BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,789
- 288,011
Kikwete anapoteua mawaziri wake ...
2009-02-08 11:02:06
Na Simon Mhina
2009-02-08 11:02:06
Na Simon Mhina
Baadhi ya wasomi na wanasiasa wa kambi ya upinzani, wamemtaka Rais Jakaya Kikwete, kuwa makini anapoteua mawaziri, ili kuepuka kuteua watu wasio na sifa za uongozi.
Wametoa wito huo, kufuatia matukio kadhaa ya hivi karibuni ya baadhi ya mawaziri kutoa kauli zenye utata au kuchukuwa maamuzi yaliyo kinyume na sheria na taratibu na kusababisha mtafaruku katika jamii.
Wakizungumza na Nipashe Jumapili kwa nyakati tofauti, wasomi na wanasiasa hao, wamesema matukio ya viongozi kutoa kauli tata au kuchukua maamuzi yaliyo kinyume na sheria na taratibu ni ishara kuwa wapo viongozi waliopewa nafasi hizo kwa bahati mbaya kwani hawajui nini maana ya dhamana ya kuwa kiongozi.
Akizungumza na Nipashe Jumapili jana, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mwesiga Baregu, alisema matukio hayo yanatia shaka juu ya baadhi ya viongozi tulionao kama wanastahili kushika nafasi walizonazo.
``Inatia hofu kwa sababu tunategemea kwamba kiongozi wa kiwango hicho anaelewa dhamana ya vitendo na kauli yake kwa jamii``, alisema.
Akizungumzia tuhuma inayomkabili Waziri wa Mambo ya Ndani, Laurance Masha, ambaye anadaiwa kuingilia mchakato wa kumpata mzabuni wa kutengeneza vitambulisho vya taifa, Profesa Baregu, alisema tukio hilo linaonyesha tabia ya ubinafsi miongoni mwa viongozi kwa kuweka mbele maslahi binafsi kuliko ya umma.
Alisema hali hiyo pia inaonyesha kuanguka kwa maadili ya uongozi kwa kiwango cha juu na kuitaka serikali isimamie ipasavyo maadili ya viongozi wake kwani endapo baadhi ya viongozi wasipodhibitiwa kauli na vitendo vyao vinaweza kusababisha matatizo makubwa ndani ya nchi.
Pia alilitaka Bunge kusimamia ipasavyo utendaji wa serikali na viongozi wake kwa wabunge kuweka mbele maslahi ya umma kuliko ya vyama vyao vya siasa.
``Bunge liisimamie vyema serikali na viongozi wake ili kuhakikisha hawaendi nje ya mipaka na hii ifanywe bila ya wabunge kujali vyama vyao na rais naye aonyeshe njia akemee mawaziri wake wanaotenda kinyume na taratibu, kinachoonekana ni kama Baraza la Mawaziri limemgeuka hawazungumzi kwa sauti moja na kuyatetea maamuzi yao, kila mmoja anazungumza lake kwa maslahi yake``, alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tanzania Labor Party (TLP), Augustine Mrema, amemtaka Rais Jakaya Kikwete, asibabaishwe na mawaziri wake wanaoboronga. [/B]
Alimshambulia Waziri wa Mambo ya Ndani, Laurance Masha, kwa kujiingiza katika matendo aliyoyaita ya aibu kutokana na kutia mkono katika tenda ya kutafuta kampuni ya kutengeneza vitambulisho vya taifa.
Mrema aliyewahi kuongoza wizara hiyo, alisema amekuwa akishangazwa na matendo ya Waziri Masha.
``Kwanza Masha mwenyewe lazima aelewe kuwa yupo kwenye Baraza la Mawaziri kwa bahati ya mtende, hana sifa za kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani``, alisema na kuongeza mambo kama haya yamfanye Rais afikirie kuvunja baraza`` [/B]
Pia alikemea tabia iliyoibuka ya baadhi ya mawaziri wanaotoa kauli ama maamuzi yaliyo kinyume cha taratibu na sheria kuishia kuomba radhi bila ya kuchukua hatua ya kujiuzulu nafasi zao.
``Ni aibu waziri kuboronga halafu ngao yake inakuwa kuomba radhi Bungeni, Kikwete avunje baraza la mawaziri, ili mwakani aingie kwenye uchaguzi mkuu na baraza jipya, safi lisilo na watu wenye tuhuma za ufisadi,`` alisema na kuongeza, ``Haya mambo ya kuomba radhi kwa makosa ya wazi kabisa yanaashiria kukata tamaa na kushindwa kazi``, alisema Mrema.
Aliongeza kusema kuwa huu si wakati wa mawaziri komba radhi bungeni, bali wanatakiwa kueleza kwamba wamefanya nini muda wote walipokuwa madarakani.
Naye Mbunge wa Chama cha Wananchi (CUF), Ali Khamis Seif (Mkoani), alisema kilichotokea kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii kuhusu vitalu vya uwindaji na ile ya Mambo ya Ndani kuhusu utengenezaji wa vitambulisho vya taifa, msingi wake ni ufisadi.
Aliwataka mawaziri wanaoboronga waachie ngazi kwa vile sio tu wanawatia hasara Watanzania, lakini wanamdhalilisha Rais aliyewateua.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sengodo Mvungi, yeye alisema hatua ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Maliasili na utalii kuliomba bunge radhi kwa nyakati tofauti kutokana na kutoa maamuzi yenye utata na yenye kukiuka katiba na maamuzi ya bunge, inaashiria kuwa wameingiwa na kiwewe.
Alisema kiwewe hicho kinatokana na ukweli kwamba mawaziri hao ambao ni wasaidizi wakuu wa rais, wamegundua kwamba mambo si shwari katika kutekeleza ilani ya CCM kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu mwakani.
``Wameingiwa na kiwewe na radhi wanazoomba ni geresha, wanajifanya wanyenyekevu kipindi hiki ambapo tunaelekea uchaguzi Mkuu,``alisema.
Dk. Mvungi, alidai kuwa kwa vile mawaziri wengi wameshindwa kutekeleza ahadi za serikali kwa kwa wananchi na hivi sasa wanataka wananchi wawaonee huruma kwa kujifanya wanyenyekevu.
``Huu ni unyenyekevu wa kutaka kuonewa huruma mwakani, huu unyenyekevu wa kuomba radhi umeanza lini? Wanachokifanya wanajenga uadilifu wa bandia wa kutaka waonewe huruma``, alisema.
SOURCE: Nipashe
Last edited: