Kikwete na 'Don Kings' wetu!

Questt

JF-Expert Member
Oct 8, 2009
3,010
422
Kikwete na 'Don Kings' wetu!


Johnson Mbwambo
Juni 23, 2010

AGOSTI 2008 niliwahi kuandika kuhusu suala la Rais Kikwete kujiruhusu kuzungukwa Ikulu na court jesters; yaani wale walamba miguu wanaopatikana katika majumba ya kifalme ambao mfalme akicheka kidogo, wao hucheka sana. Akipiga makofi kidogo, wao hupiga sana, na akinuna kidogo, wao hununa sana!

Nilisema kwamba kama Rais Kikwete ana kigugumizi cha kufanya maamuzi magumu, ni kwa sababu anawasikiliza court jesters wanaomzunguka.

Nilisema pia kwamba kama Kikwete haoni picha halisi ya umasikini ilivyo nchini, ni kwa sababu ya kuzungukwa na court jesters hao ambao hummwagia sifa feki badala ya kumwambia ukweli.

Ningekuwa leo naandika rejeo kuhusu athari za rais kuruhusu kuzungukwa na watu wa aina hiyo, ningetoa mifano michache ya fedheha zilizompata kwa kuwaamini mno watu hao; lakini hiyo nayo ni hadithi nyingine ndefu inayohitaji nafasi ya pekee kuisimulia kikamilifu.

Leo, hata hivyo, napenda kupanua kidogo suala hilo la court jesters kwa kujadili kidogo kundi jingine ambalo sikuligusia kabisa katika makala yangu ya Agosti 20, 2008. Kundi hili unaweza kabisa kuliita kuwa ni la kina Don Kings.

Wanaofuatilia ndondi za kulipwa za kimataifa wanamjua Don King ni nani na ana hulka gani. Huyu ni promota wa mchezo huo ambaye amejikusanyia utajiri mkubwa kutokana na ‘usanii’ wake wa kuwavutia mabondia maarufu duniani kupigana chini ya udhamini wake.

Wanaomfahamu vyema Don King wanajua kwamba mzee huyo atatumia kila hila na usanii kumweka chini ya himaya yake bondia anayetwaa ubingwa wa dunia ambaye aligoma kupigana chini ya udhamini wake.

Kwa hakika, kuna simulizi moja ya kusisimua inayomhusu Don King na bondia chipukizi aliyetwaa ubingwa wa dunia, na kisha akakataa kujiunga na mzee huyo. Don King alisononeka mno kwa kukosa mapesa ya kijana huyo, na akaendelea kubungua bongo kusaka mbinu ya kumnasa kijana huyo.

Kwa mujibu wa simulizi hiyo, siku moja bondia huyo chipukizi alipigiwa simu na kuelezwa kwamba baba yake amefariki. Kijana akasafiri kwenda kumzika baba yake, lakini alishangaa alipofika nyumbani alikuta maandalizi kabambe ya msiba wa baba yake yameshakamilika. Kila kitu kilikuwa ni cha gharama kubwa – kuanzia kwenye jeneza hadi gari la kubeba jeneza hilo.

Alipowauliza ndugu zake fedha za kuandaa mazishi hayo ya gharama kubwa zimetoka wapi, akajibiwa: “Zimetoka kwa God Father wako”. Alipowataka wamtajie huyo God Father, akajibiwa; “ni Don King”! Bondia yule alishangaa mno.

Lakini funga-kazi ilikuwa wakati wa mazishi yenyewe. Si tu kwamba Don King mwenyewe alijitokeza kaburini akiwa na kundi kubwa la ‘waliaji’ ambalo alilikodi, lakini yeye mwenyewe alilia kaburini kumshinda hata bondia mwenyewe mfiwa!

Don King alilia kana kwamba alipata kumfahamu marehemu yule, kumbe wapi – hakupata hata kumuona mara moja!

Ilikuwa ni ‘usanii’ mtupu, lakini uliofanya kazi; kwani siku mbili baada ya mazishi hayo alipotuma ujumbe kupeleka mkataba kwa bondia huyo ili ausaini kupigana chini ya udhamini wake, kijana alisaini bila kusita!

Simulizi inasema pia kwamba kama kuna pambano kati ya bondia wake yeyote dhidi ya bondia ambaye hayuko chini ya himaya yake, Don King hukaa katikati ya pande mbili za wasaidizi wa mabondia hao. Na kila pambano linapoonyesha kuwa bondia wake anazidiwa, Don King husogelea kidogo kidogo upande wa yule bondia anayeelekea kushinda!

Na raundi ya mwisho ikimalizika, huwa wa kwanza kuingia ulingoni kumbeba juu bondia yule aliyeshinda. Yule aliyekuja naye haendi hata kumpa pole ya kutwangwa! Humtelekeza pale pale ulingoni. Na siku inayofuata, itatangazwa (tena kwa mbwembwe) kwamba bondia aliyeshinda amehamia kwa Don King!

Huyo ndiye Don King – promota maarufu wa Marekani. Don King atamwaga hata chozi kama kufanya hivyo kutamwezesha kumnasa bondia ambaye ni bingwa duniani. Anachoona yeye mbele yake ni fursa tu ya kutengeneza mabilioni ya pesa kwa kuwatumia mabondia hao vijana.

Ndugu zangu, nimetumia nafasi kubwa ya safu hii fupi kusimulia vituko vya Don King, kwa sababu hata hapa Tanzania tuna ‘ma-Don Kings’ wetu katika nyanja ya siasa. Tuna court jesters, lakini pia tuna Don Kings.

Jumatatu, wiki hii, Rais Kikwete alikwenda kwenye ofisi za makao makuu ya CCM, mjini Dodoma, kuchukua fomu ya kuwania kuteuliwa tena na chama hicho kugombea urais wa Tanzania kwa kipindi cha pili na cha mwisho.

Kama ilivyotarajiwa, court jesters na Don Kings wengi (wakiwemo waandishi na wahariri) walijitokeza kujiweka karibu naye. Na kila mmoja alijitahidi “aonwe” na “Mzee” ili afahamu kwamba naye yumo katika kumuunga mkono!

Baadhi yao ni watu wazima na heshima zao, lakini walichokifanya si kwa sababu wanaamini kwamba Kikwete ni ‘chaguo la Mungu’; hivyo ndiye pekee anayestahili kugombea urais kwa tiketi ya CCM. Walichokifanya ni kujikomba tu ili asiwasahau kuwateua (‘kwenye ulaji’!?) kwenye ngwe yake ya mwisho ya urais.

Huwa najitahidi kuangalia kwenye luninga kipindi cha bunge na kushangazwa na idadi ya wabunge wanaoanza michango yao kwa ‘kumpongeza’ Kikwete kwa kuchukua fomu ya kugombea tena urais! Hivi katika mazingira ambapo wagombea wengine katika chama hicho hawatakiwi kujitokeza kumpinga, kuna mantiki na busara gani kumpongeza Kikwete kuchukua fomu ya kuwania urais?

Nasema huwa nawaangalia wabunge hao kwenye luninga na kujiuliza mwenyewe kimoyomoyo; ni nani miongoni mwao ni court jesters na ni nani miongoni mwao ni Don Kings.

Ndugu zangu, jambo la kukumbuka hapa ni kwamba itakapofika mwaka 2013, court jesters na Don Kings hawa, wataanza kidogo kidogo kumuacha Kikwete na kusogelea upande wa mwanasiasa mwingine anayeelekea kuwa na nguvu katika patashika za kuwania urais za mwaka 2015.

Watafanya hivyo kwa kuwa wanajua hawatakuwa tena na faida naye ifikapo Novemba 2015; maana tutakuwa na rais mpya! Kama afanyavyo Don King (promota), nao watasogea, kidogo kidogo, kuelekea upande wa ‘championi mpya mtarajiwa’ (rais mtarajiwa) ndani ya CCM hiyo hiyo!

Kwa ufupi; ukichambua kwa undani unafiki uliopo kwenye siasa za Tanzania na aina ya demokrasi tunayoiendesha, hutapata taabu kuelewa ni kwa nini tunakaribia kumaliza nusu karne tangu tupate Uhuru na bado tumezama kwenye umasikini mkubwa.

Tafakari!


Source Raia Mwema
 
Kama kuna mtu ambaye taratibu anaacha mark kwenye kazi anayoifanya basi ni huyu mwandishi mkongwe. Anaandika kwa simanzi na fikra kubwa yote yanayotuzunguka bila kuuma uma. Namtakia kila la kheri. Tanzania ijayo, naamini itapata fursa ya kunukuu baadhi ya maneno yake mengi ya hekima.
JK asiyadharau haya maneno ya Mbwambo maana yamejaa ukweli.
 
... court jesters; yaani wale walamba miguu wanaopatikana katika majumba ya kifalme ambao mfalme akicheka kidogo, wao hucheka sana. Akipiga makofi kidogo, wao hupiga sana, na akinuna kidogo, wao hununa sana!

Nilidhani court jester ni yule anaechekesha. Mwambo vipi tena?

Main Entry: court jester
Part of Speech: n
Definition: a clown or buffoon who is employed by a noble or royal for entertainment; also called fool
Example: The court jester typically wears a three-pointed hat with jingle bells attached.
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom