Kesi ya Abdallah Zombe: Mashitaka, hatia, hukumu na yanayojiri

Hili ni jeshi la polisi au jeshi la manyang'au. Mheshimiwa Masha, safisha hilo jeshi la majambazi.

Kuna jamaa aliniambia mauaji ya namna hii yako mengi tu na huko nyuma raia wengi walikuwa wanauawa kwa njia kama hizi na mapolisi fisadi.

Huyo Zombe sio tu afungwe lakini wataifishe hata mali zake zote.

Pia inaelekea jeshi letu la polisi halina maadili kabisa. Mkuu anakuambia kaue na unaenda kweli kuua, kwanini? Je hakuna sehemu kwa kwenda kutoa siri kimya kimya na kuokoa maisha ya raia wema?
Hawa wamekuwa wakigawana mapato dhalimu hivyo hakuna ambaye angeripoti mwenzie.
Amini usiamini wameuawa wengi tu ka njia hii. Na hasa kwa kisingizio cha ujambazi.
 
..Zombe ni muuaji mkubwa yule na kitanzi ni halali yake kaua wengi sana!
 
Huyu kamanda wa Tabora alikuwa mpelelezi hakuwa kwenye timu ya Zombe.

Mwandishi kachanganya mambo!
 
Kesi ya afande Zombe yahamia msituni Dar

Mmoja wa wapelelezi katika kesi ya mauaji ya watu wanne inayomkabili aliyekuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi, Abdallah Zombe na wenzake 12, jumanne aliionyesha mahakama eneo la msitu wa Pande ambalo linadaiwa kuwa mauaji hayo yalifanyika.

Wakati msafara wa Mahakama Kuu ukienda kwenye msitu huo pamoja na maeneo mengine yanayohusiana na kesi hiyo, uligeuka kuwa kivutio kwa baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam waliojitokeza barabarani kuushangaa huku wakiushangilia na wengine kuuzomea.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Alexander Mzikila, mpelelezi huyo ambaye ni shahidi wa 30 katika kesi hiyo upande wa mashtaka Edson Mmari, alionyesha pia namna watu hao wanne walivyouawa kwa kutolewa mmoja mmoja kwenye gari na kupigwa risasi wakiwa kifudifudi, kwa mujibu wa maelezo ya mshtakiwa wa 11, Rashid Lema.

Aliutoa ushahidi huo mbele ya Jaji Kiongozi Salum Massati wa Mahakama Kuu ya Kanda ya Dar es Salaam, ambako pia alionyesha eneo lililokuwa na damu na maganda ya risasi. Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya watu wakiwa na huzuni baada ya msafara huo kufika katika msitu huo ambao hauna makazi ya watu na barabara yake nyembamba kuonekana kutotumika kwa muda mrefu.

Wakati msafara huo unaondoka katika msitu huo, gazeti hili lilimsikia Zombe akijiapiza na kudai kuwa halifahamu kamwe eneo hilo labda vijana wake. “Walahi silifahamu eneo hili labda vijana wangu,” alitamka Zombe ambaye alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa.

Pamoja na eneo hilo, Mmari pia aliionyesha mahakama hiyo eneo la Ukuta wa Posta Sinza ambalo linadaiwa kutokea mapigano kati ya polisi na majambazi ambako aliionyesha matundu ya risasi pamoja na nyumba za majirani, waliohojiwa na timu ya upelelezi na kukanusha kusikia milio ya risasi.

Hata hivyo, baada ya shahidi huyo kudai kuwa kwa kutumia uzoefu wake matundu ya risasi hizo yangepasua ukuta huo zaidi kutokana na umbali uliopo katika eneo hilo, Zombe ambaye ni mshitakiwa wa kwanza, aliiomba mahakama hiyo itafute askari wa operesheni maalumu wapige risasi ukuta huo ili matundu yake yalinganishwe.

“Mimi ni askari, eneo ambalo bunduki ikipiga tutajua hii ni risasi au la, ningeomba wachukuliwe askari wa 999 ili wapige risasi tuone matundu yake yalivyo,” alidai. Hata hivyo, Jaji Masati alipinga ombi hilo na kusema kwa kufanya hivyo, kutatishia wananchi, jibu ambalo halikumridhisha Zombe ambaye pia alihoji kama Mmari ana taarifa za eneo hilo kuwa maarufu kwa ujambazi.

Mmari alimjibu kwamba kuwa kwa mujibu wa Bageni, eneo hilo ni njia ya majambazi. Awali wakati wa maelezo yake, Mmari alipima kwa hatua umbali wa ukuta huo wenye matundu na eneo la gereji ya Mzuri na kubainika kuwa ni hatua 15 pamoja na umbali wa ukuta huo na eneo linalouzwa maji ambao ulibainika kuwa ni hatua 35.

Msafara huo pia ulikwenda katika eneo ambalo inadaiwa tukio la ujambazi na kuporwa kwa fedha za kampuni ya Bidco lilitokea karibu na eneo la machimbo ya mchanga Bunju ambako pia Mmari aliionyesha mahakama hiyo eneo waliloonyeshwa na Rashid kuwa yeye na Saadi walipiga risasi hewani.

Gazeti hili lilishuhudia msafara huo ukiongozwa na king’ora cha askari Magereza, huku kukiwa na msururu wa magari zaidi ya 25 na kusababisha baadhi ya madereva kuufananisha na msafara wa rais na katika maeneo yote ambayo Mahakama ilikuwa ikiendelea kulikuwa na ulinzi mkali.

Katika baadhi ya maeneo ulikopita, watu walijitokeza wakiushangaa, huku wengine wakishangilia na wengine wakisikika wakizomea na kutoa maneno ya kashfa dhidi ya watuhumiwa. Kesi hiyo itaendelea leo ambako shahidi huyo ataendelea kutoa ushahidi wake. Katika kesi hiyo, Zombe na wenzake 12, wanatuhumiwa kuwaua Ephraim Sabinus Chigumbi, Sabinus Chigumbi (Jongo), Mathias Lung’ombe na Juma Ndugu ambaye alikuwa dereva teksi, Januari 14, mwaka 2006 katika msitu wa Pande, Mbezi Luisi wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam.
 
sasa MKIAMBIWA HII NI JESHI LA MAJAMBAZI MTAKATA WANANCHI???????

CHIKO ALIIBA NA SASA KALETWA MJINI KWANZA KAWA MTOTO WA MJINI NA VIDILI VYAKE...KAMA ALIWEZA KUCHEZA NA MAJAMBAZI NA KUMILIKI MAGARI YA WIZI DAR SI ATAPANGA RANGE ROVER.....


MAHITA YEYE KAAMUA KULA KUKU!!!!ANAJITAHIDI KUJITAKASA NA WATU ALIOUA KWA KUTOA MISAADA MISIKITINI!!!!!!

LINI MAJAMBZI POLISI WATACHUKULIWA HATUA JAMANI??????
 
Kwa kweli Zombe anapaswa kuubeba huo mzigo maana baada ya kuachiwa kukaimu ukamanda wa mkoa ndiyo ujambazi ukazidi
 
Kwa kweli Polisi hapa kuna mnuko wa ujambawazi ndani ya geshi la polisi. Angalieni Jeshi la wananchi watachukua nchi! Ufisadi, mikataba mibovu, kutojali wananchi wa chini, maisha mabaya kwa kasi mbaya, hatuendelei bila sababu ya msingi, uzembe, utovu wa nidhamu, ufuska, anasa, majidai, majivuno, kujigamba kwa viongozi, n.k. Wamesahau viongozi baadhi kuwa hii nchi ni ya wananchi na sio yao. Hili narudia tena. Ni kama mpira ukiujaza hewa siku zte hewa hutafuta pa kutokea manake "pancha". Sas nguvu ya wananchi inajazwa na viongozi wasiofanya maamuzi kwa manufaa ya wengi bali ya mtu mmoja. Kulindana. Haya itakuwa kama utani wa ngumi ujue. Hayeni jamani msalieni mtume.
 
Zombe ataka SMG

2008-09-03 10:28:18
Na Hellen Mwango

Mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini na dereva teksi mmoja, aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam,wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe, ameiomba Mahakama Kuu kuamuru zipelekwe silaha ili zifyatuliwe kwenye ukuta wa Posta kwa lengo la kuoanisha matundu yanayodaiwa na upande wa mashitaka kuwa hayakupigwa na risasi za bunduki.

Ukuta huo ndiyo sehemu ambayo Zombe na wenzake wanadai kuwa kulitokea mapambano ya kujibishana risasi kati yao na wafanyabiashara waliouawa.

Zombe alitoa madai hayo eneo la Sinza, jijini Dar es Salam baada ya Mahakama hiyo kuhamishia shughuli zake katika maeneo yanayodaiwa kuuawa marehemu hao ikiwemo Barabara ya Sam Nojuma, msitu wa Pande na Bunju jijini Dar es Salaam.

Zombe alidai kuwa yeye ni mtaalamu wa silaha hivyo matundu yanayoonekana ni ya risasi na kama hawaamini basi zipelekwe SMG zifyatuliwe na matundu yatakayotokea yalinga nishwe na yaliyopo ili kuthibitisha kama yale yanayoonekana yanaweza kuwa ya risasi au la.

``Huu ukuta ni wa zege hivyo risasi haiwezi kupenya moja kwa moja na kama hamuamini waitwe askari wa kikosi cha kupambana na uhalifu hapa wafyatue risasi ili tuone na kuhakikisha kama matundu ni ya risasi au la,`` alidai Zombe.

Hata hivyo, ombi hilo la Zombe lilikataliwa na Jaji Kiongozi Salum Massati, ambaye alisema hakuna haja ya kufanya hivyo na kwamba risasi hizo zitawashtua wanananchi.

Msafara huo ambao ulikuwa kivutio kikubwa kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ulikopita, uliondoka Mahakama Kuu majira ya saa 4: 30 asubuhi ukiwa na magari zaidi ya 20, huku ukiongozwa na magari mawili aina ya Toyota Land Cruiser zilizokuwa na askari magereza na ving`ora.

Pia kulikuwa na Land Rover Defender nyingine mbili zikiwa na askari kanzu waliosheheni silaha mbalimbali.

Zombe na baadhi ya washtakiwa wenzake walipandishwa kwenye Defender namba STK 1029 na washitakiwa wengine walipanda gari lenye namba STK 1695.

Msafara huo, ulipofika eneo la Sinza C saa 4:50 ambako inadaiwa ndiko marehemu walikamatwa kabla ya kuuwawa, Jaji Kiongozi Salum Massati anayesikiliza kesi hiyo alianza kuendesha kesi ambapo Shahidi wa 30, Emson Mmari, ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora.

Kamanda Mmari aliongozwa na Wakili wa Serikali, Alexander Mzikila wakati akitoa ushahidi wake hadi saa 5:02.

Sehemu ya mahojiano yao yalikuwa hivi:

Mzikila: Shahidi hapa ni wapi?

Shahidi: Hapa ni Sinza nyumbani kwa Alex Ngonyani na Benadetha Lyimo ambao ni shahidi wa kwanza na wa pili katika kesi hii.

Mzikila: Nini madhumuni yenu kuja hapa?

Shahidi: Kupata maelezo kwa Benadetha kama kweli marehemu alikuwa akileta fedha hapa.

Mzikila: Nyumba gani marehemu walipeleka fedha?

Shahidi: Ndiyo hii (wakati huo mahakama ilikuwa nje ya nyumba ya Benadetha).

Mzikila: Gari ya marehemu ilipaki eneo gani?

Shahidi: Ilipaki ng'ambo ya nyumba hii.

Mzikila: Shahidi ulieleza mahakama kuwa kulikuwa na gari ya polisi, je uliambiwa zilikuwa upande gani kwa hapa?

Shahidi: Gari ya ilikuwa imezuia gari waliyokuwanayo marehemu kwa mbele na ilikuja gari ya Bageni kadhalika mshitakiwa wa tatu Ahmed Makelle alikuwa na gari pia. Gari la Polisi Chuo Kikuu lilikuwa linaendeshwa na Koplo Nyangerela ambaye ni mshitakiwa wa tano.

Baada hapo mahakama ilihamishia shughuli zaka eneo la barabara ya Sam Nujoma, ambapo ilikuwa saa 5:02 hadi 5:10 asubuhi na baada ya kufika mahojiano yalikuwa hivi:-
Mzikila: Hapa ni wapi?

Shahidi: Ni barabara ya Sam Nujoma, eneo ambalo tuliambiwa lilitokea tukio la uporaji wa fedha za kampuni ya Bidco.

Mzikila: Ni gari gani ilikuwa imeporwa fedha hzio?

Shahidi: Mercedis Benz mali ya kampuni hiyo.

Mzikila: Nani aliwaongoza katika maeneo haya?

Shahidi: Ni Sajini Nikobai ambaye aliwahi kuwa katika timu ya upepelezi ya kwanza kabla Rais hajaunda tume.

Mzikila: Kuna mabadiliko makubwa katika barabara hii, ni kitu gani kinakuonyesha kuwa ni hapa?

Shahidi: Kuna alama ya eneo la Konoike ya zamani na ndio sababu ninapakumbuka vizuri.

Mzikila: Baada ya hapa mlikwenda eneo gani kama timu ya wapelelezi?
Shahidi: Tulikwenda eneo la ukuta wa Posta kunakodaiwa marehemu walipambana na polisi na kuuawa.

Saa 5:16 hadi 5:20 asubuhi msafara wa mahakama ulihamia eneo la ukuta wa Posta.

Mzikila: Hapa ni wapi?

Shahidi: Mtukufu Jaji huu ni ukuta wa Posta niliosema.

Mzikila: Hayo matundu uliyosema yako wapi?

Shahidi: Haya hapa tuliambiwa yamepigwa kwa bunduki aina ya SMG (alionyesha matundu yaliyokuwa katika ukuta huo).
Mzikila: Je, mlifanikiwa kuwahoji watu?

Shahidi: Ndiyo, kwenye gereji hii hapo ng`ambo ya ukuta na mmikili wake namkumbuka kwa jina la Mzuri.

Mzikila: Kuna umbali gani kati ya ukuta na gereji? Piga hatua tujue.

Shahidi alipiga hatua kutoka kwenye ukuta hadi ilipo gereji huku Zombe akihesabu ambapo kulikuwa na umbali wa hatua 15.

Mzikila: Urefu wa ukuta wa Posta ni mita ngapi?

Shahidi: Ni mita mbili.

Mzikila:Nani mwingine mlimhoji?

Shahidi: Muuza maji ambaye alikuwa umbali wa hatua 35 kutoka kwenye ukuta wa Posta.

Mzikila: Madhumuni ya kuwahoji waliokuwa eneo hili ni nini?

Shahidi: Kama walisikia milio ya risasi Januari 14, 2006, ambapo walituambia mimi na timu ya wapelelezi wenzangu kuwa hawakuwahi kusikia.

Mzikila: Nini kiliwafanya mje eneo hili?

Shahidi: Bageni alidai kulikuwa na kutupiana risasi kati ya waliodaiwa kuwa majambazi na polisi.

Mzikila: Katika uchunguzi wenu, polisi walijeruhiwa katika tukio hilo?
Shahidi: Polisi hawakujeruhiwa.

Baada ya mahojiano hayo msafara huo ilianza safari ya kuelekea Mbezi Luis msitu wa Pande saa 5.48 eneo hilo liko kilomita 21 kutoka Ubungo, jijini Dar es Saalaam.

Baada ya msafara huo kufika Mbezi Mwisho watu walikuwa wamejipanga pembeni ya barabara kana kwamba wanasubiri mapokezi ya Rais.

Watu hao walisikika wakisema kuwa yametimia hakuna aliye juu ya sheria, sheria ni msumeno. Sheria msumeno, Sheria msumeno, hakuna aliye juu ya Sheria, waandishi andikeni watu wajue kinachoendelea.

Msafara huo ulifika Pande majira ya saa 6:28 na mara moja mahakama ilianza shughuli zake na mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo.

Mzikila: Shahidi unaweza kutueleza hapa ni mahali gani.

Shahidi: Msitu wa serikali wa Pande.

Mzikila. Nani alikuelekeza hapa?

Shahidi: Mshtakiwa wa 11 PC Rashid.

Mzikila: Lengo la kuja huku ilikuwa nini?

Shahidi: Tulikuja hapa baada ya mshtakiwa wa 11 katika kesi hii Rashid kutueleza kuwa kule Sinza inakodaiwa kuwa wale wafanyabiashara waliuawa si kweli na alisema waliuawa hapa.
Mzikila: Alikueleza waliuawaje?

Shahidi: Alisema walikuwa wakiteremshwa kutoka kwenye gari na kulazwa kifudifudi kisha walipigwa risasi na Koplo Saad.
Mzikila: Eneo hili mlikuta nini?

Shahidi: Tulikuta damu tukaichukua na kuipeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi ili kujua kama ni ya binadamu au mnyama.

Mzikila: Zaidi ya damu nini kingine mliona?

Shahidi: Maganda mawili ya risasi na tulipiga picha eneo zima la tukio.
Mzikila: Huyo aliyewaleta aliwaambia nini kuhusu maiti.

Shahidi: Hatukuzikuta, lakini alisema walizipeleka hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Mzikila: Baada ya hapa mlienda wapi.

Shahidi: Bunju

Mzikila: Mlienda siku gani.

Shahidi: Siku hiyo hiyo Machi 7.

Baada ya mahojiano hayo, Zombe alisikika akidai kuwa hajawahi kufika eneo hilo la Pande na labda vijana wake ndio wanaopajua.

Hata hivyo, mshtakiwa wa 11 kwenye kesi hiyo, Rashid Lema, alimjibu Zombe kwa jazba akimtaka aeleze vizuri namna walivyosherehekea baada ya kufanya mauaji hayo.

Baada ya majibu hayo ya Rashid, Zombe alikaa kimya na kuingia ndani ya gari na safari ya kuelekea Bunju ilianza.

Mahojiano ya Bunju yalikuwa hivi:

Mzikila: Shahidi tueleze hapa ni wapi

Shahidi: Bunju machimbo ya mchanga

Mzikila: Nani aliwaongoza hadi eneo hili.

Shahidi: Mshitakiwa wa 11 Rashid Lema.

Mzikila: Aliwaeleza madhumuni ya kuja huku ni nini?

Shahidi: Alisema walielekezwa na Bageni (mshtakiwa wa pili) waje kufyatua risasi yeye (Rashid) afyatue tatu na Saad ambaye hajakamatwa hadi sasa alitakiwa kufyatua sita.

Shahidi: Tulipiga picha na kuchora ramani ila hatukupata maganda ya risasi kwa kuwa walishayachukua na kumpelekea Bageni.

Mzikila: Rashid alikueleza huku walikuja na nani?
Shahidi: Alikuwa na dereva, Rajabu na Koplo Saad.

Baada ya maelezo hayo, Jaji Kiongozi Salum Massati aliahirisha kesi hiyo hadi leo asubuhi ili Mmari kuendelea kutoa ushahidi wake.

Mbali na Zombe na Bageni, washtakiwa wengine ni Ahmed Makelle, Jane Andrew, Noel, Nyangerera, Imanuel Mabula, Felix Cedrick, Rashid, Rajabu Hamis na Abeneth.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Januari 14 mwaka 2006, katika msitu wa Pande Mbezi Luis waliwaua kwa kuwapiga risasi Ephraem Chigumbi, Sabinus Chigumbi, Mathias Lukombe na Juma Ndugu
 
Zombe adaiwa kutumia simu ya upepo kufanikisha mauaji ya wafanyabiashara

Na Nora Damian

SHAHIDI wa 30 katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa Mahenge na dereva teksi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam (ACP) Abdallah Zombe na wenzake jana aliieleza Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam kuwa Zombe alikuwa akiwasiliana kwa simu na mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo, Christopher Bageni ili kufanikisha mauaji hayo.

Shahidi huyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Edson Mmari aliieleza mahakama kwamba mshitakiwa wa 11 DC Rashidi Lema aliyewaeleza kuwa Zombe alikuwa akiwasiliana kwa ‘redio call' na Bageni ili kufanikisha mauaji hayo.

ACP Mmari pia aliwataja washitakiwa 10 katika kesi hiyo ambao walikwenda katika msitu wa Pande ulioko Mbezi Louis wilayani Kinondoni ambako kunadaiwa mauaji hayo yalifanyika.

Aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Christopher Bageni (mshitakiwa wa pili), ASP Ahmed Makelle (mshitakiwa wa tatu), PC Jane Andrew (mshitakiwa wa tano), CPL Emanuel Mabula (mshitakiwa wa saba) na CPL Felix Cedrick.

Washitakiwa wengine waliokwenda kwenye msitu huo ni PC Michael Sonza (mshitakiwa wa tisa), Ebeneth Saro (mshitakiwa wa 10), DC Rashidi Lema (mshitakiwa wa 11), CPL Rajabu Bakari (mshitakiwa wa 12) na CPL Festus Gwabisabi (mshitakiwa wa 13).

ACP Mmari alidai walifanikiwa kuwatambua washitakiwa hao kutokana na maelezo ya washitakiwa wa 11, 12 na 13.

Shahidi huyo alidai katika upelelezi wao walibaini kuwa wafanyabiashara na dereva teksi wanaodaiwa kuwa ni majambazi walikamatwa saa 12.30 jioni na kwamba walifikishwa katika msitu wa Pande majira ya usiku.

Shahidi huyo alieleza msitu huo ni mali ya Serikali na kwamba barabara ya kuelekea kwenye msitu huo inatumiwa na watu wa maliasili na mtu mwingine akitaka kuutumia ni hadi apate kibali kutoka maliasili.

Baadhi ya mahojiano baina ya mawakili Alexander Mzikila, Jerome Nsemwa na Gaudienus Ishengoma na shahidi huyo yalikuwa kama ifuatavyo.

Wakili Mzikila: Katika upelelezi wenu mlifahamu ni muda upi wanaodaiwa kuwa majambazi walikamatwa?

Shahidi: Walikamatwa kati ya saa 12:30 jioni na kuendelea.

Wakili: Katika upelelezi wenu kwenye msitu wa Pande wanaodaiwa kuwa majambazi walifikishwa saa ngapi?

Shahidi: Walifikishwa usiku.

Wakili: Msitu wa Pande ni aina gani ya msitu?

Shahidi: Ni hifadhi.

Wakili Nsemwa: Nani alikuwa anamuhoji Rashidi Lema (mshitakiwa wa 11)?

Shahidi: Alikuja mbele yetu na alipoonyesha yuko tayari kutoa maelezo yake, mimi niliamriwa nimpeleke kwa mlinzi wa amani.

Wakili: Aliwaeleza nini kuhusu mauaji hayo?

Shahidi: Alisema mauaji yalifanikiwa baada ya Zombe na Bageni kuwasiliana kwa ‘redio call'.

Wakili: Kama Zombe angewasiliana kwa ‘redio call' na kutoa amri ya kuua, watu si wangesikia?

Shahidi: Ndio wangesikia lakini ofisa hawezi kuzungumza na simu za kawaida mbele ya watu.

Wakili: Mlifanya uchunguzi kwenye simu za Zombe za mkononi?

Shahidi: Hatukushughulikia hilo.

Wakili: Iambie mahakama kuhusiana na timu yenu ya upelelezi ilikuwa na watu wangapi na uwataje kwa majina.

Shahidi: Kiongozi wetu alikuwa mama Mkumbi, mimi mwenyewe, Martin Ngasa, ASP Kabaleke, Sajent Filimini na Sajent David.

Wakili: Timu hiyo iliundwa na nani?

Shahidi: Iliundwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa wakati huo DCI Adadi Rajabu.

Wakili: Je mliwahoji madereva wa magari yaliyokuwa doria siku ya tukio?

Shahidi: Hapana hatukuwahoji.

Wakili: Uliwahi kuona Zombe akihojiwa na Mkumbi?

Shahidi: Sijawahi kuona na si busara kiongozi wangu ahojiwe mbele yangu.

Wakili Ishengoma: Kabla ya tukio hili kutokea, je uliwahi kwenda msitu wa Pande?

Shahidi: Tulienda Machi 7, mwaka 2006 kwa ajili ya upelelezi wa tukio hili na ilikuwa mara yangu ya kwanza.

Wakili: Wewe ulivyouona msitu ule je mtu ambaye hajawahi kwenda kule angeweza kufika majira ya usiku?

Shahidi: Siwezi kujua inategemea.

Wakili: Nani alipeleka miili ya marehemu Muhimbili?

Shahidi: Sajent James alipeleka miili ya marehemu mochwari na hadi sasa hajakamatwa.

Wakili: Je wewe ulifanikiwa kwenda mochwari?

Shahidi: Hapana sikufanikiwa.

Awali ilidaiwa katika mahakama hiyo, kuwa washitakiwa hao kwa pamoja Januari 14, mwaka 2006 katika msitu wa Pande ulioko Mbezi Louis wilayani Kinondoni waliwaua wafanyabishara watatu wa madini ambao walikuwa wakazi wa Mahenge mkoani Morogoro pamoja na dereva wa teksi, mkazi wa Manzese jijini Dar es Salaam.

Wafanyabiashara hao ni Ephraim Sabinus Chigumbi, Sabinus Chigumbi maarufu kwa jina la Jongo, Mathias Lunkombe na dereva wa teksi Juma Ndugu.

Watuhumiwa wengine mbali ya Zombe ni SP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makelle, F.5912 PC Noel Leonard, WP 4593 PC Jane Andrew, D6440CPL Emmanuel Mabula, E6712 CPL Felix Cedrick, D8289 PC Michael Sonza, D 2300CPL Ebeneth Saro, d9312D/C Rashid Lema, D4656 C/CPL Rajab Bakari na D.1367 D/CPL Festus Gwabisabi.
 
...Zombe lilikuwa ni jambazi liuaji ndani ya system ambalo lilitakiwa kulinda wananchi lakini likawa linafanya opposite kwa maslahi yake,nina uhakika kuna wengi sana ndani ya system kama Zombe,Zombe lazima afungwe maisha aozee jela(niko against death penalty lakini naona he deserve more than death),sijui kwanini halitaki kufanya confession ili kusave pesa za walipa kodi hili jangili!
 
Nina wasiwasi kama Zombe atahukumiwa kwa haki. Kwa muelekeo ulivyo jamii ishamtia hatiani kabla ya hukumu.

Hii inajenga precedence mbaya sana huko tuendako, tuiache mahakama ifanye kazi ikiwa kila mtu anakuwa hakimu ni hatari sana kwa utawala wa sheria. He is innocent until proved guilty
 
Nina wasiwasi kama Zombe atahukumiwa kwa haki. Kwa muelekeo ulivyo jamii ishamtia hatiani kabla ya hukumu.

Hii inajenga precedence mbaya sana huko tuendako, tuiache mahakama ifanye kazi ikiwa kila mtu anakuwa hakimu ni hatari sana kwa utawala wa sheria. He is innocent until proved guilty
Hawezi kutiwa hatiani kwa sababu moja tu.
Anayo kadi ya sisiemu.
Habari ndio hiyo.
 
Asipotiwa hatiani nitaona kweli hakuna haki na mahakama itakuwa imehujumiwa kwa kweli...maana naona dhahiri....ameshiriki na ndio mchezo wake sana
 
Nahisi kama haki haitatendeka tena wananchi watakosa imani na ongozi za nchi hii na siku si nyingi wataweza kuwa ndio mahakama ndio BOT ndio mamlaka zote ndio kila kitu katika kusimamia vitu vyao na sio watu wachache wanao**** nchi hii bila ******
 
Nasikia huko bongo watu wanaandamana kuunga mkono hotuba ya Kikwete bungeni.... ila je watu wakitaka kuandamana kupinga hotuba hiyo watapewa kibali??? au wataambiwa polisi wachache wa kulinda ila wa kuwazuia wapo wengi.....?
 
Ushahidi wazidi kumkaba Zombe, adaiwa kuandaa kuihadaa Tume

Na Nora Damian

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam jana ilielezwa kuwa aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam ACP Abdallah Zombe ambaye anakabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabishara watatu wa madini wa Mahenge mkoani Morogoro na dereva teksi, alimuita mshitakiwa wa 12, Koplo Rajabu Bakari katika kesi hiyo na kumpangia maelezo kwenye karatasi ili akayaeleze kwenye tume ya Jaji Kipenka iliyoundwa na rais kuchunguza tukio la mauaji hayo.

Shahidi wa 31 katika kesi hiyo, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Omar Amir Omar (4, aliieleza mahakama kuwa yeye alikuwa mmoja wa watu walioteuliwa kupeleleza tukio hilo na kwamba aliwahoji washitakiwa wanne.

ASP Omar ambaye anafanya kazi Makao Makuu ya Upelelezi Dar es Salaam, aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Koplo Emanuel Mabula (mshitakiwa wa 7), Koplo Felix Cedrick (mshitakiwa wa , Koplo Rashidi Lema (mshitakiwa wa 11) na Koplo Rajabu Bakari (mshitakiwa wa 12).

Alidai kuwa wakati anamuhoji Koplo Rajabu Bakari alimueleza kuwa siku ya tukio alipangiwa kufanya doria eneo la Mwananyamala na kwamba wakati anarudi ofisini katika kituo cha polisi cha Oysterbay, majira ya jioni alikutana Bageni ambaye alimweleza waende Sam Nujoma kwenye tukio la ujambazi la kampuni ya Bidco.

Alidai walifika Sam Nujoma saa 12.30 jioni na kwamba aliiona pick-up ya kituo cha polisi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ikiwa na watu wanne waliokuwa wamelazwa chini.

Shahidi huyo alidai kuwa, wakati mshitakiwa huyo wakiwa katika eneo hilo, Sam Nujoma, Bageni aliwahoji watu wanne ambao walikuwa ni wafanyakazi wa kampuni ya Bidco na kwamba baada ya kumaliza askari waliokuwa kwenye gari la Chuo Kikuu walishuka na kuingia kwenye gari aina ya ‘Defender’.

ASP Omar ambaye anashughulikia upelelezi wa kesi zinazohusiana na makosa ya jinai,

alidai baada ya kuingia kwenye gari, Bageni aliamuru gari ielekee upande wa Ubungo na kwamba walienda hadi kwenye msitu wa Pande ulioko Mbezi Loius wilayani Kinondoni, kulikotokea mauaji hayo.

Alidai wakati wakiwa barabarani Bageni alikuwa akizungumza na simu yake huku akijibu; ‘ndio afande’.

Alidai walipofika katika msitu huo yeye (mshitakiwa wa 12) alikuwa akiongea na ‘redio call’ kuhusu tukio la ujambazi lililotokea Kijitonyama na kwamba alishtuka baada ya kusikia mlio wa risasi lakini hakushiriki katika kuwaua wafanyabiashara hao.

Alidai baada ya tukio hilo, maiti zilipakiwa kwenye ‘defender’ na kupelekwa kwenye hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Alidai walipofika katika kituo cha polisi cha Urafiki, Makelle na Bageni walishuka na kuingia ofisini huku akiwa amebeba mkoba mweusi na kwamba baada ya muda Zombe naye alifika na kuingia katika ofisi hiyo.

Shahidi huyo, alidai mshitakiwa alimweleza kuwa siku tatu baada ya tukio hilo kutokea aliitwa kwenye tume ya Jaji Kipenka iliyoundwa na rais kuchunguza mauaji hayo.

Alidai kabla hajaenda katika tume hiyo Zombe alimuita ofisini kwake na kumpa maelezo kwenye karatasi ya jinsi atakavyokuwa akiijibu tume hiyo, wakati akihojiwa.

Baadhi ya mahojiano baina ya wakili wa serikali Angaza Mwipopo na shahidi huyo yalikuwa kama ifuatavyo.

Wakili Mwipopo: Machi 3, mwaka 2006 ulifanya nini?

Shahidi: Nilimuhoji mshitakiwa wa 12 Koplo Rajabu Bakari.

Wakili: Ulichukua muda gani?

Shahidi: Si zaidi ya masaa 2.30.

Wakili: Alikueleza nini?

Shahidi: Alinieleza kuhusu tukio la mauaji lililotokea msitu wa Pande na lile la kwenda kufyatua risasi katika machimbo ya mchanga yaliyoko Bunju.

Wakili: Ulifahamu ni lini Bakari alifikishwa mahakamani?

Shahidi: Sikumbuki kwa sababu baada ya kumaliza kuchukua maelezo yake niliendelea na shughuli zangu nyingine.

Wakili: Machi 6, mwaka 2006 ulikuwa wapi?

Shahidi: Nilikuwa ofisini.

Wakili: Je kitu gani kilitokea?

Shahidi: Mama Mkumbi ambaye alikuwa kiongozi wa timu yetu alitueleza kuwa ataletwa mshitakiwa wa 11 ili tuweze kumuhoji.

Wakili: Je aliletwa?

Shahidi: Ndiyo.

Wakili: Je, kitu gani kiliendelea?

Shahidi: Alianza kuhojiwa na akasema amekuja ili aweze kutueleza ukweli wa tukio zima lilivyotokea

Wakili: Ni ukweli upi?

Shahidi: Ukweli juu ya tukio la mauaji ya wafanyabiashara lilivyotokea.

Baada ya mahojiano hayo wakili Mwipopo aliiomba mahakama ikubali kupokea maelezo ya washitakiwa wa 11 na 12 ili yawe kielelezo katika kesi hiyo lakini mvutano mkali uliibuka baina ya mawakili wa upande wa utetezi na mahakama.

Jaji Kiongozi Salum Masatti alimuuliza Wakili Denis Msafiri wa upande wa utetezi kama analo pingamizi kuhusiana na maelezo ya mshitakiwa wa 11 kutolewa kama kielelezo na wakili huyo alimuonyesha mshitakiwa ambaye aliyakubali na kusema kuwa hana pingamizi.

Hata hivyo wakili Majura Magafu alipinga maelezo hayo kutolewa katika mahakama hiyo, kwa madai kuwa yana mapungufu kisheria.

“Sisi tunapinga kupokelewa maelezo hayo mahakamani kwa sababu hayajitoshelezi na yanaweza kuleta maswali mengine kwamba mtu huyu alikuwa amepangwa kwa ajili ya kuwamaliza wenzake,” alisema wakili Majura.

Naye wakili Dieneus Ishengoma alipinga maelezo ya mshitakiwa wa 12 kupokelewa katika mahakama hiyo, kwa madai kuwa yanawagusa washitakiwa wengine.

“Mtukufu Jaji kwa mujibu wa kifungu cha 33, kifungu kidogo cha kwanza cha sheria ya ushahidi maelezo haya ni kama ungamo sisi tunapinga kupokelewa kwa sababu kuna mapungufu wakati wa kuandika maelezo haya,” alisema wakili Ishengoma.

Wakili wa serikali Mwipopo akijibu hoja za mawakili hao wa upande wa utetezi alidai kuwa hoja zao si za msingi kwani hata washitakiwa wenyewe wameyakubali maelezo yao.

“ Hoja zao si za msingi wanaona ushahidi unaanza kuwa mzito wanaanza kuhangaika,” alisema wakili Mwipopo ambaye anaiwakilisha Serikali.

Jaji Masatti baada ya kusikiliza hoja zote alitupilia mbali hoja za mawakili hao wa upande wa utetezi na maelezo hayo yalipokelewa katika mahakama hiyo kama kielelezo.?

“Ni mtuhumiwa pekee anayejua ukweli na kisheria maelezo ya mshitakiwa hayawezi kugusa washitakiwa wengine kama hakuna ushahidi mwingine unaounga mkono maelezo hayo,” alisema Jaji Masatti.

Awali ilidaiwa katika mahakama hiyo, kuwa washitakiwa hao kwa pamoja Januari 14, mwaka 2006 katika msitu wa Pande ulioko Mbezi Louis wilayani Kinondoni waliwaua wafanyabishara watatu wa madini ambao walikuwa wakazi wa Mahenge mkoani Morogoro pamoja na teksi, mkazi wa Manzese jijini Dar es Salaam.

Wafanyabiashara hao ni Ephraim Sabinus Chigumbi, Sabinus Chigumbi maarufu kwa jina la Jongo, Mathias Lunkombe na dereva teksi Juma Ndugu.

Watuhumiwa wengine mbali ya Zombe ni SP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makelle, F.5912 PC Noel Leonard, WP 4593 PC Jane Andrew, D6440CPL Emmanuel Mabula, E6712 CPL Felix Cedrick, D8289 PC Michael Sonza, D 2300CPL Ebeneth Saro, d9312D/C Rashid Lema, D4656 C/CPL Rajab Bakari na D.1367 D/CPL Festus Gwabisabi.
 
Back
Top Bottom