuwa kampuni ile ya Richmond haikuwapo nchini kihalali, na ya kuwa haikuwa katika nafasi wala uwezo wa kuingia mkataba watawala wale wale wamekubali tu kiaina kusitisha mkataba na Dowans kampuni nyingine ambayo haijulikani ni ya wapi na ya nani (mwanzoni tuliambiwa kutoka Uarabuni, baadaye Afrika ya Kusini, na mara nyingine sehemu fulani huko visiwa vya Karibiani).

Hao hao waliolewa mvinyo huo mtamu wa madaraka tumewaona jinsi gani walivyokuwa wanatuona sisi wananchi kama vituko na hata mmoja wao alipokutwa na fedha ambazo amezifisha nje ya nchi, wao wenyewe wakaamua kumzawadia vyeo katika mambo ya maadili! Ni mtu aliyelewa tu anayeweza kufanya mambo kama hayo ya kuzawadia vyeo waliokumbwa na kashfa za ufisadi!

Tumeshuhudia pia jinsi waliolewa ulanzi huu wa madaraka walivyoweza kukaa pembeni na kushuhudia aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT) akichomoka nchini kiaina wakala njama kulificha taifa, juu ya ugonjwa na kifo chake na wakachelewa kwa makusudi kutokumhoji kuhusu wizi wa mabilioni ya fedha zetu.

Hata tulipokuwa tunawauliza mara kwa mara watawala hao wakikenua meno yao kwa dharau na kucheka kicheko cha uvivu wakatuambia tusubiri tu “wakimtaka atapatikana”! Hata pale walipopewa mara mbili nafasi na Marekani kuwa waombe tu “watapewa” watawala wetu walikaa kimya na kujifanya wanashangaa shangaa kama wale watoto waliopigwa picha juzi wakishangaa kivuko kipya cha Kigamboni!

Ni hawa hawa watawala waliolewa madaraka ambao tumeshuhudia jinsi gani walichekeana miaka nenda rudi kiasi cha kuliingiza taifa kwenye hasara ya mabilioni. Leo hii kuna kesi mahakamani, kesi ambazo msingi wake ni geresha na matokeo yake yanatabirika, kesi ambazo hazikutakiwa kabisa kufika hapa tulipofikia. Ni wazi kuwa walioingia na kuchota fedha Benki Kuu hawakuvunja kuta bali walikaribishwa na wenye nyumba na kama madai yaliyoletwa dhidi ya watuhumiwa yataonekana yana ukweli basi wizi wa Benki Kuu ulifanywa na watu waliokaribishwa, kusindikizwa, na kusimamiwa na wenye nyumba! Ni walevi tu wanaoweza kumkaribisha mwizi ndani ya nyumba yao!

Leo hii tumeshuhudia malumbano ya ajabu kati ya mtu mwenye madaraka ambaye amejiaminisha kabisa kuwa madaraka hayo ni yake. Nimeshangazwa, kukerwa na kusitushwa na kitendo cha Waziri wa Mambo ya Ndani kuthibitisha ulevi huu wa madaraka. Ninaogopa kabisa kwa mtu kama yeye kuaminiwa kwa kitu kingine kikubwa zaidi kwani ameonyesha dalili mbaya sana ya mtu mwenye madaraka. Amempa raia siku saba kutoa ushahidi ama “atakiona”!

Hivi wakati yule mwandishi wa BBC Vicky Ntetema alipoenda mafichoni baada ya taarifa yake kuhusu mauaji ya albino Waziri Laurence Masha alikuwa wapi? Nakumbuka vizuri ripoti ile ya Ntetema kwenye BBC na baadaye alipohojiwa na National Public Radio. Alidokeza kuwa katika uchunguzi wake alijua kuwa Polisi wanahusika na mauaji ya albino kwani wakati alipoenda kwa mganga mmoja alikuja mgeni ambaye alielezwa kuwa alikuwa ni afisa wa polisi aliyevaa kiraia. Taarifa hiyo ya Ntetema bado ipo, unaweza kuiona kwenye mtandao wa intaneti kwa maneno yake mwenyewe Ntetema.

Yaani, kwa madai ya Ntetema, wakati wengine tunapiga kelele dhidi ya mauaji ya albino kuna baadhi ya polisi ambao wanahusika na vitendo hivyo. Ntetema amedai hivi “yule mganga alitamba kwamba alikuwa akishirikiana na mtandao wenye nguvu sana katika Afrika ya Mashariki unaowahusisha polisi na majambazi. Nilijua wanahusika na mauaji ya albino, nikajawa na hofu”.

Sasa tupime madai ya Ntetema na madai ya Reginald Mengi. Hivi ni yapi yanatisha zaidi na ambayo yangehitaji mtu apewe siku saba? Yule aliyedai “kuna Waziri kijana” ambaye amependekeza jambo baya lenye kumletea mashaka ya kibiashara au hata madhara ya kimwili au yule aliyedai kuwa maafisa wa polisi wanahusika na mauaji ya albino?

Kwa nini Masha hakujitokeza wakati ule na kudai ushahidi kutoka kwa Ntetema, tena hadharani na kumtishia siku saba vinginevyo atakiona? Hao polisi si watendaji wa serikali vile vile, kudai polisi wanahusika na mauaji si ni sawa na kusema serikali au Jeshi la Polisi linahusika na mauaji?

Maneno na kauli ya Waziri Masha kama zilivyonukuriwa na vyombo mbalimbali vya habari kuhusu tuhuma za Mengi dhidi ya “Waziri” fulani ni maneno ya kibabe, yenye chembe za undava, na ambayo kama yasipopingwa yataashiria nguvu kubwa ya serikali kutumika dhidi ya mtu mmoja.

Waziri Masha alinukuriwa akisema “Uhuru wa vyombo vya habari si kuvitumia kutangaza vitu ambavyo vinaleta athari katika jamii, hivyo tutaliangalia suala hilo na mimi kama waziri ninayesimamia usalama ndani ya nchi, ninawajibika moja kwa moja katika jambo hili.” Kwa mwanasheria kama Masha inashangaza ni wapi anapata mantiki ya mawazo ya namna hiyo.

Kwa nje maneno hayo yanaweza kuonekana yana hekima lakini tukiyasogelea kwa karibu yanatisha. Yanaonyesha dalili za mtu ambaye amegida kombe kubwa la madaraka mapema mchana. Mtu au chombo ambacho kinaweza kuamua fulani kavuka uhuru wa aina fulani ni Mahakama baada ya mashtaka kuletwa na vyombo husika. Waziri wa Mambo ya Ndani hana uwezo wa kuamua juu ya “uhuru wa vyombo vya habari”. Tukikubali kuwa kwa vile mtu ni “Waziri” basi ana uwezo wa kurithi wa kuamua juu ya uhuru wa kuabudu, uhuru wa kwenda, uhuru wa kusema, au uhuru mwingine wowote, si tu tutakuwa tumefungulia mlango wa uimla, tutakuwa pia tumetoa baraka ya kutawaliwa kimabavu!

Waziri Masha alinukuliwa pia wiki iliyopita akisema kuhusu tuhuma za Mengi kuwa “Asipoleta ushahidi wake ndani ya siku saba, serikali ina wanasheria wake, watapitia sheria zinasemaje ili ichukue mkondo wake hawezi kutoa madai mazito eti kwa vile ana vyombo vya habari, ni hatari”. Hili pia kwa mtu asiyetafakari anaweza kuona ni hoja kweli. Hata hivyo tunajiuliza kuwa na vyombo vya habari ni jambo baya? Mbona serikali ina vyombo vyake vya habari ambavyo wakati mwingine vinatoa habari nusunusu tena za kichonganishi?

Nakumbuka vizuri taarifa ya habari ya saa mbili iliyosomwa na TBC kuelezea kifo cha Chacha Wangwe. Taarifa ile iliyosomwa na chombo cha serikali hakuna mtu anayekumbuka kwa sababu hawakugundua uzito wake. Lakini sisi wengine tuliihusisha na mapigano ya kule Tarime kwani ndani yake ilijaa uchochezi dhidi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ilitaka kuwagawa wananchi wa Tarime.

Jinsi habari mbalimbali ambazo zimekuwa zikitangazwa na shirika hilo la serikali kwa wengine wanaona hazina matatizo (na ni kweli kuwa TBC imebadilika sana) lakini wakati Masha anatoa tuhuma dhidi ya mmiliki wa vyombo vya habari yeye mwenyewe alikuwa anatumia chombo cha habari ambacho serikali inamiliki! Kwa maneno mengine ni kosa kwa Mengi kutumia vyombo vya habari anavyomiliki kwa sababu ni “hatari” lakini kwa Waziri mwenye mgogoro wa maslahi katika suala hili ni halali kwake kutumia vyombo vya habari ambavyo serikali inamiliki. Hizi ni dalili za mvinyo mkali wa mtu aliyelewa madaraka!

Lakini kauli yake ambayo imeonyesha kuwa tatizo hili la madaraka limeanza kumtafuna kijana wetu ni pale aliposema akiwa na macho makavu kuwa “Asitumie vyombo vya habari kutoa tuhuma kwa serikali. Ni kweli serikali inatambua kuwa kuna uhuru wa vyombo vya habari, ingawa uhuru hauna budi kutumiwa ipasavyo na si kutoa taarifa zisizo sahihi. Hii ni serikali si serikali ya kuifanyia mchezo.” Nimeichukulia kauli hiyo kama kitisho cha wazi dhidi ya Mzee Mengi.

Sasa inawezekana watu wana sababu ya kutompenda Mzee Mengi, kwa sababu za kikazi, au binafsi. Yawezekana hata wapo ambao wanaweza kuhalalisha chuki zao kwa sababu ya vyombo vyake vya habari. Lakini inapotokea kuwa Waziri anatangaza hadharani kuwa vyombo vya habari visitumike kuishutumu serikali anataka watu waishutumu serikali kutokea wapi, kwenye mapaa ya nyumba zao au chini ya uvungu wa vitanda vyao?

Jukumu la vyombo vya habari ni pamoja na kutoa madai na shutma dhidi ya mtu yeyote yule au chombo chochote kile. Jukumu hilo linalindwa kikatiba. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (ambayo natumaini Mhe. Masha atakuwa amewahi kuipitia) inaelezea juu ya uhuru wa maoni. Katiba hiyo hailezi maoni hayo yatolewe wapi na nani. Katiba hiyo inasema kuwa “kila Raia” na mara ya mwisho nakumbuka Mengi naye ni raia wa nchi hii.

Lakini cha kushangaza pia ni kuwa uhuru wa habari na maoni hauhusu maoni sahihi, yanayopendeza au kukubalika! Mtu akitoa maoni yake au mawazo yake juu ya jambo fulani mtu huyo ana haki ya kufanya hivyo. Kama maoni hayo hayana ukweli au mawazo hayo hayana msingi basi mtu anajitokeza na kuyaonesha ni kwa nini hayana msingi na kuyapuuza. Kama ni mawazo au maoni ambayo yanaonekana yana mwelekeo wa kuvunja sheria (kitu ambacho siamini kuwa ya Mengi yalifikia huko) basi jukumu la vyombo vya serikali ni kuyafuatilia na kuyapima kwa sheria.

Sasa Waziri anapojitokeza na kutoa siku saba kwa raia kuwa alete ushahidi vinginevyo “atakiona” ni utoto na kutokukomaa kiuongozi.

Yote hii ni mifano tu ya watu ambao wamelewa uongozi, na ambao wanapepesuka kama Mzee Pombe si Chai au yule mzee mwingine wa Tamthiliya ya Ngoswe, Mzee Chapuuka. Njia pekee ya kuwazuia watu hawa waliolewa mvinyo wa madaraka ni kuwaweka pembeni ya kileo hicho ili angalau wajifunze kufanya kazi bila kileo kichwani.

Ni kwa sababu hiyo watu kama Masha wanahitaji wao wenyewe kutafuta msaada wa kukaa pembeni ili kuelimishwa kidogo na kujifunza kutumia mvinyo vizuri na kama wanashindwa kujizuia kuutumia vibaya basi kuwanyima kabisa. Madaraka kwenye Taifa ni lazima yasimamiwe vizuri.

Madaraka ni lazima yawe kwa ajili ya utumishi na si unyanyasaji ya walio chini. Madaraka ya umma lazima yarudi kuwa kweli ni dhamana iliyojaa heshima na fahari. Vinginevyo, hawa watawala wamejijengea tabaka la watu walevi ambao kitendo chochote cha kuwanyang’anya gilasi yao ya kileo chao hicho ni kutafutana ugomvi tu.

Wakati mwingine tumechanganya kusoma na kuelemika, kupata shahada na kupata elimu. Mtu anaweza akawa amesoma sana na kupata kila aina ya shahada, lakini hiyo haina maana kuwa mtu huyo kaelemika. Mwalimu alisema vizuri kuwa elimu itusaidie kuyakabili mazingira yetu. Mtu aliyepata elimu ambaye anashindwa kutumia elimu hiyo kuyadhibiti mazingira yake au kushirikiana na wengine kufanya hivyo basi huyo hajaelemika; anayo elimu tu. Fikiria mtu wa namna hiyo anapopata uongozi!

Tumepata kuwaona watu ambao ni wasomi kweli, lakini wakionja madaraka wanakuwa kama wamekalishwa kwenye mtungi wa mbege! Madaraka matamu ndugu zangu na hatuwezi kujua mtu atakuwaje hadi pale atakapoyaonja!

Kama wanashindwa kuyasimamia madaraka vizuri au kuonyesha kuwa wana hekima katika madaraka hayo ni bora kuwanyang’anya kwa kutumia sanduku la kura au kuwaomba wapumzike kwa hiari yao au wapumzishwe kwa shurti ya aliyewapa madaraka hayo.

Vinginevyo wakiwa na madaraka haya haya na kuendelea nayo bila kusahihishwa au kukemewa, watawala wa aina hii siku moja watajaribu kuua nzi kwa shoka! Nzi aliyetua kwenye goti lao!

NIlichotaka kusema ni kuwa tumewapa madaraka lazima tuwasimamie, tusikubali kamwe watutawale wapendavyo. Kama hawawezi waachie ngazi!
 
Tunaomba soft copy ya Tamthiliya ya Ngoswe Penz Kitovu cha Uzembe
 
Back
Top Bottom