NAWEZA kudai kumfahamu Kikwete kuliko wengi wa mashabiki wake wanaohudhuria mikutano yake ya kampeni. Nimefanya naye kazi jeshini na serikalini kidogo, lakini nimefanya naye kazi sana kwenye Chama. Nimekuwa naye kwa karibu kama rafiki (siyo swahiba) kwa mambo ya kawaida. Anaweza kuandika hotuba nzuri ya kunisifia siku ya mazishi yangu. Haya yanatoka moyoni.
Mwaka 2005 yaliandikwa mengi ya kumsifia. Yakasemwa mengi ya kushadidia sifa zake muungwana, mtu wa watu, mstaarabu, chaguo la Mungu, tumaini lililorejea, mkombozi wa Watanzania, Musa wa pili na chaguo la Watanzania.
Akazoa kura nyingi zikiwamo za wapinzani, maaskofu, vijana, wasomi, wafanyakazi, wakulima, wachimbaji wadogo, wahamiaji haramu, wanajeshi, na wanafunzi. Naam, hata mama ntilie au kwa jina la utani Mama Lishe! Matumaini yalikuwa makubwa.
Tuseme ukweli, walioonya wazi juu ya hatari ya huko mbele walikuwa wachache sana, na waliodiriki kufanya hivyo kwa uwazi, ilibidi usiku wawe wanahama vyumba vya kulala!
Wapo wachache, hata nikidai mimi ni mmojawapo sitaaminiwa kwa maana hakuna ushahidi wa waliokataa ghiliba hii ndani ya chama chetu. Miaka mitano imekuwa ya mateso makubwa kwetu.
Tumesutwa, tumetukanwa na wanaojifunza kutukana. Tumeitwa majina na tumefikia kuhudhuria vikao vya chama na kuandikwa kuwa hatukuhudhuria kwa sababu ya ukimya wetu.
Kwenye vikao vya kahawa, tumetumiwa wajumbe wa kutuambia hatuwezi kumfufua aliyekwishakufa (Nyerere), hatuwezi kurudisha nyuma saa iliyokwishakwenda mbele, wakati umepita, tukae kimya. Nani atabishia simulizi yangu hii? Waliokuwa wachambuzi na wasemaji wa kuwatia moyo Watanzania wako wapi? Wote hao wamekwenda, zimebaki sifa zao!
Nirudi kwenye hoja yangu ya leo. Hivi Rais Kikwete ni msahaulifu au mzembe? Mbona anakumbuka marafiki wake wa zamani na wa karibuni lakini anasahau ahadi zake na kauli zake?
Walio karibu naye katika kampeni watakubaliana nami kuwa Kikwete ana kumbukumbu kali juu ya watu aliowahi kuwa nao zamani. Kila sehemu anayofika kwa mkutano atakuambia nani anazaliwa pale, atauliza yuko wapi siku hizi, ataagiza mwambie amtafute wazungumze au ataagiza apatiwe hiki au kile kama ameambiwa kuna shida.
Akiambiwa alikwishakufa, atabadili ratiba akahani msiba au aitiwe mzazi au mjane ampe ubani. Atakumbuka hata dondoo ndogo sana za urafiki wake na mtu huyo.
Hii inavutia wengi na waandishi wetu wameagizwa na kuamriwa kuhakikisha matukio kama hayo yanakuwa katika picha na kurasa za mbele za magazeti.
Wakati huo huo, Kikwete ni msahaulifu wa ahadi zake kwa watu binafsi na hata kwa umma. Wapo wanaodai hili si tatizo lake, ni tatizo la watendaji wake ambao wanapaswa ama kuchukua kumbukumbu na kutekeleza au kumkumbusha. Mimi nadhani ni tatizo lake nitaeleza sasa.
Uaminifu wa kutekeleza ahadi huanza na kauli. Kikwete ni msahaulifu wa aliyoyasema. Ama hatunzi kumbukumbu za aliyosema, au hafikirii madhara ya kauli zake, au yote mawili kwa wakati mmoja.
Alipoingia madarakani alisema urais wake hauna ubia. Alilenga kuwajibu waliokuwa wanamsakama kuwa ametekwa na marafiki. Juzi juzi wakati anachukua fomu ndani ya chama, pale Dodoma, akakausha macho na kusema; Urais ni suala la kifamilia.
Alilenga kuwajibu waliokuwa wanahoji kitendo cha mtoto wake Ridhiwani kuzungusha fomu ya kutafuta wadhamini. Mpaka hapa inaonyesha Kikwete amesahau alisema nini 2006 au sehemu zote mbili hakufikiri kabla ya kusema. Urais ni taasisi. Urais ni utumishi wa umma. Rais ni mbia wa urais na wananchi wa Tanzania. Ndiyo maana mtu haamki asubuhi na kujitangaza kuwa yeye ni Rais. Anakwenda kuwaomba wananchi wamchague awe rais. Akishakuwa rais, haina maana urais ni mali yake na familia yake.
Ni kituko kikubwa kwa rais kusema alivyosema Kikwete katika hafla hiyo ya Dodoma. Katika nchi zenye mifumo makini, serikali ingechukua hatua, au chama husika kingechukua hatua na kama vyote viwili vingeshindwa, basi, wananchi wangechukua hatua kupitia sanduku la kura.
Siyo siri kuwa hivi sasa familia ya Rais Kikwete imeingia kwa nguvu za ajabu katika uendeshaji wa nchi na hakuna mtu ndani ya Chama wala serikali anayeweza kuthubutu kulikemea jambo hili. Uliokuwa ubia wa urais kati ya Kikwete na marafiki zake, sasa umegeuka ubia wa Kikwete na familia.
Siku hizi si jambo la ajabu kumwona Mama Salma anaingia ndani ya vikao vya Kamati Kuu. Kamati ya maadili wananungunikia kwenye korido, Kamati Kuu wanaongelea chini chini, wajumbe wa NEC hao ndiyo basi!
Mama Salma sasa anafanya majukumu ya kichama bila kibali cha kikao chochote, na mbaya zaidi anaagiza, anakemea, anatishia, ananyanganya na kugawa madaraka. Viongozi wa serikali mikoani na wilayani wako hoi. Hawajui wafanye nini na mama huyu.
Mmoja wa wakuu wa mikoa ameniambia, safari hii, hata kwa risasi, hatakubali kuteuliwa kuendelea na ukuu wa mkoa kama mambo yanakuwa hivi. Anadai wiki hii unampokea Baba na madai yake, wiki inayofuata anakuja mtoto naye anataka uende uwanjani kumpokea, hujakaa sawa anakuja mama, unaambiwa uhame nyumba kumpisha, siku inayofuata anakuja yule mdogo wa chipukizi, unaambiwa umsindikize mpaka aondoke mkoani kwako.
Mkuu huyo wa mkoa anakangaka: Tumeteuliwa kutumikia familia? Polisi wanapiga saluti kwa mama, mtoto Ridhiwani anadai ripoti kutoka kwa Mkuu wa Mkoa? Kamati za siasa na kamati za ulinzi wanachanganyikiwa hawajui wafanye nini?
Mpaka hapa mtu unajiuliza: Kikwete aliposema hana ubia na mtu alimaanisha nini ikiwa watoto wake wawili na mkewe wanafanya kazi za Chama na serikali kwa gharama za serikali?
Matokeo ya ubia huu wa Kikwete na familia yake ni kusitasita kwa Kikwete kuchukua hatua muhimu za kurekebisha hali ya nchi.
Watu wamelia, vyombo vya habari vimelalamika na ripoti kadhaa zimeandikwa lakini hakuna hatua iliyochukuliwa dhidi ya mafisadi, wala rushwa, wazembe serikalini, wakwepaji kodi wakubwa, wezi wa nyara za taifa, wauza madawa ya kulevya na majambazi.
Kusitasita kwake kunatokana na hujuma iliyo ndani ya familia yake. Maadui wa ndani ya taifa letu ambao ni mafisadi ni wajanja.
Walipoona kelele za watu zinaanza kumwingia Kikwete na kumnyima usingizi, wakamzunguka kupitia familia yake na wanajimu. Wanajua fika hapo hawezi kunasuka. Sasa baadhi yao wamezama katika ufisadi wa kutisha. Ni Mungu tu ajuaye hatima yao.
Kabla ya kufika mwisho wa fitina zangu hizi (ndivyo JK anavyoziita makala hizi), nikumbushe na kusisitiza jambo la msingi. Pamoja na wema wake na misimamo yake tata isiyompa nafasi ya kuwa mtendaji mzuri serikalini na kwenye chama, hivi sasa Kikwete ajue yafuatayo yako ukutani.
Nitataja bila kufafanua. Kwanza, pamoja na kusita kuwachukulia hatua mafisadi, hata wao hawamtaki na hawampendi kwa sababu wanamwona ni mdhaifu asiyeweza kuwahakikishia ulinzi mbele ya wanaolalamikia ufisadi.
Wameniambia kuwa Kikwete ni mzigo kwao na kwa taifa. Pili, Kikwete hana risasi za kuwaua Watanzania wote wanaolalamika na kuteketea kwa umaskini mbele ya utajiri wa taifa letu. Hukumu yao kuna siku itatolewa, kama si mwaka huu, basi wakati mfupi ujao.
Na wakati huo hata kama atakuwa hayupo duniani (sote twaenda huko), hata kutemea mate picha yake, kutampa mtu usingizi wa siku moja.
Tatu, uongozi usio na maadili huzaa mamluki wengi. Hivi sasa siri nyingi za Ikulu zimezagaa mitaani kwa sababu tu Kikwete ameruhusu Ikulu pawe pango la mafisadi, wanajimu, wafanyabiashara na matapeli. Watu wasio na maadili hawawezi kutunza siri za nchi, ndo maana hata mikataba ya siri inavuja.
Hawa siku moja watasimama kizimbani, si kama washtakiwa, bali kama mashahidi dhidi ya uongozi wa Kikwete uliokosa mwelekeo na kushindwa
Msomaji Raia
Source: Septemba 15, 2010