Kisa Cha Anfaal - Laiti Ningelijua ........

Mahmood

JF-Expert Member
Feb 9, 2008
7,909
2,477
Anfaal, msichana wa kitajiri, alikaa bila ya stahamala katika chumba cha daktari akisubiri matokeo ya vipimo vyake. Alikuwa na haraka ya kuhudhuria sherehe na alihofia huenda akachelewa kwenye miadi yake ya kutengeneza nywele. Kabisa hakufikiria yale matokeo kwamba huenda yakawa na kitu muhimu. Ilikuwa ni tahadhari tu iliyotiliwa mkazo na familia yake.

Hakuwahi kusumbuliwa na maradhi yoyote makubwa, mbali na maumivu madogo madogo ya mwili. Baadae ilikuwa zamu yake kumuona daktari. Alifanya haraka iwezekanavyo kuingia ndani. Alishangaa kumuona daktari akiwa mwenye huzuni na aliguswa zaidi pale alipoulizwa, "Hii ni yako?"

Alijibu, "Hapana, ni ya mwanangu."

Alitaka kujua ukweli na alifikiri kwamba labda daktari angeweza kuuficha ukweli, pindi akimwambia kuwa ni yake yeye mwenyewe. Alimtaka akae, hivyo alikaa huku akihisi aina fulani ya woga. Alimuangalia daktari kwa wasiwasi , pale aliposema,

"Kwanini hukumtuma mwanamme kuchukuwa matokeo?"

Anfaal akasema, nilikuwa najia njia ya huku kwa hivyo hakukuwa na haja ya kumtuma mtu yoyote."

Daktari alimwangalia kwa huzuni akisema, "Inaonyesha wewe ni msichana mwenye elimu. Unaeelewa asili ya uhai."

Alinyamaza, hapo Anfaal alianza kutetemeka.

Akauliza, "Una maanisha nini daktari?"

Daktari akasema, "Matokeo yanaonyesha kwamba kuna ugonjwa kwenye damu." Aliziangalia zile karatasi na akabakia kimya. Anfaal alitakiwa amuulize ili afahamishwe zaidi. Alilia kwa woga, "Ni Saratani (cancer)?"

Hakumtizama, wingu la huzuni liliziba uso wake. Ilikuwa kama aliyemhukumu kifo.

Alisema katika sauti ya kuvunjika moyo, "Nimekwisha!" Hapo daktari alitambua kwamba alikuwa amesema uongo, lakini ilikuwa amechelewa kuuficha ukweli. Alimuangalia kwa huruma na kumwambia, "Pole. Kwanini ulisema uongo? Hata hivyo uhai na kifo vimo ndani ya Uwezo ya Allaah. Wapo wagonjwa wengi wanaoishi muda mrefu na wenye afya wakafariki mapema."

Anfaal alihisi kama aliyekuwa anazama, kama kwamba kuna ngumi nzito inayokandamiza moyo wake. Alijaribu kujikaza ili arudishe nguvu, akasema, "Naomba radhi. Ahsante daktari."

Daktari alimpa moyo akisema, "Kuwa mwenye nguvu na matumaini mema. Sayansi ya utibabu inaendelea kukuwa. Yale magonjwa yasiyoweza kutibika leo yanaweza kutibika kesho, bado nina matumaini. Niwachie namba yako ya simu." Aliikariri namba yake ya simu bila ya kutambua nini anachokisema. Huku akihisi mshituko mkubwa na uchungu, alimshukuru tena daktari na kuondoka.

Alipokuwa nyumbani aliuficha ukweli. Hakujua jinsi ya kuishirikisha (kadhia ile). Hata hivyo, kila mtu alikuwa kashughulika, tayari kwa sherehe. Mama yake aliuliza, "Je ulikuwa kwa daktari? Kwanini hukwenda kutengeneza nywele?" Lilikuwa ni suala la mpito tu lisilohitajia jawabu. Kwa ufupi alisema, "Siendi kwenye sherehe!"

Alipanda juu kwenye chumba chake na kujifungia mlango.

Alijinyoosha juu ya kitanda chake akiwa na nguo zake zote huku akisikiliza sauti za familia yake, kama kwamba zilikuwa zikitokea sehemu ya mbali. Aliuhisi upepo unamvumia kwa sauti ya huzuni ya mauti, ukimlilia kuwa anakaribia kifo. Alikihisi chumba kuwa ni kigeni kwake kama kwamba punde angelikiwacha. Vipi kuhusu nyumba? Isingeweza kumkumbuka. Alikuwa kama mgeni. Wengine watachukua chumba chake na kumsahau. Alijaribu kulia lakini machozi hayakumsaidia.

Kwa uchungu aliangalia vilivyomzunguka. Mapazia yote aliyojaribu kuyapata kwa taabu, yatabaki. Haitojalisha ikiwa yalitengenezwa kwa kitambaa kisichopatikana kwa urasihi, atayawacha kwa ajili ya wengine. Alitamani laiti asingelijitaaabisha nafsi yake kwa ajili ya kitu kile. Alitamani laiti angelijiwekea hakiba ya wakati wake na fedha zake kwa vitu vya manufaa, ambavyo vingeweza kumsaidia wakati wa dhiki kama huu.

Alishangaa, "Ni kitu gani muhimu kwangu?" Alikuwa msichana mrembo na tajiri mwenye kila kitu ambacho moyo wake ulitamani. Kuna chochote kati ya hivyo kingeweza kumnusuru kutokana na kifo? Daima aliutumia muda wake mrefu kwenye kazi mashuhuri yenye mshahara mzuri. Bado alikuwa nayo hiyo kazi, lakini ingeliweza kumnusuru ili aepukane na kifo?

Wazo lilimjia, Aliharakia kwenye simu ambapo kila mtu alikuwa hayupo. Alimpigia simu daktari na kumuuliza kwa bidii, "Je nitaweza kupata tiba ikiwa nitasafiri kwenda nje?"

Daktari alisema, "Hakuna jipya nje, ila ni kupoteza pesa tu."

Aliweka simu chini akakaa kwenye kiti kilicho karibu nae.

Mshahara wake au mali yake haikuweza kubadilisha jambo. Alitembea kwenye vyumba vyote kama kwamba anaaga. Alitembea kwenye bustani ndogo akaiangalia miti huku akinong'ona, "Natamani hii miti ingelielewa kuwa naondoka, mawe yote, kuta….. Natamani hii milango ingelijua kuwa karibuni mikono yangu haitoifungua tena. Natamani mauwa yote ambayo niliyapandisha na kuyamwagilia maji yangeelewa. Mara ngapi miba na mawe magumu yalinichoma mikono yangu?

Mara ngapi nilimwagilia mauwa yaliyonyauka kwa machozi yangu pindi maji yakikosekana. Natamani yangeelewa nini maana ya kuondoka duniani. Hii miti ya matunda ilikuwa midogo nilipoipandisha, nilijitahidi kadiri ya uwezo wangu kuinawirisha mpaka imekomaa na kutoa matunda. Je inaelewa kama karibuni nitaondoka? Itakumbuka masiku nilipokuwa pamoja nayo? Je na hivi viti nilivyokuwa navitumia kwa kupumzikia, vitapungukiwa kwa kutokuwepo kwangu? Je vipo tayari kwa mtu mwengine kuja kuvikalia? Na hizi dhahabu na mapambo ya thamani na fakhari yatanisaidia huko niendako? Je hizi nguo za kila aina ya mitindo zilizojaa makabatini zitanisaidia? Pia hii TV kubwa kama sinema ambalo hujiburudishia kwa kuangalia miziki na yote yaliyoharamishwa litanisaidia? Je vyote hivyo vitapungukiwa nitakapoondoka? Natamani vyote hivyo vingelijua kuwa naondoka duniani. Natamani kama vyote hivyo vingenisaidia huko niendako. Lakini la! Vyote hivyo viko tayari kuja kurithiwa! Llaiti ningeliyajua hayo nisingeliyajali maisha haya. Nisingelihisi fakhari na kiburi…….

Laiti ningelijua kwamba mimi ni mgeni katika ulimwengu huu, nisingelidanganya wala kutamani anasa zake …….!

Laiti ningeliyajua haya kwamba kuishi maisha mepesi ni rahisi kuliko kuishi maisha ya anasa….!

Laiti ningeliishi maisha mepesi, nisingeliona taabu kuyavuka maisha ya ulimwengu huu na kwenda kuishi maisha mengine. Familia yangu hivi sasa inaburudika na sherehe. Ni mara ngapi nimerefusha wakati wangu katika sherehe kama hizi! na kwa kiasi gani nilishughulikia mitindo ya mavazi na nywele! Vinaweza kunisaidia?

Anfaal alijikalisha kwenye kiti cha karibu yake kama kwamba aliutambua ukweli ambao hapo awali hakuujua.

Alisema, "Ni nini nichukuwe? Hamna isipokuwa sanda na amali zangu. Aina gani ya amali zitakazokwenda na mimi katika safari yangu ndefu? Hamna! Naam, hamna!" Alimkumbuka rafiki yake Sarah, ambaye alimtumia kwa kumpa nasaha na maelekezo ya kheri katika njia ya Allaah. Alizowea kumkumbusha Aayah za Qur-aan:

((Kila nafsi itaonja mauti. Na bila ya shaka mtapewa ujira wenu kaamili Siku ya Qiyaamah. Na atakayeepushwa na moto na akatiwa Peponi basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si kitu ila ni starehe ya udanganyifu)) [Aal ‘Imraan 3: 185]

((Enyi mlioamini! Mcheni Allaah, na kila nafsi iangalie inayoyatanguliza kwa ajili ya Kesho (Qiyaamah). Na mcheni Allaah. Hakika Allaah Anazo khabari ya mnayoyatenda))[Al-Hashr 59: 18]

Kabisa hakuzingatia umuhimu wa kufanya amali njema. Hivi sasa anahitajia amali hizo ili azihudhurishe kwa Allaah, kwani Atasimamishwa ili atowe maelezo ya hesabu yake, lakini atasema nini? Kwani hakuwa mwenye kuzikumbuka Rehma za Allaah na Maamrisho Yake?Vipi ataweza kuomba msamaha wakati hakuweza kabisa kufikiria kumtii Yeye alipokuwa na siha yake?

Alitamani laiti angelisoma Qur-aan Tukufu badala ya vile vitabu rahisi vya hadithi za kubuni (novels). Alitamani laiti angeliongeza taaluma ya dini yake kuliko kusoma magazeti. Aliendelea kutamani laiti angelitenda mambo kadha-wa-kadha, na asingelifanya mambo ya kumuasi Mola wake. Alitamani laiti asingelimkasirikia, au kusema uongo au kumsengenya mtu yoyote. Alitamani laiti asingelijivuna na kudharau maskini.

Alisema,"Natamani ningeweza kuanza maisha yangu yote upya ili nirekebishe makosa yangu na nitii Maarisho ya Allaah. Niliabudia matamanio yangu nikampuuza Muumba wangu. Natamani ningepata muda kidogo wa kuishi ili nirekebishe madhambi yangu.

Aliikumbuka Aayah za Qur-aan ambazo babu yake alizoweya kuzisoma:

((Mpaka yanapomfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu! Nirudishe)) ((Ili nitende mema sasa badala ya yale niliyoyaacha. Wapi! Hii ni kauli aisemayo yeye tu. Na nyuma yao kipo kizuizi mpaka siku watapofufuliwa)) ((Basi litapopulizwa baragumu hapo hautakuwapo ujamaa baina yao siku hiyo, wala hawataulizana)) ((Ama wale ambao mizani zao zitakuwa nzito, hao ndio wenye kufanikiwa)) ((Na wale ambao mizani zao zitakuwa nyepesi, hao ndio waliozitia hasarani nafsi zao, na katika (moto wa) Jahannam watadumu)) ((Moto utababua nyuso zao, nao watakuwa na nyuso zilizokunjana)) [Al-Muminuun 23: 99-104]

Hapo alisema, "Ewe Mola, nimekusudia ……" Machozi yalimwagika kwenye macho yake. Alilia kwa majuto na siyo kwa maumivu. Aliamua kumtii Allaah katika maamrisho Yake yote pindi akiishi zaidi kidogo tu!!. Simu ilipolia alitembea kinyonge kwenda kuipokea. Huku machozi yakimtoka alisema, "Enhe?"

Akasikia mtu akisema: "Naweza kuzungumza na Anfaal?" Alimtambua msemaji. Alikuwa ni daktari wake. Akajibu, "Ndiye anaezungumza."

Daktari alisema kwa furaha. "Hongera mtoto wangu! Huna tatizo lolote. Mshukuru Allaah!"

Alipigwa na bumbuwazi kwa mshangao. Hakujua aseme nini. "Hamna maradhi? Vipi? Je daktari unafanya mzaha!

Daktari akasema, "Allaah Anilinde kwa hayo, sifanyi mzaha. Punde mfanyakazi wa maabara ameniomba radhi. Alieleza kuwa kulitokea mchanganyiko wa majina. Jina lako liliandikwa badala ya mtu mwengine. Ripoti yako ipo mbele yangu. Wewe ni mzima kabisa. Mshukuru Allaah ewe mwanangu"

Kwa furaha alisema, "Shukrani kwa Allaah" (Nakushukuru Allaah), Ahsante daktari."

Aliweka simu chini akihisi kama kwamba ndio kwanza amezaliwa. Kuanzai hapo, alitambuwa kuwa yupo salama kwa muda tu, lakini mauti yatakuja tu siku moja. Hakuwa na muda wa kupoteza. Hata kama aliishi muda mrefu (lakini bado) yeye ni mgeni.

Kitu cha mwanzo alichokifanya ni kuswali, ambapo kwa muda mrefu alikuwa amepuuza. Aliahidi kutii Maarisho ya Allaah na Mtume Wake (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kuswali, kufunga, na kudumu kwenye mavazi ya heshima. Vile vile aliachana na yale yote Allaah na Mtume Wake waliyoyakataza. Ili asiyasahau haya, alizinakili Aayah za Qur-aan kwenye kadi kisha akazitundika kwenye ukuta.

((Na simamisheni Swalaah, na toeni Zakaah, na mtiini Mtume, ili mpate kurehemewa)) [An-Nuur 24: 56]

((Na iogopeni Siku ambayo mtarudishwa kwa Allaah, kisha kila nafsi italipwa ilichochuma. Nao hawatadhulumiwa)) [Al-Baqarah 2: 281]

Na akahofu asije kurudia makosa tena akaja kujuta tena. Akanakili pia kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) imkumbushe:

((Na rejeeni kwa Mola wenu, na silimuni Kwake, kabla ya kukujieni adhabu. Kisha hapo hamtanusuriwa)) ((Na fuateni yaliyo bora kabisa katika yale yaliyoteremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu, kabla haijakujieni adhabu kwa ghafla, na hali hamtambui)) ((Isije ikasema nafsi: Ee majuto yangu kwa yale niliyopoteza upande wa Allaah, na hakika nilikuwa miongoni mwa wanaofanya maskhara!)) ((Au ikasema: Ingelikuwa Allaah Ameniongoa, bila ya shaka ningeli kuwa miongoni mwa wenye kumchamngu)) ((Au ikasema inapo ona adhabu: Lau kuwa ningeli pata fursa nyengine, ningelikuwa miongoni mwa wafanyao mema) [Az-Zumar 39: 54-58).

Kwenye upande mwengine aliandika kauli ya ‘Umar ibn Al Khatwaab:

"Hesabuni nafsi zenu kabla ya kuhesabiwa, na zipimeni kabla ya kupimwa, kwani ni bora (wepesi) kwenu kupima (amali zenu) leo kabla ya (kupimwa) kesho kwenye Hesaabu, na jipambieni kwa siku ya Hadhara kuu,((Siku hiyo mtahudhuriwshwa haitafichika siri yoyote))"[Al-Haaqah 69:18]

Na methali ya busara:

"Tubia kabla hujafa, kwasababu huwezi kujua lini utakufa, hivyo basi daima kuwa ni mwenye kutubu."

Karibuni katika forums yetu http://www.sekenke.com/bodi
na katika site yetu http://www.sekenke.com

 
Shukran Ndugu Mahmoud... Kisa hiki kina ibra/mafundisho/maonyo kwa wale tu wenye kutumia akili zao. Kwani wale watu wasiotumia akili wanachukulia kwamba ni porojo za watu wa kale. Hawajui kwamba mauti yako yanamngojea kila mmoja wetu na kisha atasimamishwa kwa Mola siku ya Kiyama na kabla ya hapo ataulizwa kaburini mwake na Malaika watakaomshukia Munkar na Nakiir. Na kabla ya hapo kila mmoja wetu atajua mahali pake hata kabla ya kupelekwa kaburini. Kwasababu Malaika wa mauti watambashiria mara tu atakapokuwa katika mhangaiko wa mauti/sakaraatil mawti. Na inatokana na mtu mwenyewe, ikiwa ni Mwislamu mchaMungu, basi atabashiriwa Pepo. Lakini akiwa muasi aliyesahau Akhera na akapenda maisha ya dunia tu, basi Malaika watambashiria Moto wa Jahannamu. Tunamuomba Mwenzi Mungu atuongoze sote katika njia yake iliyonyooka nayo ni Siraatul Mustaqiim itakayotufikisha katika maisha ya Akhera ya raha na furaha. Amiin!!!!
 
Shukran ndugu Mahmoud kwa kisa hiki chenye maneno ya busara, na mafunzo mengi.
 
kaka thanx kwa mada yenye kufunza watu kumcha na kumtegemea mungu maana ndiye ajuaye kuja kuishi na kuondoka kwetu hapa duniani...yupo juu ya kila kitu
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom