Khatma ya Muungano

abdulahsaf

JF-Expert Member
Aug 31, 2010
858
130
[h=1][/h]Posted on April 1, 2012 by zanzibaryetu
Wakili Maarufu wa Zanzibar Awadh Ali Said akitoa mada katika kongamano la katiba lililofanyika leo katika ukumbi wa Bwawani hoteli

Tuanze kwa kueleza kuwa muungano wa chi mbili au zaidi ni suala la mashirikiano ambayo yanategemewa kusukuma mbele maslahi fulani ya nchi wanachama. Kwa ufupi. Muungano wowote ni mashirikiano ya kimaslahi . Jambo la msingi katika mashirikiano yoyote ni maslahi ya pande husika. Endapo mashirikiano fulani yanaleta maslahi mema, hapo mashirikiano hayo huimarishwa lakini endapo mashirikiano husika yanaminya maslahi husika basi mashirikiano hayo inabidi yaangaliwe upya ili kuyafanya yawe na maslahi zaidi. Katika kuangalia suala la maslahi ya kimuungano mambo kadhaa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii huangaliwa na pia muktadha wa nchi husika katika hayo. Kwa mfano tukiangalia muktadha wa kisiasa , kiuchumi na kimashirikiano ya kikanda na kimataifa yanayoikabili Tanzania bara na Zanzibar kwa wakati huu aina ya muungano inabidi uangaliwe upya katika hali hiyo na hivyo tuuangalie aina ya muungano kwa mujibu wa hali halisi ya kisiasa na kiuchumi na matakwa ya wananchi. Baadhi ya aina za muungano, uzuri na kasoro zake:
KATIBA MPYA YA TANZANIA NA HATMA YA MUUNGANO.
(Awadh Ali Said)
Muungano wa Tanzania ambao uliundwa na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika hapo tarehe 26-4-1964 unakaribia kutimiza nusu karne hivi karibuni. Zaidi ya theluthi mbili ya raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamezaliwa baada ya muungano huu kuundwa. Hivyo kwa kigezo cha umri huu ni muungano unaoweza kuingia katika kundi la kuwa umepevuka vya kutosha.
Muungano huu uliundwa na nchi mbili zilizo na tofauti nyingi kuliko mfanano. Hizi ni nchi mbili zilizokua na historia tofauti, ukubwa wa nchi tofauti, idadi ya watu wake ni tofauti sana, uwiao wa dini wa wananchi wa nchi mbili hizi nao ni tofauti,utamaduni tofauti, aina ya uchumi wao ni tofauti,maumbile yao ni tofauti – wakati nchi moja ni bara (na baadhi ya visiwa) nyengine ni visiwa tu, pia nchi hizi zilikua na tofauti za kisiasa na kijamii. Kwa hivyo ukiwacha ukaribu wa kimasafa na lugha uliopelekea muingiliano kiasi wa watu wa pande mbili hizo, takriban kwa kiwango kikubwa sana mataifa mawili haya yalikua na misingi tofauti.
Tofauti nyengine ni kuwa wakati wa kuundwa kwa Muungano, Tanganyika ilikua imeshapata uhuru wake kwa njia za amani kwa takriban miaka miwili na nusu na ilikua na utawala madhubuti, taasisi imara za uendeshaji na ilikuwa na Katiba kamili ya Jamhuri (ya 1962) baada ya kurekebisha Katiba ya mwanzo ya Uhuru (ya 1961) ,na ilikuwa na amani na utulivu wa kutosha pamoja na uzoefu wa kiutawala. Kwa upande mwengine Zanzibar iliingia katika Muungano ikiwa ni siku takriban 100 tu tokea ilipofanya Mapinduzi ya umwagaji damu hapo tarehe 12-1-1964 ambayo yaliipindua serikali iliyokabidhiwa uhuru ambayo ilidumu kwa siku 30 tu. Hivyo Zanzibar bado ilikua katika fukuto la mapinduzi, haikua katika utulivu na wakatu huo haikua hata na katiba baada ya kuifuta kwa Mapinduzi katiba ya uhuru ya 1963.
Wachambuzi wa mambo ya kisiasa na kihistoria wametofautiana sana juu ya sababu au chanzo kilicho pelekea kuundwa kwa muungano huu. Wapo wanaodai kuwa muungano huu ni matokeo ya ukaribu katika kila nyanja ya maisha ya mataifa haya. Wapo wanaounasibisha na shauku ya mataifa makubwa wakati huo wa vita baridi (Cold War period) kuyaweka mataifa katika himaya zao. Wengine wanadai ni matokeo ya jitihada za kusukuma mbele dhana ya umoja wa kiafrika (Pan-Africanism) .Wapo wanaodai kuwa muungano huu ni mradi binafsi uliokua na lengo la kuimeza Zanzibar na kuifuta katika ramani ya dunia.
Vyovyote iwavyo juu ya chanzo na sababu, lakini mambo mawili yanajidhihirisha kuwa ama yalizaa au yalisukuma mbele fikra za viongozi wakuu wa mataifa haya kwa wakati huo ya kuungana. Kwa upande wa uongozi wa zanzibar waliona kuwepo kwa muungano kungewasaidia kuimarisha utawala wao ambao ndio kwanza umetoka katika kukamata madaraka kwa njia ya mapinduzi na hivyo muungano ungesaidia kuyapa mapinduzi na utawala huo hifadhi na kinga dhidi ya jaribio la wapinga mapinduzi. Kwa upande wa uongozi wa Tanganyika , hasa Rais J.K. Nyerere aliona hiyo itakua njia sahihi ya kuweza kuidhibiti Zanzibar kutokana na hofu yake iliyojikita katika ukweli uliomo katika dhana inayosema “You pipe in Zanzibar, they dance in the lakes” –historia ni shahidi mzuri wa dhana hii. Kuingia kwa dini, ukoloni, matukio makubwa kama biashara ya utumwa na vuguvugu la uhuru yanaaminiwa kuanzia Zanzibar na kuelekea bara. Hata yalipotokea mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 katika mwenzi huohuo moto wa Mapinduzi ulisambaa Tanganyika, Uganda na Kenya ambako kote kulitokea majaribio ya mapinduzi ingawaje yalizimwa na waliokuwa wakoloni wa mataifa hayo. Hata kwa historia ya karibuni inaaminika mageuzi makubwa ya kiuchumi na kisiasa yanayoendelea yana asili yake Zanzibar (angalia vuguvugu la siasa za vyama vingi, mapambano ya kutanua Demokrasia, ubinafsishaji wa uchumi, utalii n.k). Ukweli huu ndio uliomfanya Rais J.K Nyerere atamke wazi kuwa haridhishwi kuviona visiwa vya Zanzibar vikiwa karibu naye na kama angekuwa na uwezo angevitokomeza mbali katikati ya Bahari ya Hindi.
‘ If I could tow that island out into the middle of the Indian Ocean, I would do it”
“No I am not joking….. I fear it will be a big headache for us” (Both quoted in Zanzibar and the Union Question pg 34)
Na kwa vile hilo haliwezekani, njia iliobaki ni kuvidhibiti au kuvimeza kabisa. Na ndio maana wapo wanaoamini kuwa agenda ya umezaji huo imefanifiwa lakini Zanzibar iliyomezwa imekataa kutulia ndani ya tumbo la chatu:
• “Dr Julius Nyerere, President of Tanganyika,managed half the work of a phython: he swallowed Zanzibar all right. But he did not crush its fighting force first. The live animal is a long time digesting, and its kicks are being felt hurtfully, and possibly even fattaly, deep inside Tanganyikas body politic” – (The Economist (London) Of June 13 , 1964 – Quoted in an Article by Mahadhi Juma Maalim titled The Union between Tanganyika and Zanzibar and the right of Secession under International Law)
Hivyo mbali na sababu za nje, ambazo zina ukweli mkubwa, lakini Muungano ulitoa fursa ya kila mmoja kupata stara yake kwa mujibu wa hali yake kwa wakati huo.
Leo hii muungano huu ukiwa unatimiza nusu karne tukigeuka na kuuangalia ulikoanzia tunashuhudia kuwa ni muungano uliojijengea sifa/ haiba (landmarks) kuu tatu zikiwa ni:
(1) utata mkubwa wa kisheria
(2) kiini macho katika muundo wake
(3) kukithiri kwa kero.
Katika makala hii tutajaribu, japo kwa ufupi, kuangalia mambo matatu hayo na mwishoni kudodosa haja ya kuangaliwa upya suala la muungano katika mchakato wa uundaji katiba mpya Tanzania na katika muktadha wa sasa wa kisiasa.
UTATA MKUBWA WA KISHERIA UNAOUANDAMA MUUNGANO.
Muungano huu uliundwa kwa kusainiwa Mkataba wa Muungano na Marais wawili wa Jamhuri zilizoungana yaani Rais J.K Nyerere wa Tanganyika na Rais Abeid Amani Karume wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibari. Mkataba wa Muungano ulitayarishwa na wanasheria wa Tanganyika katika usiri mkubwa na katika zoezi lote hadi kusainiwa kwake viongozi waandamizi wote wa Zanzibar hawakushirikishwa, hata Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar hakushirikishwa kabisa.
Kwa mujibu wa mfumo wa sheria uliokua/unaofuatwa na mataifa haya viongozi wakuu wa kitaifa wana uwezo wa kisheria wa kuingia katika Mikataba ya Kimataifa (International Treaty) Hata hivyo mfumo huo wa kisheria ulitaka mara baada ya kusainiwa na viongozi wakuu husika, mkataba huo ni lazima uridhiwe na bunge la nchi husika na pia upitishiwe sheria (Domestic law) ya ndani ili uwe na nguvu za kisheria. Kwa kutambua mfumo huo wa kisheria, hata mkataba wenyewe wa muungano (kifungu viii) uliweka suala la kuridhia (Ratification) kuwa ni sharti moja la awali la mkataba huo (condition precedent). Wakati Tanganyika iliridhia Mkataba huo na kutunga sheria rasmi ili kuupa nguvu na uhalali mkataba wa muungano (Act No.22/1964) Zanzibar hadi leo hii haikuridhia Mkataba Wa Muunagno (Angalia maandishi mbalimbali ya A. Jumbe, W. Dourado , I .Shivji nk )

Utata au kasoro hii ya kisheria inayaweka mambo katika sokomoko hasa kwa vile hakuna rekodi yoyote ya kuwepo kwa mkataba halisi wa muungano. Hata walipotokezea wananchi waliodai kuomba mahkamani kupatiwa nakala ya mkataba halisi wa muungano uliosainiwa na viongozi wakuu wa wakati huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alikiri kutokuwanao (Angalia kesi No 20 ya 2005 Mahkama Kuu Ya Zanzibar:Rashid Salim Adi na wenzake Dhidi ya Mwanasheria Mkuu Wa Zanzibar ). Hivyo, kutokuwepo kwa mkataba halisi, na badala yake kuwepo sheria iliyoridhia mkataba ya Tanganyika tu (Sheria No 22/1964 ) na humo kuwekwa kiambatanisho cha kinachodaiwa kuwa ndio mkataba ulioridhiwa – na ndio hadi leo hii kinachotumika kama ndio mkataba wa muungano unaleta maswali mengi yasiyo majibu.
Wanaotilia shaka kiambatanisho hicho hawawezi kunyamazishwa; wanaoeneza habari kuwa mkataba ulikua ni wa miaka 10 tu hakuna cha kuwatengua kwenye msimamo huo.
Pamoja na kuwa kasoro/utata huo unaweza usiwe na msukumo wa kuvuruga muungano kwa vile mahkama zitatumia silaha zote kuuokoa (Kama alivyodai Prof. Shivji – A court would use a number of legal stratagems in its arsenal- doctrines of necessity, acquiescence, defacto existence etc- to uphold the actually existing reality”) lakini bado ni athari ya msingi inayouandama muungano takriban miaka 50 baada ya kuundwa kwake na kuweza kutikisa uhalali wake kisheria.
KIINIMACHO CHA MUUNDO WA MUUNGANO.
Muungano huu wa mataifa mawili, yaliyo na serikali mbili yaliungana na baada ya muungano yakabaki na serikali mbili. Huu ni muundo ambao haufanani na miundo ya miungano duniani na wachambuzi wote huishia kuuita kuwa ni “muundo wa kipekee”. Msingi mkubwa wa muungano huu ni kile kilichojulikana kama “MAMBO YA MUUNGANO “ . Mkataba wa Muungano uliyaainisha mambo 11 na yakabatizwa jina kuwa ndiyo “Mambo Ya Muungano” Akili ya kawaida ilitegemea mambo haya ya muungano kutoka pande zote mbili yawekwe katika mamlaka moja ya pamoja/shirika na baadae kila mmoja abaki na yake ( na huu ndio msimamo alioushikilia na kuusisitiza na baadae uliomponza kisiasa Mh. Aboud Jumbe kama anavyofafanua bayana katika kitabu chake The Partner-ship Tanganyika Zanzibar Union 30 Turbulent Years , Angalia pia Prof. Srivastava B. P. The Constitution of the United Republic of Tanzania- some salient features some riddles) Lakini kilichofanyika ni kuwa baada ya ubatizo huo mambo hayo 11 yaliondolewa katika mamlaka ya Zanzibar na kuingizwa katika serikali ya Tanganyika ambapo nayo baadae ilibadilishwa jina na kuitwa Serikali Ya Jamhuri Ya Muungano Wa Tanganyika na Zanzibar na baadae, kama ni kwa mkakati na malengo maalum au venginevo majina ya Tanganyika na Zanzibar, ambao ni washirika wa asili na ambao walistahiki kuenziwa yaliondoshwa na kuwekwa jina jipya la Tanzania- jambo ambalo halikua ni sehemu ya makubaliano ya muungano.
Baada ya muundo huo na mambo hayo ya muungano kilichoendelea ni “kuimarisha” muungano kwa kumega mambo yasiyo ya muungano ya Zanzibar na kuyafanya ya muungano ( Yalianza 11 sasa yako 22- wengine wanadai ni 42 endapo utayachambua) na pengine siku ya kumaliza jambo la mwisho la Zanzibar lisilo la muungano na kulifanya la muungano hapo mradi wa “uimarishaji” wa muungano utakua umefikia kilele chake.
Swali la msingi ambalo wengi wamekuwa wakijiuliza ni uhalali wa kikatiba wa ongezeko hili la mambo ya muungano. Mambo yafuatayo yanastahiki kuangaliwa ili kuona uhalali au vinginevyo wa utaratibu wa maongezeko hayo.
La kwanza ni kuwa Zanzibar, tokea ilipoungana na Tanganyika ilipoteza uwezo wa kuingia mikataba ya kimataifa (SOVEREIGNITY) , na ndio maana ilibanwa kujitoa OIC kwa vile haina mamlaka hayo ( Pia inashindwa hata kujiunga FIFA ) na ikaambiwa kufanya hivyo ni kuvunja katiba na walioitoa Zanzibar katika OIC sio OIC wenyewe au wanachama wake bali ni shindikizo la Serikali ya Tanzania.
Sasa kama Zanzibar ilipoteza uwezo huo, kwa vile katika mfumo wa kimataifa ni kuwa haipo na haitambuliki, inapata wapi uwezo, nguvu na uhalali wa ku “surrender” mambo yake yasiyo ya muungano na kuyaingiza katika kapu la muungano. Huku ni kuwa na sura mbili ( double standard) kufanya Makubaliano na nchi nyenginezo haina uwezo, lakini kuyamega mambo yake na kuyatia katika muungano ina uwezo!! Ukweli ni kwamba haiwezekani kuwa na sura mbili- ama inawezekana kuingia mikataba ya kimataifa au haiwezekani, na kama haiwezekani (msimamo unaoonekana kuwa na nguvu) basi ndio madai kuwa mambo ya ziada ( baada ya yale 11 ya asili) hayana uhalali na wengine husema yameingizwa “kinyemela.”
La pili, ni kuwa hata kama Zanzibar ina uwezo wa kuingia mikataba ya kimataifa katika haya yaliyoongezwa ameingia mkataba na Taifa lipi kwa vile mshirika wake wa asili katika muungano huu alishajificha, ingawaje yupo na huyo aliezaliwa ni sehemu ya nafsi yake- Jee mtu anaweza kujiuzia mali yake yeye mwenyewe?
La tatu, ambalo hili ni kiinimacho cha dhahiri ni juu ya utaratibu unaotumika katika kuongeza mambo ya muungano. Ieleweke kuwa kwa Katiba zote mbili, ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mgawanyo wa madaraka katika utungaji sheria kwa Bunge la Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania na Baraza La Wawakilishi uko wazi. Tuziangalie katiba 2 juu ya mamlaka ya utungaji sheria kuhusu mambo ya pande mbili za muungano:
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 kifungu 64(2) kinaeleza:
“Mamlaka yote ya kutunga sheria katika Tanzania Zanzibar juu ya mambo yote yasiyo ya muungano yatakuwa mikononi mwa Baraza la Wawakilishi.”
Na Kifungu 64 (3) kinaeleza :
“ Endapo sheria yoyote iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi inahusu jambo lolote katika Tanzania Zanzibar ambalo liko chini ya mamlaka ya Bunge, sheria hiyo itakuwa batili na itatanguka na pia endapo sheria yoyote iliyotungwa na Bunge inahusu jambo lolote ambalo liko chini ya mamlaka ya Baraza La Wawakilishi, sheria hiyo itakuwa batili na itatanguka”
Katiba ya Zanzibar, 1984 kifungu 132 (1)
“ Hakuna sheria yoyote itakayopitishwa na bunge la muungano ambayo itatumika Zanzibar mpaka sheria hiyo iwe ni kwa ajili ya mambo ya muungano tu ……”
Hivyo ni wazi kwa mujibu wa katiba hizi mbili mamlaka ya kutunga sheria ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni juu ya mambo ya muungano tu LAKINI mambo yasiyokuwa ya muungano Bunge haliwezi kuyatungia sheria, INGAWAJE, tena kwa mshangao mkubwa bunge ambalo halina uwezo wa kulitungia sheria jambo lisilo la muungano LIMEJIPA uwezo wa kulifanya jambo lisilo la muungano kuwa la muungano!!
La mwisho la kuangalia katika kiinimacho hiki ni kuwa unaposoma vifungu vya 94 na 68 vya katiba ya Jamhuri ya muungano ya Tanzania ni kuwa bunge la JMTZ limepewa uwezo wa kuchukua kwa upande mmoja tu ( unillaterally ) mambo yote ya Zanzibar yasiyo ya muungano na kuyafanya ya muungano na hivyo huweza kupelekea kutoweka kwa Zanzibar moja kwa moja.

KERO ZA MUUNGANO
“One wave never settles down before another starts” Mahadhi pg 157.
Katika uhai wake wa takriban miaka 50 muungano wa Tanganyika na Zanzibar, neno muungano na kero yamekuwa kama maneno pacha, tena pacha mfanano . Tume kadhaa wa kadhaa zimeundwa kuangalia kero hizi na pengine unaweza kuwa ni Muungano unaoongoza kwa kuundiwa Tume. Ni wazi kuwa Muundo wenyewe wa Muungano ndio kiwanda cha kuzalisha Kero na kwa vile kiwanda kipo bidhaa zitaendelea kuzalishwa. Prof Yash Ghai ameeleza kiusahihi aliposema:
“In the circumstances, the surprise is not that the union has run into difficulties, but that it has survived at all” Quoted in Second Expanded Edition of the Legal Foundations of The Union by Prof Shivji.
MCHAKATO WA KATIBA NA SUALA LA MUUNGANO
Tanzania imeshaamua kuandika upya katiba yake. Mchakato huu umeanza kwa kupitishwa sheria no 8/2011. Tayari mwanzo mbaya (false-start) imeonekana katika mchakato unaoundwa na sheria hiyo.
Kasoro kubwa ya sheria hii ni kuwa HAITOI FURSA YA WAZI kwa wananchi kuujadili muungano – na ukweli ni kuwa muungano ni nguzo kuu ya katiba yenyewe. Hasa hasa kwa upande wa Zanzibar, ambako wananchi wa Zanzibar uhusiano wao juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kupitia muungano. Yote yaliyo nje ya mambo ya muungano, upande wa Zanzibar hawana haki nayo kama ambavyo watanzania bara hawana haki na mambo ya Zanzibar (yasiyokuwa ya muungano). Ukisoma vifungu vya 8, 9 na 17 vya sheria hiyo ambavyo vimeainisha hadidu rejea (terms of reference) au mipaka (na kuna umuhimu wa kuwekea wananchi mipaka kuhusiana na mjadala wa Katiba yao?) ya kazi za tume ya katiba hamna hadidu rejea yoyote inayaotaja kuangalia suala la muungano . Na baya zaidi vifungu vya 9(1) (C) na 17(1) na 17(2)(d) vimeielekeza tume kutayarisha na kuwasilisha ripoti kwa “kuzingatia hadidu za rejea” – hivyo ni kuwa HATA kama wananchi watazungumza sana juu ya suala la muungano lakini kwa mujibu wa sheria hii tume haitoandika chochote kuhusu mambo haya ya muungano. (tujikumbushe mkwaruzano uliotokea juu ya ripoti ya Jaji Kisanga iliposhambuliwa kwa kutoka nje ya hadidu rejea ilipozungumzia suala la muundo wa muungano)
Tukizingatia ukweli wa kuwa wananchi wa nchi mbili hizi hawajawahi kupata fursa ya kutoa maoni yao juu ya suala la muungano ilitegemewa muungano uwe ndio hoja kuu ya mjadala wa katiba na kuacha kabisa kuendeleza utamaduni wa muda mrefu wa kulitenga suala la muungano na wananchi wenyewe – kulifanya halifikiki, halijadiliki wala haligusiki.
Ukweli ni kuwa sio tu kuwa suala la muungano liwe ni msingi katika mjadala wa katiba lakini suala la muungano lilistahiki kuamuliwa mwanzo na ndiyo baadae lije suala la katiba. Muungano ndio uliozaa katiba tulizonazo, katiba zote mbili (ya Zanzibar 1984 na ya Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania 1977) ni matokeo ya muundo wa muungano uliokubaliwa. Muundo ambao uliunda mamlaka tatu (three Jurisdictions): ya Tanganyika, ya Zanzibar, na ya Muungano na baada ya hapo mamlaka mbili za Tanganyika na ya Muungano zikachanganywa (fused) na kuwa chini ya serikali moja na mamlaka ya Zanzibar kuwa chini ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hivyo pakawa na Serikali mbili na katiba mbili.
Na huu ndio msingi unaowafanya wengi ( Aboud Jumbe, 1994 & Dourado, 1999 nk) wakasisitiza kuwa mkataba wa muungano ulikusudia mamlaka 3 na serikali 3 na ule utaratibu wa mamlaka 3 chini ya serikali 2 na hivyo katiba mbili ulikuwa ni wa muda wa mwaka mmoja tu mpaka utapoundwa mfumo wa katiba mpya ndani ya mwaka mmoja kuanzia siku uliposainiwa mkataba wa muungano. Mkataba wa Muungano unataja kipindi hicho kuwa ni “interim period” – Angalia kifungu (iii) cha Mkataba wa Muungano:

“During the interim period the Constitution of United Republic shall be the constitution of Tanganyika so modified as to provide for :”
Mkataba ulielekeza kuundwa kwa tume ya katiba( kifungu vii) ambayo ingeundwa kwa makubaliano kamili ya Marais wawili wa nchi zilizoungana. La kushangaza ni kuwa hilo lilikwepwa kabisa, tena kwa amri ya upande mmoja tu (Tanganyika) ulipoamua kivyake-vyake tu (uniletarally) kupitisha sheria ( Act no 18 of 1965). na kuliakhirisha hilo kwa muda usiojulikana mpaka hapo lilipoibuka tena miaka 14 baadae kwa kuunda katiba ya 1977 wakati huo ikiwa ni sawa na kuvuta shuka wakati kumeshakucha kwani mkataba wenyewe ulishajeruhiwa vya kutosha. Sheria hii ndio iliyovuruga kabisa Mkataba wa Muungano na ikafungua milango kwa upande mmoja wa Muungano kuamua watakalo . Wakati mkataba wa muungano uliosainiwa kwa pamoja ulisema Tume ya Katiba ingeundwa na Marais wawili hao ‘ KWA MAKUBALIANO YA PAMOJA” sheria hii iliyopitishwa na Bunge la Tanganyika na kusainiwa na J.K. Nyerere ilisema;
“This Act may be cited as the Constituent Assembly Act 1965 and shall be read as one with the Acts of Union of Tanganyika and Zanzibar”
“Notwithstanding the provisions of the Acts of Union of Tanganyika and Zanzibar or the Articles of Union between the former Republic of Tanganyika and the former Peoples Republic of Zanzibar , the President of the United Republic shall not be required to appoint a Commission to make proposal for a Constitution for the United Republic … within one year … but shall appoint such Commission and sommon such Constituent Assembly at such times as shall be opportune”
Hivyo uandikaji wa katiba mpya Tanzania bila ya kwanza kuliangalia na kuliamua suala la muungano kwa mujibu wa ridhaa na matakwa ya wananchi wa pande mbili za muungano ni sawa na kufanya mambo kinyume-mbele.
Mchakato huu unaanza , kwa mujibu wa sheria iliyotungwa , ikiwa kama kwamba uamuzi umeshafanywa kuwa muungano utabaki na muundo wa serikali mbili kama ulivyo, hili si sahihi, na ni kupandikiza uamuzi kwa wananchi, ni kinyume na kanuni zote za demokrasia na ni kinyume na Haki Za Kitaifa na za kizalendo za wananchi husika . Tujiulize endapo wananchi wataamua, katika maoni yao, kuwa hawataki muungano – ni vipi bunge la katiba litakuwa na wajumbe kutoka Zanzibar ; au wakiamua wanataka muungano wa serikali 3 ni vipi iandikwe katiba moja!!! – lakini zaidi ya yote hata maoni hayo hayatofanyiwa kazi kwani si sehemu ya hadidu rejea na hivyo hayatakua sehemu ya ripoti ya Tume wala sehemu ya rasimu ya katiba.
Katika uandikaji wa katiba mpya ya Tanzania, busara, uhalisia na ukweli wa mambo unataka kwanza liamuliwe suala la muungano, na baadae lifuate la katiba. Ikiamuliwa wananchi wanataka muungano wa serikali moja, tutakuwa na katiba moja. Ikiamuliwa wananchi wanataka muungano au serikali mbili ( katika muundo wa sasa) tutabaki na katiba mbili, ikiamuliwa wananchi wanataka muungano wa serikali tatu , tutakuwa na katiba 3, wakiamua hawataki kabisa muungano , tutarudi tulivyokuwa kabla ya muungano na kila nchi na katiba yake na mambo yake, wakiamua wanataka mashirikiano ya aina ya makubaliano ya kimkataba ( Treaty) watakuwa na katiba zao na Mkataba Wa Ushirikiano – hivyo akili ya kawaida ingetuelekeza kwanza tupate uamuzi juu ya muungano na muundo wake baadae zije katiba.
Kasoro nyengine ni kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inajumuisha mambo 2 – mambo ya Tanganyika na mambo ya muungano, ambayo haya ni ya ushirika baina ya Zanzibar na Tanganyika. Hivyo haki ya Wazanzibari ni kujadili na kuamua juu ya yale ya ushirika tu – ni kinyume kuwashirikisha Wazanzibari kuamua mambo ya Tanzania Bara. Ni sawa na uingiliaji wa mambo ya ndani ya nchi nyengine. Na hili limekuwa ni moja ya tatizo sugu la muda wote kuwa hata katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wabunge wa Zanzibar wanashiriki katika mijadala na maamuzi juu ya mambo ya Tanganyika , yasiyo ya muungano na hivyo kuingilia yasiyowahusu. Baya zaidi sasa kwa mchakato huu tunataka kuhamisha kero sugu hii iwe ndio msingi wa uundaji katiba mpya. Hii itakuwa ni sawa na watu wa nchi nyengine kuifanyia maamuzi juu ya mfumo wa kikatiba na utawala nchi nyengine. Mfumo huu umeondoka katika medani za sasa za kisiasa na kiutawala duniani. Hatari zaidi ni kuwa katiba haitopita ila iungwe mkono na zaidi ya nusu ya wananchi wa pande mbili tofauti – yaani ikubaliwe na zaidi ya nusu ya wazanzibari na ikubaliwe na zaidi ya nusu ya watanzania bara . Tujaalie wazanzibari , kwa hisia za mapenzi ya kidini tu , wakaikataa katiba kwa sababu haikuingiza Mahkama za Kadhi kwa Tanzania Bara – jambo ambalo sio la muungano na wao Wazanzibari wanazo zao, na hili ni suala nyeti kwa siasa za Tanzania bara – jee nini matokeo ya mchanganyiko huu ??
Pia sheria hii imeanza kutekelezwa bila kuzingatia matakwa ya Katiba ya Zanzibar kifungu 132(1)(2) ambacho kinasema hakuna sheria yoyote itakayopitishwa na Bunge la la Muungano ambayo itatumika Zanzibar “ ila sheria kama hiyo lazima ipelekwe mbele ya Baraza la Wawakilishi na Waziri anayehusika”. Tayari sheria hii imeanza kutumika na mapendekezo ya wajumbe wa tume yamepelekwa kwa mamlaka ya uteuzi bila mazingatio ya katiba ya Zanzibar kwa vile haijapelekwa Baraza La Wawakilishi .
KATIBA MPYA NA MUUNDO WA MUUNGANO.
Tuanze kwa kueleza kuwa muungano wa chi mbili au zaidi ni suala la mashirikiano ambayo yanategemewa kusukuma mbele maslahi fulani ya nchi wanachama. Kwa ufupi. Muungano wowote ni mashirikiano ya kimaslahi . Jambo la msingi katika mashirikiano yoyote ni maslahi ya pande husika. Endapo mashirikiano fulani yanaleta maslahi mema, hapo mashirikiano hayo huimarishwa lakini endapo mashirikiano husika yanaminya maslahi husika basi mashirikiano hayo inabidi yaangaliwe upya ili kuyafanya yawe na maslahi zaidi. Katika kuangalia suala la maslahi ya kimuungano mambo kadhaa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii huangaliwa na pia muktadha wa nchi husika katika hayo. Kwa mfano tukiangalia muktadha wa kisiasa , kiuchumi na kimashirikiano ya kikanda na kimataifa yanayoikabili Tanzania bara na Zanzibar kwa wakati huu aina ya muungano inabidi uangaliwe upya katika hali hiyo na hivyo tuuangalie aina ya muungano kwa mujibu wa hali halisi ya kisiasa na kiuchumi na matakwa ya wananchi. Baadhi ya aina za muungano, uzuri na kasoro zake:
MUUNGANO WA SERIKALI MOJA
Hii ni aina ya Muungano ambayo mataifa ya asili yanayoungana yanapotea kabisa na kutandaza mfumo mmoja wa kiserikali na nchi. Si aina ya Muungano unaopendelewa sana hasa kwa nchi zilizo na tofauti kubwa kama Zanzibar na Tanganyika. Kwa upande wa Zanzibar huu haujawahi kuwa muundo ambao uliwahi kupita katika fikra za Viongozi waliounda Muungano na hata wananchi walio wengi.
MUUNGANO WA SERIKALI MBILI
Muundo wa serikali mbili uliopo hivi sasa umekuwa ndio chanzo cha migogoro karibu yote ya muungano huu. Watanzania wote ni mashahidi wa jinsi muundo huu ulivyoshindwa kuweka utulivu na maridhiano katika mahusiano ya muungano . Zaidi ya yote umeshapitwa na wakati na hauwezi kuhimili mageuzi ya kikanda na kimataifa yanayotokea. Mbali na kero kadhaa za humuhumu ndani lakini tuchukulie mfano mdogo wa kuwepo kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na ushiriki wa Tanzania. Zanzibar haimo kama mwanachama katika Jumuiya hii bali iliyomo ni Tanzania . Kati ya mambo 18 yanayoshughulikiwa na Jumuiya hii ni 4 tu ambayo ni ya muungano na ambayo Tanzania ina mamlaka ya kisheria kuiwakilisha Zanzibar. Kwa yaliyobakia Tanzania kuiwakilisha Zanzibar ni kwenda kinyume na Katiba . Hata suala la Zanzibar kujiunga na OIC lilikwamishwa kutokana na mfumo wa muundo huu na Tanzania ikadai ingejiunga kwa vile ndio yenye mamlaka . Takriban inakaribia miaka 20 tokea kutolewa kwa ahadi hio lakini umma haujaelezwa maombi yalikwama wapi. Hata hivyo hili la OIC ni utashi wa kisiasa au kidini tu ndio uliokwamisha; lakini muundo wa Muungano huu unasutwa hata na maumbile ya mataifa haya yaliyoungana. Kwa mfano upo umoja wa visiwa vya Bahari ya Hindi ambao Zanzibar kama kisiwa wanastahiki kujiunga lakini haina mamlaka na hio Tanzania yenye mamlaka haiwezi kujiunga kwa vile sio kisiwa -hii imepelekea Zanzibar kukosa haki zake mbali mbali.
MUUNGANO WA SERIKALI TATU.
Huu ni aina ya Muungano wa Shirikisho. Nchi zilizoungana hubaki na serikali zao na serikali ya Shirikisho hubaki na yale mambo ya Muungano tu. Wapendekezaji wa muundo huu wanaeleza kuwepo na Serikali ya Tanganyika, ya Zanzibar na ya Muungano. Hapa zitakuwepo nchi mbili, mamlaka tatu na serikali tatu. Kwa kuangalia uendeshaji wa mambo ya ndani ya nchi ,huu unaweza kuwa muundo unaoweza kuondoa kidogo mtafaruku uliopo ; lakini ukiangalia uwakilishi wa nchi hizi na serikali zao katika mambo ya nje muundo huu nao umeshapitwa na wakati. Tujiulize kwa mfano , kwa kuangalia mfano ule ule wa karibu wa Jumuiya Ya Afrika Mashariki , ni ipi kati ya serikali hizi 3 itajiunga na EAC? Kama ni serikali hizi 2 za Zanzibar na Tanganyika suali linakuja jee ni nani atawakilisha kuhusiana na masuala yaliyo chini ya serikali ya Muungano/Shirikisho ambayo serikali mbili hizi hawatakuwa na mamlaka nayo. Na vivyo hivyo endapo itayojiunga ni Serikali ya Muungano nayo itawakilishaje kuhusiana na yale mambo yaliyo chini ya Serikali ya Zanzibar na Tanganyika ambayo haina mamlaka nayo. Huu ni muundo ambao umeshapitwa na wakati.
MUUNGANO WA MKATABA
Huu ni muungano ambao kila nchi inabaki na serikali yake, na uendeshaji wa mambo yake , utaifa wake nk na huingia katika mashirikiano kwa njia ya Mkataba (Treaty) juu ya mambo na kwa utaratibu wanaokubaliana hizo pande mbili au zaidi zinazoungana. Mifano ya miungano ya aina hii ni kama EAC ( Kenya , Uganda , Tanzania Rwanda na Burundi) na EU( ulio na nchi 27). Uzuri wa muundo huu ni kuwa unatoa fursa kwa nchi zilizoungana kuweza kuuagalia kila inapobidi ule mkataba wao bila vikwazo vya Kikatiba na hivyo kusukuma mbele maslahi yao bila kumezana , kubebana au kuoneana.
[h=3][/h]
 
Back
Top Bottom