Kikwete agonga msumari wa mwisho kwa mawaziri............hii inaashiria nini hasa?

Apr 30, 2012
21
7
ASEMA ALIFURAHIA MJADALA MKALI BUNGENI, AJIPANGA KUTEKEKELEZA MAPENDEKEZO................WAKATI akitarajiwa kufanya mabadiliko makubwa katika safu yake ya Baraza la Mawaziri muda wowote kuanza sasa, Rais Jakaya Kikwete amesema amefurahishwa na mjadala mkali ulioibuka bungeni kuhusu kuwajibishwa kwa wasaidizi wake wakuu serikalini.Kwa muda wa wiki mbili sasa, kumekuwa na mjadala mkali juu ya matokeo ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Ripoti tatu za Kamati za Bunge za mwaka 2009/10, ambazo zimependekeza kuwajibishwa kwa baadhi ya watendaji serikalini wakiwamo mawaziri wanane.

Akihutubia katika sherehe ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), zilizofanyika jana kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Rais Kikwete alisema ndiye aliyeagiza Ripoti ya CAG iwe inajadiliwa kwa uwazi bungeni kila mwaka, hivyo yote yaliyoanishwa na kuthibitika wahusika watajibishwa.

“Kuna mambo matatu nataka kuyazungumza kabla ya kumaliza hotuba yangu... Bungeni kulikuwa na mjadala mkali kweli kuhusu Ripoti ya CAG na Ripoti nyingine tatu za Kamati za Bunge. Mimi nilikuwa Marekani, lakini niliporudi yakazungumzwa mambo mengi kweli,” alisema na kuongeza:

“Mara Kikwete ampinga Pinda, mara nimepanda ndege kwenda Dodoma. Mengine yamesemwa ya kweli, mengine yameongezewa na mengine ni ya uongo kabisa. Lakini, mjadala ulikuwa ni mkali kweli bungeni. Wengi wakitaka mawaziri waliotajwa kwenye ripoti hiyo wawajibishwe, ninachowaahidi ni kwamba tumejipanga vizuri kutekeleza mapendekezo ya wabunge na Kamati za Bunge.”

“Sikukasirishwa na wala kufedheheka na mjadala ule, nilifurahia ripoti kujadiliwa kwa uwazi. Tatizo watu wanasahau mapema. Mimi ndiye niliyeamua ripoti hii ya CAG ijadiliwe kwa uwazi bungeni tangu mwaka 2007. Nilifikia uamuzi huo baada ya kuona wapo baadhi ya watu ambao ni mchwa wanaokula fedha za umma.”

“Kwa hiyo mjadala ule ulipokuwa unaendelea bungeni nikaona sasa tunaelekea kufanikiwa katika kujenga nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali.”

Alisema kabla ya utaratibu huo aliouasisi, ripoti ya CAG ilikuwa haisikiki wala haijadiliwi kwa uwazi na kina jambo ambalo liliwafanya baadhi ya watendaji kuendeleza wizi wa fedha za Serikali kwani ripoti hiyo ilikuwa ikiwasilishwa tu bungeni kama ‘Order paper’.

“Hata ripoti hiyo ilipowataja baadhi ya watendaji wa Serikali kuhusika katika matumizi mabaya ya fedha za Serikali, hawakujali waliendelea na matumizi hayohayo,” alisema.

Rais Kikwete alisema ulishajengeka utamaduni kwamba ripoti ya CAG ilipokuwa inatolewa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya wezi wa fedha za umma.

Alimsifu CAG, Ludovick Utouh akisema amekuwa akifanya kazi hiyo kwa ufanisi na kuongeza: “Huyu sasa yuko huru. Katiba inasema wazi huyu akishateuliwa huwezi kumuondoa na wala huwezi kusema kuna chombo cha kumdhibiti. Kama kuna kitu umeona hakijakufurahisha unapaswa kwenda Mahakama Kuu kupinga siyo kusema tumdhibiti, hamuwezi.”

“Mfano, hata akinitaja mimi siwezi kusema nimdhibiti nitabaki na kinyongo cha roho. Ninachotaka sasa ni nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, niliwahi kuwaita mawaziri nikamwambia awaambie matatizo yao kila mmoja, nikawaita makatibu wakuu nikamwambia nao awaambie na Aprili 28, wenyeviti wa halmashauri nikamwambia awaambie.”

“Niliiboresha taasisi hiyo ili iweze kufanya kazi vizuri na uwazi mnaouona hivi sasa wa wabunge kuijadili ripoti ya CAG ni mambo ambayo niliyaanzisha mwenyewe,” alisema Rais Kikwete.

IKULU YAFAFANUA........
Awali Ikulu, kupitia kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ilisema mchakato wa mabadiliko ya mawaziri unaotarajiwa kufanywa ni wa kawaida na utafanyika kwa umakini ili kutenda haki kwa watuhumiwa.

Ikulu imetoa ufafanuzi huo siku moja baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuanza kuwachunguza watendaji wote waliohusika, wakiwamo mawaziri wanaokabiliwa na tuhuma zilizoanikwa kwenye ripoti ya CAG.
Tayari Kamati Kuu (CC) ya CCM imebariki uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete kulisuka upya baraza kama hatua mojawapo katika kutekeleza maazimio ya Bunge kutaka mawaziri na watendaji waliotajwa katika ripoti ya CAG, wawajibishwe.

Mawaziri waliotajwa katika ripoti hiyo ya CAG ni William Ngeleja (Nishati na Madini) Omari Nundu (Uchukuzi), Mustafa Mkulo (Fedha), George Mkuchika (Tamisemi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Dk Cyril Chami (Waziri wa Viwanda na Biashara).

Balozi Sefue alisema licha ya kukabiliwa na tuhuma, lazima maziri husika wachunguzwe ili kujiridhisha kama ni kweli wanahusika.

“Ripoti imetolewa lakini lazima yapimwe ili kama unafanywa uamuzi uwe ni sahihi na kutenda haki,” alisema Balozi Sefue.
 
Back
Top Bottom