Kikwete, nani hawa walioficha fedha zetu Uswisi?

rosemarie

JF-Expert Member
Mar 22, 2011
6,887
3,412
KATIKA toleo Na. 229, niliandika kwenye safu hii kuwauliza watawala wetu ni lini hasa Tanzania itawakamata kina James Ibori wetu.

Niliandika makala hiyo kufuatia tukio la wiki hiyo la fisadi la kimataifa lililokuwa gavana wa jimbo la Niger Delta la Nigeria, James Ibori, kutiwa hatiani na mahakama moja huko Uingereza.
James Ibori alikuwa akichunguzwa kwa miaka saba na Polisi wa London kwa makosa mbalimbali ya ufisadi alioufanya nchini mwake na nje ya nchi ukiwemo wa kushiriki kwenye biashara chafu ya fedha (money laundering).

James Ibori ni fisadi ambalo katika miaka minane tu ya ugavana wake wa jimbo hilo lilikwiba fedha za umma zinazofikia pauni za Uingereza milioni 250.
Kwa ufisadi huo, si tu liliishi maisha ya kifahari ikiwa ni pamoja na kujinunulia magari ya kifahari ya Range Rover yasiyopenya risasi na majumba kadhaa huko Ulaya, lakini pia lilidiriki hata kujaribu kujinunulia ndege binafsi.

Lakini, hatimaye, maisha ya ufisadi ya James Ibori yalifikia ukingoni alipokamatwa na polisi wa kimataifa (Interpol) huko Dubai wakati akijaribu kununua ndege hiyo kwa pauni milioni 17. Alirejeshwa Uingereza ambako alifunguliwa mashitaka hayo na kuhukumiwa kifungo cha miaka 13. Sasa ‘bilionea' huyo anasota jela kunakomstahili!

Katika makala hiyo, niliutumia mfano wa ufisadi huo wa James Ibori kuwahimiza watawala wetu nchini nao wafanye juhudi za kuwasaka na kuwafikisha mahakamani mafisadi wetu wa sampuli yake.
Baadhi ya wasomaji wangu walioisoma makala hiyo hawakuamini kwamba Tanzania nasi tuna mafisadi wakubwa wa sampuli ya James Ibori. Kwa hakika, wengine hawakuamini kwamba tuna Watanzania mafisadi waliokwiba fedha nchini na kuzificha kwenye mabenki ya nje.

Nafarijika kwamba waliokuwa hawaaamini nilichokiandika katika safu hiyo, sasa wana kila sababu ya kuamini baada ya wiki iliyopita ripoti ya mwaka ya Benki Kuu ya Uswisi kuweka mambo hadharani.
Katika ripoti hiyo ya Swiss Central Bank, iliyotolewa mwanzoni mwa wiki iliyopita, Tanzania ni miongoni mwa nchi 11 barani Afrika ambazo vigogo wake wa kibiashara, kitawala na kisiasa wameficha, kwa siri, mabilioni ya pesa katika mabenki ya Uswisi.

Habari hizo ambazo zimepewa kipaumbele mitandaoni na pia na magazeti mawili makubwa ya Kiingereza ya Afrika Mashariki kwenye matoleo yao ya Jumamosi; yaaniThe Guardian la Tanzania na The Monitor la Uganda, zinataja nchini nyingine za Afrika kuwa ni Kenya, Uganda, Zimbabwe, Misri, Shelisheli, Afrika Kusini, Rwanda, Sierra Leone, Somalia na Sudan.
Kwa upande wa Tanzania, mapesa ambayo yamefichwa huko ni dola milioni 196.87 sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 315.5! Hebu jiulize; mapesa haya tuliyoibiwa yangetusaidia kiasi gani kama yangerejeshwa nchini na kutumbukizwa kwenye miradi ya kuboresha huduma za jamii?
Lakini pia hebu jiulize swali jingine la pili: Je, hata baada ya Benki Kuu ya Uswisi kuturahisishia mambo kwa kututobolea ukweli kwamba tumeibiwa, na kwamba wezi wetu wameficha hizo pesa Uswisi, watawala wetu wana dhamira ya kuanzisha mchakato ili wahusika wafikishwe mahakamani na fedha hizo zirejeshwe nchini?
Nachelea kuwa na jibu la ‘ndiyo' kwenye swali la pili, na kuchelea kwangu kutoa jibu la namna hiyo kunatokana na namna watawala wetu walivyoacha (kwa makusudi) kuchukua hatua zilizopaswa kuchukuliwa kuhusu tuhuma zile dhidi ya Andrew Chenge za kuweka dola milioni moja (yeye aliviita visenti!) katika akaunti ya siri kwenye benki moja huko Ughaibuni!

Lakini si hivyo tu. Hata kauli za mtawala wetu kama ile ya "mafisadi wakubwa ni wajanja, hawakamatiki" zinanifanya nisiamini kama kweli watawala wetu wana dhamira ya dhati ya kuanzisha michakato ya kuwanasa mafisadi wetu hawa wa kimataifa wa sampuli ya James Ibori.
Kwa hiyo, hata baada ya ripoti hiyo ya Swiss Central Bank inayoeleza wazi kwamba vigogo wetu wameficha huko Uswisi fedha walizotuibia kiasi cha Sh. bilioni 315, bado siwatarajii watawala wetu kuchukua hatua zozote bila kwanza kushinikizwa.
Katika hilo la kuchukua hatua, tumemsikia, kwa mfano, Mkurugenzi wa TAKUKURU, Edward Hoseah, alivyojibu alipoulizwa kuhusu ripoti hiyo mpya ya Swiss Central Bank. Hosea alisema eti ataiandikia barua benki hiyo Jumatatu kuomba wapatiwe ripoti hiyo ili waifanyie kazi! Hivi kweli hawezi kuanza mara moja uchunguzi, angalau kwa upande huu wa Tanzania, mpaka kwanza atumiwe ripoti hiyo kutoka Geneva?
Hivi kweli Hoseah hafahamu kuwa hata hatua ya Uswisi kuamua, katika miaka ya karibuni, kuondoa usiri mkubwa kwenye mapesa yanayokwibwa na kuficho huko kulitokana na shinikizo la kimataifa na si kwa utashi wake, na kwamba hata ripoti zake hizo hazitaji moja kwa moja majina hayo?
Hivi kweli hajui kuwa kuyapata majina hayo na kuwachukulia hatua wahusika kunategemea shinikizo la kisheria la kila nchi moja moja kwa benki hizo za Uswisi yalikofichwa mapesa hayo?

Ninachojaribu kueleza hapa ni kwamba, kuomba ripoti hiyo si jambo baya, lakini TAKUKURU kuacha kuanza uchunguzi haraka mpaka kwanza itumiwe ripoti hiyo, ni jambo linalotia shaka kuhusu uwezo wa taasisi hiyo kushughulikia ufisadi mkubwa kama huo wenye sura ya kimataifa.

Isitoshe, swali la kujiuliza ni kwamba TAKUKURU walikuwa wapi muda wote huo mpaka nao washitushwe na ripoti hiyo kama walivyoshitushwa wananchi wa kawaida? Lazima kuwe na tofauti ya kujua mambo kati ya mwananchi wa kawaida na vyombo vyetu vya usalama wa taifa ikiwemo TAKUKURU.
Labda nihitimishe tafakuri yangu ya leo hivi: Baada ya Swiss Central Bank kuweka mambo hadharani na kutuhakikishia kwamba fedha zetu zilizoibwa zimefichwa katika akaunti za siri kwenye mabenki ya Uswisi, ni jukumu letu Watanzania kuwashinikiza watawala wetu kuchukua hatua.
Watanzania wote – kuanzia wananchi wa kawaida hadi kwa wabunge, wanasiasa, NGOs, wasomi, viongozi wa dini nk, lazima tushinikize ili tuwafahamu vigogo hawa wa kibiashara, kiutawala na kisiasa nchini mwetu waliotuibia fedha zetu na kuzificha kwenye mabenki hayo ya Uswisi.
Na si tu tushinikize kuwajua kwa majina ni kina nani; bali tushinikize pia ili fedha hizo zirejeshwe nchini na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao ili hatimaye nao waende kifungoni kama alivyokwenda James Ibori, na fedha walizotuibia zirejeshwe nchini.

Na kama watawala wetu hawatatusikiliza katika hili, basi, tuhamishie shinikizo letu kwa wafadhili wa kigeni kwa kuwaomba wasitishe fedha walizoiahidi Tanzania kwenye bajeti hadi hapo itakapochukua hatua dhidi ya hao waliotuibia na kuficha fedha hizo kwenye mabenki hayo ya Uswisi.

Nina hakika wahisani wa nje watatusikiliza; maana sehemu ya hizo fedha zinazokwiba na kufichwa huko Uswisi yawezekana, kwa namna moja au nyingine, zinatokana na misaada au mikopo yao kwetu!
Lakini nihitimishe tafakuri yangu kwa kusema pia hivi: TAKUKURU haina uwezo wa kulichunguza suala hili na kututajia majina ya vigogo waliokwiba na kuficha fedha hizo Uswisi. Tuambizane ukweli; hayo ni maji marefu kwao, na hivyo tusiwategemee kutufanikishia kazi hiyo.
Hata wenzao wa Nigeria – Economic and Financial Crimes Commission (EFCC)walimshindwa James Ibori hadi Polisi wa London na Interpol walipoingilia kati kupeleleza na kukusanya ushahidi mbalimbali na hatimaye kumkamata na kumshitaki kwa kujihusisha na biashara chafu ya pesa nchini Uingereza.

Ingekuwa ni EFCC, pengine Wanigeria wangeelezwa, hadi leo, kuwa "upepelezi dhidi ya James Ibori unaendelea, na kwamba hakamatiki".

Ushauri wangu, hivyo basi, ni kwamba kwa kuwa haya ni maji marefu kwa TAKUKURU yetu, basi, natuikasimu kazi hii ya kupeleleza na kuwafikisha mahakamani mafisadi hawa walioficha mapesa yetu Uswisi kwa vyombo vya kimataifa vilivyobobea kwenye uchunguzi wa namna hiyo – mathalan Interpol, Scotland Yard nk.
Au tukishindwa kabisa kuikasimu kazi hiyo kwa asasi hizo za Uingereza, basi, tumpe zabuni hiyo lile gwiji la kimataifa la kusaka fedha za madikteta wa Afrika zilizokwibwa na kufichwa Uswisi, Enrico Monfrini. Gwiji hilo ndilo lililoiwezesha Nigeria kurejeshewa mabilioni yaliyokwibwa na San Abacha na kufichwa kwenye mabenki ya Uswisi.

Najua watawala wetu watakimbilia kujitetea kuwa, Tanzania hatuna fedha za kutoa kwa vyombo hivyo ili vitufanyie kazi hiyo. Jibu langu kwao ni kwamba, hata Nigeria haikutoa senti hata moja katika gharama za uchunguzi uliofanywa na Polisi wa London naInterpol kumtia hatiani James Ibori.
Fedha za uchunguzi wote uliochukua miaka saba uliogharimu pauni milioni 5.4 zilitolewa na Idara ya Uingereza ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID). Kwa hiyo, nasi pia, tunaweza kuwaomba wafadhili wetu wa nje kugharimia uchunguzi huo wa kuwatia mbaroni kina James Ibori wetu hao waliotuibia na kuficha fedha zetu kwenye mabenki ya Uswisi. Uchunguzi huo pia utatuwezesha kurejeshewa mapesa hayo.

Sioni sababu kwa nini wasitusaidie sisi; hata kama ni kwa kutupunguzia misaada na kuelekeza fedha hizo kwenye mchakato wa kuwatia mbaroni mafisadi hao ili tutoe fundisho kwa wengine wote kwamba hakuna mahali salama wanakoweza kuyaficha mabilioni ya pesa wanazotuibia.

Na mwisho kabisa nimsisitizie Rais Kikwete kwamba; baada ya ripoti hiyo ya Swiss Central Bank kuweka mambo hadharani, sasa Watanzania wanataka majina ya vigogo hao waliotuibia na kuficha fedha hizo Uswisi.
Ni wajibu wake (Kikwete) kama rais kuhakikisha kuwa, hatimaye, Watanzania wanatajiwa majina ya vigogo hao na hatua zilizochukuliwa dhidi yao.
Tafakari!
 
Ninachoogopa,..ni kuwa, hawa Ma afisa wa Interpol, Scotland Yard watafanya kazi beneti na Mafisadi.
 
Back
Top Bottom