RAIS Jakaya Kikwete amesema, tangu aingie madarakani Desemba 2005, hajawahi kuidhinisha kunyongwa kwa mtu yeyote.
Kikwete amesema, atatoa uamuzi wa kunyongwa au la kwa watu waliotiwa hatiani kwa kuua albino, suala hilo likifika mezani kwake.
Rais Kikwete alibainisha hayo juzi kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa, wakati akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa kampeni kuomba achaguliwe tena kuongoza Tanzania.
"Tuliendesha kura za maoni hapa juu ya suala la watu wanaoua albino.Baada ya kura hizo, wengine wanachunguzwa hadi sasa, wengine wamefungwa na mahakama," alisema Rais Kikwete na kuongeza:
"Baada ya hukumu ya mahakama, baadhi ya viongozi wa albino wamenitumia ujumbe na kutaka wale waliohukumiwa kunyongwa, niwanyonge.
"Sijawahi kunyonga hata mtu mmoja tangu niingie madarakani, lakini nitaamua suala hilo likifika mezani kwangu."
Mahakama Kuu ya Tanzania katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga, imetoa hukumu za kifo hadi kunyongwa mwaka jana kwa watu wapatao saba ambao iliwatia hatiani kwa mauaji ya albino.