kikwete ni rais anayekabiliwa na changamoto nyingi

Kipepeo

Senior Member
Feb 5, 2008
186
11
Jakaya Mrisho Kikwete ni Rais wa Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokea madaraka toka kwa Benjamin William Mkapa mwaka 2005 hadi wakati huu Tanzania Bara inapotimiza miaka 50 ya uhuru wake .Maisha yake
Jakaya Mrisho Kikwete amezaliwa Oktoba 7, 1950 katika kijiji cha Msoga kata ya Lugoba ,tarafa ya Msoga wilayani Bagamoyo katika mkoa wa Pwani ni mtoto wa sita kati ya watoto tisa wa mzee Khalfan Mrisho.
Kikwete amezaliwa katika familia ya mwanasiasa Mzee Khalfan Mrisho Kikwete aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Pangani na vilevile Chifu wa Wakwere na Mama Kayaka.
Alianza elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Lugoba darasa la kwanza mpaka la nne kuanzia mwaka 1958 hadi 1961. Nakuendelea na shule ya kati ( middle School ) Lugoba mwaka 1962 hadi 1965..
Baada ya kumaliza shule ya kati (middle school) na kufaulu aliendelea na elimu ya sekondari katika Sekondari ya Kibaha mwaka 1966 mpaka 1969 na Sekondari ya Tanga mwaka 1971 na 1972 kwa masomo ya kidato cha tano na sita.
Mwaka 1972 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na alifanikiwa kuhitimu shahada yake ya kwanza katika masuala ya uchumi mwaka 1975.
Hatimaye alijiunga na Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kupata mafunzo ya uofisa katika chuo cha Uongozi wa kijeshi huko Monduli.
Mwaka 1976-1977 alifanikiwa kutunikiwa kamisheni na kuwa Luteni. Tena mwaka 1984-1985 alijiunga na chuo hicho katika mafunzo ya ukamanda wa kombania.
Haiba ya uongozi toka shuleni

Kipaji chake cha Uongozi cha Rais Kikwete kilianza kuonekana toka akiwa shule ya kati Lugoba (middle school) na hata baadaye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alichaguliwa kwenye baraza la wanafunzi katika shule ya sekondari Kibaha pia akawa naibu kiranja mkuu katika shule ya sekondari Tanga.
Alipofika Chuo Kikuu, Kikwete alishika nyandifa mbali mbali katika uongozi ikiwamo kuchaguliwa kuwa makamu wa rais wa serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu upande wa mlimani mwaka 1973/74.
Akiwa mstari wa mbele kutetea na kupigania haki za wanafunzi na pia alikuwa mstari wa mbele kupinga ukandamizaji na ubaguzi.
Ndani ya chama wakati huo kikiwa chama cha TANU kipaji chake cha uongozi kilianza kuonekana akiwa katika shule ya sekondari Kibaha na Tanga ambapo alikuwa mwenyekiti wa umoja wa vijana wa TANU (TANU Youth League).
Alipokuwa Chuo Kikuu, Jakaya Kikwete alikuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Vijana chama cha TANU.
Mwaka 1978 alichaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Taifa ya Umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ajira na uongozi
Baada ya kumaliza elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama kijana mzalendo aliamua kujiunga na kufanya kazi ndani ya chama TANU na baadaye CCM badala ya serikalini au kwenye mashirika ya umma ambapo kulikuwa na maslahi zaidi.
Mwaka 1977 mpaka 1980 alianza utumishi ndani ya chama cha TANU kama Katibu msaidizi wa TANU Mkoa wa Singida.
Ilipofika mwaka 1980 Kikwete alihamishiwa katika ofisi ndogo ya Chama Cha Mapinduzi makao makuu Dar es Salaam kama mkuu wa Utawala na mkuu wa Idara ya Ulinzi na Usalama .
Mwaka 1981 alipelekwa kuwa katibu mtendaji wa CCM mkoa wa Tabora alipokaa mpaka mwaka 1983 hatimaye akarudishwa jeshini kuwa kamisaa na mkufunzi mkuu wa siasa katika chuo cha Uongozi wa Jeshi Monduli.
Mwaka 1986 alikuwa katibu wa CCM wilaya ya Nachingwea na kuhamishiwa katika wilaya ya masasi mwaka 1988.

Uongozi ndani ya serikali ulianza Novemba 7, 1988, ambapo Kikwete aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini.
Mwaka 1990 alishika nyandifa ya kuwa Waziri wa Nishati na Madini hadi mwaka 1994 alipoteuliwa kuwa Waziri wa Fedha.

Mwaka 1995 katika serikali ya awamu ya tatu alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa hadi mwaka 2005. Akiwa kama Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Nje kukaa muda mrefu kwa kipindi cha miaka kumi hadi alipochaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vilevile Kikwete amekuwa mbunge toka mwaka 1990 hadi mwaka 1995, katika jimbo la Bagamoyo,kabla ya jimbo hilo kugawanywa katika majimbo mawili na yeye kuwa mbunge wa jimbo la Chalinze kuanzi mwaka 1995 hadi 2005.
Akiwa waziri, Kikwete alitumikia wizara hizo na kuleta ufanisi akiwa katika Wizara ya Maji na Madini alileta mfumo wa ununuzi wa madini kwa kutumia leseni, hiyo ilisababisha kuokoa madini yaliyokuwa yanauzwa kimagendo.
Ndani ya Wizara ya Fedha alipelekea kuanzishwa kwa mamlaka ya kodi Tanzania (TRA). Katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alikuwa muasisi wa sera ya Diplomasia ya Uchumi.
Kipindi cha urais 2005 mpaka sasa
Aliingia madarakani kwa kishindo kwa asilimia karibia 80.23 ya kura zote, hiyo ikiwa ni asilimia kubwa toka uchaguzi wa vyama vingi uanze hapa nchini mwaka 1995.
Chini ya serikali yake katika kipindi cha miaka mitano hadi sasa akiwa bado Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameweka mkazo katika uendelezaji wa elimu ya msingi mpaka sekondari .
Serikali yake ikwa chini ya aliyekuwa Waziri mkuu Edward Lowassa (kabla ya kujiuzulu) alijenga shule nyingi za sekondari maarufu kama shule za “Kata”.
Pia ameleta Mpango wa Maendeleo wa Shule za Sekondari (MMES) pamoja na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Juu. Amesaidia kuhamasisha ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ambacho kina uwezo wa kuchukua wanafunzi 40 elfu.
Kikwete amekuwa karibu na makundi yote ya kijamii huku akiruhusu uhuru wa habari kwa kiasi kikubwa na kuongoza nchi chini ya utawala bora na kufuata haki za binadamu. Katika uongozi wake ameendeleza mapambano dhidi ya rushwa ingawa safari bado inakabiliana na changamoto kadhaa.
Leo baada ya miaka hamsini ya Uhuru na Jakaya Mrisho Kikwete akipata bahati ya kuwa Rais katika kipindi hichi, changamoto ni nyingi zaidi kuliko katika vipindi vilivyopita.
Alilazalimika kuvunja baraza la mawaziri na kuunda tena baada ya kashfa ya rushwa ya Richmond iliyosababisha mawaziri watatu kujiuzulu akiwamo Waziri Mkuu.
Changamoto kubwa nyingine ni hasa uzalendo na uwajibikaji wa viongozi walio chini yake ukitia shaka machoni mwa wananchi.
Huku maisha ya mtanzania yakiwa yamepanda kutokana na mfumuko wa bei yakimgusa mwananchi wa kawaida kabisa na kuporomoka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania.
Lakini wakati tunasonga mbele wakati huu taifa likiwa na umri wa miaka 50. Wananchi wa kawaida kabisa wa vijijini wanataka rasilimali zao ziwasaidie kwa dhati katika kusonga mbele katika kipindi kingine cha miaka hamsini ijayo.
 
Back
Top Bottom