kipi kinachokufanya, makwetu kuturudia

Ngambo Ngali

JF-Expert Member
Apr 17, 2009
3,517
1,360
Mbili ziro ziro tano, kwetu ulijipitisha,
Ukaita mikutano, sera zako kutupasha,
Katika ule mtoano, oktoba uliokwisha,
kipi kinachokufanya makwetu kuturudia?

Siku zile ulisema, tena ukiwa bayana
Picha yako nacho chama, pale zilipoambatana
Kura zetu ulisema, hapo ndipo patafana
kipi kinachokufanya makwetu kuturudia?

Kama hiyo tungefanya, ushindi ungeupata,
Nao ungekupa mwanya, kiti jengoni kupata
Hivi ndivyo tulifanya, na ubunge ukapata
kipi kinachokufanya makwetu kuturudia?

Ahadi zilikuwa nyingi, ambazo ulizitoa
Na tutaingia kingi, jengoni ukiingia
Kumbe ulaghai mwingi,binafsi ulijipangia
kipi kinachokufanya makwetu kuturudia?

Hakika uliyasema, maji kwako ni muhimu
Akina dada na mama, ndoo mitungi sumu
Hata na vile visima, utavifanya adimu
kipi kinachokufanya makwetu kuturudia?

Barabara nazo pia, ulisema umeona
Hakika zemechakaa, lami tutaiona
Kipindi kinaishia, hakuna tulichoona
kipi kinachokufanya makwetu kuturudia?

Na afya ulipayuka, umeweka mikakati
Zahanati tukifika, matibabu tutapata
Na muda utapofika, magonjwa hatutapata
kipi kinachokufanya makwetu kuturudia?

Hukusahau elimu, msingi na sekondari
Ulisema ni muhimu, ili tuwe mahodari
Navyo vyuo vitatimu, kusomesha daktari
Kipi kinachokufanya makwetu kuturudia?

Ni kweli ulijitapa, maisha yatakuwa bora
Kila kitu chapachapa, kulinganisha na sera
Ambazo ulijitapa, ili ujipatie kura
kipi kinachokufanya makwetu kuturudia?

Mbili ziro ziro kumi, waanza kujipitisha
Tumesikia uvumi, muda wako umekwisha
Sasa wataka utemi, wajinga kupagawisha
kipi kinachokufanya makwetu kuturudia?

Sasa tumeerevuka, siri yako twaijua
Akili zimepevuka, mbinuzo kuzitambua
Ujinga umetutoka, na vyote tumevijua
kipi kinachokufanya makwetu kuturudia?

kura zetu huzipati, pasipo kutueleza
Itakuwa hatihati, serazo kuzieleza
Kama jibu hatupati, uongozi kupoteza
kipi kinachokufanya makwetu kuturudia?
 
Juzi umetutusi, kura zetu si za maana
Umetufanya mijusi, tubaki kukanyagana
wewe uende urusi, sie twala wali jana
kipi kinachokufanya makwetu kuturudia?

Leo kwetu umekuja, kura wanyenyekea
Kwani umesahau ja, makosa janyenyekea
kweli muenda huja, kurani twakungojea
kipi kinachokufanya makwetu kuturudia?

Kesho utayarudia, makosawe ulofanya
ila hatutongojea, matapishi kutapanya
kura yangu tangojea, utaishia kuhanya
kipi kinachokufanya makwetu kuturudia?
 
Back
Top Bottom