Kigogo CCM John Barongo asafishwa kashfa ya ubadhirifu

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Imeandikwa na Jasmin Shamwepu, Dodoma; Tarehe: 1st May 2011

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Dodoma kimepokea ripoti ya Tume iliyoundwa mwishoni mwa mwezi uliopita kuchunguza tuhuma za ubadhirifu wa Sh milioni 373 za mradi wa ujenzi wa hosteli ya chama hicho zilizokuwa zinamkabili Katibu wa CCM wa Mkoa wa Dodoma, Kapteni mstaafu John Barongo.

Fedha hizo zilidaiwa kutumika bila kufuata taratibu za mahesabu huku kiasi cha Sh milioni 50 zikidaiwa kutafunwa na kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Mwenyekiti wa CCM Mkoani Dodoma, William Kusila alisema makadirio halisi ya ujenzi wa jengo hilo ni Sh 182,574,000, tofauti na ilivyotangazwa kwenye vyombo vya habari huku upande wa pili ulioibua malalamiko ukikaririwa kupitia madai ya Katibu Mwenezi wa CCM Mkoani hapa Donald Mejiti kuwa fedha za mradi huo zimetafunwa na kigogo mmoja wa chama hicho mkoani hapa.

Akitangaza matokeo ya Tume hiyo iliyoshirikisha wajumbe watatu, Wales Lusingu, Hydar Gulamali na Anthony Mavunde, Mwenyekiti huyo wa CCM Dodoma alisema Kamati yake imejiridhisha kuwa tuhuma hizo hazina ukweli na kwamba Tume hiyo bila kuacha mashaka imeridhika kuwa thamani ya fedha katika ujenzi wa mradi huo inalingana na matumizi halisi kwa kiwango kilichofikiwa.

“Tume haikupata ushahidi wa kuliwa hata shilingi moja na kazi iliyofanyika hadi sasa ni kubwa ambapo fedha halisi zilizotumika ni shilingi 155.786,147,” alifafanua Kusila.

Aidha alisema pamoja na kazi ya kuchunguza tuhuma za ubadhirifu wa fedha hizo Tume hiyo ilipewa jukumu la kuchunguza tuhuma nyingine za kukodishwa kwa gari kwa ajili ya matumizi ya halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kusafirisha mitihani ambapo Sh milioni 9, zinadaiwa kutumika kinyume cha utaratibu, tuhuma ambazo pia alitupiwa Katibu wa CCM Mkoani hapa.

Kwa mujibu wa Kusila tuhuma zote alizotupiwa Barongo ambaye pia alidaiwa kutumia Sh milioni 4 kwa gharama ya matengenezo ya gari hilo hazina ukweli.

“Ukweli ni kwamba fedha zilizotumika kwa matengenezo ya gari ni shilingi 586,000 na magari yote yaliyohusika kwenye zoezi la kusambaza mitihani hiyo yalifanyiwa matengenezo chini ya Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ambapo jumla ya Sh milioni 4 zilitumika. Hii haimhusu Katibu wetu ni masuala ya Manispaa,” alisema Kusila.

Kusila alizungumza na waandishi wa habari huku Katibu wa CCM mkoani hapa na wajumbe wa Tume ya Uchunguzi wakiwa wameondoka ambapo taarifa yake haikuzungumzia mapendekezo ya Tume na chanzo cha malumbano ya Katibu Mwenezi wa Itikadi na Siasa wa Mkoa wa Dodoma, Donald Mejiti na Katibu wake.

Hata hivyo, taarifa hiyo ambayo gazeti hili imeona nakala yake imeeleza mambo kinyume kabisa na ufafanuzi uliotolewa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dodoma huku kukiwa na maamuzi yaliyofikiwa na Kamati ya Siasa ya mkoa huo.

Alipoulizwa hatua za kinidhamu zitakazochukuliwa dhidi ya Katibu Mwenezi kwa kile kilichoonekana kuwa ni utovu wa nidhamu kwa kupinga maamuzi ya Kamati ya Siasa juu ya tuhuma za ubadhirifu, Kusila alitumia neno moja, “Tutaona,” akimaanisha kikao cha kamati hiyo kilichofanyika Aprili 28, hakikufikia uamuzi wa adhabu.

Akizungumza na waandishi wa habari kueleza matokeo ya uchunguzi huo Katibu Mwenezi, Mejiti aliridhika na matokeo ya ripoti ya Tume hiyo ambayo alisema imefanya kazi nzuri na kuibua ukweli wa madai yake.

Alisema wajumbe wa kamati ya mkoa wamepokea taarifa hiyo na kuipitia kwa undani na hatimaye kukubali kuzingatia ushauri na mapendekezo yaliyotolewa na tume hiyo

Awali alisema tume imebainisha mapungufu 10 ya utekelezaji wa mradi huo ambapo Katibu wa CCM Mkoani hapa ametajwa kuhusika na tuhuma hizo akidaiwa kutoshirikisha kamati ya sekretarieti na kamati ya siasa kikamilifu katika hatua za ujenzi wa mradi wa hosteli hiyo.

“Alichukua madaraka makubwa kutoa idhini ya malipo na mabadiliko ya mradi bila kutumia vikao halali vya juu vya maamuzi huku akiandika barua ya uteuzi wa mshauri bila kikao cha kumpitisha na kuidhinisha malipo yake,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Taarifa hiyo imeonyesha kiasi cha shilingi 47,602.26 zilizoongezeka kwenye mradi kutokana na uamuzi wa kufanya mabadiliko ya michoro ya jengo hilo huku mshauri wa mradi akidaiwa kuchora, kusimia na baadaye kujiidhinishia malipo ya mkandarasi, “jambo linalotia mashaka makubwa,” imetamka ripoti hiyo.

Imebainishwa pia kuwa mkataba wa mradi huo ulitiwa saini bila kushuhudiwa kisheria na kwamba sehemu kubwa ya mambo yaliyoainishwa kwenye mkataba huo yamekiukwa na kusababisha ongezeko la gharama za mradi huo.

Kutokana na taarifa hiyo Tume hiyo imependekeza malipo hayo yasifanyike na kushauri kamati ya siasa kupima juu ya uzito wa suala hilo ikiwezekana kusimamishwa kwa mshauri wa mradi ambaye ni mhandisi wa Mkoa wa Dodoma aliyetajwa jina moja la Mkwata.
 
Back
Top Bottom